Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Uchaguzi Uganda 2026: 'Siko nyumbani, nilikwepa uvamizi wa jeshi na polisi' asema Bobi Wine

Kuhusu alipo kwa sasa, Wine amesema “Nataka kuthibitisha kwamba nilifanikiwa kuwatoroka. Kwa sasa, siko nyumbani, ingawa mke wangu na wanafamilia wengine bado wako chini ya kizuizi cha nyumbani.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga na Peter Mwangangi

  1. Kiongozi wa Iran akiri maelfu ya watu kuuawa wakati wa maandamano

    Kiongozi mkuu wa Iran kwa mara ya kwanza amekiri hadharani kwamba maelfu ya watu waliuawa, “baadhi yao kwa njia isiyo ya kibinadamu na ya kikatili,” wakati wa maandamano ya hivi karibuni.

    Kwa mujibu wa shirika la Iran Human Rights Activists News Agency (HRANA) lenye makao yake Marekani, ukatili dhidi ya maandamano nchini Iran umesababisha vifo vya watu 3,090.

    Machafuko hayo yalianza tarehe 28 Desemba kutokana na hali ya uchumi. Kuzimwa kwa mtandao kumeifanya iwe vigumu sana kupata taarifa sahihi.

    Katika hotuba yake siku ya Jumamosi, Ayatollah Ali Khamenei alisema maelfu ya watu waliuawa wakati wa machafuko hayo, akiwalaumu waliowaita “wachochezi wa ghasia.”

    Rais wa Marekani Donald Trump hivi karibuni aliwahimiza waandamanaji wanaopinga serikali ya Iran “waendelee kuandamana” na akatishia kuingilia kijeshi endapo vikosi vya usalama vitawaua.

    Tangu wakati huo, maandamano hayo yamegeuka kuwa wito wa kumaliza utawala wa kiongozi mkuu wa Iran.

    Serikali ya Iran imeyataja maandamano hayo kama “ghasia” zinazodaiwa kuungwa mkono na maadui wa Iran.

    Waandamanaji wamekabiliwa na nguvu za kikatili zilizosababisha vifo, na video zinazoonesha vikosi vya usalama vikifyatua risasi kwa waandamanaji zimethibitishwa na BBC Persian pamoja na BBC Verify.

    Kumekuwa pia na kuzimwa karibu kabisa kwa huduma za mtandao na mawasiliano nchini Iran. Siku ya Jumamosi, muunganisho wa mtandao kwa ujumla ulibaki takriban asilimia 2 tu ya kiwango cha kawaida, kulingana na shirika la ufuatiliaji wa mtandao NetBlocks.

    Unaweza kusoma;

  2. Meya wa Japan aomba msamaha kwa kuwaita wafanyakazi 'takataka'

    Meya wa Yokohama ameomba msamaha kwa kuwatukana wenzake baada ya afisa mmoja kumshutumu hadharani kwa kutoa matamshi ya kuchukiza.

    Katika mkutano na waandishi wa habari, mkuu wa rasilimali watu katika mji huo wa Japan, Jun Kubota, alidai kuwa Meya Takeharu Yamanaka ametumia maneno kama vile "mpumbavu" na "'takataka ya binadamu'" kuwadharau wafanyakazi.

    Nchini Japan, ni nadra sana kwa afisa wa jiji anayehudumu kumshtaki meya na kutaka aombe msamaha.

    Awali, Yamanaka alikanusha madai hayo, lakini baadaye alikiri baadhi ya madai hayo. "Nataka kuomba radhi kwa kumpa mkurugenzi wa wafanyakazi mzigo wa kisaikolojia," alisema.

    Katika mkutano na wanahabari siku ya Alhamisi, Kubota alimshutumu Meya Yamanaka kwa kutoa matamshi mara kwa mara dhidi ya maafisa - ikiwa ni pamoja na kumlenga yeye binafsi - ambayo yanaweza kuchukuliwa kama unyanyasaji katika eneo la kazi.

    Meya alishutumiwa kwa kuwaita viongozi "watu wasio na maana", "wajinga" na "watu bure", pamoja na kutoa maoni kuhusu muonekano wa wenzake na kuwafananisha na wanyama.

    Yamanaka alisema uchunguzi unazingatiwa kuanzishwa chini ya usimamizi wa naibu meya, akiongeza kuwa atatoa ushirikiano "wa dhati" ikiwa uchunguzi utafanyika.

    Lakini kwa kujibu kauli hiyo, Kubota alisisitiza kuwa Yamanaka pia alitamka maneno ambayo hajakiri kutamka, akisema: "Meya haelewi chochote. Siwezi kukubali msamaha wake. Nataka abadilike."

  3. Bobi Wine:Siko nyumbani, nilikwepa uvamizi wa jeshi na polisi

    Mgombea urais wa upinzani nchini Uganda kupitia chama cha National Unity (NUP) Robert Ssentamu Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine ametoa kauli kuhusu mahali alipo kwa sasa, huku taarifa za kukinzana zikiendelea kusambaa na kutoa wasi wasi kuhusu hali yake.

    Kupitia ujumbe uliochapishwa kupitia ukurasa wake wa Facebook, Wine amesema kwamba jeshi na polisi walivamia nyumbani kwake Magere Ijumaa usiku, ambapo ‘walizima umeme na baadhi ya kamera za CCTV’, huku helikopta zikizunguka juu ya nyumba yake.

    Kuhusu alipo kwa sasa, Wine amesema “Nataka kuthibitisha kwamba nilifanikiwa kuwatoroka. Kwa sasa, siko nyumbani, ingawa mke wangu na wanafamilia wengine bado wako chini ya kizuizi cha nyumbani. Najua kuwa wahalifu hawa wananitafuta kila mahali, na ninajaribu niwezavyo kuwa salama.”

    Awali Jumamosi, polisi nchini Uganda walikanusha madai kwamba Wine pamoja na mke wake Barbara Kyagulanyi wamekamatwa, na kusisitiza kwamba wapo nyumbani kwao mtaani Magere, wilayani Wakiso, mjini Kampala.

    Msemaji wa polisi nchini humo Kituuma Rusoke alisema kwamba maafisa wa usalama wameyazingira makazi yake Wine kwa sababu ya kisheria kwa kuwa yeye ni mgombea Urais na inawalazimu kuhakikisha usalama wake.

    Alisisitiza kwamba madai ya kukamatawa kwao ambayo yamechapishwa na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi hayana msingi wowote, kwani hakuna aliyethibitisha madai hayo.

    Kwa kuwa mtandao wa intaneti umeminywa kabisa nchini Uganda, imekuwa vigumu kuthibitisha madai kuhusu alipo Bobi Wine.

    Unaweza kusoma;

  4. Imam aliyepewa heshima kwa kuokoa maisha ya Wakristo Nigeria, afariki dunia akiwa na miaka 90

    Imam wa Kijnigeria aliyepata umaarufu wa kimataifa kwa kuokoa mamia ya maisha ya jamii ya Wakristo wakati wa vurugu amefariki akiwa na umri wa miaka 90.

    Abubakar Abdullahi alikuwa akiugua tatizo la moyo na alikuwa akitibiwa hospitalini, ambapo alifariki usiku wa Alhamisi, kama ilivyothibitishwa na mwanawe kwa BBC Hausa.

    Mnamo mwaka 2018, imam huyo aliona familia nyingi zikiwa na hofu na kutoroka zikielekea kijiji chake kilichoko Jimbo la Plateau, katikati ya Nigeria, na aliamua kuhatarisha maisha yake ili kuokoa maisha yao.

    Aliwahifadhi watu 262 nyumbani kwake na kwenye msikiti wake.

    Kwa kutambua alichokifanya, Abdullahi alipewa heshima moja ya juu za kitaifa na tuzo ya uhuru wa kidini na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

    “ Mungu aliumba binadamu tofauti, lakini anataka tuishi pamoja kwa amani na mshikamano, na tusidhuru wengine,” Abdullahi aliripotiwa kusema wakati huo.

    Watu aliowaokoa walikuwa wametoka kijiji jirani. Walikuwa wakikimbia watu takriban 300 wenye silaha nyingi, wanaoshukiwa kuwa wafugaji wa ng’ombe, ambao kwa kawaida ni Waislamu waliokuwa wanapiga risasi mara kwa mara na kuchoma nyumba zao, BBC iliripoti mwaka 2018.

    Baadhi ya wale walioweza kutoroka walikimbilia jirani ambapo walikuwa wengi Waislamu, eneo ambako imam huyo aliishi.

