Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, ni kweli Marekani 'inaifadhili' Nato kwa asilimia 100?
- Author, BBC Verify
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Katika hotuba yake kwa viongozi wa ulimwengu katika Kongamano la Kimataifa la Kiuchumi mjini Davos, Uswizi, Rais Trump alitoa madai ya kutatanisha kuhusiana na masuala kadhaa.
Trump aligusia azma yake ya kutaka kuichukua Greenland kutoka kwa Denmark - jambo ambalo alilolitaja kama "ombi dogo", kwa mchango wa Marekani kwa Nato, na nishati ya upepo nchini China.
Hotuba yake - iliyodumu kwa zaidi ya saa moja ilijumuisha madai ya kadhaa yanayotiliwa shaka ambayo BBC Verify inachanganua.
Je, Marekani 'iliirudisha Greenland' baada ya Vita vya Pili vya Dunia?
Kwa majuma kadhaa, Trump amezungumzia nia yake ya kuimiliki Greenland, eneo huru la Denmark linalojitawala. Amesema ni muhimu kwa mkakati wa usalama wa kitaifa wa Marekani.
Katika mjini Davos,alisema kwamba baada ya Vita vya Pili vya Dunia "tuliirudishia Denmark eneo la Greenland ," akiongeza kusema: "Tulikuwa wajinga kiasi gani?"
Lakini halikuwa eneo la Marekani kupeana.
Mnamo 1933 mahakama ya kimataifa - iliyokuwa mbele ya ya mahakama ya sasa ya kimataifa ya haki (ICJ) - iliamua kwamba Greenland ni eneo la Denmark.
Mnamo 1941 - baada ya Ujerumani kujisalimisha kwa Denmark mwaka uliotangulia - wawakilishi wa Marekani na Denmark walitia saini makubaliano ya kuruhusu Marekani kuilinda Greenland dhidi ya unyakuzi wa Wanazi .
Hii ilisababisha ujenzi wa kambi za Marekani katika kisiwa hicho na kupelekwa kwa wanajeshi wa Marekani.
Lakini, makubaliano hayo hayakuhusisha umiliki wa eneo hilo, ikimaanisha Greenland haikuwahi kuwa eneo la Marekani.
Je, Marekani 'inagharamia 100%' ya ulinzi wa Nato?
Rais wa Trump aliikosoa Nato na kudai kwamba "Marekani inagharamia karibu kila kitu kwa salilimia 100".
Alisema kiwango cha michango kutoka nchi ambazo ni wanachama wa muungano wa kijeshi: "ilikuwa 2% na hawakilipa, sasa wanalipa 5%.
Madai yote mawili sio sahihi.
Katika miaka ya hivi karibuni matumizi ya Marekani katika ulinzi yalichangia karibu 70% ya jumla iliyotumiwa na nchi za Nato.
Mnamo 2024, kiwango cha matumizi kilishuka hadi 65% na, mnamo 2025, inakadiriwa kuwa 62%, kwani wanachama wote wa Nato walipangiwa kutumia takribani asilimia mbili ya Pato lao la Taifa kwa ulinzi kwa mara ya kwanza.
Rais wa Marekani amezifanya nchi hizi kujitolea kutumia zaidi katika ulinzi lakini asilimia tano ambayo Trump anazungumza ni lengo la muda mrefu - linatarajiwa kufikiwa ifikapo 2035.
Hivi sasa, hakuna mwanachama wa Nato anayetumia kiasi hicho, kwani hata Poland - nchi inayotumia zaidi Pato la Taifa katika ulinzi - inakadiriwa kutumia chini ya 4.5% katika 2025..
Ni kweli Marekani haijanufaika na chochote kutoka kwa Nato?
Trump alidai kwamba Marekani haijawahi "kupata chochote" kutoka kwa Nato na "hatujawahi kuomba lolote".
Tovuti ya Nato inasema kwamba "michango ya pamoja ni kanuni ya msingi ya NATO"na Kifungu cha 5 cha mkataba wake wa uanzilishi kinasema kwamba "shambulio la silaha dhidi ya mwanachama mmoja wa NATO litachukuliwa kuwa shambulio dhidi yao wote".
Marekani ndiyo mwanachama pekee wa muungano huo kutumia Kifungu cha 5, ikifanya hivyo baada ya mashambulizi ya 9/11.
Mataifa ya Nato yalichangia wanajeshi na zana za kijeshi katika vita vilivyofuata vilivyoongozwa na Marekani nchini Afghanistan.
Miongoni mwa nchi zilizochangia ni Denmark, ambayo ilikumbwa na viwango vya juu zaidi vya vifo vya wanajeshi wake kati ya washirika wa Marekani. Kwa kiasi kikubwa walipelekwa katika maeneo yaliyokumbwa na mapigano makali pamoja na vikosi vya Uingereza katika jimbo la Helmand.
Kwanini China haina mashirika ya uzalishaji wa nishati ya upepo?
