Sarafu 10 dhaifu zaidi duniani 2026

    • Author, Abdalla Seif Dzungu
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Dola ya Marekani ndiyo sarafu inayouzwa zaidi duniani hata iwapo, sio sarafu yenye nguvu zaidi duniani (haki hizo za thamani ya juu kwa sasa zinakwenda kwa sarafu ya Dinari ya Kuwait).

Lakini kwa upande mwingine wa kiwango, sarafu dhaifu zaidi duniani zinafanya biashara kwa kiwango cha chini dhidi dola ya Marekani.

Kulingana na jarida la Forbes, baadhi zinahitaji makumi ya maelfu ya fedha hizo ili kununua $1 tu.

Zifahamu sarafu 10 dhaifu zaidi duniani

1. Pauni ya Lebanon (LBP)

Pauni ya Lebanon kwa kiasi fulani, ndiyo sarafu dhaifu zaidi duniani inapopimwa dhidi ya dola ya Marekani. Pauni moja ya Lebanon inanunua $0.000011. Kwa njia nyingine, hii inamaanisha kuwa $1 ina thamani ya pauni 89,556.36 za Lebanon.

Lebanon inapakana na Bahari ya Mediterania, pamoja na Israeli na Syria katika Mashariki ya Kati. Nchi hii ina uchumi unaotegemea huduma na pia inauza nje vito vya thamani, vyuma, bidhaa za kemikali, vyakula na vinywaji.

Kulingana na Forbes pauni ya Lebanon imekuwa chini ya shinikizo dhidi ya dola ya Marekani kwa miaka kadhaa kutokana na kushuka kwa uchumi, mfumuko wa bei na ukosefu wa ajira, mgogoro wa benki na machafuko ya kisiasa.

2. Rial ya Iran (IRR)

Kulingana na kibadilisha fedha kilichotimiwa na Shirika la forbes, Rial moja ya Iran kwa sasa ina thamani ya $0.000024, ambayo ina maana kwamba $1 ingenunua rial 42,112.50 za Iran.

Rial ya Iran ilianzishwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwa miaka ya 1700. Sarafu hiyo imesalia kuwa katika kiwango hicho cha ubadilishaji dhidi ya dola kwa miaka kadhaa.

Iran iko kwenye Ghuba ya Uajemi kati ya Iraq na Afghanistan. Ni muuzaji mkuu wa kimataifa wa mafuta na gesi asilia, lakini vikwazo vya kiuchumi vimeweka shinikizo kali kwa sarafu ya nchi hiyo.

3. Dong ya Vietinam (VND)

Kulingana na Forbes, Dong ya Vietinamu inaorodheshwa ya tatu kwenye orodha yetu, na kila kitengo cha sarafu kinaweza kununua $0.000038. Hii inamaanisha $1 inaweza kununua dong 26,345 za Vietinamu.

Vietnam inapakana na Bahari ya China Kusini, na Uchina, visiwa vya Laos, na Cambodia zikiwa majirani. Huduma huchangia sehemu kubwa zaidi ya pato la taifa, kwa ufanisi kipimo cha pato la kiuchumi la taifa, ikifuatiwa na viwanda kama vile umeme, nishati na nguo.

Fedha za nchi hiyo zimelemewa na vikwazo kwa mauzo ya nje na kushuka kwa mauzo ya nje hivi karibuni, pamoja na kipindi endelevu cha kupanda kwa viwango vya juu vya riba nchini Marekani.

4. Laotian kip (LAK)

Laotian, au Lao, kip ilianzishwa katika miaka ya 1950 na ni sarafu ya nne dhaifu ikiwa na kilo 1 sawa na $0.000046. Hiyo inafanya $1 kuwa na thamani sawa na Lak 21,663.26.

Laos ni nchi isiyo na bahari iliyopakana na Vietnam, Thailand, Cambodia na Uchina. Inategemea sana mauzo ya nje kama vile shaba, dhahabu na mbao.

Nchi hiyo imekumbwa na ukuaji duni wa uchumi, kupanda kwa deni la nje na mfumuko mkubwa wa bei, ambayo imesaidia kuweka shinikizo katika sarafu ya Laos.

