Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ajali ya ndege Iran: Balozi ashutumiwa kupanga maandamano Iran
Uingereza imeilaumu Iran kwa kumkamata balozi wa Uingereza nchini Iran na kukiuka utaratibu wa sheria za kimataifa.
Rob Macaire alishikiliwa na polisi baada ya kuhudhuria ibada ya waliokufa katika ndege iliyodukuliwa na jeshi la Iran siku ya jumatano.
Balozi huyo ambaye aliondoka mara baada ya ibada hiyo kugeuka kuwa maandamano.
Lakini kabla ya hajafika katika makazi yake ubalozini, balozi huyo alikamatwa kwa madai kuwa alisaidia kupanga maandamano hayo.
Katika ujumbe wake wa tweet, bwana Macaire alikataa kuhusika na maandamano hayo , waziri wa mambo ya nje Dominic Raab amelaumu vikali kukamwatwa kwa balozi huyo.
Bwana Macaire alisema kuwa alihudhuria ibada ile kwa sababu ni jambo la kawaida kwa watu kukusanyika na kutoa heshima za mwisho kwa marehemu na vilevile kulikuwa na raia wa Uingereza waliopoteza maisha katika ndege hiyo.
Balozi aliongeza kuwa :" Kumkamata mwanadiplomasia ni kinyume cha sheria kwa nchi yeyote ile"
Waandamanaji walikusanyika barabarani katika mji mkuu wa Tehran, wakionyesha hasira zao kwa maafisa huku wakiwaita waongo kwa kukataa kuidukua ndege ya Ukrainne.
Siku ya jumamosi, Iran ilikiri kuhusika kuidondosha ndege hiyo kwa bahati mbaya, siku tatu baada ya watu 176 kufariki katika ajali ya ndege.
Waziri wa ulinzi, Brandon Lewis alisema kuwa kukamatwa kwa balozi wa Uingereza ni jambo ambalo halikubaliki kabisa.
"Iran inapaswa kujirekebisha na vitendo vyake ili kuweza kushirikiana na mataifa mengine kwa utaratibu husika," Bwana Lewis alisema.
Chini ya makubaliano ya Vienna, wanadiplomasia hawawezi kushitakiwa au kukamatwa katika nchi waliyoenda kufanyia kazi.
Ofisi ya mambo ya nje, inatakiwa kutoa maelezo zaidi kuhusu tukio hilo.
Bwana Raab aliongeza kusema kuwa: "Kukamatwa kwa balozi mjini Tehran bila maelezo yoyote ni kwenda kinyume na sheria za kimataifa.
"Serikali ya Iran inavuka mipaka, Ikiendelea hivi inaweza kutengwa kisiasa na kiuchumi, kama haitachukua hatua madhubuti kukabiliana na mvutano huu ambao unawajumuisha hata wanadiplomasia."
Bwana Macaire alishikiliwa kizuizini kwa saa tatu baada ya kukamatwa nje ya duka la kinyozi akiwa anaelekea ubalozini.
Gazeti la Iran la Etemad lilionyesha picha za balozi huyo katika kurasa za Twitter mara baada chombo cha habari cha Tasnim kutangaza kukamatwa kwake.
Siku ya jumatano, Iran ilikanusha kuhusika na ajali hiyo iliyoua watu 176 ,wanne wakiwa waingereza.
Lakini jumamosi , rais Hassan Rouhani alikiri kuwa jeshi la Iran lilidondosha ndege ile kwa bahati mbaya wakati ikirusha makombora katika kambi za jeshi za Marekani.
Rais Rouhani alisema kuwa kosa hilo halisameheki hivyo waliohusika wote watachukuliwa hatua.
Ajali hiyo ilitokea saa chache baada ya Iran kurusha makombora katika kambi mbili za jeshi la Marekani zilizopo Iraq.
Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson alisema kuwa alitaka Iran ifanye uchunguzi wa janga hilo la ajali kubwa.
Alisema kuwa uchunguzi wa ndege hiyo unapaswa kuwa wa wazi, huru na uangalie kila kitu, na kuongeza kuwa atashirikiana na mataifa mengine yaliyopoteza raia wake kama Canada na Ukraine.
Serikali ya Uingereza imetaja raia waliokuwa katika ndege ya Ukraine iliyopata ajali ni Mohammed Reza Kadkhoda Zadeh, ambaye alikuwa mmiliki wa mashine za kufulia huko West Sussex, Mhandisi wa BP Sam Zokaei kutoka Twickenham,na mwanafunzi wa chuo kikuu(PhD on Engeneering) na mhandisi Saeed Tahmasebi, aliyekuwa akiishi Dartford.
Bwana Tahmasebi alikuwa na mke wake , Niloufar Ebrahim,raia wa Iran.
Kushambuliwa kwa ndege hiyo kulikuja baada ya Marekani kuwa na mvutano na Iran mara baada ya kumuua kiongozi wa kijeshi wa Iran jenerali Qasem Soleimani tarehe 3 Januari.
Iran iliapa kulipiza kisasi mauaji ya kiongozi wa jeshi, tukio ambalo rais Trump alitoa amri.