Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tunajua nini kuhusu binti wa Kim Jong Un – mrithi wake mtarajiwa?
Kuwasili kwa Kim Jong Un nchini China katika mkutano na nchi hiyo kumebeba vichwa vya habari.
Lakini msichana aliyevalia nadhifu aliyesimama nyuma yake alipokuwa akitoka kwenye treni yake ya kivita ndiye aliyevutia zaidi: Kim Ju Ae, bintiye kiongozi wa Korea Kaskazini.
Kulingana na shirika la kijasusi la Korea Kusini, Ju Ae ndiye anayetarajiwa kuwa mrithi wa babake.
Ju Ae, anaaminika kuwa mtoto wa pili wa Kim Jong Un na mke wake, Ri Sol-Ju, wakiwa na watoto watatu. Hata hivyo Kim ni msiri sana kuhusu familia yake, alimtambulisha mkewe kwa umma baada ya muda mrefu kupita tangu kuoana.
Kim Ju Ae ndiye mtoto wao pekee ambaye kuwepo kwake kumethibitishwa na uongozi wa nchi hiyo. Hakuna mtoto mwingine ambaye ameonekana hadharani.
Habari za kuwepo kwake ziliibuka kwa mara ya kwanza kutoka kwa mchezaji wa mpira wa vikapu Dennis Rodman, ambaye alifichua kwa gazeti la The Guardian mwaka 2013 kwamba "alimbeba mtoto Ju Ae" wakati wa safari ya kwenda katika nchi hiyo.
Kim Ju Ae
Hakukuwa na taarifa nyingi kuhusu binti huyo hadi Novemba 2022, alipoonekana pamoja na baba yake wakati wa uzinduzi wa kombora la masafa marefu (ICBM).
Februari mwaka uliofuata, alikuwa akionekana mara kwa mara na kuhudhuria karamu za maafisa wakuu.
Shirika la Kitaifa la Ujasusi la Korea Kusini (NIS) lilitoa maelezo machache kwa wabunge kuhusu msichana huyo, kulingana na shirika la habari la AP.
Shirika hilo lilisema binti huyo anapanda farasi, kuteleza kwenye theluji na kuogelea, na alisomeshwa nyumbani katika mji mkuu Pyongyang. Na ana umri wa miaka 10.
Kufikia Januari 2024, NIS lilitoa taarifa nyingine: msichana huyo ndiye "mwenye uwezekano mkubwa" wa kumrithi Kim Jong Un - ingawa walibaini kuwa bado kuna uwezekano wa kurithi nafasi nyingine kwa sababu baba yake bado ni mdogo.
Tangu wakati huo, ameonekana kando ya baba yake mara nyingi. Akiwa amesimama karibu naye katika uzinduzi wa ICBM na gwaride la kijeshi, amepokea saluti za kijeshi kutoka kwa makamanda wakuu wa kijeshi.
Lakini Jumanne ilikuwa mara yake ya kwanza kuonekana nje ya Korea Kaskazini, na safari hiyo huenda ikachochea zaidi uvumi kuwa huenda akamrithi babake.
Familia ya Kim, ambayo imetawala Korea Kaskazini tangu 1948, inawaambia raia wa nchi hiyo kuwa familia hiyo inatoka kwenye damu takatifu, kumaanisha wao pekee ndio wanaweza kuongoza nchi.
Hata hivyo, kuna uvumi kwamba Kim amemtambulisha binti yake katika hatua hii ili kujaribu kuondokana na chuki katika nchi yenye mfumo dume, ambayo haijawahi kuongozwa na mwanamke.
Kuna uwezekano akawa mrithi?
Korea Kaskazini imejitenga sana na haijulikani kwa ulimwengu wa na wengi wanajiuliza kwanini kuonekana kwa Kim Ju Ae karibu na baba yake imekuwa mara kwa mara.
Raia wa Korea Kaskazini wanaambiwa kuwa Kims anatoka kwenye damu takatifu, ikimaanisha tu hao ndio watu wanaweza kuongoza nchi na baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa kumtambulisha kwa umma katika umri mdogo kama huo inaweza kuwa njia ya kiongozi wa Korea Kaskazini ya kuhakikisha kuwa binti yake anajiimarisha muda mrefu kabla ya kuchukua madaraka.
Hakuna pendekezo kwamba huenda kurithishwa kwake mamlaka kukatokea wakati wowote hivi karibuni, na uvumi wa zamani kwamba Kim Jong Un alikuwa katika hali mbaya ya afya umetupiliwa mbali.