Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kashiwazaki-Kariwa: Kinu cha nyuklia kikubwa duniani kilichoanzishwa tena na Japan
- Author, Koh Ewe
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Japani imeanzisha tena shughuli katika kiwanda kikubwa zaidi cha nyuklia duniani kwa mara ya kwanza tangu janga la Fukushima lilipoilazimisha nchi hiyo kufunga mitambo yake yote ya nyuklia miaka 15 iliyopita.
Uamuzi wa kuanzisha upya kinu nambari 6 huko Kashiwazaki-Kariwa, kaskazini magharibi mwa Tokyo, umefanywa licha ya wasiwasi wa usalama kutoka kwa wakazi wa eneo hilo.
Uzinduzi wake ulicheleweshwa kwa siku moja kutokana na kengele ya tahadhari na kitaanza operesheni za kibiashara mwezi ujao.
Japani, ambayo inategemea sana uagizaji wa nishati kutoka nje, ilikuwa moja ya nchi za kwanza duniani kutumia nishati ya nyuklia.
Hata hivyo, mwaka 2011 mitambo yake 54 ya nyuklia ilibidi izimwe baada ya tetemeko kubwa la ardhi na tsunami kusababisha kuharibika Fukushima, na kusababisha moja ya maafa mabaya zaidi ya nyuklia katika historia.
Hii ni hatua ya hivi karibuni katika kufufua nguvu za nyuklia za Japani, ambayo bado ina safari ndefu.
Uwezo umepungua
Kinu cha saba cha huko Kashiwazaki-Kariwa hakitarajiwi kuanza kazi hadi 2030, na vingine vitano vinaweza kukongolewa. Hatua hizo zinakiacha kiwanda hicho na uwezo mdogo sana kuliko ilivyokuwa wakati vinu vyote saba vilipokuwa vikifanya kazi na kuzalisha gigawati 8.2.
Kuharibika kwa vinu vya nyuklia huko Fukushima Daiichi, kilomita 220 kaskazini mashariki mwa Tokyo, kulisababishwa na tetemeko la ardhi lenye nguvu zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Japani, na kusababisha uvujaji wa mionzi kwenye pwani ya nchi hiyo.
Jamii za wenyeji zilihamishwa na nyingi hazijarudi licha ya hakikisho rasmi kwamba ni salama kurudi.
Wakosoaji wanadai kwamba mmiliki wa kiwanda hicho, Kampuni ya Umeme ya Tokyo (Tepco), haikuwa imejiandaa na hakukuwa na utaratibu nzuri wa ushughulikiaji wa tatizo hilo kwa kampuni hiyo na kwa serikali.
Ripoti huru kutoka serikalini iliiita "janga lililosababishwa na mwanadamu" na kuilaumu Tepco, ingawa baadaye mahakama iliwaachilia huru watendaji wake watatu kwa makosa ya uzembe.
Hata hivyo, hofu na ukosefu wa uaminifu vilichochea upinzani wa umma dhidi ya nishati ya nyuklia, na Japani ilisimamisha mitambo yake 54 ya nyuklia muda mfupi baada ya janga hilo.
Katika muongo mmoja uliopita, nchi ilijaribu kufufua mitambo hii ya umeme, kwa lengo la kutozalisha hewa chafu ili dunia kufikia lengo hilo ifikapo mwaka wa 2050.
Tangu mwaka 2015, Japani imeanzisha upya vinu 15 kati ya 33 vinavyofanya kazi. Kiwanda cha Kashiwazaki-Kariwa ndicho cha kwanza kati ya vinu vya Tepco kuanza upya.
Kabla ya mwaka 2011, nishati ya nyuklia ilichangia karibu 30% ya umeme wa Japani, na nchi hiyo ilipanga kufikia 50% ifikapo mwaka 2030.
Mpango wake wa nishati mwaka jana ulifichua kuwa Japani inataka nishati ya nyuklia ifikie 20% ya mahitaji yake ya umeme ifikapo mwaka 2040.
Lakini hilo linaweza kuwa gumu.
Matumizi ya Nyuklia
Nishati ya nyuklia inazidi kupata kasi duniani kote. Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki linakadiria kwamba uwepo wa nishati ya nyuklia duniani unaweza kuongezeka mara mbili ifikapo mwaka 2050.
Nchini Japani, nishati ya nyuklia ilichangia asilimia 8.5 ya umeme mwaka 2023.
Waziri Mkuu wa Japani Sanae Takaichi, aliyeingia madarakani mwezi Oktoba, amesisitiza umuhimu wa nishati ya nyuklia kwa ajili ya kujitosheleza kwa nishati ya Japani, hasa kwa kuzingatia ongezeko la mahitaji ya nishati kutokana na vituo vya data na utengenezaji wa semiconductor.
Viongozi wa Japani na makampuni yao ya nishati kwa muda mrefu wamekuwa wakipigia upatu nishati ya nyuklia.
Wanadai ni ya uhakika zaidi kuliko nishati mbadala, kama vile nishati ya jua na upepo, na inafaa zaidi kwa Japani nchi yenye milima.
Hata hivyo, wakosoaji wanasema msisitizo wa kutumia nishati ya nyuklia unakuja kwa gharama ya kupuuza uwekezaji katika nishati mbadala ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.
Huku Japani ikijaribu kufufua matarajio yake ya nishati ya nyuklia, gharama za uendeshaji wa vinu vya nyuklia zimepanda, kwa kiasi fulani kutokana na ukaguzi mpya wa usalama unaohitaji uwekezaji mkubwa kutoka kwa makampuni yanayojaribu kuanzisha upya mitambo hiyo.
