Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mwanamuziki na kiongozi mwenye mamlaka makubwa: Yote unayostahili kujua kuhusu uchaguzi wa Uganda 2026
- Author, Wycliffe Muia
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Raia wa Uganda wanapojitayarisha kupiga kura Alhamisi wiki hii, wanakabiliwa na uamuzi mzito: kuendeleza utawala wa rais ambaye angeingia katika muongo wa tano madarakani, au kumuunga mkono mgombea anayetafuta kutumia hamu ya mabadiliko inayojitokeza miongoni mwa sehemu ya jamii.
Rais Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81 na aliyeingia madarakani mwaka 1986, anawania muhula wake wa saba mfululizo. Mpinzani wake mkuu ni Bobi Wine, mwenye umri wa miaka 43, mwanamuziki wa pop aliyegeuka mwanasiasa, ambaye ameahidi mageuzi makubwa ya kiutawala na mabadiliko ya msingi katika uongozi wa nchi.
Hata hivyo, kampeni za uchaguzi zimekumbwa na changamoto kubwa, ikiwemo kuvurugwa kwa shughuli za upinzani, kukamatwa kwa wanaharakati na kusambaratishwa kwa mikutano ya kampeni na vyombo vya dola.
Kwa kuwa zaidi ya nusu ya wananchi wa Uganda wako chini ya umri wa miaka 30, na viwango vya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana vikiwa juu, masuala ya uchumi yamekuwa kiini cha mjadala katika kampeni.
Uchaguzi wa Uganda utafanyika lini?
Uchaguzi mkuu wa Uganda utafanyika Alhamisi tarehe 15 Januari. Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa moja asubuhi kwa saa za Uganda na kufungwa saa kumi jioni. Mpiga kura yeyote atakayekuwa kwenye foleni wakati huo ataruhusiwa kupiga kura.
Wananchi watakuwa wanachagua kina nani kupitia sanduku la kura?
Jumla ya wapiga kura milioni 21.6 waliosajiliwa watashiriki katika chaguzi tatu:
Uchaguzi wa Rais, unaoshirikisha wagombea wanane
Uchaguzi wa Bunge, ambapo wabunge 353 wa majimbo watachaguliwa
Uchaguzi wa wawakilishi wa wanawake, wabunge 146, mmoja kutoka kila wilaya
Nani ana nafasi ya kuwa rais ajaye?
Kati ya wagombea wanane wote wanaume, Yoweri Museveni na Bobi Wine wanaonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi.
Hii ni mara ya pili kwa wawili hao kukabiliana katika uchaguzi wa rais.
Katika uchaguzi wa 2021, Museveni alishinda kwa asilimia 58 ya kura, huku Bobi Wine akipata asilimia 35. Uchaguzi huo ulitawaliwa na madai ya wizi wa kura na ukandamizaji wa upinzani.
Yoweri Museveni - National Resistance Movement (NRM)
Museveni aliingia madarakani takribani miaka 40 iliyopita baada ya kuongoza jeshi la msituni lililoahidi kurejesha demokrasia kufuatia miaka ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na utawala wa kidikteta wa Idi Amin.
Awali, alionekana kama sehemu ya kizazi kipya cha viongozi wa Afrika waliotarajiwa kuleta mabadiliko ya kidemokrasia. Hata hivyo, kwa miaka ya karibuni, tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa wapinzani wa kisiasa zimeendelea kuharibu taswira hiyo.
Wakosoaji wanasema ametawala kwa mkono wa chuma, na baada ya kubadilisha katiba ili kuondoa ukomo wa vipindi na umri wa urais, ameendelea kushikilia madaraka. Kwa Wauganda wengi, Museveni ndiye rais pekee waliyezoea kumjua.
Museveni, ambaye anaorodheshwa watatu kwa viongozi waliodumu madarakani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika anasisitiza kuwa yeye ndiye nguzo ya uthabiti na maendeleo ya Uganda.
Bobi Wine - National Unity Platform (NUP)
Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, anachukuliwa kuwa mpinzani mwenye nguvu zaidi wa Museveni. Akiwahi kuitwa "rais wa mitaa", Bobi Wine anaonekana kuwakilisha matamanio ya kizazi cha vijana wanaotamani mabadiliko ya kisiasa na kijamii.
Katika uchaguzi wa 2021, alimaliza nafasi ya pili na kusaidia kupunguza idadi ya kura za Museveni kuliko wakati mwingine wowote. Chama chake, National Unity Platform (NUP), kilijitokeza kama chama kikuu cha upinzani bungeni.
Hata hivyo, tangu uchaguzi huo, Bobi Wine ameendelea kukumbana na manyanyaso na vikwazo kutoka kwa vyombo vya usalama, kwa mujibu wa mashirika ya haki za binadamu.
