Jinsi roketi ya utafiti wa hali ya hewa ya Norway ilivyokaribia kusababisha vita vya nyuklia

Muda wa kusoma: Dakika 5

Katika siku ya baridi kali ya majira ya baridi, tarehe 25 Januari 1995, dunia ilikabiliwa na tukio lililokaribia kuigeuza historia ya mwanadamu.

Kwa zaidi ya saa moja, hofu ya vita vya nyuklia iliyodhaniwa kuwa imepita pamoja na mwisho wa Vita Baridi ilirejea kwa nguvu.

Ilikuwa alasiri ya kawaida ya Jumatano wakati mafundi wa kijeshi katika vituo vya kaskazini mwa Urusi walipobaini ishara isiyo ya kawaida kwenye mifumo yao ya rada.

Kombora lilikuwa limerushwa kwa kasi kubwa kutoka eneo lililoko karibu na pwani ya Norway. Mwelekeo wake haukuwa wazi, wala nia yake haikujulikana.Ilikuwa hatari? Bila shaka, watu wengi walifikiri kwamba mvutano wa nyuklia ulikuwa umeisha wakati Ukuta wa Berlin ulipoanguka.

Kwa vikosi vya ulinzi wa anga vya Urusi, hali hiyo ilikuwa ya kutisha.

Walifahamu kuwa endapo kombora hilo lingekuwa limerushwa kutoka manowari ya Marekani katika maji hayo, lingeweza kufikisha vichwa nane vya nyuklia mjini Moscow ndani ya dakika 15 tu.

Taarifa hiyo ilifikishwa kwa haraka hadi ngazi za juu za uongozi, na hatimaye kwa Rais wa Urusi wa wakati huo, Boris Yeltsin.

Kwa mara ya kwanza katika historia, kiongozi wa taifa alilazimika kuamsha kile kilichojulikana kama kifaa cha nyuklia, mfumo maalumu wenye maagizo na teknolojia ya kuidhinisha shambulio la nyuklia.

Tangu mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia, mataifa yenye silaha za nyuklia yamejikita katika sera ya kuzuiana (deterrence), inayotegemea wazo kwamba shambulio la nyuklia kwa kiwango kikubwa lingesababisha maangamizi kwa pande zote, hivyo kuzuia yeyote kuthubutu kuanzisha vita kama hivyo.

Katika dakika chache zilizokuwa zimejaa hofu na msongo mkubwa wa mawazo, Yeltsin na washauri wake walitakiwa kuamua kwa haraka hatua ya kuchukua. Hatimaye, kama tunavyofahamu leo, taharuki hiyo haikusababisha maafa.

Baadaye usiku huo, simulizi la tukio hilo liliripotiwa kwa mtazamo mwepesi mwishoni mwa taarifa ya habari, likiambatana na wimbo wenye ucheshi mzito wa Tom Lehrer, "We'll All Go, When We Go," kama ishara ya afueni baada ya hatari kubwa kupita.

Mtangazaji wa kipindi cha BBC Newsnight, Jeremy Paxman, alifafanua hali hiyo kwa kusema:

"Kabla hatujaendelea, ni lazima tueleze wazi kuwa leo hakukutokea vita vya nyuklia, licha ya taarifa zilizotolewa mapema na wakala wa habari wa Urusi."

Alieleza kuwa saa 13:46 kwa saa za Moscow, vyombo vya habari vilianza kuripoti kwamba Urusi ilikuwa imerusha kombora.

''Waandishi wa habari, wakidhani wanashuhudia mwanzo wa janga, waliwasiliana mara moja na Wizara ya Ulinzi. Msemaji mmoja alijibu kwa kejeli akisema, "Nina uhakika Waingereza hawajarusha kombora kuelekea Urusi." Pentagon, kwa upande wake, ilisema ilikuwa na taarifa chache sana zaidi ya zilizokuwa zinaripotiwa.

Baada ya saa kadhaa za sintofahamu, chanzo cha ulinzi cha Urusi kilisema masoko ya fedha duniani yalitikiswa, huku viongozi wa kisiasa, makamanda wa kijeshi na wanahabari wakisaka ukweli wa kilichokuwa kimetokea.