    Kiongozi wa dini huyo mara moja aliwasaidia.

    “Niliwachukua wanawake kwanza kwenda nyumbani kwangu ili kuwaficha. Kisha niliwachukua wanaume kwenda msikitini,” Abdullahi aliambia BBC Pidgin.

    Wakati washambuliaji waliposikia kwamba wakazi wa kijiji walikimbilia kuelekea msikitini, waliitaka imam awatoe wale aliokuwa anawaficha.

    Lakini alikataa.

    Pamoja na wengine katika jamii ya Waislamu, alianza kulia kwa sauti kubwa, akiwasihi waendoke.

    Na kwa mshangao , wafugaji hao waliondoka lakini kisha walichoma moto makanisa mawili yaliyokuwa karibu.

    Shambulio hilo lilikuwa sehemu ya wimbi la vurugu, ambalo linaendelea hadi leo, katika eneo la kati la Nigeria ambapo jamii za wakulima na wafugaji wa ng’ombe hukutana kwa migongano, mara nyingi juu ya haki za ardhi na malisho.

  5. Blair na Rubio miongoni mwa walioteuliwa kwenye “Bodi ya Amani” ya Gaza

    Serikali ya Rais Donald Trump imemtaja Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Tony Blair, kuwa miongoni mwa wajumbe wa “Bodi ya Amani” ya Gaza.

    Mjumbe wa Trump katika eneo la Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, pamoja na mkwe wa rais, Jared Kushner, pia watakuwa wajumbe wa “bodi ya utendaji,” Ikulu ya White House ilisema katika taarifa yake Ijumaa.

    Trump atahudumu kama mwenyekiti wa bodi hiyo, ambayo ni sehemu ya mpango wake wa vipengele 20 wa kumaliza vita kati ya Israel na Hamas.

    Bodi hiyo inatarajiwa kusimamia kwa muda uendeshaji wa Gaza na kusimamia mchakato wa ujenzi upya wa eneo hilo.

    Unaweza kusoma;

  6. Uchaguzi Uganda 2026: Museveni aelekea kushinda uchaguzi, mpinzani wake mkuu adai kuwepo kwa udanganyifu

    Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ameongoza kwa kishindo katika uchaguzi wa urais uliofanyika Alhamisi, akiwa mbali mbele ya mpinzani wake mkuu Bobi Wine, ambaye chama chake tayari kimeanza kuhoji uhalali wa matokeo.

    Takwimu zilizopo hadi sasa zinaonesha Museveni akiwa na asilimia 75 ya kura, huku Wine akiwa na asilimia 21, kwa mujibu wa matokeo kutoka asilimia 70 ya vituo vya kupigia kura.

    Chama cha Wine kilisema kwenye mitandao ya kijamii kuwa helikopta ilitua katika eneo la nyumba yake jijini Kampala na kwamba “alichukuliwa kwa nguvu na kupelekwa kusikojulikana.”

    Mtandao wa intaneti umezimwa, jambo linalofanya iwe vigumu kuthibitisha madai hayo. Polisi wa eneo hilo waliiambia BBC kuwa hawakuwa na taarifa zozote kuhusu tukio hilo.

    Hapo awali, Wine alisema kuwa amewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani, huku vikosi vya usalama vikizingira makazi yake.

    Katika hatua hiyo, msemaji wa polisi Kituuma Rusoke aliliambia shirika la utangazaji la ndani NBS kwamba kama mgombea urais, Wine alikuwa “mtu wa kuangaliwa”, na akaongeza kuwa uwepo mkubwa wa usalama kuzunguka nyumba yake ulikuwa kwa usalama wake mwenyewe.

    Baadhi ya waandishi wa habari wa ndani walisema kuwa vikosi vya usalama vilikuwa vimewazuia kufika nyumbani kwa kiongozi huyo wa upinzani katika eneo la Magere, jijini Kampala.

    Wine pia aliwaambia wafuasi wake wapuuze “matokeo ya uongo” yaliyotangazwa, akisema kuwa mamlaka “zinaiba kura”. Hakutoa ushahidi wowote kuhusu madai yake, na mamlaka husika hazijajibu tuhuma hizo.

    Unaweza kusoma;

  7. Habari za asubuhi, karibu kwenye taarifa zetu za leo