5. Rupiah ya Indonesia (IDR)

Sarafu ya kitaifa ya Indonesia ilianzishwa mwaka wa 1946. Rupia moja kwa sasa ina thamani ya $0.000059, ambayo ina maana kwamba $1 inaweza kununua sawa na rupiah 16,849.37.

Indonesia inajumuisha zaidi ya visiwa 17,000 katika bahari ya Pasifiki, vikiwemo Java, Sumatra, na sehemu za Borneo na New Guinea.

Kwa upande wa Pato la Taifa, nchi hiyo ndiyo kubwa zaidi kusini-mashariki mwa Asia hasa kutokana na sekta yake ya huduma.

Indonesia pia ina utajiri wa bidhaa, lakini sarafu yake ya kitaifa imeshuka ikilinganishwa na zingine kutokana na mchanganyiko wa mfumuko wa bei na hofu ya kushuka kwa uchumi.

6. Uzbekistan som (UZS)

Som ilianzishwa mnamo 1993 na Som moja ya sarafu ya kitaifa ya Uzbekistan kwa sasa inanunua $0.00008. Kwa njia nyingine, $1 ni sawa na 11,861.84.79 som.

Uzbekistan ni taifa lililopo katikati mwa Asia, ni jamhuri ya zamani ya Muungano wa Sovieti. Ni mojawapo ya wauzaji wa pamba wanaoongoza duniani na ina akiba kubwa ya madini, mafuta na gesi.

Kulingana na Forbes ni nchi ambayo imetekeleza mageuzi ya kiuchumi, lakini inaendelea kupambana na ukuaji mdogo wa uchumi, mfumuko mkubwa wa bei na ukosefu wa ajira na rushwa.

7. Faranga ya Guinea (GNF)

Faranga ya Guinea ilianzishwa mwaka 1959 na leo ina thamani ya $0.000115. Hiyo inafanya $1 kuwa na thamani ya faranga za Guinea 8,658.25.

Guinea ni koloni la zamani la Ufaransa katika Afrika ya Jangwa la Sahara. Ina wingi wa maliasili kama vile dhahabu na almasi, lakini imepambana na mfumuko mkubwa wa bei, machafuko ya kijeshi na kufurika kwa wakimbizi kutoka nchi jirani za Liberia na Sierra Leone.

8. Faranga za Burundi (BIF)

Jamhuri ya Burundi, ni taifa lisilo na bandari katika Afrika Mashariki. Faranga moja ya Burundi kwa sasa ina thamani ya $0.00011, na kufanya dola moja ya Marekani kuwa na thamani ya Faranga za Burundi 8,754.96.

Nchi hiyo ina wakazi zaidi ya milioni 14 na inapakana na Rwanda upande wa kaskazini, Tanzania upande wa mashariki/kusini-mashariki, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo upande wa magharibi. Kahawa na chai vinajumuisha 90% ya mauzo yake ya nje.

9. Ariari ya Madagascar (MGA)

Kulingana na Forbes Ariari Ilianzishwa mwaka wa 1961, sarafu hiyo ya Kimalagasi ilichukua nafasi rasmi ya faranga mwaka 2005. Ariary moja kwa sasa ina thamani ya $0.00021, na kuifanya dola kuwa na thamani ya ariary 4,637.73.

Madagascar ni nchi ya kisiwa iliyo karibu na pwani ya kusini-mashariki mwa Afrika. Kilimo, madini, uvuvi na misitu ni mambo makuu ya nayokuza uchumi wa nchi hiyo. Mauzo ya nje ni pamoja na vanila, chuma cha nikeli na karafuu.

10. Guarani ya Paraguay (PYG)

Ilianzishwa kwa mara ya kwanza mnamo 1952. Guarani ya Paraguay kwa sasa inanunua $0.00015 ikimaanisha $1 ina thamani ya guarani 6,619.11.

Paraguay haina bandari, inapakana na Brazili, Argentina na Bolivia. Nchi inaongoza kwa uzalishaji wa soya, mbadala wa sukari, nyama ya ng'ombe na mahindi.

Sarafu hiyo imekuwa chini ya shinikizo la mfumuko wa bei, ufisadi na sarafu ghushi.