Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Samir Halila: Mfahamu mtu anayepigiwa upatu kutawala Ukanda wa Gaza
- Author, Mahmoud Al-Najjar
- Nafasi, BBC Arabic
- Akiripoti kutoka, BBC Arabic
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Katika siku za hivi karibuni, mfanyabiashara wa Kipalestina Samir Halila amekuwa akitajwa zaidi katika vyombo vya habari vya Kiarabu na kimataifa, huku kukiwa na mazungumzo juu ya uwezekano wa kuchukua utawala wa Ukanda wa Gaza baada ya vita kumalizika.
Haya yalianza baada ya ripoti ya gazeti la Israel la Yedioth Ahronoth kufichua mazungumzo mazito ya kumteua Halila kuwa gavana wa Ukanda wa Gaza, kwa ujuzi wa Mamlaka ya Palestina.
Pendekezo hilo, ilisema, lilikubalika kwa Waarabu, Waisraeli na Wamarekani. Ripoti hiyo ilizua taharuki kubwa katika duru za Kiarabu na kimataifa.
Kwa upande wake, Halila aliibuka kidedea na kuzungumza na vyombo kadhaa vya habari. Akizungumza na kituo cha redio cha Palestina Ajyal amesema kuwa, kile ambacho Yedioth Ahronoth ameripoti kuhusu kuteuliwa kwake si jambo jipya na kwamba kwa hakika amepokea simu kutoka kwa mwanakandarasi wa Canada anayefanya kazi na utawala wa Marekani kuchukua utawala wa Gaza baada ya vita.
Alibainisha kuwa baada ya kupokea ofa hiyo, alijadili suala hilo na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina mara kadhaa ili kupata uungwaji mkono wake, na kuviambia vyombo vya habari vya Kiarabu kwamba idhini yake ilitokana na idhini ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina.
Shirika rasmi la habari la Mamlaka ya Palestina, WAFA, baadaye lilijibu taarifa hizo.
Shirika hilo lilikanusha suala hilo lote, likielezea kama uwongo ulioenezwa na Halila, ambaye anajaribu kuihusisha Mamlaka ya Palestina na maafisa wake wakuu katika suala hilo, na kukwepa msimamo rasmi wa Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina na Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina, ambayo inakataa "kutenganisha Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi" kama sehemu ya mradi wa shirika la Israel.
Shirika hilo limesema kuwa ofisi ya rais wa Palestina inathibitisha kuwa utawala wa Ukanda wa Gaza uko chini ya mamlaka ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na serikali ya Palestina.
Samir Halila ni nani?
Halila alizaliwa mwaka 1957 katika Ukingo wa Magharibi wa mji wa Yeriko.
Alisoma Ramallah, akipata BA katika Sosholojia na Masomo ya Mashariki ya Kati kutoka Chuo Kikuu cha Birzeit katika Ukingo wa Magharibi mwaka 1981, na MA katika Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Marekani cha Beirut mwaka 1983.
Mnamo 1984, alifanya kazi kama mwalimu katika Chuo Kikuu cha Birzeit na akawa Mkuu wa Masuala ya Wanafunzi.
Nyadhfa alizoshika
Samir Huleileh ni mtu mashuhuri wa uchumi wa Palestina na mfanyabiashara mashuhuri katika Mamlaka ya Palestina.
Ameshikilia nyadhifa nyingi za kiuchumi na kisiasa, zikiwemo kama mjumbe wa ujumbe wa Palestina unaojadili masuala ya kiuchumi ya Makubaliano ya Oslo na Israel.
Pia aliwahi kuwa Naibu Katibu Msaidizi katika Wizara ya Uchumi na Biashara hadi 1997.
Halila aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Serikali ya Palestina kuanzia mwaka 2005 katika serikali ya marehemu Ahmed Qurei hadi Machi 2006.
Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Sera za Kiuchumi ya Palestina, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kituo cha Biashara cha Palestina (PalTrade), na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni kubwa ya Maendeleo ya Palestina na Uwekezaji wa Palestine (PAD).
Mnamo Agosti 2022, Halila alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Soko la Hisa la Palestina, nafasi aliyoshikilia hadi Machi 2025. Pia alichaguliwa katika Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Arka Real Estate mnamo 2023.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla