"Tulidanganywa": Jinsi mwanamke alivyowarubuni wanaume wa kigeni kupigana kwenye mstari wa mbele wa Urusi

Muda wa kusoma: Dakika 8

Miali ya moto inagusa kingo za pasipoti ya Omar.

"Inaungua vizuri," anasema mwanamke asiyeonekana , akiongea kwa Kirusi, katika video hiyo.

Omar, mfanyakazi wa ujenzi raia wa Syria mwenye umri wa miaka 26, alikuwa tayari ametumwa kwa takribani miezi tisa kwenye mstari wa mbele wa vita vya Urusi nchini Ukraine wakati video hiyo ilipomfikia kwenye simu yake.

Aliitambua mara moja sauti ya mwanamke huyo. Ilikuwa ya Polina Alexandrovna Azarnykh, ambaye Omar anasema alimsaidia kujiunga na mapigano upande wa Urusi, akimuahidi kazi yenye mshahara mkubwa na uraia wa Urusi. Lakini sasa, mwanamke huyo alikuwa amekasirika.

Katika mfululizo wa ujumbe wa sauti uliorekodiwa nchini Ukraine, Omar, ambaye anatumia jina bandia kwa sababu za kiusalama, anaelezea jinsi alivyonaswa na kuishi kwa hofu kubwa ndani ya eneo la vita.

Anadai kuwa Azarnykh alimuahidi kwamba ikiwa atamlipa dola 3,000, atahakikisha hatatumwa kupigana vitani. Lakini kwa mujibu wa maelezo yake, alitumwa mstari wa mbele baada ya mafunzo ya siku 10 tu. Kwa sababu hiyo, alikataa kulipa pesa hizo, na hatimaye Azarnykh akaichoma pasipoti yake.

Anasema alijaribu kukataa kushiriki katika oparesheni moja, lakini wakubwa wake walimtishia kumuua au kumtia gerezani.

"Tulidanganywa… mwanamke huyu ni tapeli na muongo," anasema Omar.

Uchunguzi wa BBC Eye umefuatilia jinsi Azarnykh, mwalimu wa zamani mwenye umri wa miaka 40, anavyotumia kituo cha Telegram kuwavutia vijana wa kiume, hasa kutoka nchi masikini, kujiunga na jeshi la Urusi.

Ujumbe wa video wa mwalimu huyo wa zamani, akiwa anatabasamu, pamoja na machapisho yake yenye matumaini, yanatoa ofa za "mikataba ya mwaka mmoja" ya "kutumikia jeshi."

Idhaa ya BBC World Service imeandika karibu kesi 500 ambapo iligundua kuwa alikuwa akitoa nyaraka zinazoitwa "mialiko", ambazo humruhusu mpokeaji kuingia Urusi ili kujiunga na jeshi.

Mialiko hiyo ilitumwa kwa wanaume, hasa kutoka Syria, Misri na Yemen, ambao inaonekana walimpa taarifa zao za pasipoti ili kujiandikisha.

Hata hivyo, wapiganaji hao wapya na ndugu zao waliiambia BBC kwamba aliwadanganya wanaume hao waamini kuwa wangeepuka vita, hakuwafahamisha wazi kuwa hawangeweza kuondoka baada ya mwaka mmoja, na aliwatishia wale waliompinga. Alipowasiliana na BBC, alikanusha tuhuma hizo.

Familia kumi na mbili ziliiambia BBC kuhusu vijana waliodaiwa kuajiriwa kwa njia hiyo, ambao sasa wameripotiwa kufa au kutoweka.

Ndani ya nchi, Urusi imepanua uandikishaji wa lazima jeshini, imeajiri wafungwa, na imetoa bonasi kubwa zaidi za kujiunga na jeshi ili kuendeleza operesheni zake nchini Ukraine, licha ya kupoteza wanajeshi wengi.

Kwa mujibu wa NATO, zaidi ya wanajeshi milioni moja wa Urusi wameuawa au kujeruhiwa tangu kuanza kwa uvamizi mwaka 2022, wakiwemo wanajeshi 25,000 mwezi Desemba 2025 pekee.

Utafiti wa BBC News Russian, uliotegemea matangazo ya vifo na kumbukumbu nyingine za umma, unaonesha kuwa idadi ya wanajeshi wa Urusi waliouawa nchini Ukraine imeongezeka kwa kasi zaidi kuliko wakati wowote katika mwaka uliopita.

Ni vigumu kubaini idadi halisi ya wageni waliojiunga na jeshi la Urusi. Hata hivyo, uchambuzi wa BBC Russian, uliotazama pia idadi ya wageni waliouawa au kujeruhiwa, unaonesha kuwa takribani watu 20,000 wameandikishwa, wakiwemo raia wa nchi kama Cuba, Nepal na Korea Kaskazini.

Ukraine nayo imepata hasara kubwa miongoni mwa wanajeshi wake, na pia imewaingiza wapiganaji wa kigeni katika safu zake.