Hatimaye, saa 14:52 kwa saa za GMT, Interfax ilirekebisha taarifa yake na kueleza kuwa, ingawa mfumo wa onyo la mapema wa Urusi ulikuwa umegundua kombora, halikuwa shambulio. Wizara ya Ulinzi ya Norway ilithibitisha kuwa roketi hiyo ilirushwa kwa usalama kama sehemu ya utafiti wa kisayansi.

Roketi hiyo ilikuwa sehemu ya mpango wa kawaida wa utafiti wa hali ya anga, uliolenga kukusanya taarifa kuhusu tukio la kiasili lijulikanalo kama Taa za Kaskazini (Aurora Borealis).

Roketi hiyo ilitua baharini kama ilivyopangwa karibu na kisiwa cha Aktiki cha Spitzbergen, mbali kabisa na anga ya Urusi.

Kwa mujibu wa Interfax, ilibidi "uamuzi wa haraka" ufanywe mara tu rada za onyo la mapema zilipopokea ishara hiyo, ili kubaini kama ilikuwa ni jaribio au tishio halisi.

Urusi imekuwa ikichukua tahadhari kubwa kuhusu ulinzi wa anga tangu mwaka 1987, wakati kijana kutoka Ujerumani ya Magharibi, Mathias Rust, alipofanikiwa kuruka zaidi ya kilomita 750 kupitia mifumo yote ya ulinzi ya Kisovieti kwa ndege ndogo ya injini moja na kutua karibu na Kremlin.

Ingawa Vita Baridi vilikuwa vimekwisha, tukio hilo lilikuwa kumbukumbu kwamba hofu ya tishio la nyuklia haikuwa imepotea kabisa.

Mtaalamu Adolfsen alieleza kuwa tahadhari ya Warusi ilichochewa zaidi na ukweli kwamba ilikuwa mara ya kwanza roketi kufikia urefu wa kilomita 1,457 kiwango kisicho cha kawaida kwa aina hiyo ya urushaji.

Aliongeza kuwa, ''Tarehe 14 Desemba, taarifa ilikuwa imesambazwa kwa nchi zote husika kupitia Wizara ya Mambo ya Nje, ikieleza kuwa jaribio la roketi lingefanyika''.

Hata hivyo, kwa sababu zisizojulikana, ujumbe huo haukufika katika ofisi muhimu.

Tukio hilo lilikuwa funzo chungu kuhusu jinsi kosa dogo la mawasiliano linavyoweza kuweka dunia katika hatari kubwa.

Tangu kuanza kwa enzi ya silaha za nyuklia, dunia imeshuhudia matukio mengi ya karibu kusababisha maangamizi kuliko inavyopendeza kukumbuka.

Si mgogoro mkubwa pekee kama ule wa Makombora ya Cuba wa mwaka 1962, ambao ulikaribia kuibua vita kamili vya nyuklia kati ya Marekani na Umoja wa Kisovieti.

Mwaka 2020, BBC Future ilionya kuhusu hatari za tahadhari za uongo.

Mwaka 1958, ndege moja ilidondosha kwa bahati mbaya bomu la nyuklia kwenye bustani ya familia moja na kwa bahati nzuri kuku pekee ndio waliopoteza maisha.

Mwaka 1966, ndege mbili za kijeshi za Marekani zilianguka katika kijiji cha mbali nchini Hispania, mojawapo ikiwa imebeba makombora manne ya nyuklia.

Mwaka 2010, Jeshi la Anga la Marekani lilipoteza mawasiliano kwa muda na makombora 50 ya nyuklia, hali iliyozua hofu kubwa ya usalama wa dunia.

Kwa wakati huo, Warusi wengi walipuuza madai ya Yeltsin kwamba alikuwa ameamirisha kifaa cha nyuklia, wakisema ilikuwa ni mbinu ya kisiasa ya kugeuza mawazo ya umma kutoka vita vya Chechnya.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid