Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jenerali wa kijeshi wa China ambaye serikali ina wasiwasi naye
Wizara ya Ulinzi ya China imesema imeanzisha uchunguzi dhidi ya Jenerali wa ngazi ya juu zaidi wa kijeshi nchini humo, ikimtuhumu kwa "ukiukaji mkubwa wa nidhamu na sheria."
Wizara haikufichua maelezo mengine yoyote kuhusiana na madai dhidi ya Jenerali Zhang Yaoshia.
Zhang Yaoshia anachukuliwa kuwa mshirika wa karibu wa kijeshi wa Rais Jinping.
Neno "vibaya" hutumiwa sana nchini Uchina kurejelea ufisadi.
Wizara hiyo ilisema afisa mwingine mkuu wa kijeshi, Jenerali Liu Zhenli, pia anachunguzwa.
Anatambulika kama mshiriki wa karibu wa Xi Jinping
Majenerali tisa wa vyeo vya juu walifutwa kazi mwezi Oktoba, ikiwa ni mabadiliko makubwa zaidi ya kijeshi katika miongo ya hivi karibuni.
Zhang, 75, ni makamu mwenyekiti wa Tume Kuu ya Kijeshi ya Chama cha Kikomunisti (CMC), kundi linaloongozwa na Rais Xi Jinping. Ana udhibiti kamili juu ya vikosi vya usalama vya China.
Zhang pia ni mwanachama wa Politburo yenye wanachama 24, chombo cha juu zaidi cha kufanya maamuzi.
Baba yake alikuwa mmoja wa majenerali waanzilishi wa Chama cha Kikomunisti cha China.
Zhang alijiunga na jeshi mwaka wa 1968. Alikuwa mmoja wa viongozi wachache waandamizi waliokuwa na uzoefu wa vita.
Alibakia madarakani hata baada ya umri wa kawaida wa kustaafu katika jeshi la China, jambo linalothibitisha imani ya Rais Jinping kwa Zhang.
Tuhuma zilianza mwezi Desemba
Tangazo hilo linakuja huku kukiwa na uvumi kwamba Zhang na Liu wangechunguzwa baada ya kushindwa kuhudhuria mkutano wa ngazi ya juu wa chama mwezi Desemba.
Tangu aingie madarakani, Rais Jinping ameanzisha kampeni kubwa ya kupambana na rushwa katika sekta nyingi, hivi majuzi ikilenga jeshi.
Xi Jinping alitaja ufisadi kuwa "tishio kubwa" kwa Chama cha Kikomunisti, akisema vita dhidi ya ufisadi ni vikali.
Wakati wafuasi wa serikali wakisema kuwa uchunguzi wa ufisadi unachangia katika utawala bora, wengine wanaona ni chombo cha kuwaondoa wapinzani wa kisiasa.
Kwa kufunguliwa kwa uchunguzi kuhusu Zhang na Liu, idadi ya wanachama katika CMC imepungua zaidi.
Kutoka kwa wajumbe saba, ni Mwenyekiti Xi Jinping na Zhang Shengmin tu, ambaye anasimamia nidhamu ya kijeshi, wamesalia.