Nini kimeibadilisha Man United na kupata matokeo ya kushangaza?

    • Author, Danny Murphy
    • Nafasi, BBC Sport column
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Ushindi wa Jumapili dhidi ya Arsenal ulikuwa ushindi na matokeo mengine ya kushangaza kwa Manchester United, walivutia kwa jinsi walivyoupata ushindi.

Kama ilivyokuwa kwenye ushindi wao wa wiki iliyopita dhidi ya Manchester City, mafanikio haya yalitokana kwa kiasi kikubwa na ukweli kwamba wachezaji wao wakubwa sasa wanaonyesha kiwango chao bora. Kila mmoja alionekana bora Emirates.

Harry Maguire alikuwa bora sana katika safu ya ulinzi, Casemiro alitawala kiungo kwa kutumia uzoefu wake wote, Bruno Fernandes akiwa amerudi katika nafasi yake pendwa ya namba 10 alikuwa na ubora wa kiwango cha juu, na mbele Bryan Mbeumo alikuwa tishio kubwa kwenye kufunga mabao, huku pia akiweza kumiliki mpira na kuwatisha mabeki wa Arsenal kwa kasi na nguvu zake.

United walifunga mabao mawili mazuri, lakini ushindi wao haukutegemea tu ubora wa mtu mmoja mmoja au matukio ya ghafla.

Badala yake, ilikuwa ni juhudi ya timu nzima, na kocha Michael Carrick anastahili sifa kwa kuweza kutengeneza mfumo uliowaunganisha wote.

'Wachezaji wa United wanaendana na mfumo wa United wa sasa'

Kikosi cha kwanza cha United dhidi ya Arsenal kilikuwa kilekile kilichocheza katika mechi ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Manchester City wiki iliyopita.

Watu wengi watafananisha kiwango cha sasa cha United na kile walichokuwa wakicheza chini ya Ruben Amorim, kwa kweli ni kama unatazama timu mbili tofauti kabisa.

Hakuna shaka kuwa motisha na kutoka kwa Carrick imechangia, lakini jambo muhimu zaidi ni kwamba wachezaji wote walionekana kuwa huru na wenye kuelewa vizuri mfumo waliocheza.

Walionekana wenye furaha zaidi, lugha yao ya mwili ilikuwa nzuri, walitaka mpira, na waliaminiana walipokuwa nao. Kulikuwa na kujiamini kunakoonekana wazi.

Sababu ni rahisi, kuwachezesha wachezaji katika mfumo unaowafaa na wanaouelewa huleta tofauti kubwa, jambo ambalo mara nyingi halizungumzwi vya kutosha baada ya matokeo kama haya.

United walicheza kwa mfumo wa 4-2-3-1 au 4-4-1-1, Fernandes akiwa nyuma ya Mbeumo. Amad Diallo na Patrick Dorgu walikuwa tayari kusaidia ulinzi kwa sababu wamewahi kucheza kama wing-back hapo awali.

Hii ilimaanisha kuwa wakati mwingine United walijilinda kwa kutumia wachezaji sita, lakini Diallo na Dorgu walijua bado ni wachezaji wa pembeni timu yao inaposhambulia.

Kila mmoja alijua jukumu lake. Fernandes alishuka kuwasaidia Mainoo na Casemiro, ambao walilinda safu ya ulinzi kwa nidhamu kubwa.

Kwa msingi huo, mpangilio huu uliwawezesha United kujilinda kwa idadi kubwa ya wachezaji, na walipopata nafasi walishambulia kwa kasi kubwa. Kwa wachezaji wao wenye mbio, walikuwa hatari sana.

Kufungwa bao la kutangulia kuliinua ari ya United

Ili kushinda katika Uwanja wa Emirates, nyumbani kwa Arsenal lazima uwe bora sana ukiwa na mpira na pia bila mpira.

Unahitaji kuwa imara kiulinzi ikiambatana na mpangilio mzuri na nidhamu huku kila mmoja akijua wakati gani wa kuizuia Arsenal kucheza.

Lakini pia lazima uwe tayari kushambulia unapopata nafasi, iwe ni kwa mashambulizi ya kushtukiza au kwa kujenga mashambulizi kwa umiliki wa mpira, na unapofika mbele lazima uwe tishio.

United walifanya yote haya tangu mwanzo wa mchezo. Hawakukaa nyuma tu walijaribu kuwapa presha Arsenal na kukabia juu, jambo lililoonekana la ujasiri mkubwa Emirates, lakini lilifanya kazi.

Arsenal walianza mchezo vizuri na walimiliki mpira, na walipoongoza 1-0 kila. tu alidhani wangetawala kabisa mchezo. Lakini badala yake, bao hilo liliwapa ari zaidi United.

Walicheza kwa uhuru zaidi, walikuwa hatari zaidi, na kwa msaada wa makosa ya Arsenal wakarejea tena mchezoni.

Kuanzia Mbeumo alipofunga bao la kusawazisha, United walionekana kujiamini sana. Bao la Dorgu baada ya mapumziko lilikuwa la kushangaza, na kuanzia hapo United walikuwa na kitu cha kulinda huku wakitumia mashambulizi ya kushtukiza.

Nadhani pia Arsenal waliwasaidia kwa kufanya mabadiliko ya wachezaji wanne kwa wakati mmoja, hatua iliyoonekana kama ya hofu kutoka kwa Mikel Arteta. Wakapoteza mpangilio na kasi yao.

Ingawa Mikel Merino alisawazisha bao kupitia kona, United bado walikuwa wakicheza vizuri. Dakika chache kabla ya kipyenga cha mwisho, matokeo yakisomeka sare ya 2-2 ungefikiri ni matokeo mazuri kwa pande zote, lakini United waliendelea kujiamini.

Bao la ushindi la Matheus Cunha lilikuwa la kiwango cha juu kabisa zawadi ya ujasiri ikichangiwa na mbinu zao.

Je, huu ni wakati muhimu kwa Arsenal msimu huu?

Arsenal walianza vizuri sana mchezo dhidi ya United. Hata walipokuwa mbele 1-0, walionekana wakifanya makosa mengi ya "kitoto'.

Ukosefu wao wa utulivu ulishtua, labda kutokana na presha ya kupigania ubingwa.

Nimewahi kupitia hilo mwenyewe. Msimu wa 2001-02 nikiwa Liverpool, tulikaribia ubingwa lakini presha ilizidi kadri msimu ulivyoendelea, na tulishindwa kuhimili.

Hilo linaweza kutokea kwa timu yoyote, hasa ikiwa ni nyumbani na matarajio ni makubwa.

Arsenal bado wanaongoza ligi kwa pointi nne na wana kikosi chenye ubora mkubwa na uzoefu zaidi sasa.

Ndiyo maana naamini watapokea pigo hili kama funzo na watarejea kwa nguvu.

United waliwaonyesha kuwa Arsenal wanaweza kushindwa, lakini huu ulikuwa ni kipigo chao cha kwanza nyumbani msimu huu.

Haimaanishi wataporomoka.

Walihitaji tu mshtuko mdogo na United waliwapa huo.