Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Walikaribia kuwa Wamarekani - ila Trump akafuta sherehe zao za uraia
Sanam, mhamiaji kutoka Iran aliyekwenda Marekani zaidi ya muongo mmoja uliopita, alikuwa karibu kuwa raia wa Marekani. Miaka mingi ya makaratasi, vibali, vipimo, na uchunguzi wa usalama, ilimfikisha katika hatua ya mwisho: sherehe ya uraia.
Lakini siku mbili tu kabla ya kula kiapo chake tarehe 3 Desemba, serikali ya Marekani ilikifuta kiapo hicho ghafla.
Sanam alishtuka na kuchanganyikiwa - hakukuwa na maelezo. Hakuelewa ni kwa nini sherehe hiyo imefutwa wakati hajafanya kosa lolote, ameiambia BBC.
Baadaye, aligundua kuwa ni kwa sababu ya mahali alipozaliwa.
Sanam - ambaye anataka kutotajwa jina lake kwa kuhofia kuandamwa - anaishi Oregon na mumewe, raia wa Marekani kutoka Kansas.
Kesi yake ni mojawapo ya nyingi – ambapo mapema mwezi huu utawala wa Trump ulianza kufuta sherehe za uraia za wahamiaji kutoka nchi 19 ambazo tayari watu wake wamepigwa marufuku kuingia Marekani, ikiwemo Iran.
Uamuzi huo wenye utata uliwaacha baadhi ya wakazi halali wa kudumu kama Sanam - watu ambao tayari wamepitia kila hatua ya mchakato huo ili kuwa raia wa Marekani na wakisubiri tu utaratibu wa mwisho - katika hali kutokuwa na uhakika.
Hili limemfanya Sanam kuanza kufikiria upya kama inafaa kubaki Marekani. Bado ana familia nchini Iran, wakiwemo wazazi wake wazee, na hajui ni lini ataweza kuwaona tena.
Nchi 19 zilizoathiriwa na marufuku
Kufutwa kwa sherehe za kiapo ni sehemu moja tu ya juhudi za hivi karibuni za utawala wa Trump za kuimarisha sheria za uhamiaji. Wahamiaji kutoka nchi 19 ambazo tayari zimepigwa marufuku ya kusafiri wamesitishiwa mchakato wao wa uhamiaji bila kujali wako wapi katika mchakato huo, si wale walio katika hatua ya mwisho tu.
Hatua hiyo, na nyingine kama hiyo, ilikuja siku chache baada ya raia wa Afghanistan kuwafyatulia risasi maafisa wa Jeshi huko Washington DC Novemba 26, na kumuua mmoja na kumjeruhi mwingine vibaya.
Utawala wa Trump umetumia tukio hilo kama kisingizio katika juhudi mpya za kupunguza uhamiaji, ikiwa ni pamoja na kutuma wanajeshi 500 wa ziada huko DC, kupunguza muda wa uhalali wa viza ya kazi kutoka miaka mitano hadi miezi 18, na kusitisha maamuzi yote ya madai ya kuomba hifadhi.
Idara ya Uraia na Uhamiaji ya Marekani imesema vikwazo hivyo ni muhimu ili kulinda usalama wa taifa, kulinda maisha ya Wamarekani, na kuhakikisha usalama wa umma.
Lakini Mario Bruzzone, makamu wa rais wa masuala ya sera katika Shirika la Muungano wa Wahamiaji wa New York, linalowakilisha mamia ya makundi ya wahamiaji, amesema vikwazo hivyo vinawaweka wahamiaji wanaohitaji ulinzi katika hali hatari.
"Kusitisha kwa muda usiojulikana ni sawa na marufuku, na wanatumia ufyatuaji risasi wa hivi karibuni huko DC kama kisingizio cha kuongeza mashambulizi dhidi ya wahamiaji na wakimbizi," Bw. Bruzzone aliambia BBC.
Mhamiaji mmoja wa Venezuela, Jorge, pia alikuwa karibu kuwa raia wa Marekani kabla ya sherehe yake ya tarehe 2 Desemba, alipoambiwa sherehe hiyo imefutwa bila maelezo.
"Nilikuwa nimeandaa kila kitu, ikiwa ni pamoja na kuhudhuria sherehe hiyo na mwanangu. Kufutwa kwake siku moja kabla, bila sababu yoyote iliyo wazi, kulituacha tukiwa hatujui kipi kinachofuata," Jorge alisema.
Jorge, ambalo si jina lake halisi, ameomba kutotajwa jina, lakini utambulisho wake umethibitishwa na BBC. Alisema alipata ukaazi wa kudumu mwaka 2017 kupitia fani yake.
Jorge anakubaliana na utawala wa Trump kwamba kunapaswa kuwepo kwa "uchunguzi mkubwa" juu ya wahamiaji, aliiambia BBC. Anaulaumu utawala wa Biden kwa kuruhusu wahamiaji wengi mno kuingia nchini, na akaongeza kwamba kama angeweza kupiga kura, angemuunga mkono Rais Donald Trump.
Kinachomtia wasiwasi, alisema, ni kwamba wakazi wa muda mrefu ambao hawana historia ya uhalifu wamewekwa kundi moja na watu ambao anaamini wanahitaji uchunguzi wa kina.
"Nataka tu sisi ambao tumefuata kila sheria tuweze kuendelea na kesi zetu - na kwa wale ambao wamefanya ulaghai au uhalifu kukabiliana na matokeo yanayofaa ya kisheria," amesema Jorge.
Bruzzone wa NYIC amesema wahamiaji wengi kutoka nchi 19 - wakiwemo wakimbizi, wanaotafuta hifadhi, na wakaazi halali wa kudumu kama Sanam na Jorge - tayari wamepitia uchunguzi wa kina ambao unachukua miaka mingi na una safu nyingi za ukaguzi wa usalama na ukaguzi wa afya.
Katika jimbo la New York pekee, kuna takriban watu 132,000 waliozaliwa Venezuela hadi mwaka 2023, kulingana na data iliyokusanywa na Muungano wa Wahamiaji wa New York.
Kusitishwa huko kumevuruga maisha ya watu katika kila hatua, na kuwaacha wakisubiri bila kuwa na uhakika,” anasema Bruzzone.
Mume wa Sanam, ambaye alichagua kutotaja jina lake kwa kuhofia kuandamwa, ameiambia BBC ratiba ya matukio inaonekana ya kushangaza.
"Kama wale wanajeshi wa Jeshi wasingeshambuliwa wiki iliyopita, wiki hii, [mke wangu] angekuwa raia hivi sasa," aliambia BBC siku moja baada ya sherehe ya kiapo cha Sanam iliyotarajiwa kufanyika kufutwa.
"Akili yako inachanganyikiwa kuhusu jinsi utaratibu wa kubadilisha sera hizi ulivyofanyika haraka,” anasema.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi