Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mpasuko wa 'chungwa' ndio kifo cha chama cha Raila Odinga - ODM?
- Author, Laillah Mohammed
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Neno 'Chungwa' linapotajwa kwenye taarifa hii usipotee kwa kudhani mwandishi anazungumzia tunda ambalo wengi huku Afrika Mashariki wanalipenda sana.
''Chungwa'' ni nembo ya chama cha Orange Democratic Movement nchini Kenya ambalo limekuwepo kwa miongo miwili sasa, na ambalo kwa sasa baadhi ya wafuasi wake na hata wachambuzi wa kisiasa wanasema kwamba huenda likapasuka vibaya, kufa na kuzikwa kama mwanzilishi wake na kinara wa muda mrefu Raila Odinga aliyefariki mwezi Oktoka 2025.
''Mtu anapokufa hatangazi kifo chake, hutangazwa kwamba amekufa. Na ndipo sisi husema tumetangaza kifo cha mtu fulani. Kwa hivyo ODM tayari kama ile ODM tuliyoijuwa nyakati za Raila Amollo Odinga imeshafariki. Hakipo tena,'' alisema mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Kenya Barack Muluka.
Matamshi yake yanaonekana kuwa mojawapo ya masuala ambayo huenda yanamtia wasiwasi kinara wa sasa Daktari Oburu Oginga ambaye alimrithi kaka yake mdogo baada ya kifo chake nchini India mwezi Oktoba mwaka jana.
Hata kabla ya kujifahamisha vyema kuhusu usimamizi wa chama, Dkt. Oburu Oginga aliandaa hafla ya kuadhimisha miaka 20 ya chama alichokianzisha Raila Odinga mnamo 2005 katika jiji la Mombasa, pwani ya Kenya na ni hapo ndipo mambo yalionekana kupamba moto zaidi ya jinsi ilivyokuwa katika mazishi ya Raila Odinga mwezi mmoja tu kabla ya hapo.
''Mimi nazungumza kama msemaji wa chama na alipokuwa hai, Baba {Raila Odinga} alitamka kwa mdomo wake kwamba chama kitatoa muelekeo wa hatua itakayochukuwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.''
''Na suala la kuunga mkono chama tawala cha UDA halikuwepo kamwe?'' alisema Katibu Mkuu wa ODM – Edwin Sifuna huko Mombasa.
Matamshi yake yakazusha cheche za maneno hasa kutoka upande wa uongozi ambão unataka sana ushirikiano kati ya ODM na UDA kuendelea.
''Chama kitashirikiana na chama tawala cha UDA kama alivyokuwa amepanga Raila Odinga. Na wala hakuna mpango wowote wa kukiuka Azimio hilo la ''baba'' alisema Naibu Mwenyekiti wa chama na Gavana wa Mombasa Abdulswammad Shariff Nassir katika hafla hiyo..
Lakini badala ya moto kuzima, moshi umeendelea kufuka huku Daktari Oginga akijipata kwenye njia panda wengi wakisubiri kujua atafanya vipi kuliokoa ''Chungwa'' ambalo linaendelea kugawanyika.
Oburu Odinga ataweza kuvivalia viatu alivyoviacha Raila Odinga?
Mchambuzi wa siasa Barack Muluka ambaye aliwahi kufanya kazi kwa ukaribu sana na Raila Odinga katika kampeni yake ya 2007, anasema kwamba kaka mkubwa wa Odinga ana kibarua kigumu cha kukiongoza chama cha chungwa ambacho kwa sasa kinaonekana kukumbwa na mvutano hata ndani ya família ya Odinga kuhusu jinsi chama kinavyoendeshwa.
Muluka anasema, ''Nadhani ana changamoto kubwa sana. Kwanza kabisa nadhani yeye hajawahi kuwa na uchu wa uongozi kama kaka yake mdogo. Nadhani hakuna wakati ambapo alitaja kwamba angechukuwa majukumu ya aina hiyo.''
''Kwa sababu utaona kwamba Raila Odinga ambaye yeye anajaribu kumrithi alikuwa nduguye mdogo. Na nduguye mdogo ndiye alikuwa kwenye upeo wa uongozi katika siasa, Oburu Oginga akiwa kama abiria tu! Katika vyombo ambavyo aliviunda na kuviongoza Raila Odinga.''
Mpasuko wa chama unaonekana kupanuka hadi nyumbani kwa Marehemu Jaramogi Oginga Odinga ambaye ni baba yao Daktari Oburu Odinga na Raila Amollo Odinga.
