Kwa nini hakuna nchi ya Amerika Kusini iliyo na silaha za nyuklia?

    • Author, Angel Bermudez*
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Katika nusu ya pili ya karne ya 20, wanadamu waliishi na hofu ya uwezekano wa maangamizi makubwa kutokana na silaha za nyuklia.

Hofu ya kutokea makabiliano ya silaha za nyuklia kati ya Marekani na Umoja wa Kisovieti, ilichangiwa na wasiwasi wa kuenea kwa silaha za nyuklia, na hilo lingeweza kusababisha nchi nyingine zaidi, au mashirika ya kigaidi kupata silaha hizo.

Ili kujaribu kuzuia uwezekano huu, utawala wa Rais wa Marekani Dwight Eisenhower ulizindua mpango wa "Atoms for Peace" mwaka 1953, ambao ulilenga kufanikisha matumizi ya nyuklia kwa matumizi ya amani kwa nchi ambazo zilikataa kutumia nyuklia kuunda bomu.

1957, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) liliundwa kama sehemu ya shirika la Umoja wa Mataifa; na zaidi ya miaka kumi baadaye, mwaka 1968, Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia (NPT) ulianzishwa ili kushughulikia tishio hili.

Mipango hii, hata hivyo, haijafaulu kuzuia nchi nyingine kutengeneza silaha za nyuklia duniani.

Marekani na Urusi (mrithi wa mwisho wa Soviet) na nchi za Ulaya (Uingereza na Ufaransa); katika Asia (China, Korea Kaskazini, India, na Pakistan); katika Mashariki ya Kati (Israel, ingawa haijakiri rasmi kuwa na bomu la nyuklia); na hata Afrika (Afrika Kusini, ambayo ndiyo nchi pekee iliyotengeneza bomu hilo na kisha kuliondoa kwa hiari).

Kwa hivyo, mataifa katika kila bara la dunia yana au yaliwahi kuwa na silaha za nyuklia, isipokuwa: Amerika ya Kusini. Na hili halikutokea kwa bahati mbaya, kuna sababu.

Pia unaweza kusoma

Mzozo wa makombora ya Cuba

"Sababu ya Amerika Kusini kutokuwa na silaha za nyuklia inaanza wakati wa mzozo wa makombora ya Cuba Oktoba 1962, wakati Umoja wa Kisovieti ulipoweka makombora Cuba, na kusababisha mgogoro kati ya Marekani na Umoja wa Kisovieti," anasema Luis Rodríguez, mtafiti wa masuala ya Usalama na Ushirikiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Stanford (CISAC).

"Nchi kadhaa za Amerika ya Kusini ziliamua kuanza kuunda mpango ili kuzuia mzozo mwingine wa makombora katika eneo hilo. Hii ni mara ya kwanza kwa nchi za Amerika ya Kusini kuona hatari za nyuklia karibu na nyumbani," mtaalam huyo anaongeza.

Rodríguez anaeleza kwamba tangu mwishoni mwa miaka ya 1950, hoja iliibuka ya kuzuia nchi nyingine kufanya yale ambayo Marekani iliyafanya Hiroshima. Huko Ulaya, Ireland ilikuwa mojawapo ya nchi zilizoibua wazo hili, na Amerika ya Kusini, ilikuwa ni Costa Rica.

Mgogoro wa makombora ulitatuliwa kwa njia ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Washington na Moscow, lakini nchi nyingi za Amerika ya Kusini ziliona kuundwa kwa eneo lisilo na silaha za nyuklia kama njia ya kuzuia mgogoro kama huo kutokea katika siku zijazo.

Kwa hivyo, kanda hiyo ilianza mchakato wa mazungumzo ambayo yalifikia kilele Februari 1967 na kuundwa kwa Mkataba wa Tlatelolco, ambao unakataza maendeleo, upatikanaji, majaribio, na kupeleka silaha za nyuklia Amerika ya Kusini na caribbean.

Mkataba huu ulianza kutekelezwa mwaka 1969, lakini haukumaliza hatari ya kuenea kwa nyuklia katika eneo hilo, kwani mataifa mawili katika eneo hilo yalisita kuukubali kikamilifu mkataba huo.

Brazil na Argentina

Ingawa Brazil ilikuwa mojawapo ya nchi za awali kutaka eneo lisiwe na silaha za nyuklia, lakini ilibadilisha msimamo wake juu ya suala hilo, na kukabidhi uongozi kwa Mexico.

Juhudi za Mexico zilisababisha mkataba huo kupewa jina la Tlatelolco, makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Mexico wakati huo, na kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwanadiplomasia wa Mexico, Alfonso García Robles mwaka 1982.

Luis Rodríguez anaeleza kwamba wakati huo, iliaminika kwamba nishati ya nyuklia ingeweza kuwa chombo cha kuharakisha maendeleo ya nchi za Amerika ya Kusini na vinu vya nyuklia vingeweza kutumiwa kuendesha migodi, mifereji, au hata kwa miradi ya kuzalisha umeme kwa maji.

"Hilo ndilo lililopelekea nchi kama Brazili na Argentina kubuni baadhi ya programu za teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya kiraia au kijeshi, ambazo zlisababisha mvutano fulani, hasa na mashirika ya kimataifa," anasema Rodríguez.

Lakini hakuna ushahidi kwamba serikali za Argentina na Brazil zilikuwa na mipango ya kutengeneza silaha za nyuklia, ingawa kuna dalili kwamba kulikuwa na watu ndani ya serikali zao ambao waliunga mkono uwezekano huu.

Lakini mwanzoni mwa miaka ya 1990, nchi zote mbili ziliweka kando haki yao ya kutumia nyuklia kwa miradi ya kiraia, na kuamua kijiunga kikamilifu na Mkataba wa Tlatelolco, na baadaye zilijiunga na Mkataba wa Kuzuia Uenezi wa Nyuklia.

Sababu nyingine

Mbali na athari za mzozo wa makombora ya Cuba, mambo mengine yalichangia nchi za Amerika ya Kusini kutokuwa na silaha za nyklia.

Ryan Musto, mkurugenzi wa jukwaa la utafiti katika taasisi ya Global Research ya chuo kikuu cha William and Mary, Virginia, Marekani, anasema, eneo hilo halikuwa na aina ya ushindani mkali na migogoro kama iliyotokea katika sehemu nyingine za dunia.

"Ndiyo, Brazil na Argentina ni wapinzani, lakini hilo halikufikia hatua ya kuwa na mzozo mkali wa kusababisha mashindano ya silaha. Kwa ujumla, Amerika ya Kusini inaonekana kuwa eneo lenye utulivu linapokuja suala la migogoro baina ya mataifa," mtaalam huyo anabainisha.

Jambo lingine lililochangia haswa katika kesi ya Brazil na Argentina ni kwamba nchi zote mbili zilipitia mpito wa demokrasia katikati ya miaka ya 1980.

Gharama kubwa ya mpango wa silaha za nyuklia pia inaweza kuwa sababu nyingine.

"Kutengeneza silaha za nyuklia ni gharama sana. Inahitaji kiasi kikubwa cha miundombinu, wataalam wengi, na ujuzi mwingi ili kuweza kutekeleza mpango huu," anasema Luis Rodríguez.

Gharama hii kubwa inapimwa si tu kwa kiasi cha fedha kinachohitajika kwa ajili ya mpango wa silaha za nyuklia, bali pia gharama za kidiplomasia na kwenda kinyume na makubaliano ya jumuiya ya kimataifa dhidi ya kuenea kwa silaha za nyuklia na kupoteza fursa ya kuwa na matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.

Kwa hivyo, ilifika hatua ambapo nchi zote mbili ziliona faida na fursa kubwa zaidi ikiwa zitaunganishwa katika taasisi za kimataifa zinazodhibiti matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia kuliko kama zingejaribu kushikilia kutumia nyuklia wao wenyewe.