Idadi ya vifo kutokana na moto katika maduka ya jumla Pakistani yaongezeka hadi 67
Idadi ya vifo kutokana na moto uliozuka katika maduka ya jumla ya biashara Pakistan imefikia watu 67, imethibitishwa na polisi.
Polisi wanasema kuwa familia za watu 77 bado zinatafuta wapendwa wao waliopotea kufuatia moto uliozuka kwenye Gul Plaza, katika jiji kubwa zaidi la Pakistan, Karachi, Jumamosi jioni.
Hata hivyo, kiwango kikubwa cha uharibifu kilichosababishwa na moto huo ambao ulichukua zaidi ya saa 24 kuuzima kimepunguza kasi ya juhudi za uokoaji, huku mamlaka zikiendelea kuchunguza mabaki ya jengo lenye ukubwa wa mita za mraba 6,500 (sq ft 70,000).
Ingawa baadhi ya maiti zilizopatikana ni mabaki tu, mamlaka zimehesabu miili ya binadamu 67, amesema Naibu Kamishna wa Polisi, akizungumza na BBC.
Mchakato wa kutambua maiti unaendelea, na hadi sasa watu 15 wametambulika.
Sababu ya moto bado haijafahamika, ingawa mashahidi walisema awali kwa BBC kwamba ukosefu wa njia za dharura zinazofanya kazi pamoja na msongamano wa wanunuzi na vibanda vilivyopangwa vibaya ndani ya jengo vilizidisha madhara.
Kwa kuwa kituo hicho kilikuwa kinaelekea kufungwa hivi karibuni, milango mingi ya kituo cha biashara ilikuwa imefungwa, mashahidi walisema.
Afisa mkuu wa polisi, Syed Asad Raza, alisema kwa shirika la habari la Reuters kuwa milango yote isipokuwa mitatu kati ya 16 ya kituo hicho ilikuwa imefungwa.
Soma Pia: