Kilichotokea Gaza tangu kusitishwa kwa mapigano na sababu za mgogoro kuendelea

    • Author, Paula Rosas
    • Nafasi, BBC News Mundo
  • Muda wa kusoma: Dakika 9

Israel na Hamas walitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano Oktoba 10, 2025, yaliyokusudia kumaliza mizozo ya miaka miwili iliyoharibu Ukanda wa Gaza.

Hata hivyo, wiki sita baada ya makubaliano hayo, mauaji yanaendelea Gaza.

Raia wa Palestina bado wanauawa kila siku kutokana na risasi za Israeli na mashambulizi mengine.

Ingawa mapigano yamepungua kwa nguvu, idadi ya waathirika bado inaongezeka, ingawa kwa kiwango kidogo.

Msaada wa kibinadamu umeanza tena kuingia Gaza baada ya miezi kadhaa ya kizuizi kigumu, lakini bado haukidhi mahitaji ya idadi ya watu walioko, wengi wakihama na kuishi katika eneo lililoachwa bila miundombinu muhimu.

Kusitishwa kwa mapigano kumewezesha Umoja wa Mataifa kuanza kufungua shule zilizoharibiwa, ambazo nyingi zilikuwa zikitumika kama makazi ya muda kwa familia zilizokimbia, huku huduma za afya zikibaki chache.

Hospitali 36 tu kati ya Gaza ndizo zinazofanya kazi maeneo kadhaa, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Hamas, ingawa imezidiwa na changamoto, inakataa kuachilia silaha.

Siku moja baada ya makubaliano kuanza, ilituma wanajeshi 7,000 kudhibitisha udhibiti wa maeneo yaliyokuwa yameachwa na majeshi ya Israeli.

Hata hivyo, udhibiti wake unapingwa na makundi mengine ya silaha yaliyosambaa katika ukanda huo, tayari kuyakabili.

Wapalestina bado wanangojea mpango wa amani wa Rais wa Marekani, Donald Trump, ambapo kusitishwa kwa mapigano kulikuwa ni hatua ya awali pekee, ili kuanza upya ujenzi wa eneo ambalo bado linadhibitiwa kwa kiasi kikubwa na jeshi la Israeli.

Zaidi ya 350 waliuawa katika mashambulizi ya Israel

Msuruari wa mauaji tangu kusitishwa kwa mapigano haujakoma.

Zaidi ya watu 350 wameuawa Gaza tangu wakati huo, na kuongeza idadi ya waathirika wa Palestina kufikia 70,100, wengi wakiwa wanawake na watoto, kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza.

Wapiganaji wa Hamas bado wanadhibitiwa na jeshi la Israeli, lakini walio wengi wa waathirika ni raia.

Mifano ni pamoja na mpiga picha Mahmud Wadi aliyefariki kutokana na shambulizi la ndege zisizo na rubani na ndugu Fadi na Juma Abu Assi, wenye umri wa miaka 8 na 11, waliopoteza maisha walipokuwa wakikusanya kuni.

Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) liliihakikishia BBC kuwa limewapiga risasi washukiwa wawili waliovuka "Mstari wa Njano, eneo linalodhibitiwa na Israel.

Hata hivyo, idadi kubwa ya Wapalestina haielewi mipaka hii, jambo linalosababisha vifo mara nyingine.

Mashambulizi ya mabomu yameendelea katika maeneo yenye watu wengi, kama ilivyokuwa Oktoba 28, ambapo Wapalestina 104 waliuawa katika miji kadhaa ya Gaza.

Wapiganaji wa IDF na Hamas wamekashifiana mara kwa mara ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Tarehe 21 Novemba msemaji wa UNICEF Ricardo Pires alibainisha kuwa, tangu kusitishwa mapigano, wastani wa watoto wawili wamefariki kila siku huko Gaza.

"Hizi sio takwimu. Kila mmoja wao alikuwa mtoto mwenye familia, ndoto, maisha yaliyokatizwa mara kwa mara na vurugu zinazoendelea," Pires aliwaambia waandishi wa habari.

Nini kimetokea kwa misaada ya kibinadamu?

Kizuizi kigumu cha Israeli kabla ya makubaliano kilisababisha njaa na vifo vya zaidi ya watu 200.

Makubaliano yalihakikisha kuruhusiwa kuingizwa kwa mabasi 600 ya msaada kila siku ili kukidhi matakwa ya raia milioni 2., lakini kiwango hicho hakijaafikiwa.

Lishe bado ni duni, na vyakula vyenye protini kama nyama na kuku vinapatikana kwa uchache, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Ufikiaji wa misaada ya kibinadamu bado una vikwazo vingi, kama ilivyolaaniwa hivi majuzi na kundi la wataalam wa Umoja wa Mataifa, miongoni mwa mambo mengine kwa sababu ni vivuko viwili tu kati ya sita ambavyo vimefunguliwa tena.

"Kiasi cha malori ya misaada yanayoingia Gaza hakijawahi kufikia lengo lililokubaliwa la 600 kwa siku na mara nyingi imekuwa chini ya nusu ya idadi hiyo," walisema wataalamu hao, akiwemo Francesca Albanese, Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa maeneo ya Palestina.

