Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Daftari la wapiga kura wa Uganda lapelekwa Uholanzi kuhakikiwa

Gazeti la Daily Monitor la Uganda linaripoti kuwa daftari la kitaifa la wapiga kura limepelekwa Uholanzi kwa ajili ya kuhakikiwa.

Moja kwa moja

  1. Tumefika mwisho wa matangazo ya moja kwa moja hii leo, Asante na tuonane tena Jumatatu

  2. Umoja wa Mataifa umesema mauaji ya Tigray yanaweza kuwa uhalifu kivita

    Kamishna wa anayeshughulikia masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa ripoti za mauaji ya watu nchini Ethiopia iwapo zitathibitishwa , vitendo hvyo vitakuwa uhalifu wa kivita.

    Tahadhari hii imekuja baada ya Amnesty International kuripoti idadi ya raia waliouawa katika jimbo la Tigray.

    Akizungumza mjini Geneva, Michelle Bachelet ametoa wito ufanyike uchunguzi kuwabaini waliohusika ili wawajibishwe. Mamlaka za Tigray zimekana ripoti za mashuhuda kuwa vikosi vya Tigray vilitekeleza mauaji.

    Bi. Bachelet amesema kipaumbele sasa ni kumaliza mapigano. UN inahofu kuwa mzozo unaweza huo unaweza kushika kasi na kwenda nje ya mipaka ya Ethiopia.

    Maelfu ya watu tayari wamekimbia mapigano na kuingia nchi jirani ya Sudan.

    Shirika la wakimbizi la Umoja wa mataifa limesema wengi wanaowasili ni watoto ambao huingia wakiwa wamechoka na wenye hofu.

  3. Serikali ya Ethiopia yateua gavana wa mpito wa Tigray

    Serikali ya Ethiopia imeteua mtawala wa mpito wa jimbo la Tigray ambapo operesheni ya kijeshi ya kuondoa mamlaka ya jimbo hilo ikiendelea.

    Taarifa fupi iliyotolewa na Waziri Mkuu Abiy Ahmed amesema Dkt Mulu Nega ameteuliwa kuwa Mtendaji mkuu wa Jimbo hilo.

    "Mtendaji mkuu atateua wakuu kuongoza vyombo vya serikali vya jimbo kutoka vyama vya siasa vinavyofanya kazi kihalali katika eneo hilo," Bw Abiy alisema.

    Hapo awali, wabunge walikuwa wamepitisha azimio la kuanzisha utawala wa mpito utakaowajibika kwa serikali katika jimbo la Tigray.

    Uteuzi huo unaonesha azma ya Bwana Abiy ya kukiondoa chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) mamlakani.

    Siku ya Alhamisi, bunge la taifa lilimvua kinga ya kutoshtakiwa gavana wa Tigray .

    Debretsion Gebremichael alichaguliwa kuwa rais wa jimbo tarehe 24 mwezi Septemba baada ya jimbo hilo kufanya uchaguzi wake wakikiuka uamuzi wa serikali ya Ethiopia ya kuahirisha uchaguzi kitaifa kutokana na Covid-19. Bw.

    Debretsion amekuwa akikaimu nafasi ya ugavana tangu Januari mwaka 2018.

  4. Ajichoma moto akipinga 'rushwa na hali ngumu ya maisha'

    Mwanaume mmoja raia wa Misri amejichoma moto, kisha kuokolewa na polisi na wapita njia katika uwanja wa Tahrir, jijini Cairo, mtu huyo alifanya hivyo kupinga "rushwa na hali mbaya ya maisha".

    Mtu huyo alifukuzwa kazi katika benki kwa kuanika vitendo vya rushwa vilivyowahusisha maafisa wa serikali, kwa mujibu wa makala ya Middle East Eye.

    Katika matangazo ya moja kwa moja ya Facebook, mwanaume huyo alisema maisha yake yameharibiwa na kuwa hana uwezo wa kupata kipato

    Kisha alijimwagia kimiminika chenye uwezo wa kushika moto na kuwaambia maafisa wa usalama uwanja wa Tahrir kuwa wasimkaribie.

    Alisema nchi imekuwa ikiharibiwa vibaya na kundi dogo la "wezi".

    Mtu huyo alijiwasha moto na kisha alipambana na maafisa wa usalama ambao waliuzima moto huo.

  5. Daftari la wapiga kura wa Uganda lapelekwa Uholanzi kuhakikiwa

    Gazeti la Daily Monitor la Uganda linaripoti kuwa daftari la kitaifa la wapiga kura limepelekwa Uholanzi kwa ajili ya kuhakikiwa.

    Tume ya uchaguzi imeipa zabuni kampuni ya Uholanzi kuondoa majina ya watu walioandikishwa zaidi ya mara moja wakati nchi hiyo ikielekea kwenye uchaguzi mkuu mwezi Januari.

    "Tumeanza mchakato wa kuwathibitisha wapiga kura ili kuhakikisha kuwa wapiga kura wanaostahili tu wanaonekana kwenye daftari na kwamba watapiga kura mara moja," msemaji wa tume hiyo Paul Bukenya amenukuliwa akisema.

    Haijulikani kama vyama vya siasa vilijulishwa kuhusu hatua hiyo.

    Raia wa Uganda watapiga kura kuchagua rais na wabunge tarehe 14 mwezi Januari. Wagombea 11- akiwemo Rais Yoweri Museveni- watawania nafasi hiyo ya juu.

  6. Leo bungeni: Rais Magufuli afungua rasmi bunge la 12 Tanzania

    Rais wa Tanzania, John Magufuli amefungua Bunge la 12 mjini Dodoma na kulihutubia Bunge hii leo.

    Akiwahutubia wabunge hii leo, Magufuli ametoa dira ya serikali yake baada ya kumaliza awamu ya kwanza.

    Rais Magufuli amesema mambo muhimu anayoyapa kipaumbele katika miaka mitano ijayo ni;

    Kuendelea kulinda na kudumisha tunu za taifa, yaani amani, umoja na mshikamano , uhuru wa nchi, Muungano na mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

    "Katika hilo ninaahidi kushirikiana kwa ukaribu sana na Rais mpya wa Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi. Kamwe hatutakuwa na mzaha na yeyote mwenye kutaka kuhatarisha amani ya nchi yetu. Mwenye nia ya kuvuruga umoja na mshikamano wetu, pia mwenye kutaka kutishia uhuru wetu, Muungano pamoja na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar." alisema Rais Magufuli.

    Rais Magufuli amemuahidi Dkt Hussein Mwinyi kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania itafanya kazi kwa karibu sana na Serikali ya Zanzibar ili kuleta maendeleo kwa pande zote mbili za Muungano.

    MAPAMBANO DHIDI YA UFISADI

    Rais Magufuli ameahidi kuimarisha utawala bora hasa kusimamia nidhamu katika utumishi wa Umma pamoja na kupambana na ufisadi, wizi , rushwa na ubadhirifu wa mali za Umma.

    " Kwenye miaka mitano iliyopita tuliwachukulia hatua za kinidhamu watumishi 32,555 na kuiwezesha nchi yetu kushika nafasi ya kwanza kati ya nchi 35 za Afrika kwa kupambana na rushwa, kwa mujibu wa Transparency International na pia kushika nafasi ya 28 kati ya nchi 136 duniani kwa matumizi mazuri ya fedha za Umma kwa mujibu wa utafiti wa Jukwaa la uchumi la dunia (World economic forum) wa mwaka 2019." Alisema Magufuli.

    Hata hivyo, Magufuli amesema kuwa watumishi wazembe, wala rushwa, wezi na wabadhirifu wa mali za Umma bado wapo, hivyo amesema miaka mitano ijayo ataendelea kushughulikia suala hilo.

    "Na kwa kifupi niseme, utumbuaji wa majipu utaendelea'' alisema.

  7. Wanajeshi 14 wa Burkina Faso wauawa

    Wanajeshi 14 wa Burkina Faso wameuawa baada ya wanaoshukiwa kuwa wanamgambo kuwashambulia Kaskazini mwa nchi hiyo.

    Shambulio hilo lilitokea katika mji wa Oudalan, karibu na mpaka wa Mali na Niger, kwa mujibu wa wizara ya mawasiliano.

    Wizara ilisema siku ya Alhamisi kuwa vikosi vya usalama vimepelekwa katika eneo hilo kuwafuatilia waliohusika na tukio hilo. Shambulio hilo lilitokea siku ya Jumatano.

    Rais Roch Kaboré ameahirisha kampeni zake kwa saa 48 kwa ajili ya heshima ya wanajeshi waliouawa. Burkina Faso inatarajia kufanya uchaguzi wa urais tarehe 22 mwezi Novemba.

    Rais Kaboré ameahidi kudumisha amani ikiwa atachaguliwa tena na kuutaka upinzani kutotumia ugaidi kama chombo cha kampeni.

  8. Rais Magufuli afanya uteuzi

    Rais Magufuli amefanya uteuzi wa Mawaziri wawili katika Baraza jipya la Mawaziri.

    Kwanza, Rais Magufuli amemteua Prof. Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

    Pia amemteua Dkt Philip Mpango kuwa Waziri wa Fedha na Mipango. Mawaziri hao wateule walikuwa wakishikilia nyadhifa hizo katika Baraza la Mawaziri lililopita.

  9. Waziri Mkuu wa Ethiopia ashutumu vikosi vya Tigray kutekeleza mauaji

    Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, ameshutumu vikosi vya serikali vya Tigray kwa kutekeleza mauaji siku ya Jumatatu ambayo shirika la Amnesty International limesema raia wengi huenda wameuawa.

    Katika taarifa ya video iliyochapishwa kwenye mtandao wa Facebook, Bwana Ahmed alisema vikosi vyake vimekomboa sehemu ya Magharibi ya Tigray kutoka kwenye udhibiti wa chama cha TPLF baada ya shambulio hilo la kikatili.

    Amnesty ilisema waathiriwa walichomwa visu hadi kufa katika mji wa Mai-Kadra Kusini Magharibi mwa Tigray.

    Maafisa wa Tigray wamekana shutuma kuwa vikosi vilivyo vitiifu kwa TPLF vilijihusisha na mauaji.

  10. Rais Magufuli kufungua bunge leo Tanzania,

    Rais wa nchi Tanzania John Magufuli hii leo atalihutubia taifa kupitia bunge la 12 na kulifungua rasmi huko katika mji mkuu wa Dodoma.

    Watanzania kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wanaisuburi kwa hamu hotuba ya rais ambayo inategemewa kutoa dira ya serikali baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita na kumpa ushindi wa asilimia 84.4 huku chama tawala kikijizolea ushindi wa wabunge kwa zaidi ya asilimia tisini.

    Hata hivyo, mpaka sasa baadhi ya vyama vya upinzani nchini humo hawajakubali matokeo ya Uchaguzi uliopita kwa madai uligubikwa na mazingira ambayo hayakuwa huru.

    Tuhuma hizo zimetupiliwa mbali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi

  11. Habari za asubuhi, karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya taarifa zetu,