"Miili kila mahali"

Omar alikutana kwa mara ya kwanza Azarnykh mwezi Machi 2024, wakati alikuwa hana pesa kabisa kwenye uwanja wa ndege wa Moscow pamoja na Wasyria wengine 14.

Ajira nchini Syria zilikuwa chache na zenye malipo duni. Omar anasema kuwa meneja wa ajira alikuwa amewaahidi kazi waliyodhani ni ya raia ya kawaida ya kusimamia miundombinu ya mafuta nchini Urusi. Waliruka hadi Moscow, kisha kugundua kuwa walidanganywa.

Wakati wakitafuta njia mbadala mtandaoni, Omar anasema kuwa mmoja wa wanakundi hilo alimkuta Azarnykh kwenye jukwaa la Telegram na kumtumia ujumbe.

Alikutana nao uwanjani baada ya saa chache na kuwaongoza kwa treni hadi kituo cha kuajiri Bryansk, magharibi mwa Urusi, alisema.

Huko, anasema, aliwapa mikataba ya mwaka mmoja na jeshi la Urusi, yenye mshahara wa mwezi wa takribani dola 2,500 na bonasi ya kujiunga ya dola 5,000, kiasi ambacho kwao kilionekana kama ndoto tu nchini Syria.

Omar anaeleza kuwa mikataba hiyo iliandikwa kwa Kirusi, lugha ambayo hakuna aliyeifahamu, na kwamba alichukua pasipoti zao, akiahidi kuwa atawapata uraia wa Urusi. Pia aliwaahidi kuwa wataweza kuepuka kazi za kupigana ikiwa kila mmoja atamlipa dola 3,000 kutokakwenye bonasi yao, aliongeza.

Lakini, anasema, katika takribani mwezi mmoja, alijikuta kwenye mstari wa mbele akiwa na, kwa maelezo yake, mafunzo ya siku 10 tu na bila uzoefu wa kijeshi.

"Tutaaga dunia hapa asilimia 100," alisema katika mojawapo ya ujumbe wake wa sauti, aliotuma kwa timu ya wachunguzi wa BBC.

"Wengi wamejeruhiwa, milipuko mingi, mabomu mengi. Usipokufa kwa mlipuko, utakufa chini ya mabaki yanayokupoteza," alisema mwezi Mei 2024.

"Miili kila mahali… nimeiona kwa macho yangu, mtu anapokufa wanamweka kwenye begi la taka na kumuacha kando ya mti," aliongeza.

Baada ya karibu mwaka mmoja, aligundua kile ambacho Azarnykh hakumweleza: amri ya Urusi ya mwaka 2022 inaruhusu jeshi kuendeleza mikataba ya wanajeshi moja kwa moja hadi mwisho wa vita.

"Ikiwa wataongeza mkataba, nimekwisha, Mungu wangu," alisema.

Mkataba wake umeongezwa.

Mtandao wa Telegram wa Azarnykh una wanachama 21,000. Katika machapisho yake, mara kwa mara huwaalika wasomaji wanaotaka kujiunga na jeshi la Urusi kumtumia nakala iliyoskaniwa ya pasipoti yao.

Baadaye, huchapisha nyaraka za mialiko, mara nyingine zikihusishwa na orodha ya majina ya wanaume waliokuwa wametengwa.

BBC imeandika zaidi ya mialiko 490 kama hiyo ambayo ilitumwa katika mwaka uliopita kwa wanaume kutoka nchi kama Yemen, Syria, Misri, Moroko, Iraq, Côte d'Ivoire na Nigeria.

Machapisho yake yameelezea uajiri wa "kikosi cha kimataifa cha kipekee" na yanaweka wazi kwamba watu walioko Urusi bila mpangilio rasmi, ikiwa ni pamoja na wale ambao visa zao vimekwisha muda wake, wanaweza kuomba kujiunga.

Tulizungumza na wapiganaji wa kigeni wanane, ikiwa ni pamoja na Omar, ambao walikuwa wameajiriwa na yeye, pamoja na familia za wanaume 12 waliopotea au waliokufa.

Wengi waliamini kuwa Azarnykh aliwadanganya au kuwahudumia wapiganaji hao kwa manufaa yake binafsi. Walisema kwamba wanaume hao walijua wanajiunga na jeshi, lakini hawakutarajia kuhudumu kwenye mstari wa mbele.

Wengi, kama Omar, walihisi hawakupata mafunzo ya kutosha au walidhani wangeweza kuondoka baada ya mwaka mmoja.

Nchini Misri, Yousef, ambaye pia tumebadilisha jina lake, aliiambia BBC kwamba kaka yake mkubwa Mohammed alikuwa ameanza masomo ya chuo kikuu mjini Yekaterinburg, Urusi, mwaka 2022.

Lakini alikumbana na mgogoro wa kulipa ada za shule, Yousef anasema, na aliiambia familia yake kwamba mwanamke mmoja wa Kirusi aitwaye Polina alianza kumpa msaada mtandaoni, ikiwemo kumpa ofa ya kazi katika jeshi la Urusi ambayo alisema ingemruhusu kuendelea na masomo yake.