Amnesty International pia imelaani kwamba Israel inaendelea kuzuia "kuingia kwa vifaa vinavyohitajika kukarabati miundombinu muhimu na kuondoa vifaa visivyolipuka, uchafu na maji taka," shirika hilo lilisema hivi karibuni katika taarifa.

Israel inasema tangu usitishaji mapigano uanze, wastani wa lori 600 hadi 800 zinazobeba chakula, malazi na vifaa vya matibabu zimeingia Gaza kila siku, kulingana na Mratibu wa Shughuli za Serikali katika Wilaya (COGAT). COGAT inakadiria kuwa 41% ya malori haya yanaenda kwa sekta binafsi.

Kulingana na OCHA, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu, ingawa mara kwa mara Wagaza wanakula katika kaya nyingi, "matumizi ya chakula yanasalia chini ya viwango vya kabla ya migogoro," na lishe inategemea zaidi nafaka, kunde na kiasi cha wastani cha maziwa na mafuta, na upatikanaji mdogo sana wa vyakula vya lishe kama vile nyama, mboga na matunda.

Kama Sami Matar, kutoka shirika lisilo la kiserikali la Anera, ambalo linaendesha jiko la jumuiya huko Gaza, aliiambia BBC, "tunalazimika kupika hasa aina tatu za milo kwa wiki: wali, pasta na dengu (...) Tunahitaji chakula kiwe cha aina mbalimbali zaidi, ili kuhakikisha mboga mpya na protini muhimu kama vile nyama na kuku."

Bidhaa hizi, anasema, "haziwezi kuingia Gaza kwa usambazaji kama msaada wa kibinadamu," na zinaagizwa tu na wachuuzi wa ndani, ingawa Wagaza wengi hawana pesa za kuzinunua.

Shirika lenye utata la Gaza Humanitarian Foundation (GHF), lililoundwa na Marekani na Israel ili kukwepa mfumo wa jadi wa msaada wa Umoja wa Mataifa, limesitisha shughuli zake huko Gaza miezi sita baada ya kuzinduliwa.

Mamia ya watu waliuawa na moto wa Israel wakati wa uwasilishaji wake wa masanduku ya misaada ya kibinadamu.

Jeshi la Israeli na udhibiti wa Gaza

Makubaliano yalibainisha kwamba jeshi la Israeli lingeondoa wanajeshi hatua kwa hatua, lakini hadi sasa IDF bado inaendelea kudhibiti sehemu ya Gaza inayoitwa Mstari wa Njano.

Ramani iliyosambazwa na Ikulu ya White House wakati huo ilionyesha hatua tatu zilizopendekezwa za kuondolewa kwa wanajeshi wa Israeli, ambayo katika awamu ya kwanza, moja pekee iliyokubaliwa hadi sasa, iliacha asilimia 53% ya Gaza, ukanda wote unaoenea kwenye mpaka na Israeli, chini ya udhibiti wa Israeli.

Katika awamu zifuatazo, eneo hili linapaswa kupunguzwa hadi asilimia 40% katika hatua ya pili na hadi asilimia 15% katika hatua ya mwisho, aina ya "mzunguko wa usalama" ambao "utabaki hadi Gaza imelindwa ipasavyo dhidi ya kuibuka tena kwa tishio la kigaidi."

Kwa sasa, IDF inasalia nyuma ya kile kinachojulikana kama 'Mstari wa Njano', katika eneo ambalo, kulingana na uchunguzi wa BBC Verify kwamba kuchambua video na picha za satelaiti, ni kubwa kuliko ilivyotarajiwa katika makubaliano na Hamas.

Katika baadhi ya maeneo, alama zilizowekwa na wanajeshi wa Israel kuashiria mgawanyiko huo zilikuwa mamia ya mita zaidi ndani ya Ukanda huo kuliko ilivyotarajiwa kulingana na njia ya kuondoka.

Katika eneo hili, Israel pia imeharibu vitongoji vyote katika kile kinachoonekana kuwa ubomoaji wa kimakusudi.

Kulingana na uchambuzi wa BBC Verify, angalau majengo 1,500 yalibomolewa mwezi wa kwanza baada ya kusitishwa kwa mapigano.

Israel inahoji kuwa ubomoaji huu haukiuki makubaliano, kwani kwa mujibu wa masharti ya kusitisha mapigano, "miundombinu yote ya ugaidi, ikiwa ni pamoja na mahandaki, lazima ivunjwe huko Gaza.

Israel inachukua hatua kujibu vitisho, ukiukaji, na miundombinu ya ugaidi," alisema msemaji wa IDF.

Lakini baadhi ya wachambuzi na wataalam wa sheria za kimataifa wanaamini kwamba ubomoaji huu unaweza kuwa unakiuka sheria za vita, ambazo zinakataza uharibifu wa mali ya kiraia na mamlaka inayokalia, pamoja na kuhatarisha makubaliano ya kusitisha mapigano.

