Je, Marekani inajiandaa kuishambulia tena Iran?

    • Author, Jonathan Beale
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Rais wa Marekani Donald Trump alituma ujumbe kwa waandamanaji nchini Iran muda mfupi baada ya maandamano ya hivi karibuni kuanza, akisema kuwa "msaada uko njiani."

Tangu wakati huo, kumekuwa na ongezeko la taratibu lakini la wazi na kubwa la uwepo wa kijeshi wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Marekani, yenye jeshi lenye nguvu zaidi duniani, tayari imeshawahi kuonyesha uwezo wake wa kuishambulia Iran. Mnamo Juni mwaka jana, ilitekeleza operesheni iliyopewa jina Operation Midnight Hammer, iliyolenga vituo vya nyuklia vya Iran.

Zaidi ya ndege 100 za kivita zilishiriki katika operesheni hiyo, ikiwemo ndege za kisasa zisizoonekana kirahisi na rada aina ya B-2, ambazo ziliruka moja kwa moja kutoka ardhi ya Marekani na kurusha mabomu maalum ya ardhini, yanayojulikana kama bunker busters, kwenye vituo vya nyuklia vya Iran. Operesheni hiyo ilifanyika bila mwanajeshi yeyote wa Marekani kupoteza maisha.

Sasa swali linaloulizwa ni: Je, Marekani inajiandaa kuishambulia Iran tena?

Chapisho la hivi karibuni la Donald Trump kwenye mtandao wa kijamii wa Truth linaashiria uwezekano huo. Alionya Iran kuwa endapo haitafikia makubaliano ya kuzuia mpango wake wa nyuklia, basi "shambulio lijalo litakuwa baya zaidi."

Rais huyo wa Marekani alisema kuwa "msafara mkubwa wa kijeshi" unaelekea Iran na, akirejea operesheni ya Marekani nchini Venezuela ambapo Nicolas Maduro alitekwa, akasema Marekani iko "tayari, ina uwezo na iko tayari kutekeleza jukumu lake kwa kasi na nguvu endapo italazimika."

Aliitaka Iran kurejea mezani kwa mazungumzo, lakini akaongeza kuwa muda "unaendelea kuisha."

Kwa sasa, Marekani tayari ina uwepo mkubwa wa kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, ikiwa na wanajeshi wapatao 50,000 walioko katika eneo hilo.

Takriban wanajeshi 10,000 kati yao wako katika kambi ya anga ya Al Udeid nchini Qatar. Marekani pia ina kambi za kijeshi nchini Jordan, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Oman na Bahrain.

Katika wiki za hivi karibuni, ripoti za kijasusi zinazotegemea vyanzo huria zimekuwa zikifuatilia kuwasili kwa makumi ya ndege za kijeshi za Marekani katika eneo hilo.

Picha za anga zilizopigwa Jumapili katika kambi ya Al Udeid nchini Qatar – kituo kikubwa zaidi cha kijeshi cha Marekani Mashariki ya Kati zinaonyesha miundombinu mipya ikijengwa katika eneo la pembezoni mwa kambi hiyo.

Pentagon haiweki wazi orodha ya kina ya harakati hizi za kijeshi, lakini wachambuzi na vyanzo vinavyofuatilia mienendo ya kijeshi kupitia mitandao ya kijamii vimeripoti kuwasili kwa ndege za kivita aina ya F-15, ndege za kusambaza mafuta angani, pamoja na ndege za usafirishaji.

Inaaminika kuwa baadhi ya ndege hizo za usafiri zimebeba mifumo ya ziada ya ulinzi wa anga. Hatua hiyo inaweza kuashiria maandalizi ya Marekani kujilinda pamoja na kulinda washirika wake katika Ghuba ya Uajemi dhidi ya mashambulizi ya kulipiza kisasi endapo Trump ataamuru shambulio dhidi ya Iran.

Uingereza pia imetuma kikosi cha ndege za kivita aina ya Typhoon katika eneo hilo, ikisema lengo ni "kuimarisha usalama wa kikanda."

Jeshi la Anga la Marekani limetangaza kuwa linaendesha zoezi kubwa la kijeshi katika eneo hilo, likilenga kuonyesha "uwezo wa kupeleka, kusambaza na kuendeleza nguvu ya anga ya kivita" katika eneo linalosimamiwa na Kamandi ya Kati ya Marekani (CENTCOM).

Stephen Watkins, mtaalamu anayefuatilia mienendo ya meli za kivita na kuchapisha taarifa zake mtandaoni, ameripoti kuwasili kwa ndege kadhaa za Marekani, ndege ambazo pia zilihusika katika Operesheni Midnight Hammer. Miongoni mwao ni RC-135, E-11E na E-3G Sentry. Anasema hali hiyo "inaweza kuashiria" kuwa mashambulizi yako karibu kutekelezwa.

Kuingia kwa kikundi cha mashambulizi cha Marekani katika eneo hilo ni hatua nyingine muhimu.

Manowari ya kubeba ndege za kivita USS Abraham Lincoln ilikuwa katika eneo la Indo-Pasifiki kabla ya kuamriwa kubadili mwelekeo na kuelekea Ghuba ya Uajemi. Kikundi hicho, chenye zaidi ya ndege 70 za kivita, ni moja ya alama kubwa zaidi za nguvu za kijeshi za Marekani.

Ndani ya USS Abraham Lincoln kuna ndege za kisasa zaidi zisizoonekana kirahisi na rada aina ya F-35, zenye uwezo wa kupenya mifumo ya ulinzi wa adui.

Donald Trump amesema: "Tunatuma msafara mkubwa katika eneo hilo na tutaona kitakachotokea."

Malengo yanayoweza kulengwa

Matthew Sewell, mkurugenzi wa sayansi ya kijeshi kutoka taasisi ya Royal United Services Institute nchini Uingereza, anasema kwa mujibu wa nguvu zilizopo sasa, Marekani "inaweza kushambulia karibu sehemu yoyote ya Iran na kulenga karibu kila aina ya shabaha isipokuwa vituo vilivyo chini sana ya ardhi," ambavyo vingehitaji ndege za B-2 kuvishambulia.

Iwapo rais wa Marekani ataamuru shambulio, malengo yake yangekuwa yapi?

Bw Sewell, ambaye pia amewahi kushughulika na sera za Iran ndani ya serikali ya Uingereza, anasema Marekani ina chaguo kadhaa.

Chaguo la kwanza ni kuvuruga uwezo wa kijeshi wa Iran, "kama makombora ya masafa marefu au mifumo ya makombora ya pwani," jambo ambalo lingeweza kupunguza uwezo wa Iran kulipiza kisasi.

Iran bado ina hifadhi kubwa ya makombora ya masafa mafupi na ndege zisizo na rubani za masafa marefu, hali inayotia wasiwasi baadhi ya washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba, ambao tayari wameweka wazi kuwa hawataunga mkono mashambulizi mengine dhidi ya Iran.

Chaguo jingine ni kulenga serikali yenyewe. "Wanaweza kulenga vituo vya nguvu za kijeshi, ikiwemo Jeshi la walinzi wa mapinduzi ya kiislamu na pengine vikosi vya Basij vinavyokandamiza waandamanaji," anasema Sewell.

Hata hivyo, kujaribu kuwaondoa viongozi wa juu wa Jamhuri ya Kiislamu ni jambo gumu na hatari zaidi.

Israel iliwalenga maafisa wakuu wa Iran wakati wa vita vya siku 12, ikiwemo kwa kufuatilia walinzi wao binafsi ili kubaini walipo. Lakini tangu wakati huo, inaaminika Iran imeimarisha ulinzi na kutawanya vikosi vyake.

Kwa mujibu wa Sewell, Marekani "inaweza kubaini na kuwaondoa wahusika wakuu, lakini haijulikani matokeo ya mwisho ya hatua hiyo yangekuwa yapi."

Anaongeza:

"Huenda tunashuhudia mapambano ya mwisho ya serikali ya sasa kabla ya kuanguka, lakini tatizo ni kwamba mchakato huu unaweza kuchukua miezi au hata miaka."

Ingawa Trump ameonyesha utayari wa kutumia nguvu za kijeshi, amekuwa wazi pia kuwa hapendezwi na vita virefu vinavyochukua muda mrefu.

Mashambulizi ya kijeshi aliyoyatekeleza hadi sasa yamekuwa ya haraka, mafupi na yenye mipaka.

Pia hajaondoa uwezekano wa suluhu ya kidiplomasia, ambayo ingehitaji Iran kukubali kuzuia mpango wake wa nyuklia.

Kwa mujibu wa Sewell, Donald Trump sasa anakabiliwa na jukumu gumu la kuweka sawa nia yake ya kuonekana kuwa thabiti na uwezekano wa kufanikisha matokeo ya kweli na ya kudumu.