Mwezi huu wa Januari Oburu aliandaa mkutano katika eneo ambalo Raila alilitaja mwenyewe kama 'BEDROOM' Yaani ngome yake ya kisiasa. Oburu na kundi la maafisa wakuu wakiongozwa na Mwenyekiti Gladys Wanga na Naibu wake Abdulswammad Nassir walifika katika uwanja wa Kamukunji uliopo mtaani KIbra Nairobi ambapo Odinga aliandaa mikutano yake muhimu na wafuasi wake.
Katika kikao hicho, hakuwepo Katibu Mkuu Edwin Sifuna wala mbunge maalum wa bungee la Afrika Mashariki -EALA Winnie Odinga ambaye ni mwana wa marehemu Raila Odinga.
Mkutano huo, ulitarajiwa kutuliza hali miongononi mwa wafuasi wa chama ambao wametatizwa na malumbano ya hadharani kati ya viongozi wakuu wa chama ambapo Sifuna amenukuliwa akimchamba kiranja wa wachache bungeni na mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed.
Muluka anasema kwamba changamoto zinazomkabili kinara wa chama kuhusu malumbano hayo inaweza kuangaziwa kwa mtazamo wa aliyekuwa kinara wa chama Raila Odinga.
'Kwamba wakati ambapo Raila Odinga alikuwa bado yuko hai, wana ODM walikuwa na mazoea ya kusema kwamba Raila ni ODM na ODM ni Raila. Na hapawezi kuwepo chama bila ya Raila. Hivyo basi kwa kuwa Raila ameshafariki, kufuata huo msimamo na hayo mazoea ya kuchukuwa hicho kama kielelezo chamani kwamba Raila ndio chama basi pale ambapo anapumzika Raila , chama cha ODM pia kinapumzika,'
Oburu alijaribu kuwapatanisha viongozi hawa wawili wakuu wa chama, ila imeonekana kwamba alitumia maji machache tu kuuzima moto ambao kwa sasa unaonekana kuwa na moshi mkubwa na huenda ukazuka upya na kuwa na athari mbaya kabisa.
Rais Ruto anachochea mpasuko wa ODM ?
Alipohudhuria sherehe za madhimisho ya miaka 20 ya chama cha ODM, Rais William Ruto alisema kwamba yeye ni mmoja wa waanzilishi wa chama hicho na kwamba hana haja ya kupewa au kunyimwa mualiko kuhudhuria maadhimisho hayo ya chama ambacho alikipigania miaka hiyo ya awali.
''Mimi nilikuwa katika PENTAGON ambayo ilikuwa jopo la viongozi wakuu kabisa chamani mnamo 2007 na wakati huo tulimpigania Raila Odinga na moyo wetu wote alipowania Urais wa Kenya mwaka huo.
Na tulipokubaliana kuunda serikali ya ushirikiano yaani BROADBASED Government' ilikuwa kama kurejea nyuma kwani Raila alikuwa kama Mwalimu wetu wa siasa za nchi, '' alisema Rais Ruto.
Kuendeela kuwepo na ushirikiano kati ya chama cha UDA anachokiongoza Rais Ruto na chama cha ODM ambacho sasa kinaongozwa na Oburu Oginga kumeleta mgawanyiko mkubwa ndani ya chama huku mwana wa Raila Winnie Odinga akionekana kukinzana na babayeka mkubwa.
'Ni nani alisema kwamba chama kitaendelea kushirikiana na UDA hadi mwakani wakati wa uchaguzi?' aliulizwa Winnie Odinga katika mkutano aliouandaa katika uwanja ule ule wa Kamukunji katika eneo bungee la Kibra siku ya Jumapili Januari 18.
''Sisi hatuondoki chamani na tutahakikisha kwamba chama kinasimama imara kama alivyoazimia baba. Na wala hatutatishwa wala kushurutishwa,'' aliendelea kusema mbunge huyo maalum wa EALA.
Ikiwa imesalia chini ya miezi 24 kwa Kenya kuelekea uchaguzi mkuu huo wa 2027 siasa zimeanza kushika kasi huku wengi wakihisi kwamba kutokuwepo kwa Raila Odinga kuna mpa fursa kubwa Rais Ruto kuingia ndani ya chama cha chungwa na kukiimarisha upya kwa ajili ya kupanua uungwaji mkono katika maeneo ambayo Raila Odinga alikuwa na umaarufu mkubwa .
Wachambuzi wanasema kwamba japo ni mbinu ya Rais Ruto kujipatia nafasi bora ya kurejea Ikulu, anaonekana kama 'mdudu' ambaye lengo lake ni kuliozesha tunda kwa ajili ya kunufaika pakubwa na kuwaacha wenyeji wa tunda hilo bila nguvu.
Huku ODM ikionekana kunyauka, Barack Muluka anasema kwamba kifo chake baba kimesababisha vifo vya wengi chamani.
''Mtazamo wa pili ni kwamba kulikuwepo wale waliomfuata Raila Odinga kwa kumuenzi sera zake na aideolojia zake, ruwaza na mawazo yake. Lakini pia kulikuwepo na kupe.
Na kupe ni mdudu ambaye amezoea kuwa na mwenyeji na kumfyonza damu. Wakati ambapo Raila Odinga hayupo, ambaye ndiye aliyekuwa mwenyeji wa kupe hao, basi lazima watafute mwenyeji mpya na huyo mwenyeji mpya wamempata katika William Ruto na hawana kitu cha muhimu wanachokitafuta ila tu kule kuweza kunusurika kisiasa na watanusurika kisiasa kwa kumdandia William Ruto.
Vita vya urithi wa chama cha ODM?
ODM inatarajiwa kuandaa mkutano wa kupanga mikakati ya chama na pia uchaguzi wa kuwachaguwa viongozi wake wapya katika miezi michache ijayo.
Katika mkutano uliondaliwa mjini Mombasa aliyekuwa mbunge wa Malindi Aisha Jumwa aligusia suala la kumtaka 'Mpwani' kukiongoza chama cha chungwa ambacho 'wapwani' wamekuwa wafuasi wake kwa miongi miwili sasa.
Jumwa alitoa kauli ya ''Wapwani kumtaka aliyekuwa gavana wa Mombasa Hassan Ali Joho ambaye sasa anashikilia wadhifa wa uwaziri katika serikali ya Rais William Ruto – kuwa mrithi wa Raila au kama sivyo awe na wadhifa wa juu chamani.
Kabla ya kuingia serikalini, Joho alihudumu kama mmoja wa manaibu wanne wa chama cha ODM kwa pamoja na aliyekuwa gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ambaye kwa sasa pia ni waziri ndani ya serikali ya Ruto.
Wawili hao wameonyesha azma yao ya kuwania Urais katika siku za usoni na wote wawili wangependa kukitumia chama cha ODM kama gari ambãlo wanatazamia litawaingiza ikulu ya Rais, Nairobi.
Daktari Oburu ambaye kwa sasa ndiye Kinara wa chama ameeleza azma yake ya kuendelea kukiongoza chama' japo wengi wanahisi kwamba umri, maradhi, na kutokuwa na uzoefu wa uongozi huenda ukawa ndio sababu kuu ya yeye kushindwa kukiweka pamoja chama cha chungwa.
Muluka anasema kwamba kwa mtazamo wake urithi haupandi juu kama ilivyo sasa, na kwamba unashuka chini kutoka mkubwa hadi mdogo na kwamba uwepo wa Winnie Odinga kutakuwa donda sugu mgongoni mwa baba yake mkubwa Oburu kwani amejitokeza kama mmoja wa vijana ambão wanatazamia kukileta chama cha ODM kwa karne ya 21 na kuwajumuisha vijana zaidi.
Kwa sasa Katibu Mkuu Edwin Sifuna na mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino wameonekana kama sura mpya ya vijana ambayo inatishia mibabe wa chama na kuweka mtazamo hasi kinyume na ule wa wazee chamani.
Nini kitarajiwe kufanyika kulirejesha chungwa pamoja?
Wataalamu wa siasa wanasema kwamba ni sharti wakuu wa chama wafanye vikao na wafuasi wake kote nchini kwa ajili ya kusikiliza maoni yao na kuyapa kipau mbele katika mpangilio wao wa uongozi kwenda mbele.
Mvutano kati ya vijana na wazee umetakiwa kutatuliwa mara moja ili kuzuia mapasuko zaidi kwani chama cha ODM kimekuwa na umuhimu mkubwa sio tu Kenya bali Afrika Mashariki kwa jumla.
Wengi wamewafananisha Raila Odinga na kinara wa CHADEMA Tundu Lissu kwa misimmao ya kisiasa na jinsi wote walivyokamatwa na kukabiliwa na mashtaka ya uhaini katika mataifa hayo mawili japo mashtaka hayo yametokea katika muda wa zaidi ya miaka thelathini.
Odinga alikuwa mshirika mkubwa wa Lissu huku wengi wakifannanisha siasa za Edwin Sifuna – katibu Mkuu wa chama kama zile za Naibu wmenyekii wa CHADEMA John Heche.
Huku CHADEMA ikishikilia masimamo wake wa upinzani nchini Tanzania, ODM imeonekana kusuasua na kujikuta chumba kimoja na serikali, jambo ambalo badhi ya Wakenya wanahisi ni kinyume na alivyokuwa Raila Odinga .
Je, Chungwa kitasimama na kustahmili mawimbi makali ya mipasuko ya ndani? Muda tu na maamuzi ya wakuu chamani ndio yataamua hilo.