"Nishati ya nyuklia inazidi kuwa ghali zaidi kuliko unavyofikiria," anasema Dkt. Florentine Koppenborg, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Technical cha Munich, Ujerumani.
Serikali inaweza kutoa ruzuku kwa gharama hizo au zikalipwa na watumiaji, lakini chaguzi zote si sahihi kwa viongozi wa Japani, ambao kwa miongo kadhaa wamesifu kuwa umeme wa nyuklia ni wa gharama nafuu.
Kashfa
Mbali na hofu ya janga lingine kama Fukushima, mfululizo wa kashfa pia ulidhoofisha imani ya umma. Kiwanda cha Kashiwazaki-Kariwa, haswa, kilihusika katika kashfa hizo.
Mwaka 2023, mmoja wa wafanyakazi wao alipoteza rundo la hati baada ya kuliweka juu ya gari lake na kusahau kwamba ameziweka juu ya gari kabla ya kuwasha gari na kuondoka.
Mwezi Novemba, iligundulika kuwa mfanyakazi mwingine alifanya uzembe kuhusu nyaraka za siri.
Msemaji wa Tepco alisema kampuni hiyo iliripoti matukio hayo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nyuklia (NRA) na kuongeza kuwa lengo lake lilikuwa kuboresha usimamizi na usalama.
Ufichuzi huu ni "ishara nzuri" ya uwazi, Koppenborg anasema. Lakini pia inaonyesha kwamba Tepco "ina tatizo katika kubadilisha mbinu zake za usalama."
Mapema mwezi huu, NRA ilisitisha ukaguzi wake ili kuanzishwa upya mitambo ya nyuklia katika kiwanda cha Chubu Electric cha Hamaoka katikati mwa Japani baada ya kugundua kwamba kampuni hiyo ilifanya hila juu ya data za mitetemeko ya ardhi katika majaribio yake.
Kampuni hiyo iliomba radhi na kusema: "Tutaendelea kujibu kwa uaminifu na kwa ukamilifu kadiri iwezekanavyo, maagizo na miongozo ya NRA."
Hofu na kutoaminiana
Tukio la Fukushima lilisababisha maoni ya umma kupinga kile nishati ya nyuklia. Maelfu ya wakazi waliwasilisha kesi za madai dhidi ya Tepco na serikali ya Japani, wakidai fidia kwa uharibifu wa mali, msongo wa mawazo, na matatizo ya kiafya yanayodaiwa ni kutokana na mionzi.
Katika wiki zilizofuata baada ya janga la Machi 2011, 44% ya watu wa Japani waliamini kwamba matumizi ya nishati ya nyuklia yanapaswa kupunguzwa, kulingana na utafiti wa Kituo cha Utafiti cha Pew.
Idadi hiyo iliongezeka hadi 70% mwaka 2012. Lakini tafiti zilizofanywa na gazeti la biashara la Japani Nikkei mwaka 2022 zilionyesha kuwa zaidi ya 50% ya watu waliunga mkono nishati ya nyuklia ikiwa usalama utahakikishwa.
Hofu na kutoaminiana bado vinaendelea. Mwaka 2023, kutolewa kwa maji yaliyoondolewa mionzi kutoka katika mtambo wa nyuklia wa Fukushima Daiichi kulisababisha wasiwasi na hasira ndani na nje ya nchi.
Na wengi wanaendelea kupinga kuanzishwa tena kwa mitambo ya nyuklia.
Mwezi Desemba, mamia ya waandamanaji walikusanyika nje ya Bunge la Wilaya ya Niigata, huko Kashiwazaki-Kariwa iko, wakielezea wasiwasi wao kuhusu usalama.
"Kama kitu kitatokea katika kiwanda cha umeme, sisi ndio tutapata athari," mwandamanaji mmoja aliambia Reuters .
Wiki iliyopita, kabla ya kuanzishwa tena kwa kinu cha Kashiwazaki-Kariwa, umati mdogo ulikusanyika mbele ya makao makuu ya Tepco kupinga tena.
Viwango vya usalama wa nyuklia viliimarishwa baada ya janga la Fukushima.
NRA, chombo cha ufuatiliaji kilichoanzishwa mwaka 2012, sasa kinasimamia uanzishaji mpya wa mitambo ya nyuklia ya Japan.
Huko Kashiwazaki-Kariwa, kuta za kuzuia maji zenye urefu wa mita 15 zimejengwa ili kutoa ulinzi dhidi ya tsunami kubwa, na milango isiyopitisha maji imewekwa ili kulinda vifaa muhimu vya kituo hicho.
"Kulingana na viwango vipya vya usalama, viwanda vya nyuklia vya Japani vinaweza kustahimili hata tetemeko la ardhi na tsunami sawa na ile ya mwaka 2011," anasema Nei, afisa mkuu wa zamani wa usalama wa nyuklia.
Hata hivyo, Koppenborg bado ana wasiwasi kuhusu hali hiyo: "Wamejiandaa kwa yale yaliyokwisha pita hapo awali, lakini si kwa yale yajayo."
Baadhi ya wataalamu wana wasiwasi kwamba hatua hizo za usalama hazitoi hakikisho kutokana na kupanda kwa viwango vya bahari kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, au tetemeko kubwa la ardhi ambalo Japani hulitarajia mara moja katika karne moja.
"Ikiwa historia itajirudia, Japani imejiandaa vyema sana," anakubali Koppenborg.
"Lakini ikiwa kitu kisichotarajiwa kitatokea na tsunami kubwa kuliko ilivyotarajiwa kutokea, hatujui."