Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi Uganda 2026: Watu 7 wauawa katika ghasia za baada ya uchaguzi, polisi wasema
Msemaji wa polisi wa eneo hilo, Lydia Tumushabe, amepinga kauli hizo akisisitiza kuwa polisi walilazimika kutumia nguvu kwa kujilinda baada ya kile alichokitaja kama shambulio la “kundi la wahuni wa chama cha NUP” dhidi ya kituo cha polisi.
Muhtasari
- Raia wa Uganda na Iran wageukia Bitchat, intaneti ikiminywa na mamlaka
- Marekani yatoa tahadhari ya kiusalama kwa raia wake wanaoishi Uganda
- Watu 7 wauawa katika ghasia za baada ya uchaguzi wa Uganda, polisi wasema
- Kada wa chama cha Upinzani Uganda ashinda ubunge akiwa mahabusu
- Kenya yawatahadharisha raia kushiriki mashindano ya "kukumbatia miti" kwa muda mrefu
- Shirika la haki za binadamu yatilia shaka uwazi wa matokeo ya awali ya uchaguzi Uganda
- Nyumba ya Bobi Wine yazingirwa kijeshi, Museveni aongoza kwa 76%
- Marekani yakosoa Afrika Kusini kwa kushiriki mazoezi ya baharini na Iran
- Marekani yaambia UN chaguzi zote ziko wazi kuzuia mauaji Iran
- Rais wa zamani wa Korea Kusini Yoon apatikana na hatia ya kutumia vibaya madaraka
- Raia wa Uganda kufahamu rais waliemchagua siku ya Jumamosi
- Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Venezuela amkabidhi Trump Tuzo yake
- Mamlaka Iran yadai pesa nyingi kwa ajili ya kurejesha miili ya waandamanaji, BBC yafahamishwa
- Samia ahurumia wanadiplomasia baada ya kufungwa kwa mtandao wakati wa Uchaguzi
- Uchaguzi Uganda 2026: Museveni achukua uongozi wa mapema wa kura zilizohesabiwa kufikia sasa
Moja kwa moja
Asha Juma & Mariam Mjahid
Raia wa Uganda na Iran wageukia Bitchat, intaneti ikiminywa na mamlaka
Kuminywa kwa huduma za intaneti kunakotekelezwa na serikali za Iran na Uganda kumezalisha shinikizo kwa raia wao kutafuta mbinu mbadala za mawasiliano, hali iliyochangia kuongezeka kwa matumizi ya mtandao wa Bitchat.
Mtandao huo, unaomilikiwa na mwanzilishi mwenza wa Twitter, Jack Dorsey, hauhitaji intaneti wala kadi ya simu ili kuwaunganisha watumiaji.
Badala yake, unatumia teknolojia ya Bluetooth kuruhusu ujumbe kusambazwa kutoka simu moja hadi nyingine hadi kufikia mlengwa anayekusudiwa.
Bitchat ilizinduliwa rasmi mwezi Julai 2025 na imekuwa suluhisho muhimu katika maeneo yasiyo na mawimbi ya intaneti au katika nchi ambako serikali zimezuia au kudhibiti upatikanaji wa huduma hiyo.
Mwaka huu pekee, programu hiyo imepakuliwa mara 28,000, idadi inayoashiria kukumbatiwa kwa kiwango kikubwa na watumiaji.
Nchini Uganda, kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, aliwahimiza wafuasi wake kupakua Bitchat, akionya kuwa hatua ya serikali ya kuminyia intaneti ingewanyima fursa ya kufuatilia matokeo ya uchaguzi na maendeleo ya kisiasa kwa wakati.
Vilevile, Bitchat imepata umaarufu mkubwa miongoni mwa waandamanaji nchini Iran, ambako serikali imekuwa ikikata au kudhibiti intaneti ili kudhibiti maandamano yaliyoendelea kwa zaidi ya wiki moja.
Katika mazingira hayo, programu hiyo imekuwa nyenzo muhimu ya mawasiliano na uratibu miongoni mwa waandamanaji.
Kwa ujumla, mwenendo wa kuminywa kwa intaneti unaendelea kuongezeka duniani.
Kwa mujibu wa ripoti za mashirika ya haki za kidijitali Access Now na KeepItOn Coalition, visa 296 vya kufungiwa au kudhibitiwa kwa intaneti vilirekodiwa katika mataifa 54 mwaka 2024, ongezeko kubwa ikilinganishwa na visa 78 vilivyoripotiwa mwaka 2016.