Trump pia aliikosoa uzalishaji wa nishati inayotegemea upepo - matamshi ambayo amekuwa akitoa kulenga kile alichokiita "kashfa mpya".
Aliitaja China moja kwa moja, akidai kwamba ingawa inatengeneza mitambo mingi ya upepo, "hajafanikiwa kukubuni mashirika yoyote ya kuzalisha nishati ya upepo nchini China."
China ina moja wapo ya mashirika makubwa ya kuzalisha nishati ya upepo duniani katika eneo la Gansu, ambalo linaweza kuonekana kutoka angani.
China inazalisha nishati zaidi ya upepo kuliko nchi nyingine yoyote, kulingana na shirika la Our world in data . Takwimu zake zinaonyesha kuwa mwaka 2024 China ilizalisha terawati 997 kwa saa kutokana na upepo.
Hiyo ilikuwa zaidi ya mara mbili ya ile ya Marekani - ambayo ilikuwa katika nafasi ya pili.
Je, Uingereza inachukua 92% ya mapato ya mafuta ya Bahari ya Kaskazini?
Rais Trump pia aliitaja Uingereza, akikosoa sera zake za nishati.
Akizungumzia mafuta ya Bahari ya Kaskazini, Trump alisema kimakosa: "Wao [Uingereza] huzuia makampuni ya mafuta kufika eneo hilo, wanachukua 92% ya mapato."
Makampuni ya mafuta na gesi yanayofanya kazi katika Bahari ya Kaskazini hulipa ushuru wa 30% wa shirika kwenye faida zao na kiwango cha ziada cha 10%. Hii ni ada kubwa kuliko ushuru wa 25% wa shirika unaolipwa na kampuni zingine kubwa.
Mnamo Novemba 2024, serikali ilipandisha ushuru wa mwisho kwa kampuni za mafuta na gesi kutoka 35% hadi 38%.
Hiyo inachukua jumla ya ushuru wa North Sea Oil hadi 78%, ambayo hulipwa kwa faida sio mapato.
Ushuru wa matayo yasiyotarajiwa, ambao ulianzishwa na Conservatives mnamo 2022 kudhibiti gharama za uzalishaji wa nishati zinazoongezeka, unatarajiwa kukomeshwa mnamo 2030.
Je, Trump amepatia Marekani uwekezaji wa thamani ya dola trilioni 18?
Rais Trump pia alizungumza kuhusu uwekezaji ambao utawala wake ulikuwa umeipata Marekani.
Alisema, "tumepata ahadi za takribani dola trilioni 18", na baadaye kurudia, "dola trilioni 18 zimewekezwa".
Hii sio mara ya kwanza anatoa madai kama hayo - mnamo Oktoba alisema Marekani ilikuwa imevutia uwekezaji wa thamani ya $17tn (£12.7tn) - lakini hakuna ushahidi unaopatikana hadharani kuunga mkono takwimu kubwa kiasi hiki.
Tovuti ya White House, ambayo iliwekwa taarifa mpya mwishoni mwa Novemba mwaka jana, ina lenga kufuatilia "uwekezaji mpya katika utengenezaji wa bidhaa za Marekani, teknolojia na miundombinu". Inasema kuwa uwekezaji chini ya Trump jumla ya $9.6tn (£7.1tn).
Uwekezaji wa kiwango cha juu katika orodha yake ni mradi wa uzalishaji na viwanda wenye thamani ya dola trilioni 1.4 kati ya Marekani na Milki za Kiarabu (UAE).
Tovuti ya ubalozi wa UAE huko Washington DC inasema UAE "inafanya kazi na Utawala wa Trump kufikia uwekezaji wa kihistoria wa takribani dola trilioni 1.4 nchini Marekani katika muongo ujao".
Greg Auclair, mtaalamu wa masuala ya takwimu katika Taasisi ya Kimataifa ya Peterson inayoangazia masuala ya kiuchumi, aliiambia BBC Verify kwamba uwekezaji wa Ikulu ya White House "inajumuisha ahadi ambazo hazitatimia - kwa mfano makubaliano ya biashara ya Umoja wa Ulaya ambayo sasa inakabiliwa na tishio la kukwama kutokana na mivutano ya Greenland".
Siku ya Jumatano kamati ya biashara ya kimataifa ya Bunge la Ulaya ilisema inasitisha uidhinishaji wa makubaliano hayo "hadi Marekani itakapoamua kujihusisha tena katika njia ya ushirikiano badala ya makabiliano".
Auclair aliongeza kuwa ingawa kumekuwa na ongezeko la uwekezaji wa kigeni nchini Marekani katika mwaka uliopita, "itachukua miaka kadhaa kabla ya matokeo ya msukumo wa uwekezaji wa utawala wa Trump kuwa wazi".
Ripoti ya Tom Edgington, Lucy Gilder, Matt Murphy, Nicholas Barrett na Anthony Reuben.