End of Pia unaweza kusoma:
Wagombea wengine na hali ya upinzani
Wagombea wengine ni Frank Bulira, Robert Kasibante, Joseph Mabirizi, Nandala Mafabi, Mugisha Muntu na Mubarak Munyagwa.
Mwanasiasa mashuhuri wa upinzani Kizza Besigye, ambaye amewahi kugombea urais mara nne dhidi ya Museveni, hajashiriki katika uchaguzi huu, akiwa gerezani kwa tuhuma za uhaini baada ya kukamatwa nchini Kenya mwaka 2024. Amekana mashtaka hayo.
End of Pia unaweza kusoma:
Masuala yanayowahusu wapiga kura
Masuala ya uchumi, hususan ukosefu wa ajira, ndiyo yanayopewa uzito mkubwa na wapiga kura.
Ingawa kipato cha mtu mmoja mmoja kimekuwa kikiongezeka taratibu tangu janga la UVIKO-19, ukuaji wa ajira hauendani na idadi kubwa ya vijana wanaotafuta kazi.
Aidha, kuna wasiwasi kuhusu miundombinu hafifu, pamoja na tofauti kubwa katika upatikanaji wa elimu na huduma za afya.
Hata hivyo, Uganda imefanikiwa kuepuka ongezeko kubwa la gharama za maisha lililoathiri nchi nyingi za ukanda huu.
Rushwa bado ni changamoto kubwa. Uganda iko nafasi ya 140 kati ya nchi 180 kwenye Kielezo cha Mtazamo wa Rushwa cha Transparency International, hali inayoashiria kuwepo kwa rushwa na upendeleo katika taasisi za umma.
Je, uchaguzi utakuwa huru na wa haki?
Historia ya uchaguzi nchini Uganda imekuwa ikikosolewa mara kwa mara. Ingawa serikali inasema uchaguzi huu utakuwa wa haki, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameonya kuwa mazingira ya hofu yanaweza kuathiri uhuru wa uchaguzi.
Mashirika ya haki za binadamu yameripoti kukamatwa kwa wafuasi wa upinzani na kuvunjwa kwa mikutano ya kampeni, hasa ya Bobi Wine ikilinganishwa na ya Yoweri Museveni.
Amnesty International ilielezea matumizi ya gesi ya machozi, dawa ya pilipili, vipigo, na vitendo vingine vya ukatili kama "kampeni ya kikatili ya ukandamizaji" kabla ya kura.
Serikali, kwa upande wake, inasema hatua hizi ni muhimu kulinda amani na kuzuia vurugu siku ya uchaguzi.
Linapokuja suala la uchaguzi wenyewe, Bobi Wine amewataka wapiga kura kukaa katika vituo vya kupigia kura na kulinda kura zao ili kusaidia kuzuia wizi wa kura.
Lakini wasimamizi wa uchaguzi wamesema watu wanapaswa kupiga kura zao kwa amani na kisha kuondoka, wakihakikisha kwamba ujumlishaji na mchakato wa kuhesabu kura utakuwa wa wazi na kuzingatiwa na mawakala wa vyama, vyombo vya habari na waangalizi wa uchaguzi. Wakosoaji, hata hivyo, wametilia shaka uhuru wa tume ya uchaguzi.
Licha ya serikali kukanusha, pia kuna hofu, kulingana na uzoefu wa awali, wa kuzima kwa mtandao wakati wa uchaguzi kwa lengo la kuzuia watu kuthibitisha matokeo. NUP inasema ina programu ya ufuatiliaji wa kura ambayo inaweza kuepuka suala hili kwa kutumia teknolojia ya Bluetooth.
Matokeo yatatangazwa lini?
Kwa mujibu wa sheria, Tume ya Uchaguzi lazima itangaze matokeo ya urais ndani ya saa 48 baada ya upigaji kura kukamilika.
Endapo kila kitu kitaenda kama ilivyopangwa, matokeo yanatarajiwa kutangazwa Jumamosi tarehe 17 Januari jioni. Upigaji kura utakamilika saa kumi alasiri Alhamisi.
Mfumo wa uchaguzi wa rais uko vipi?
Ili kushinda katika raundi ya kwanza, mgombea lazima apate zaidi ya asilimia 50% ya kura zote zilizopigwa kitaifa. Endapo hakuna atakayefikia kiwango hicho, uchaguzi wa marudio utafanyika ndani ya siku 30 kati ya wagombea wawili waliopata kura nyingi zaidi.
Hadi sasa, Museveni amekuwa akishinda kwa zaidi ya asilimia 50% katika raundi ya kwanza kila mara.
Imetafsiriwa na Mariam mjahid