Pia unaweza kusoma:
Marekani yatoa tahadhari ya kiusalama kwa raia wake wanaoishi Uganda
Ubalozi wa Marekani umetangaza kiwango cha 3 cha tahadhari ya usafiri kwenda Uganda ikimaanisha kuwa ina shauriwa kuepuka safari zisizo za lazima kuelekea nchini humo.
Aidha wameeleza kuwa inaripotiwa vikosi vya usalama vinatumia gesi za kuwasha kutawanya wanaokusanyika na kuwahimiza raia wake kuepuka mikusanyiko ya watu na maandamano na kuendelea kufuatilia taarifa za vyombo vya habari vya ndani.
Taarifa hiyo imetolewa kwenye tovuti ya ubalozi huo na kuwashauri raia wake kudumisha tahadhari binafsi, kuwa makini na mazingira yanayowazunguka, na kubeba simu za mkononi zenye chaji pamoja na namba za dharura.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, raia wa Marekani wanaotaka msaada wameelekeza utaratibu wa kufuata.
''Wale wanaohitaji msaada wasiliana na Ubalozi wa Marekani kwa maelekezo zaidi'', yasema taarifa hiyo.
Raia wa Marekani pia wamehimizwa kubeba vitambulisho halali wakati wote, ikiwemo pasipoti ya Marekani yenye visa halali ya Uganda.
Hata hivyo, Serikali ya Marekani imewahakikishia itafuatilia kwa karibu hali ya usalama nchini Uganda na kutoa taarifa zaidi kadri itakavyohitajika.
Haya yanajiri baada ya ripoti kuibuka watu saba wameuawa usiku wa Uchaguzi nchini humo walipokuwa wamekusanyika wakifuatilia matokeo yanayotangazwa.
Tume ya Uchaguzi ilitangaza Ijumaa mchana kuwa, kwa kuzingatia matokeo kutoka asilimia 60 ya vituo vya kupigia kura, Rais Museveni alikuwa anaongoza kwa asilimia 75 ya kura zote zilizohesabiwa, akifuatiwa na kiongozi wa upinzani Bobi Wine kwa asilimia 21.
Hadi sasa, matokeo rasmi ya uchaguzi huo bado hayajatangazwa.
Soma Pia:
Watu 7 wauawa katika ghasia za baada ya uchaguzi wa Uganda, polisi wasema
Takribani wafuasi saba wa upinzani nchini Uganda wameuawa katika vurugu zilizotokea usiku kucha katika mazingira yanayozua mabishano makubwa ya kisiasa, wakati Rais Yoweri Museveni akiongoza kwa kiwango kikubwa katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais uliofanyika Alhamisi.
Kwa mujibu wa upinzani, wafuasi wao walishambuliwa na vikosi vya usalama walipokuwa wamekusanyika katika makazi ya mbunge wa upinzani Muwanga Kivumbi huko Butambala, takribani kilomita 55 kusini-magharibi mwa mji mkuu Kampala.
Hata hivyo, polisi wamekanusha madai hayo na badala yake kuilaumu upinzani kwa kuchochea vurugu.
Tume ya Uchaguzi ilitangaza Ijumaa mchana kuwa, kwa kuzingatia matokeo kutoka asilimia 60 ya vituo vya kupigia kura, Rais Museveni alikuwa anaongoza kwa asilimia 75 ya kura zote zilizohesabiwa, akifuatiwa na kiongozi wa upinzani Bobi Wine kwa asilimia 21.
Akizungumza na shirika la habari la AFP, Mbunge Muwanga Kivumbi alisema askari na polisi walifyatua gesi ya kutoa machozi na baadaye risasi za moto dhidi ya mamia ya watu waliokuwa wakifuatilia matokeo ya awali katika makazi yake.
Alidai kuwa watu kumi waliuawa ndani ya nyumba yake.
Madai hayo yalithibitishwa na mwanaharakati wa haki za binadamu, Agather Atuhaire, katika mazungumzo na shirika la habari la Reuters.
Hata hivyo, msemaji wa polisi wa eneo hilo, Lydia Tumushabe, amepinga kauli hizo akisisitiza kuwa polisi walilazimika kutumia nguvu kwa kujilinda baada ya kile alichokitaja kama shambulio la “kundi la wahuni wa chama cha NUP” dhidi ya kituo cha polisi, pamoja na mpango wa kuvamia kituo cha kujumlisha kura.
Alidai kuwa washambuliaji walikuwa wamejihami kwa mapanga, mashoka na vifaa vya kuwasha moto, na kwamba angalau watu saba walipoteza maisha.
Wakati huohuo, waandishi kadhaa wa habari wa ndani wameripoti kuzuiwa na vikosi vya usalama kufika katika makazi ya kiongozi wa upinzani Bobi Wine, yaliyoko eneo la Magere, Kampala.
Chama cha NUP kilidai kupitia mtandao wa X kuwa maafisa wa usalama walivuka uzio wa makazi hayo kinyume cha sheria na kuanza kuweka mahema ndani ya kiwanja chake.
Kwa upande wake, msemaji wa polisi Kituuma Rusoke aliambia kituo cha televisheni cha NBS kuwa Bobi Wine, kama mgombea wa urais, alikuwa “mtu wa kuzingatiwa,” akiongeza kuwa uwepo mkubwa wa vikosi vya usalama katika eneo la makazi yake ulikuwa ni kwa lengo la kuhakikisha usalama wake binafsi.
Tukio hili limeongeza mvutano wa kisiasa nchini Uganda, huku mashirika ya haki za binadamu na wadau wa demokrasia wakitaka uchunguzi huru na wa haraka kuhusu vifo na matumizi ya nguvu katika kipindi cha uchaguzi.
Soma Pia:
Kada wa chama cha Upinzani Uganda ashinda ubunge akiwa mahabusu
Msemaji wa chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP) nchini Uganda, Alex Waiswa Mufumbiro, ameshinda ubunge.
Katika uchaguzi wa ubunge wa Jimbo la Nakawa Mashariki uliofanyika jana, tarehe 15 Januari 2026, wananchi wa jimbo hilo walimchagua kuwa mbunge wao kupitia chama cha National Unity Platform (NUP).
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uganda, matokeo ya uchaguzi yanaonyesha kuwa Mufumbiro aliwashinda wagombea wote waliokuwa katika kinyang’anyiro hicho, akipata asilimia 78 ya kura zote halali zilizopigwa.
Ushindi huo umetangazwa rasmi akiwa bado kizuizini, hali iliyowashangaza wengi, hasa ikizingatiwa kuwa hakufanya kampeni yoyote kutokana na kuwepo gerezani.
Mfumbiro, alitekwa nyara mwaka jana, 2025, akiwa nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kawempe, Kampala, alipokuwa amekwenda kuhudhuria kesi ya Eddie Mutwe, ambaye ni mkuu wa ulinzi wa kiongozi wa NUP, Bobi Wine.
Baada ya tukio hilo, Alex Waiswa Mufumbiro aliunganishwa katika kesi moja na Eddie Mutwe, na wote wawili wakazuiliwa katika Gereza la Luzira, Kampala.
Tangu wakati huo, hawajawahi kuachiwa huru.
Kufikia sasa, Mufumbiro amekaa kizuizini kwa takribani siku 78.
Ushindi wa Alex Waiswa Mufumbiro umetafsiriwa na wachambuzi wa siasa na wananchi wengi kama ishara ya imani kubwa ya wapiga kura wa Nakawa Mashariki, pamoja na ujumbe mzito wa kisiasa kuhusu hali ya demokrasia na haki za kisiasa nchini Uganda.
Soma zaidi:
Kenya yawatahadharisha raia kushiriki mashindano ya “kukumbatia miti” kwa muda mrefu
Wizara ya Afya nchini Kenya imeibua wasiwasi juu ya mwelekeo unaoibuka wa watu kushiriki katika shughuli za kukumbatia miti kwa muda mrefu, huku ripoti zikionyesha kuwa baadhi ya washiriki wamepatwa na matatizo ya kiafya yaliyozidi kiasi cha kuhitaji kupelekwa hospitalini.
Akihutubia wakazi wa Ngiriambu, Jimbo la Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga, nchini humo, Katibu Mkuu wa Afya ya Umma, Mary Muthoni, alisema kwamba watu wanapaswa kufanya vipimo vya afya vya kina kabla ya kushiriki katika shughuli zinazohitaji nguvu za mwili, ili kubaini hali za kiafya zinazoweza kuhatarisha maisha yao.
Muthoni aliongeza kuwa shughuli zinazojulikana kuwa haziwezi kuwa hatari zinaweza kuwa hatari ikiwa mtu hajajiandaa ipasavyo, na kuwa wale wanaokusudia kushiriki mazoezi yanayohitaji nguvu nyingi wanapaswa kuhakikisha wako tayari vizuri na wamefanya mazoezi ya awali kabla ya kushiriki.
Awali kuna watu kadhaa nchini humo waliojaribu kukumbatia mti na kuanguka kwa sababu za kiafya.
