Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Trump anaiyumbisha dunia kuliko rais yeyote tangu Vita vya Pili vya Dunia
- Author, Lyse Doucet
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Siku ya kwanza, aliuambia ulimwengu.
"Hakuna kitakachotuzuia," Rais Donald Trump alitangaza, huku makofi yakipigwa kwa nguvu, alipomaliza hotuba yake ya kuapishwa katika majira ya baridi kali huko Washington siku kama ya leo mwaka jana, mwanzoni mwa muhula wake wa pili.
Katika hotuba yake alizungumzia itikadi ya karne ya 19 ya “manifest destiny” – ni itikadi kwamba Marekani imeteuliwa na Mungu kupanua eneo lake katika kila bara, na kueneza maadili ya Marekani.
Wakati huo, alikuwa akivutiwa na Mfereji wa Panama. "Tutauchukua tena," Trump alitangaza.
Na sasa anaweza kuichukua Greenland. "Lazima tuichukue," ndiyo kaulimbiu mpya.
Historia ya Marekani imejaa uvamizi, shughuli za siri za Marekani zenye utata za kuwaangusha watawala na serikali. Lakini, katika karne iliyopita, hakuna rais wa Marekani aliyetishia kunyakua ardhi ya mshirika wake wa muda mrefu na kuitawala kinyume na matakwa ya watu wake.
Hakuna kiongozi wa Marekani aliyetishia kuvunja ushirikiano wa muda mrefu ambao umeimarisha utaratibu wa dunia tangu mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia.
Trump sasa anaelezewa kama rais anayeleta mageuzi zaidi nchini Marekani - akishangiliwa na wafuasi wake ndani na nje ya nchi, akishitua wengine katika miji mikuu kote ulimwenguni, na kimya cha kuangalia huko Moscow na Beijing.
"Ni mabadiliko kuelekea ulimwengu usio na sheria, ambapo sheria ya kimataifa inakanyagwa, na sheria pekee inayoonekana kuibuka ni ya mwenye nguvu mpishe," ni onyo la Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwenye Jukwaa la Uchumi la Davos, bila kumtaja Trump moja kwa moja kwa jina.
Kuna wasiwasi unaoongezeka kuhusu vita vya kibiashara vinavyoweza kusababisha maumivu makali, na wasiwasi kwamba muungano wa kijeshi wa Nato wenye umri wa miaka 76 unaweza kuwa hatarini ikiwa kamanda mkuu wa Marekani atajaribu kuichukua Greenland kwa nguvu.
Wafuasi wa Trump wanazidi kuunga mkono ajenda yake ya "Marekani Kwanza," dhidi ya utaratibu wa ujumuishi baada ya vita.
Alipoulizwa na BBC ikiwa kuiteka Greenland kutakiuka katiba ya Umoja wa Mataifa, mbunge wa chama cha Republican Randy Fine amesema: "Nadhani Umoja wa Mataifa umeshindwa kabisa kuwa chombo kinachounga mkono amani duniani."
Fine aliwasilisha muswada unaoitwa "Sheria ya Kuitawala Greenland" katika Bunge wiki iliyopita.
Washirika wa Marekani
Kuna kauli nyingi zimesemwa kuhusu misukosuko ya kidiplomasia na njia bora ya kukabiliana na rais na amiri jeshi mkuu wa Marekani ambaye hatabiriki.
"Tunahitaji kumchukulia kwa uzito lakini si kwa uhalisia," inatoka kwa wale wanaosisitiza kwamba haya yote yanaweza kutatuliwa kupitia mazungumzo.
Mara nyingi Trump hugeuka, wiki moja hadi nyingine, kutoka kuitetea Ukraine au ghafla kuwa karibu na Urusi, kisha hurudi kuelekea Ukraine, kisha hurudi tena kwenye mzunguko wa Urusi.
Wengine wanamuona Trump kuwa ana msimamo mkali, kama mbinu zake za kupata mikataba kutoka enzi zake za umiliki wa nyumba huko New York.
Kuna ukweli wa hilo katika vitisho vyake vya mara kwa mara vya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran – na hilo bado liko mezani.
Hazungumzi kama mwanasiasa wa kawaida," anaelezea Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alipoulizwa kuhusu mbinu za Trump.
"Anasema kisha hufanya alichosema," ndiyo sifa yake kubwa, anasema katika namna ya kudhihaki rekodi ya viongozi waliopita.
Rubio ni mmoja wa watu wanaojaribu kupunguza ukali wa vitisho vya Trump dhidi ya Greenland, akisisitiza kwamba anataka kununua eneo hili, si kulivamia.
Kwamba Trump anataka kununua kisiwa hicho kikubwa zaidi duniani, ili kukabiliana na vitisho vya China na Urusi.
Lakini hakuna shaka kwamba mbinu za Trump za mabavu, dharau, na ana imani kwamba jambo hilo ni sahihi.
"Na nguvu, na aina ya uongozi kama mafia," anasema Zanny Minton Beddoes, mhariri wa jarida la Economist.
"NATO haiogopiwi na Urusi wala China. Hata kidogo," Trump aliliambia gazeti la New York Times katika mahojiano mapema mwezi huu. "Ila sisi tunaogopwa sana."
Kama ni kuhusu usalama, Marekani tayari ina vikosi ardhini huko Greenland na chini ya makubaliano ya 1951 inaweza kutuma wanajeshi zaidi na kufungua vituo zaidi.
"Nahitaji kuimiliki Greeland," ndivyo Trump anavyosema waziwazi.
Na mara nyingi huweka wazi, "Napenda kushinda."
Trump na Mashariki ya Kati
Katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh mwezi Mei, tulitazama jinsi hotuba yake katika safari yake ya kwanza ya kigeni katika muhula wake wa pili ilivyopokelewa kwa furaha kubwa.
Trump aliwakosoa "waingiliaji kati" wa Marekani kwa "kuharibu mataifa mengi zaidi kuliko waliyoyajenga... katika jamii ambazo hata hawakuzielewa."
Mwezi Juni wakati Israeli iliposhambulia Iran, Trump inaripotiwa alimwonya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu asiweke diplomasia yake hatarini kwa vitisho vya kijeshi dhidi ya Tehran.
Mwishoni mwa wiki, alipoona mafanikio ya Israeli katika kuwaua wanasayansi wakuu wa nyuklia na wakuu wa usalama, Trump alisema: "Nadhani ni Mashambulizi mazuri.”
"Watetezi wa Trump, hufanya kazi kusafisha sera zake," Edward Luce aliandika katika safu yake ya hivi karibuni katika jarida la Financial Times.
Mpango wake wa kusitisha mapigano Gaza, ilikuwa ni diplomasia ya Trump yenye misuli iliyomlazimisha Netanyahu, pamoja na Hamas, kukubaliana nayo. Yalikuwa ni mafanikio makubwa ambayo Trump pekee ndiye angeweza kuyafikia.
Trump na Ulaya
Wakati mwingine anaonekana kama anataka kujitenga, wakati mwingine kama mingiliaji kati. Lakini kauli mbiu iliyomrudisha madarakani haibadiliki - Make America Great Again.
Na barua yake kwa Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Støre akieleza kuchukizwa kwake kwa kutoshinda Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka huu.
Trump amemweleza Støre: "Sihisi tena wajibu wa kufikiria amani pekee, ingawa sitoiweka kando, lakini sasa nafikiria kile kilicho kizuri na kinachofaa kwa Marekani."
Majibu ya Ulaya bado yanaendelea.
Macron ameapa kuzindua "tarumbeta la biashara" kwa EU kukabiliana na ushuru na kuweka vikwazo kufanya Biashara na soko lenye faida kubwa la EU.
Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, mmoja wa washirika wa karibu wa rais wa Marekani barani Ulaya, amezungumzia kwa ufupi kuhusu "tatizo la uelewa na kutoelewana."
Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer ametetea vikali na hadharani eneo la Greenland lakini anataka kulinda uhusiano imara alioujenga mwaka uliopita kwa kuepuka ushuru wa kulipiza kisasi.
Sir Keir Starmer amedumisha uhusiano mzuri na Trump tangu alipoanza muhula wake wa pili kama rais
Trump amechapisha jumbe za faragha anazopokea kutoka kwa viongozi wa serikali kujaribu kumweka upande wao.
"Tule chakula cha jioni pamoja jijini Paris siku ya Alhamisi kabla ya hujarudi Marekani," aliandika rais wa Ufaransa ambaye pia aliuliza, "sielewi unachofanya huko Greenland."
"Nitafurahi kukuona," aliandika Katibu Mkuu wa Nato, Mark Rutte, ambaye aliwahi kumuita Trump "baba" kwa jinsi alivyoshughulikia vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel mwaka jana.
Rutte, na wengine, wamesifu vitisho vya Trump kwa kuwalazimisha wanachama wa Nato kuongeza kwa kiasi kikubwa matumizi yao ya ulinzi katika miaka ya hivi karibuni.
"Tunapaswa kuutazama ulimwengu jinsi ulivyo, si jinsi tunavyotaka uwe," ni kauli ya wazi ya Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney katika safari yake nchini China wiki iliyopita.
Ilikuwa ziara ya kwanza ya kiongozi wa Canada huko Beijing tangu 2017, baada ya miaka mingi ya mvutano, na ilituma ishara kuhusu maadiliko ya ulimwengu.
Tishio la Trump la kuichukua nchi hiyo jirani yake kaskazini liliibuka tena wiki hii katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na Canada na Greenland.
Wacanada wanajua bado kuna hatari kwamba nchi yao inaweza kufuata baada ya Greenland.
Carney alipopanda jukwaani huko Davos Jumanne, na kusema "Tuko katikati ya mpasuko, si mpito."
Siku ya Jumatano Trump atazungumza kutoka jukwaa hilo hilo huku ulimwengu ukimtazama.
Alipoulizwa na New York Times mwezi huu ni nini kinachoweza kumzuia, Trump alijibu: "Maadili yangu mwenyewe. Akili yangu mwenyewe. Ndicho kitu pekee kinachoweza kunizuia."
Hayo nidio mawazo ya Trump huku kundi la washirika wakitaka kumshawishi, kumbembeleza na kumlazimisha - abadilishe mawazo yake.
Wakati huu, hakuna uhakika kama watafanikiwa.