Greenland: Je, Ulaya itaachana na mbinu ya upole kwa Trump?

    • Author, Katya Adler
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Siku ya Jumatatu rais wa Marekani, Donald Trump alisisitiza tena, kwamba Marekani inaitaka Greenland kwa sababu za usalama wa taifa.

Je, yuko tayari kutumia nguvu kuiteka, waandishi wa habari walimwuliza? "Sina la kusema," alisema rais, akituma ujumbe wa mashaka kwa wakazi wenye wasiwasi wa Greenland.

Greenland ni eneo lenye uhuru wa ndani, liko chini ya Denmark - mwanachama wa EU na Nato. Rais Trump anataka washirika wa Denmark katika miungano hiyo miwili kuachana na Copenhagen na kuiacha Marekani ichukue udhibiti wa Greenland, au nchi hizo zikabiliwe na adhabu ya ushuru kwa bidhaa zao zote zinazouzwa nje kwenda Marekani.

Ni hali ya kutisha kwa uchumi wa Ulaya. Hasa kwa nchi zinazotegemea kuuza nje kwenda Marekani, kama vile magari ya Ujerumani na soko la bidhaa za kifahari la Italia.

Siku ya Jumatatu waziri wa fedha wa Ujerumani alisema, "hatutakubali kutishwa" baada ya mkutano wa dharura na mwenzake wa Ufaransa.

Vitisho vya Trump vilisababisha mshtuko Ulaya na Uingereza, nchi hizo zilikuwa zimeshafikia makubaliano juu ya ushuru na rais wa Marekani mwaka jana.

"Hatujawahi kuona jambo kama hili. Mshirika, rafiki wa miaka 250, anafikiria kutumia ushuru ... kama silaha," amesema Waziri wa Fedha wa Ufaransa Roland Lescure.

Mwenzake wa Ujerumani Lars Klingbeil aliongeza: "Mstari umevukwa... Sisemi kitu gani kitatokea. Lakini jambo moja lazima liwe wazi: Ulaya lazima iwe tayari."

Ghafla, mbinu ya kutumia upole dhidi ya Trump, ambayo viongozi wa Ulaya walikuwa wanaitumia tangu aliporejea kwa muhula wa pili katika Ikulu ya White House, inaonekana kuishiwa na muda.

Ulaya itajibu nini?

Ni mapema mno kusoma ibada za mwisho kuhusu mahusiano ya Ulaya na Marekani.

Viongozi wa Ulaya wanamwambia Rais Trump kwamba watamuunga mkono katika kuweka kipaumbele usalama wa Aktiki, kwa hivyo hakuna haja ya kuichukua Greenland peke yake.

Wakati huo huo, wanadiplomasia wa EU wametangaza kwamba wanafikiria kutoza ushuru wa euro bilioni 93 (pauni bilioni 80) kwa bidhaa za Marekani au hata kuweka vikwazo kwa biashara za Marekani, ikiwezekana zikiwemo benki na kampuni za teknolojia - katika soko kubwa la umoja huo, ikiwa Trump ataendelea na "ushuru wake.”

Hatua hizi za kulipiza kisasi huenda zikawa na athari kubwa kwa wanunuzi wa Marekani pia.

Wawekezaji wa Umoja wa Ulaya wamewekeza karibu majimbo yote 50 ya Marekani na wamewaajiri karibu Wamarekani milioni 3.4.

EU ina sauti dhaifu katika diplomasia ya kimataifa. Kambi hiyo inaundwa na nchi 27 na zinagombana mara kwa mara. Lakini ina ushawishi mkubwa linapokuja suala la uchumi wa dunia na biashara, ambapo maamuzi kwa kiasi kikubwa hufanywa na Tume ya Ulaya kwa niaba ya wanachama wa soko moja la EU.

Umoja wa Ulaya ndio mfanyabiashara mkubwa zaidi wa bidhaa na huduma duniani, ukichangia karibu 16% ya biashara ya dunia mwaka wa 2024.

"Kipaumbele chetu ni kuzungumza, na si kuongeza mvutano," naibu msemaji wa Tume ya EU, Olof Gill alisema Jumatatu.

"Trump anawalazimisha watu wa Ulaya kukuza ujasiri," anasema Niclas Poitiers, mchumi na mtaalamu wa biashara ya kimataifa katika Taasisi ya fikra tunduizi ya Bruegel yenye makao yake makuu Brussels.

"[Ingawa] athari za ushuru wa [Trump] zinadhibitika sana Ulaya ... swali kubwa zaidi hapa si la kiuchumi bali ni usalama na sera za kigeni."

"EU haiwezi kuvumilia kutojibu"

Siku ya Jumatatu, Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent, akizungumza huko Davos, alionya kwamba Ulaya kulipiza kisasi kwa ushuru si jambo la busra.

Kwa sasa Ulaya inajihisi imekwama. Kuna hasara ikiwa itachukua hatua. Na kuna hasara ikiwa haitachukua hatua.

Baadhi ya watu barani Ulaya wana wasiwasi kwamba ikiwa Ulaya itakabiliana zaidi na Trump, kuna hatari ya Marekani kukaa mbali zaidi na Ulaya.

Na ukweli ni kwamba: Ulaya inaihitaji Washington ili kupata makubaliano ya Ukraine na kwa usalama wake wa bara. Licha ya kuahidi matumizi zaidi ya ulinzi, Ulaya bado inaitegemea sana Marekani.

Sir Keir Starmer, waziri mkuu wa Uingereza, alikuwa na wakati mgumu siku ya Jumatatu, akisema ni kwa maslahi ya Uingereza kuendelea kufanya kazi na Marekani linapokuja suala la ulinzi, usalama na ujasusi.

"Kuzuia nyuklia ndio silaha yetu kuu. Linapokuja suala la kulinda usalama wa kila mtu nchini Uingereza ni jukumu langu kubwa na hilo linatuhitaji kuwa na uhusiano mzuri na Marekani."

Lakini ikiwa Ulaya itaendelea kwenda polepole na rais Trump, badala ya kumpinga, wakati anapotishia uhuru wa mshirika wa Nato (Denmark), na kuweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya washirika wengine ikiwa wataiunga mkono Copenhagen, basi bara hilo lina hatari ya kuonekana dhaifu kupita kiasi.

Katika mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumatatu, mwanadiplomasia mkuu wa EU, Kaja Kallas aliandika, "Hatuna nia ya kuanzisha mvutano, lakini tutashikilia msimamo wetu.”

Akiwa waziri mkuu wa zamani wa Estonia, nchi inayoogopa kivuli kinachokuja cha Urusi katika upanuzi, ana hamu ya kuionyesha Moscow kwamba Ulaya inaweza - na itajitahidi - kudhihirisha nguvu yake, ikiwa italazimishwa.

"Watu wa Ulaya hawaogopi tena," Tara Varma aliniambia. Yeye ni mtaalamu wa usalama na siasa za kijiografia katika Taasisi ya fikra tunduizi, German Marshall Fund.

Bodi ya Amani ya Trump

Wanaotazama haya yote kutoka pembeni si Urusi pekee, China pia. Machoni mwao, Magharibi - Marekani na Ulaya zikiwa zimeungana, zimetawala kwa miongo kadhaa siasa za kimataifa - sasa zinavunjika.

Dunia inazidi kutawaliwa na mataifa makubwa mengine, ikiwa ni pamoja na Urusi na China, lakini pia India, Saudi Arabia na, kwa kiasi fulani, Brazil.

China inatumai kuwa mvutano wa Donald Trump na washirika wake unaweza kuifanya Beijing ionekane kuwa mshirika imara wa kumtegemewa zaidi katika kuendesha biashara za kimataifa.

Canada, ambayo Rais Trump ametishia kuifanya jimbo la 51 la Marekani, imekubali makubaliano ya biashara na Beijing. Inajaribu kupunguza utegemezi wa Washington.

Rais wa Marekani pia anaonekana hajali sana kuhusu Taasisi kama vile Nato na Umoja wa Mataifa zilizoanzishwa na mataifa ya magharibi baada ya vita vya pili vya dunia, ili kusimamia utaratibu wa kimataifa.

Baadhi wanasema kuhusu Bodi ya Amani ambayo Rais Trump anaianzisha sasa, kwamba anataka kuandaa sherehe ya utiaji saini Alhamisi hii huko Davos. Viongozi wengi wa dunia na wafanyabiashara mashuhuri wanahudhuria mkutano huo.

Bodi hiyo imeundwa kwa njia inayoonekana kusimamia ujenzi mpya wa Gaza baada ya mashambulio mabaya ya miaka miwili ya Israel, kwa lengo la kuiangamiza Hamas kufuatia shambulio dhidi ya Israeli la tarehe 7 Oktoba 2023.

Katiba ya Bodi inasema ni "chombo cha kimataifa cha kujenga amani kwa wepesi na ufanisi zaidi," ikidokeza kwamba jukumu lake litakuwa kubwa zaidi, labda kuzidi Umoja wa Mataifa.

Chanzo cha habari kilicho karibu na Emmanuel Macron kilitoa taarifa Jumatatu kikisema Ufaransa haina mpango wa kukubali mwaliko huo, wa kujiunga na Bodi ya Amani.

Kremlin ilisema Jumatatu kwamba Vladimir Putin pia aliombwa kujiunga na Bodi, ikisema kwamba Trump ana nia ya kudumisha uhusiano na rais wa Urusi, licha ya vita vya miaka minne vya Moscow dhidi ya Ukraine na kushindwa kwake hadi sasa kukubali mpango wa amani unaoungwa mkono na Marekani.

Maswali pia yameibuka kuhusu jukumu la Trump katika Bodi, na madai yake kwamba viongozi wa dunia walipe dola bilioni 1 kwa uanachama wa kudumu.