Haya yanajiri baada ya msichana mwenye umri wa miaka 21, Truphena Muthoni kuvunja rekodi yake mwenyewe na kuweka rekodi mpya duniani kwenye Guinness World Record kwa kukumbatia mti kwa muda mrefu zaidi, saa 72 (yaani kwa siku tatu mfululizo).
Rekodi yake ya awali ilikuwa saa 48.Alisema amechagua njia hiyo ya maandamano kupinga ukataji ovyo wa miti na uharibifu wa misitu.
Ni hatua ambayo ilimpa umaarufu mkubwa hata katika rubaa za kimataifa na hadi kukabidhiwa cheo cha mazingira na Rais William Ruto.
Soma pia:
Shirika la haki za binadamu yatilia shaka uwazi wa matokeo ya awali ya uchaguzi Uganda
Shirika la haki za binadamu, Human Rights Defender, limeonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu uwazi wa matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais.
Kwenye taarifa yake ya mtandao wa X, Human Rights Defender imeeleza:
“Ukosefu wa ufuatiliaji na kutokueleza ni wilaya zipi matokeo yanatoka unasababisha wasiwasi mkubwa na unachochea madai ya hila ya kisiasa. Tunawataka waangalizi wa uchaguzi kuhakikisha wanarekodi na kuripoti kila tukio la ukosefu wa utaratibu kwa wakati halisi.”
Wakati huo huo, Mweka hazina wa chama hicho, Benjamin Katana, pia amekosoa Tume ya Uchaguzi (EC) kwa kutangaza matokeo bila kueleza vituo vya kupigia kura ni vipi vilivyowasilisha matokeo hayo.
Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi Uganda EC Yoweri Museveni anaongoza kwa asilimia 76%.
Iwapo Museveni atashinda aitakuwa ni muhula wa saba akiwa madarakani.
Inaaminika kuwa anapendelea mtoto wake wa kiume ambaye ni mkuu wa majeshi Uganda Muhoozi Kainerugaba kumrithi, hata hivyo alikana kuwa anamfunza mikoba ya uongozi.
Matokeo ya Urais kutangazwa Jumamosi ya tarehe 16 Januari 2026.
Soma pia:
Nyumba ya Bobi Wine yaripotiwa kuzingirwa kijeshi, Museveni aongoza kwa 76%
Nyumba ya mgombea urais wa NUP, Robert Kyagulanyi, yaripotiwa kuwa imezingirwa, kwa mujibu wa maafisa wa NUP.
''Nyumba ya Bobi Wine imezingirwa tangu jana jioni, hawezi kuwasiliana na mawakala wake wa uchaguzi. Iwapo amefanya kosa anapaswa kushtakiwa,kufikishwa mahakamani na utaratibu wa kesi uanze kulingana na sheria. Nyumba yake haijarasimishwa kuwa ni kizuizi'' anasema Mweka hazina wa NUP, Benjamin Katana.
Hata hivyo, msemaji wa polisi Kituuma Rosoke amewaambia wanahabari kuwa hana ufahamu kuwa Kyagulanyi amezuiwa kama inavyodaiwa na chama chake.
Mnamo mwaka 2021, katika uchaguzi mkuu Bobi Wine alishikiliwa na majeshi nyumbani kwake. Aliibuka wa pili na kura asilimia 35%. Ni hatua hiyo ambayo Marekani waliikemea wakitaja uchaguzi haukuwa wa hakina wazi, dai ambalo mamlaka za Uganda zilikanusha.
Haya yanajiri, huku matokeo ya uchaguzi mkuu yakiendelea kutangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Uganda, ikimuonyesha Museveni anaongoza kwa asilimia 76 ya kura zilizohesabiwa kutoka vituo vya kupigia kura 22,758.
Kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotangazwa mapema leo, Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine anamfuata kwa nyuma na kura 1,312,047 zikiwa ni asilimia 19.85% za kura zilizohesabiwa.
"Matukio ya masanduku kujazwa kura yameripotiwa kila mahali," alidai mgombea wa urais wa chama cha upinzani cha NUP Ssentamu Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii, bila kutoa uthibitisho madai hayo.
Mamlaka inayosimamia uchaguzi huo haijatoa kauli yoyote kuhusu madai ya udanganyifu katika uchaguzi, wala madai ya Bobi Wine kwamba mawakala "wengi" wa wapiga kura na wasimamizi wa chama chake cha NUP "walitekwa nyara, na wengine kufukuzwa katika vituo vya kupigia kura".
Wakati huo huo, Mweka hazina wa chama hicho, Benjamin Katana, pia amekosoa Tume ya Uchaguzi (EC) kwa kutangaza matokeo bila kueleza vituo vya kupigia kura ni vipi vilivyowasilisha matokeo hayo.
Matokeo rasmi ya uchguzi wa urais yatatangazwa jumamosi ya tarehe 17 Januari 2026.
Soma Pia:
Marekani yakosoa Afrika Kusini kwa kushiriki mazoezi ya baharini na Iran
Marekani imeonyesha upinzani wake dhidi ya uamuzi wa Afrika Kusini kushiriki katika zoezi la kijeshi la majini la kimataifa linalohusisha Iran, ikiielezea Tehran kama “mhusika anayevuruga utulivu wa kimataifa na mfadhili wa ugaidi.”
Marekani imeonya kuwa ushiriki wa Iran katika zoezi hilo unatishia usalama wa kikanda na wa baharini.
Kupitia taarifa rasmi, Ubalozi wa Marekani nchini Afrika Kusini ulisema Washington ilipokea kwa “wasiwasi mkubwa na hofu” taarifa kuwa Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini pamoja na Jeshi la Ulinzi la Taifa la Afrika Kusini (SANDF) waliendelea kuruhusu ushiriki wa Iran katika mazoezi hayo yanayoendelea, licha ya madai kuwa kulikuwa na maelekezo ya serikali yaliyopinga hatua hiyo.
Ubalozi huo ulisisitiza kuwa kuijumuisha Iran katika mazoezi ya pamoja ya kijeshi, kwa namna yoyote ile, kunadhoofisha usalama wa baharini na uthabiti wa kikanda.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa ni jambo “lisilokubalika kimaadili” kwa Afrika Kusini kuwapokea wanajeshi wa Iran wakati ambapo, kwa mujibu wa Marekani, mamlaka za Iran zinaendelea kuwanyanyasa raia wake kwa kuwapiga risasi, kuwafunga gerezani na kuwatesa wale wanaoshiriki shughuli za kisiasa kwa amani.
Aidha, ubalozi huo uliikosoa sera ya kigeni ya Afrika Kusini, ukidai kuwa nchi hiyo haiwezi kudai kusimamia misingi ya haki na usawa kimataifa huku ikiimarisha uhusiano na Iran.
Ubalozi uliongeza kuwa kuruhusu vikosi vya kijeshi vya Iran kufanya shughuli katika maji ya Afrika Kusini, au kuonyesha mshikamano wa kisiasa na Tehran, kunavuka mipaka ya sera ya kutofungamana na upande wowote.
“Hatua hii ni sawa na kuchagua kusimama upande wa utawala unaowakandamiza raia wake kwa ukatili na kujihusisha na vitendo vya kigaidi,” taarifa hiyo ilisema.
Malalamiko haya ya kidiplomasia yanajiri wakati Afrika Kusini ikiandaa Zoezi la WILL FOR PEACE 2026, zoezi la kimataifa la majini linalohusisha majeshi ya wanamaji kutoka China, Urusi, Iran na Afrika Kusini, huku China ikiwa kiongozi wa zoezi hilo.
Zoezi hilo lilianza rasmi tarehe 10 Januari 2026 kwa gwaride la ufunguzi lililofanyika katika mji wa Simon’s Town, likiashiria mwanzo wa shughuli za pamoja zinazofanyika katika maeneo ya mafunzo na katika maji ya eneo la Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa Jeshi la Afrika Kusini, zoezi hilo linalenga kuziunganisha nchi wanachama wa 'BRICS Plus' katika kuimarisha usalama wa baharini, kuongeza uwezo wa kufanya kazi kwa pamoja, na kuendeleza ushirikiano wa kijeshi wa kimataifa.
Brics iliundwa kutafuta njia za kuleta mageuzi katika taasisi za fedha za kimataifa kama vile IMF na Benki ya Dunia, ili kuunda "sauti kubwa na uwakilishi" kwa mataifa yanayoibukia kiuchumi.
Hadi sasa, Afrika Kusini haijatoa majibu ya kina hadharani kuhusu ukosoaji wa Marekani, ingawa maafisa wake wamewahi kusisitiza kuwa mazoezi ya aina hiyo yanaendana na sera ya nchi ya kutofungamana na upande wowote pamoja na dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano wa kimataifa.
Pia unaweza kusoma:
Marekani yaambia UN chaguzi zote ziko wazi kuzuia mauaji Iran
Rais Donald Trump "ameweka wazi kuwa chaguzi zote ziko wazi kuzuia mauaji yanayoendelea Iran na kuongeza kuwa iko pamoja na "watu jasiri wa Iran", Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Mike Waltz aliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi.
Trump ametishia mara kwa mara kuingilia kati kuwaunga mkono waandamanaji nchini Iran, ambapo maelfu ya watu wameripotiwa kuuawa katika msako mkali dhidi ya waandamanaji wanaopinga utawala wa kidini.
Lakini siku ya Alhamisi, Trump alitangaza kuwa amearifiwa kwamba mauaji hayo yamesitishwa na kwamba anaamini kuwa sasa hivi hakuna mpango wa kutekeleza mauaji makubwa.
Waltz alipuuza madai ya Iran kwamba maandamano hayo ni "njama ya nchi za kigeni kuchochea kuchukuliwa kwa hatua za kijeshi."
Kwa upande wake, naibu Balozi wa Umoja wa Mataifa wa Iran, Gholamhossein Darzi, alisema Iran haitafuti ongezeko la mzozo au mapambano na akamshutumu Waltz kwa kutumia "uongo, upotoshaji wa ukweli, na kampeni ya makusudi ya kutoa taarifa potofu ili kuficha ushiriki wa moja kwa moja wa nchi yake katika kusababisha machafuko nchini Iran na vurugu."
"Hata hivyo, kitendo chochote cha uchokozi - cha moja kwa moja au kisicho cha moja kwa moja - kitakabiliwa na jibizo kali, na halali," aliambia Baraza la Usalama. "Hili si tishio; ni taarifa ya uhalisia wa kisheria."
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia aliishutumu Marekani kwa kuitisha Baraza la Usalama kwa lengo la "kuhalalisha uchokozi wa wazi na kuingilia mambo ya ndani ya nchi huru" na vitisho vya "kutatua tatizo la Iran kwa njia inayopenda: kupitia mashambulizi yanayolenga kupindua utawala usiotakikana."
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anahimiza "kujizuia kwa kiwango cha juu kipindi hiki na kuwataka wahusika wote kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha vifo zaidi au kuchochea ongezeko kubwa la machafuko kikanda," afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa Martha Pobee aliambia baraza hilo.
Soma zaidi:
Rais wa zamani wa Korea Kusini Yoon apatikana na hatia ya kutumia vibaya madaraka
Rais aliyeondolewa madarakani wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol amepatikana na hatia ya kutumia vibaya madaraka na kughushi nyaraka kuhusu jaribio lake la sheria ya kijeshi lililoshindwa mwaka 2024.
Mahakama ya Seoul sasa inajadili kama pia alizuia utekelezaji wa haki kwa kukwepa kukamatwa. Waendesha mashtaka wameomba ahukumiwe kifungo cha miaka 10 jela kwa mashtaka haya.
Hii ni hukumu ya kwanza kati ya hukumu nne zilizotolewa katika kesi zilizohusishwa na amri yake ya kushangaza ya sheria ya kijeshi.
Ingawa ilikuwa ya muda mfupi, hatua hiyo iliiingiza nchi katika msukosuko, na kusababisha maandamano huku wabunge wakikimbilia bungeni ili kubatilisha uamuzi wa Yoon.
Uamuzi wa Ijumaa unatoa vidokezo kuhusu jinsi kesi zingine za Yoon zinavyoweza kwenda.
Mashtaka yanaanzia matumizi mabaya ya madaraka hadi ukiukaji wa sheria za kampeni.
Soma zaidi:
Raia wa Uganda kufahamu rais waliemchagua siku ya Jumamosi
Tume ya uchaguzi Uganda (EC) imeahidi kufuata katiba kwa kumtangaza mshindi wa matokeo ya uchaguzi ndani ya saa 48 kulingana na kifungu cha 103 (5) cha katiba ya mwaka 1995.
Jaji Simon Byabakama ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi alisema rais atatangazwa Jumamosi kabla ya saa kumi na moja jioni.
Alishukuru raia wa Uganda waliojitokeza kuchagua viongozi wao na kutimiza haki yao ya kikatiba na kusisitiza kuwa kila raia wa Uganda aliyetimiza miaka 18 ana haki ya kupiga kura.
Jaji Byabakama pia alishukuru raia kwa kudumisha amani siku ya uchaguzi na kuwarai k wagombea na wafuasi wao kuendelea kuwa na subira wakati matokeo ya uchaguzi yanaendelea kupokelewa kutoka vituo vya kupiga kura.
Shughuli ya upigaji kura ilikumbwa na changamoto kutokana na mashine za kupiga kura kushindwa kufanya kazi na kulazimu vituo vingi kuanza upigaji kura kuchelewa.
Soma zaidi:
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Venezuela amkabidhi Trump Tuzo yake
Kiongozi wa upinzani wa Venezuela María Corina Machado anasema kwamba amemkabidhi Rais Donald Trump Tuzo yake ya Amani ya Nobel katika mkutano wa faragha wa Ikulu ya White House siku ya Alhamisi.
"Nadhani leo ni siku ya kihistoria kwetu Wavenezuela," alisema baada ya kukutana na Trump, mara ya kwanza wawili hao kukutana ana kwa ana.
Hili linatokea wiki kadhaa baada ya vikosi vya Marekani kumkamata Rais wa Venezuela Nicolás Maduro huko Caracas na kumshtaki katika kesi ya biashara haramu ya dawa za kulevya.
Trump alitoa shukrani zake katika chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii, akisema hatua hiyo ilikuwa "ishara nzuri ya kuheshimiana".
Rais wa Marekani amekataa kumuunga mkono Machado, ambaye harakati zake zilidai ushindi katika uchaguzi wa 2024 uliokuwa na ushindani mkubwa, kama kiongozi mpya wa Venezuela.
Pia unaweza kusoma:
Mamlaka Iran yadai pesa nyingi kwa ajili ya kurejesha miili ya waandamanaji, BBC yafahamishwa
Familia za watu waliouawa katika maandamano nchini Iran zimeiambia BBC kwamba mamlaka zinadai kiasi kikubwa cha pesa ili kurejesha miili yao kwa ajili ya mazishi.
Vyanzo vingi vimeiambia BBC Persian kwamba miili inashikiliwa katika vyumba vya kuhifadhia maiti na hospitali na kwamba vikosi vya usalama havitawaachilia hadi jamaa zao watakapotoa pesa.
Takriban watu 2,435 wameuawa katika maandamano ya zaidi ya wiki mbili kote nchini.
Familia moja katika mji wa kaskazini wa Rasht iliambia BBC kwamba vikosi vya usalama vilidai dola milioni 700 za Marekani ($5,000; £3,700) ili kuachilia mwili wa mpendwa wao.
Mwili huo unashikiliwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Poursina, pamoja na miili mingine ya waandamanaji isiopungua 70, walisema.
Wakati huo huo huko Tehran, familia ya mfanyakazi wa ujenzi wa msimu wa Kikurdi ilienda kuchukua mwili wake, lakini wakaambiwa lazima walipe bilioni moja ya dola ($7,000; £5,200) ili kuupokea.
Familia hiyo iliiambia BBC kwamba hawakuweza kumudu ada hiyo na walilazimika kuondoka bila mwili wa mwana wao. Mfanyakazi wa ujenzi nchini Iran kwa kawaida hupata chini ya $100 kwa mwezi.
Katika baadhi ya matukio, wafanyakazi wa hospitali wamewapigia simu jamaa za waliofariki ili kuwapa onyo mapema, waje kuchukua miili ya wapendwa wao kabla ya vikosi vya usalama kudai fedha zozote.
BBC Persian imeambiwa kuhusu mwanamke - ambaye hatujamtambulisha kwa usalama wake - ambaye hakujua mumewe aliuawa hadi alipopokea simu mnamo Januari 9 kupitia simu yake kutoka kwa wafanyakazi wa hospitali.
Walimwambia aje haraka kuchukua mwili wa mume wake kabla ya vikosi vya usalama kufika na kudai malipo ya kuachiliwa kwake.
Maandamano yalianza katika mji mkuu, Tehran, mnamo tarehe 29 Desemba, kufuatia kushuka kwa kasi kwa thamani ya sarafu ya Iran dhidi ya dola. Maandamano yalipofika katika miji na majiji mengine mengi, yaliwageukia watawala wa kidini wa Iran na vikosi vya usalama vilianzisha msako mkali.
Maandamano hayo yaliongezeka kwa kiasi kikubwa Alhamisi iliyopita na yalikabiliwa kwa nguvu kali na mamlaka.
Kulingana na Shirika la Habari la Haki za Binadamu (HRANA) lenye makao yake Marekani, takriban waandamanaji 2,435 wameuawa tangu machafuko hayo yaanze, pamoja na watoto 13 na watu 153 wanaohusishwa na vikosi vya usalama au serikali. Shirika hilo pia linaripoti kwamba waandamanaji wengine 18,470 wamekamatwa.
Wakati huo huo, kukamatwa kumeendelea kote nchini. Vikosi vya usalama na vitengo vya ujasusi vya Walinzi wa Mapinduzi vimewakamata wanaharakati, wanasheria, na raia wa kawaida.
Soma zaidi:
Samia ahurumia wanadiplomasia baada ya kufungwa kwa mtandao wakati wa Uchaguzi
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewahurumia wanadiplomasia na raia wa kigeni wanaoishi nchini humo kufuatia vikwazo vya mtandao vilivyowekwa nchini kote wakati wa machafuko yanayohusishwa na uchaguzi wa Oktoba.
Ni mara ya kwanza kwa Rais kutoa maoni yake hadharani kuhusu kuzimwa kwa mtandao, ambako kulidumu kwa zaidi ya wiki moja wakati wa machafuko hayo.
Akizungumza na mabalozi, makamishna wakuu na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa Alhamisi katika mji mkuu wa Dodoma, Rais Samia alitaka kuwahakikishia wajumbe hao usalama wao, akisema serikali itaendelea kuwa macho ili kuzuia kurudiwa kwa usumbufu huo.
Samia alisema, "Kwa washirika wetu katika jumuiya ya wanadiplomasia na wageni wanaoishi hapa Tanzania, poleni kwa hali ya kutokuwa na uhakika, vikwazo vya huduma na kuzimwa kwa mtandao mliokumbana nako."
Rais Samia alikiri kuwa vurugu zilitokea siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi, lakini akatetea hatua zilizochukuliwa na serikali, akisema madhumuni ya hatua hizo ilikuwa kulinda utulivu wa kikatiba na raia.
"Ninawahakikishia kuwa tutaendelea kuwa macho ili kuhakikisha usalama wenu na kuzuia kujirudia kwa matukio kama hayo," Samia alisema.
Rais Samia alishinda uchaguzi wa Oktoba kwa asilimia 98 ya kura, baada ya wagombea wakuu wa upinzani kutoshiriki katika uchaguzi huo.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema mamia ya watu waliuawa wakati wa machafuko hayo, ingawa serikali haijatoa takwimu rasmi za majeruhi hadi sasa.
Wakati wa hotuba ya hadhara mwezi Desemba, Samia alitetea hatua za vikosi vya usalama wakati wa ghasia za uchaguzi kwa kusema nguvu iliyotumika ilikuwa "muhimu" kulinda amani na kuzuia kile alichokitaja kama mapinduzi yaliyopangwa.
Soma zaidi:
Matokeo ya Uchaguzi Uganda 2026: Museveni anaongoza katika matokeo ya awali
Tume ya Uchaguzi Uganda inaendelea kupokea matoke ya uchaguzi uliofanyika jana Alhamisi kutoka vituo mbali mbali vya kupiga kura ambapo matokeo ya awali yaliyotangazwa yanaonyesha kuwa Yoweri Museveni amepata asilimia 76.25 ya kura zilizohesabiwa kufikia sasa kulingana na hesabu kutoka karibu nusu ya vituo vya kupigia kura.
Robert Kyagulanyi ambaye pia anafahakima kama Bobi Wine ndiye anayefuata akiwa na 19.85%, huku kura zilizosalia zikigawanywa kati ya wagombea wengine sita.
Baada ya kupiga kura hapo jana, Museveni aliwaambia waandishi wa habari kwamba alitarajia kushinda kwa 80% ya kura "kama hakutakuwa na udanganyifu".
Awali, Jaji Simon Byabakama ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi alisema kuwa siku ya uchaguzi ilikwenda vizuri ingawa uchaguzi huo ulikumbwa na changamoto za hitilafu ya kiufundi ikiwa ni pamoja na mashine za kupiga kura kushindwa kufanyakazi na kulazimisha shughuli ya upigaji kura kuendelea kwa njia ya kawaida.
Mgombea wa upinzani Robert Kyagulanyi amedai uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu.
"Matukio ya masanduku kujazwa kura yameripotiwa kila mahali," alidai mgombea wa urais wa chama cha upinzani cha NUP Ssentamu Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii, bila kutoa uthibitisho madai hayo.
Mamlaka inayosimamia uchaguzi huo haijatoa kauli yoyote kuhusu madai ya udanganyifu katika uchaguzi, wala madai ya Wine kwamba mawakala "wengi" wa wapiga kura na wasimamizi wa chama chake cha NUP "walitekwa nyara, na wengine kufukuzwa katika vituo vya kupigia kura".
Matokeo rasmi ya uchaguzi huu huo yanatarajiwa kutolewa ndani ya saa 48 baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika.
Soma zaidi:
Hujambo! Karibu katika matangazo yetu mubasahara tarehe ni 16/01/2026.