Zaidi ya asilimia 90% ya wakazi wa Gaza wameyakimbia makazi yao wakati wa miaka miwili ya vita, na wengi wanaendelea kuishi katika mahema ya muda.

Wengi hawawezi kurudi makwao kwa sababu hawapo tena.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, asilimia 80% ya majengo katika Ukanda wa Gaza yameharibiwa.

Katika Jiji la Gaza, kituo kikuu cha mijini cha eneo hilo, idadi hii inaongezeka hadi asilimia 92%.

Pia unaweza kusoma:

Kukua kwa makundi yenye silaha yanayopingana na Hamas

Makundi mapya ya silaha yameenea Gaza, baadhi yakiwa na msaada wa Israeli.

Hamas inakataa kuachia udhibiti wa ukanda huo, na video zinaonyesha wapiganaji wake wakipiga au kuua wanakundi wapinzani waliodaiwa kushirikiana na Israel.

Baadhi ya makundi haya yanatamani hatimaye kuwa sehemu ya vikosi vya polisi vya baadaye vya Gaza na kudai, ingawa haijathibitishwa, kwamba yanafanya kazi kwa uratibu na Bodi ya Amani, chombo cha kimataifa kitakachosimamia Gaza chini ya mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump.

Kutumwa kwake kunazua shaka miongoni mwa baadhi ya wakazi wa Gaza na Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina, ambao hawana imani na uungaji mkono ambao Israel inaonekana kutoa kwa baadhi ya makundi hayo.

"Israel inaweza kudai kuunganishwa kwa wanamgambo hao, kutokana na masuala yake mahususi ya kisiasa na kiusalama," Jenerali Anwar Rajab, msemaji wa vikosi vya usalama vya Mamlaka ya Palestina, aliambia mwandishi wa BBC Mashariki ya Kati, Lucy Williamson.

Lakini madai ya Israel, aliendelea, "si lazima yawanufaishe Wapalestina. Israel inataka kuendelea kuweka udhibiti wake kwa njia moja au nyingine katika Ukanda wa Gaza."

Kurudishwa kwa miili ya mateka

Makubaliano yalihakikisha kurudishwa kwa mateka wa Israeli na miili ya waliokamatwa.

Mateka wote hai waliachiliwa huru Oktoba 13, kwa kubadilishana na wafungwa wa Palestina 250 na 1,718.

Miili 27 ya wazalia imekabidhiwa, ikiwemo Israeli 23, Thai 2, Mnepali 1, na Mtanzania 1. Miili ya Wapalestina 345 imekabidhiwa, wengi wakiwa hawajafahamika.

Mchakato unaoendeshwa polepole umesababisha kutokuwa na maendeleo katika hatua ya pili ya mpango wa amani wa Rais Donald Trump, ikiwa ni pamoja na udhibiti wa Gaza, uondoaji wa wanajeshi wa Israeli, kuachilia silaha kwa Hamas, na ujenzi upya.

Majadiliano ya awamu ya pili ya mpango wa amani yamefikia wapi?

Mara baada ya kuafikiwa, pande hizo zilipaswa kuendelea na hatua zinazofuata, ambazo ni pamoja na kutumwa kwa Kikosi cha Kimataifa cha Kuimarisha Utulivu (ISF) na, katika siku zijazo, njia inayowezekana kuelekea kuanzishwa kwa taifa la Palestina, jambo ambalo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amelikataa.

Mnamo tarehe 17 Novemba, mpango uliowasilishwa na Marekani uliungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo lingeruhusu maendeleo kutoka kwa usitishaji mapigano kuelekea ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza.

Azimio hilo linatazamia kuundwa kwa "Bodi ya Amani" ambayo itasimamia utawala wa kamati ya kiteknolojia na kisiasa ya Wapalestina na kufuatilia ujenzi mpya wa Gaza na utoaji wa misaada ya kibinadamu, ingawa haielezi ni nani atakuwa sehemu ya bodi hiyo.

Pia haijulikani kwa wakati huu ni nchi zipi zingechangia wanajeshi katika vikosi hivi vya kuleta utulivu, wala ni jukumu gani Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina itachukua huko Gaza, ambayo mpango huo unahitaji kufanyiwa mageuzi makubwa.

Mpango huo pia unatoa wito wa kuondolewa kijeshi kwa Hamas na makundi mengine katika Ukanda wa Gaza, jambo ambalo wanamgambo wa Kiislamu wamekataa kufanya.

Kwa mujibu wa azimio hilo, kikosi cha kuleta utulivu kitashirikiana na Israel na Misri, pamoja na kikosi kipya cha polisi cha Palestina kilichopata mafunzo na kuchaguliwa ipasavyo, kusaidia kulinda maeneo ya mpaka na kuhakikisha mchakato wa kudumu wa kupokonya silaha kwa makundi yasiyo ya kiserikali yenye silaha, ikiwa ni pamoja na Hamas.

Kutokuwa na uhakika kwa masuala haya yote kumepunguza kasi ya kuanza kwa awamu ya pili ya mpango wa amani, ambayo bado hakuna tarehe.

Soma pia:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid