Maandamano Iran: Je, Kim Jong-un ana wasiwasi?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Je, Korea Kaskazini, ambayo, kama Iran, imekuwa chini ya vikwazo vikali na shinikizo la kiuchumi kwa miaka mingi, inatathmini vipi maandamano ya Iran?

Mamlaka ya Iran imeanzisha msako mkubwa na kukamatwa kwa watu wengi, na ingawa hakuna idadi rasmi ya vifo, Shirika la Kutetea Haki za Kibinadamu la Iran lenye makao yake makuu nchini Norway linasema takriban watu 3,428 wameuawa katika maandamano ya hivi majuzi nchini humo.

Ufuatiliaji huru wa hali hiyo nchini ni mgumu kutokana na mtandao na mawasiliano kukatwa na mamlaka.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema anaitazama hali ya Iran kwa umakini mkubwa na anazingatia chaguzi ngumu. Iran imeacha mlango wazi kwa mazungumzo lakini imeonya kuwa itajibu iwapo Marekani itachukua hatua za kijeshi.

Hali nchini Iran imezua maswali ya kutatanisha kwa serikali nyingine za kimabavu, na Korea Kaskazini huenda inafuatilia kwa karibu matukio hayo.

Je, Korea Kaskazini ilitangaza habari za maandamano makubwa nchini Iran?

Jibu rasmi la Korea Kaskazini kwa maandamano ya Iran limekuwa dogo sana. Vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini vimeangazia suala hilo kwa kiasi kidogo, vikitoa maelezo machache kuhusu wakati maandamano yalianza, sababu zao, au jinsi yameenea.

Badala yake, lengo kuu limekuwa katika kulaani "kuingilia Marekani" au kukosoa "tabia ya kinafiki ya vikosi vya uadui."

Kwa mujibu wa gazeti la Chama cha Wafanyakazi wa Korea Kaskazini, tangu mgogoro wa Iran uanze tarehe 28 Disemba mwaka jana, ripoti nane zimechapishwa zikirejelea "Iran." Kwa kuwa ripoti mbili kati ya hizi zinaihusu Israel, sita kati yake zimelenga Iran.

Gazeti hilo liliripoti kwamba Iran "ilikataa kabisa uingiliaji wa Marekani katika masuala yake ya ndani," "ilifichua tabia ya unafiki ya vikosi vya uhasama," "ililaani sera za Marekani dhidi ya Iran," "ililaani vitisho vya kijeshi vya Marekani," na "kufichua uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran."

Shirika Kuu la Habari nchini Korea pia limechapisha ripoti kumi na moja zenye "Iran" katika kichwa cha habari tangu mwanzo wa mgogoro wa Iran.

Bila kurejelea moja kwa moja maandamano yenyewe, shirika hilo la habari lilitangaza kuwa Iran "imefichua uingiliaji wa Marekani katika nchi yake," na kuongeza kuwa "ushahidi umepatikana kwamba Marekani ilihusika katika shughuli za kigaidi nchini Iran na kuna video za silaha zinazosambazwa kati ya watu binafsi."

Hakuna vyombo hivi vya habari vilivyotoa maelezo yoyote kuhusu historia ya maandamano au idadi ya waathiriwa. Lengo kuu limekuwa juu ya vitisho vya kigeni na ujumbe dhidi ya Marekani na Israel.

Mbinu hii inatafsiriwa kuwa kimya cha makusudi kwa upande wa Korea Kaskazini ili kuzuia dhana ya "maandamano" kuenea miongoni mwa raia wake.

Park Won-gun, profesa wa masomo ya Korea Kaskazini katika Chuo Kikuu cha Ewha Womans, aliambia BBC kwamba Korea Kaskazini "hufuatilia maandamano ambayo watu katika nchi nyingine hushikilia dhidi ya serikali au kutoa madai kwa uangalifu sana, lakini mara chache huyaripoti."

Je, Korea Kaskazini inaionaje hali ya Iran?

Ujumbe wa wazi wa Korea Kaskazini katika suala hili huenda ukawa na sauti ya kisiasa inayozingatia udhibiti wa ndani na propaganda.

Wataalamu wanasema kinachoendelea Iran kinaweza kuwa suala nyeti kwa uongozi wa Korea Kaskazini. Hasa, hali ya kutoridhika kwa umma kati ya vikwazo vya muda mrefu na shinikizo la kiuchumi linaweza kuonekana kuwa tishio kwa Korea Kaskazini.

Cho Han-beom, mtafiti katika Taasisi ya Umoja wa Korea, aliambia BBC kwamba Korea Kaskazini itakuwa "na wasiwasi mkubwa." Aliongeza: "Kwa kuwa Korea Kaskazini imeona kuanguka ghafla kwa tawala nyingi za kidikteta, ikiwa ni pamoja na Nepal katika Asia ya Kusini, hali ya Iran itakuwa mbaya sana kwa ajili yake."

Profesa Park alisema tawala zote mbili ni serikali zenye nguvu za kimabavu, na kwa kuwa hali ya Iran inasababishwa na matatizo ya kiuchumi na inachukuliwa kuwa changamoto ya mamlaka kamili, Korea Kaskazini itafuatilia maendeleo ya Iran "kwa uangalifu mkubwa."

Iran na Korea Kaskazini; tofauti lakini zinafanana

Iran na Korea Kaskazini zote zina mifumo ya kimabavu ya serikali na kudumisha mtazamo wa pamoja kwamba mamlaka ya kiongozi ni juu ya mfumo mzima.

Nchini Iran, Kiongozi Mkuu Ali Khamenei ndiye mwenye mamlaka kuu katika muundo wa utawala, na huko Korea Kaskazini, Kim Jong-un ana udhibiti kamili wa kisiasa, kijeshi na kiitikadi.

Mifumo yote miwili inaona changamoto za umma kwa mamlaka ya viongozi kama changamoto kwa utawala.

"Iran na Korea Kaskazini ni tofauti sana, lakini kimuundo zinafanana, kwa sababu kiongozi ametakaswa katika mifumo yote miwili," Bw. Cho alisema. "Unaweza kuona mgogoro wa Iran kama hali sawa na Korea Kaskazini na kuona kama tishio kwa mfumo."

Hata hivyo, kuna tofauti ya wazi katika kiwango cha uwazi na uhuru wa kijamii.

Nchini Iran, inawezekana kusafiri nje ya nchi na kupata taarifa za kigeni, na kutoa maoni kwenye mtandao ya kijamii pia inaruhusiwa kwa kiasi kikubwa, ikilinganishwa na Korea Kaskazini.

Lakini nchini Korea Kaskazini, upinzani wa kisiasa na kutoridhika ni nadra sana kuvumiliwa katika ngazi ya jamii, mbali na uhuru wa habari . Kwa hivyo, utumiaji wa moja kwa moja wa mivutano ya kisiasa na kutoridhika kwa kijamii kunakoonekana nchini Iran kuna vikwazo kwa hali ya Korea Kaskazini.

"Sababu kuu ya matatizo ya kiuchumi ya nchi zote mbili ni vikwazo," Bw. Park alisema, akiongeza kuwa wote wamekabiliwa na vikwazo tangu walipoanza juhudi zao za maendeleo ya nyuklia.

Ameeleza kuwa licha ya tofauti kubwa zilizopo, kuna mambo mengi yanayofanana, ndiyo maana Korea Kaskazini lazima iangalie kwa karibu zaidi hali ya Iran.