"Alimuahidi nyumba, uraia… na posho ya kila mwezi," anafafanua. "Ghafla, alitumwa Ukraine. Alijikuta katika mapigano," anasema Yousef.

Simu yake ya mwisho ilikuwa Januari 24, 2024, Yousef alisema. Takriban mwaka mmoja baadaye, Yousef anasema alipokea ujumbe kwenye Telegram kutoka nambari ya Kirusi ulioonesha picha za mwili wa Mohammed.

Familia hatimaye iligundua kuwa alikuwa ameuawa karibu mwaka mmoja uliopita.

''Wengine wamechanganyikiwa''

Azarnykh amekuwa "mmoja wa waajiri muhimu zaidi" wa jeshi la Urusi, anasema Habib, mwingine Msyria aliyehudumu katika jeshi la Urusi. Alikubali kurekodiwa kwenye video, lakini alitaka kuzungumza kwa jina bandia kwa hofu ya kadhia za kisiasa.

Habib anadai kuwa yeye na Azarnykh "wamefanya kazi pamoja kwa takribani miaka mitatu juu ya mialiko ya kupata visa za kuingia Urusi." Hakutoa maelezo zaidi na hatukuweza kuthibitisha nafasi yake katika mchakato huo. Picha iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii mwaka 2024 inaonesha akiwa pamoja naye.

Asili yake ni kutoka mkoa wa Voronezh, kusini magharibi mwa Urusi, Azarnykh aliendesha kundi la Facebook lililosaidia wanafunzi wa Kiarabu kusoma Moscow, kabla ya kuanzisha kituo chake cha Telegram mwaka 2024.

Habib anasema kuwa wengi wa wapiganaji wa kigeni waliwasili wakiwa na wazo kwamba wangepewa jukumu la kulinda miundombinu au kusimama zamu kwenye vituo vya ukaguzi.

"Waarabu wanaokuja wanakufa mara moja. Wengine wamechanganyikiwa: ni vigumu kuona miili," anaeleza.

Habib alisema alikutana na Omar na kundi la Wasyria kwenye kituo cha mafunzo ya kijeshi.

"Aliwaahidi uraia, mishahara mizuri na usalama," anasema Habib.

"Lakini mara tu unapopatiwa mkataba hapa, huwezi kuondoka."

"Hakuna kati yao aliyejua jinsi ya kutumia silaha. Hata walipolengwa, walichagua kutorudisha na kumshambulia mtu… Ukipiga risasi, utauawa," anaeleza.

"Polina alikuwa anawaondoa wanaume hawa, akijua watakufa."

Anaongeza kuwa "alikusanya dola 300 kutoka jeshi kwa kila mtu aliyeajiriwa." BBC haikuweza kuthibitisha taarifa hii, lakini wapiganaji wengine pia walisema kuwa walidhani alilipwa.

"Hakuna cha bure"

Machapisho ya Azarnykh kuanzia katikati ya mwaka 2024 yanaanza kutaja kuwa wapiganaji watashiriki katika mapigano na yanataja wapiganaji wa kigeni waliouawa kwenye mapigano.

"Nyote mliijua vizuri kuwa mnaenda kwenye vita," alisema katika video ya Oktoba 2024.

"Mlidhani mnaweza kupata pasipoti ya Kirusi, kutofanya chochote na kuishi katika hoteli ya nyota tano?... Hakuna kitu kinachotolewa bure."

Katika tukio jingine mwaka 2024, BBC ilisikiliza ujumbe wa sauti uliotumwa na Azarnykh kwa mama mmoja ambaye mwanawe alikuwa akihudumu katika jeshi.

Azarnykh anadai kuwa mwanamke huyu "alichapisha jambo baya kuhusu jeshi la Urusi." Akiwa na laana nyingi, alitishia maisha ya mwana huyo na kumuonya mama huyo: "Nitakutafuta wewe na watoto wako wote."

BBC imejaribu kuwasiliana mara kadhaa na Azarnykh. Kwanza, alikubali kuhojiwa iwapo tungeenda Urusi, lakini BBC ilikataa kwa sababu za usalama.

Baadaye, alipoulizwa kwenye simu kama wapiganaji waliahidiwa kazi zisizo za mapigano, alikata simu. Katika ujumbe wa sauti aliotuma baadaye, alisema kazi yetu ilikuwa "isiyo ya kitaalamu" na alitishia kufungua kesi za kashfa. Pia alisema,

"Waarabu wetu wapendwa wanaweza kuweka madai yao popote ninapofikiria."

BBC iliwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi na Wizara ya Ulinzi ya Urusi kwa maoni, lakini haikupokea jibu lolote.

Mnamo Machi 2022, Rais Putin aliunga mkono ajira kwa wanaume kutoka Mashariki ya Kati, akisisitiza kuwa walihamasishwa na sababu za kiitikadi na si kifedha:

"Kuna watu wanaotaka kuja kwa hiari, hasa si kwa pesa, na kusaidia wananchi."