Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Raia wa mataifa ya Afrika Mashariki ruksa kumiliki kampuni ya mafuta ya Kenya
- Author, Peter Mwangangi
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Ikiwa wewe ni raia wa Afrika Mashariki na una Ksh 9 (Tsh 180, UGX 240), unaweza kununua na kumiliki hisa za kampuni ya kusafirisha na kuhifadhi mafuta ya Kenya Pipeline.
Hisa za kampuni hiyo zilianza kuuzwa Januari 19, 2026 na zitaendelea kuuzwa kwa mwezi mmoja, huku serikali ikilenga kuchangisha Ksh 106.3b ($825m) kwa kuuza asilimia 65 ya umiliki wake katika kampuni hiyo.
Raia wa jumuiya ya Afrika Mashariki (Tanzania, Uganda, Jamhuri ya Demokrasi ya Congo DRC, Burundi, Sudan Kusini na Somalia) wametengewa asilimia 20 ya hisa hizo, huku wawezekaji wa Kenya (watu binafsi na makampuni) wakipewa asilimia 60%, na asilimia 20 iliyosalia ikitengewa wawekezaji wa nchi za kigeni.
Kampuni hiyo husimamia bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,342 ambalo husafirisha mafuta kutoka bandari ya Mombasa hadi miji tofauti ndani ya Kenya.
Aidha Uganda, Sudan Kusini na eneo la mashariki mwa DRC hunufaika kutokana na miundombinu ya kampuni hiyo japo kwa viwango tofauti.
Kiwango cha chini kabisa cha hisa ambazo mtu anaweza kununua ni hisa 100.
Hii ni mara ya kwanza ndani ya miaka 18 ambapo Kenya inauza hisa zake katika kampuni ya umma kupitia soko la hisa la Nairobi.
Mara ya mwisho kwa hilo kufanyika ilikuwa ni mwaka 2008 na ilihusisha kampuni ya mawasiliano ya Safaricom.
Kwanini Kenya imechukua mkondo huu?
Serikali ya Kenya pia imetangaza mipango ya kupunguza umiliki wake katika kampuni ya Safaricom, na katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikilenga kubinafsisha baadhi ya mashirika yake ya umma.
Lengo kuu ni kuchangisha fedha za kufadhili miradi ya maendeleo, kubadilisha mfumo wa uongozi katika mashirika hayo na pia kuleta mageuzi kwa mashirika ambayo yamekuwa yakitegemea ufadhili kutoka hazina ya kitaifa badala ya kuzalisha mapato ya kutosha kujiendesha yenyewe.
Kwa upande wa Kenya Pipeline, shirika hilo limekuwa likipata faida lakini serikali inaamini kwamba inaweza kupata thamani zaidi kifedha kutokana na shirika hilo.
Katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025, shirika hilo lilipata faida ya Ksh 7.49b ($58m) baada ya kodi, kutokana na mapato ya jumla ya Ksh 38.59b ($299m).
Waziri wa fedha wa Kenya John Mbadi amesema kwamba serikali imelazimika kutumia njia mbadala kama hii ili kufadhili miradi ya kimaendeleo.
"Mbinu za kawaida za kufadhili bajeti yetu kama kutoza ushuru na mikopo hazitupi nafasi kubwa kufanya mengi, kutokana na hali ya sasa," alisema Mbadi.
Kwa miaka minne sasa, mamlaka ya kukusanya ushuru nchini Kenya (KRA) imekuwa ikikosa kutimiza malengo yake ya kukusanya kodi.
Hali pia ilikuwa hivyo katika miezi sita ya kwanza ya mwaka wa kifedha unaoendelea wa 2025/2026, ambapo KRA ilikosa lengo lake kwa Ksh152.2b ($1.18b) - kuashiria changamoto zilizopo katika ukusanyaji wa ushuru, ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya miaka mitano ya utawala wa rais William Ruto kukamilika. Nyongeza ya kodi ilikuwa sababu kuu ya vijana wa Gen Z kuandamana barabarani katika mnamo Juni mwaka 2024, huku wakitaka uwajibikaji zaidi serikalini hususan matumizi ya fedha za umma.
Aidha mikopo imesababisha deni la kitafia la Kenya kupanda hadi karibu asilimia 68 ya pato la taifa (GDP), huku malipo ya mikopo hiyo ikiwa ni zaidi ya theluthi moja ya ushuru unaokusanywa na serikali kwa mujibu wa takwimu za wizara ya fedha nchini Kenya.
Hali hii inafanya iwe vigumu kupata fedha za miradi muhimu ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara, kuimarisha sekta za nishati, elimu, afya na nyinginezo.