Ni timu gani zimeyaaga mashindano ya Klabu Bingwa Ulaya?

    • Author, Ahmed Bahajj
    • Nafasi, BBC News Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Msimu wa Klabu Bingwa Ulaya (Champions League) wa mwaka 2025-26 umeanza kuchanja mbuga na kufikia katika hatua ya kuwatofautisha timu ndogo na timu vigogo.

Ijapokuwa kila timu imesalia na mechi za raundi moja kabla ya hatua ya muondowano wa raundi ya 16, tayari kuna timu ambazo zimeyaaga mashindano hayo ya kifahari zaidi barani Ulaya.

Mfumo huu mpya wa klabu bingwa ulaya ulioanzishwa msimu uliopita, unajumuisha jumla ya timu 36, timu 24 zitafuzu kuingia hatua ya mchujo wa muondowano yaani KO. Kutoka hapo timu 16 zitaingia raundi ya 16 nazo timu 12 zitafungashwa virago na kujaribu tena mwakani.

Hebu tuanze na timu ambazo zishatolewa katika ngarambe hizi, ya kwanza ni Villarreal ya Uhispania.

Timu hiii inayoshikilia nafasi ya tatu katika ligi kuu ya soka nchini Uhispania imewashangaza mashabiki wengi jana usiku baada ya kurindimwa na Ajax ya Uholanzi kwa kichapo cha mabao 2-1 tena wakiwa uwanja wa nyumbani Estadio de la Cerámica.

Timu ya pili ilitolewa kwenye michuano hii ni Kairat Almaty kutoka Kazahkstan.Walitolewa baada ya kipigo cha mabao 4-1 dhidi ya Club Brugge ya Ubelgiji.

Hata hivyo timu hii imejifunza mengi kwani ndio mara ya kwanza katika historia kushiriki katika michuano hii.

Kwa mantiki hiyo,baada ya mechi za Jumanne usiku mabingwa mara 15 wa klabu bingwa Real Madrid ya Uhisania,Tottenham, Sporting CP, Inter Milan, Atletico Madrid wote wamejikatia tiketi ya kufuzu hatua ya muondowano wakiungana na Arsenal iliyofuzu hata kabla ya mechi ya jana dhidi ya Inter Milan.

Bayern Munich na Liverpool pia wamefuzu hata kabla ya mechi zao za leo dhidi ya Union Saint Gilloise na Marseille mtawalia.

Matokeo ya Mechi ya Jumanne

Kairat 1-4 Club Brugge

Bodo Glimt 3-1 Manchester City

Fc Copenhagen 1-1 Napoli

Inter Milan 1-3 Arsenal

Olympiacos 2-0 Leverkusen

Real Madrid 6-1 AS Monaco

Sporting 2-1 PSG

Tottenham 2-0 Borrussia Dortmund

Villareal 1-2 Ajax

Mla ni mla leo mla jana kalani?

Katika ratiba ya leo ,kuna mitanange tisa ya kupiganiwa

Galatasaray wa Uturuki itachuana dhidi ya Ateltico Madrid ya Uhispania

FC Qarabag wa Azerbaijan itatiana vikumbo dhidi ya Frankfurt wa Ujerumani katika uga wa Tofic

Atalanta ya Italia itatiana nguvuni dhidi ya Athletic Club ya Uhispania

Chelsea wa England wataminyana dhidi ya Pafis katika uwanja Stamford Bridge

Bayern Munich wa Ujerumani watailika USG Alliance Arena

Juventus watakabiliana na Benfica wa Ureno

Newcastle wa England watakuwa St James park dhidi ya PSV wa Uholanzi

Nao Liverpool ambao washafuzu watakipiga dhidi ya Marseille ya Ufaransa

Slavia Prague wa Czech wataonja makali ya miamba wa Uhispania Barcelona

Mfumo wa kufuzu muondowano ni upi?

Katika mfumo huu wa Timu 36,timu 24 zitafuzu hatua ya muondowano.

Timu nane za kwanza katika msimamo, zitafuzu moja kwa moja hatua ijayo.Timu ya tisa hadi ya 24 zitashiriki katika mechi za mchujo wa KO ama muondowano wa awali.

Timu zilizofuzu kwenye raundi ya 16 kufikia sasa ni Atalanta,Atletico Madid,Inter Milan,Liverpool,Manchester City,Real Madrid,Sporting CP,Tottenham.PSG

Mechi za mchujo wa kabla ya raundi ya 16 zitagaragazwa tarehe 15/18 na wamu ya pili tarehe 24 /25 Mwezi Februari.

Mechi rasmi za raundi ya 16 zitapigwa kuanzia tarehe 10/11 na pia awamu ya pili ni 17/18 Mwezi Machi.