Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maeneo sita muhimu ya nyuklia ya Iran
- Author, BBC News Persian
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Uvumi unazidi kuongezeka kwamba Israel inapanga kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran - kulipiza kisasi baada ya Tehran kufanya shambulio kubwa zaidi la kombora kuwahi kuishambulia Israel Oktoba 1.
Vituo vya nyuklia vya Iran vimejengwa juu ya ardhi na chini ya ardhi.
Kiwanda cha kurutubisha uranium cha Natanz
Natanz ni eneo kuu la kurutubisha uranium nchini Iran, liko kilomita 250 kusini mwa mji mkuu wa Iran, Tehran. Lina sehemu mbili: Kiwanda cha Majaribio cha Kurutubisha Mafuta (PFEP) na Kiwanda kikubwa cha Urutubishaji Mafuta (FEP), ambacho ni kituo kikuu katika mpango wa Iran.
Sehemu yake kuu imejengwa chini ya ardhi ili kuilinda kutokana na mashambulizi. FEP kilijengwa kwa ajili ya kurutubisha kwa kiwango kibiashara. Kituo hicho kinaweza kuhifadhi mitambo 50,000 ya kutenganisha uranium nzito na nyepesi.
Mitambo hiyo iitwayo centrifuge ipo 14,000 katika kituo hicho kwa sasa, takribani 11,000 kati yake ikifanya kazi, kusafisha uranium hadi usafi wa 5%. Hiyo inaweza kutumika kuzalisha mafuta kwa ajili ya mitambo ya nyuklia.
Chini ya mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015 (Joint Comprehensive Plan of Action, JCPOA), Iran ilikubali kupunguza urutubishaji hadi asilimia 3.67, lakini baada ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano hayo mwaka 2018, Iran ilianza kurutubisha hadi 60%. Urutubishaji wa uranium unaohitajika kuunda silaha ya nyuklia ni 90% au zaidi.
Kituo cha Natanz kimekuwa kikilengwa na mashambulizi ya mtandao na hujuma, ikiwa ni pamoja na virusi vya kompyuta vya Stuxnet, vilivyogunduliwa mwaka 2010 na inaaminika ilikuwa ni operesheni ya pamoja ya Marekani na Israel.
Kulikuwa pia na mlipuko kwenye eneo hilo 2021, na Iran iliilaumu Israel. Kituo hicho ndicho kitovu cha mazungumzo ya kimataifa na kinakaguliwa kwa ukaribu na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya nyuklia.
Kiwanda cha kurutubisha mafuta cha Fordow
Kiwanda cha kurutubisha mafuta cha Fordow ni kituo cha chini ya ardhi cha kurutubisha uranium karibu na Qom, karibu kilomita 160 kusini mwa Tehran.
Kimejengwa ndani kabisa ya mlima, ujenzi wake wa siri ulifichuliwa mwaka 2009, na kuibua wasiwasi wa kimataifa kuhusu nia ya nyuklia ya Iran. Kinaweza kuhifadhi karibu mitambo 3,000 ya kusafishia uranium, Fordow kinalindwa dhidi ya mashambulizi ya kijeshi.
Chini ya JCPOA 2015, Iran ilikubali kukibadilisha Fordow kuwa kituo cha utafiti na kusitisha urutubishaji wa uranium kwa miaka 15. Lakini, baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano hayo mwaka 2018, Iran ilianza tena shughuli za kurutubisha, na kufikia uranium safi ya 20% hadi 2021.
Novemba 2022, Iran ilizidisha urutubishaji wake hadi 60% huko Fordow - hatua muhimu kuelekea uwezo wa kiwango cha silaha - na kutangaza mipango ya upanuzi mkubwa wa uwezo wake wa kurutubisha, kulingana na IAEA.
Kufikia 2024, ongezeko la shughuli za urutubishaji huko Fordow na teknolojia ya hali ya juu zinaendelea kutoa changamoto kwa juhudi za kimataifa za kuzuia mpango huo.
IAEA inafuatilia eneo hilo, lakini viwango vya juu vya urutubishaji na uwezo uliopanuliwa vimeongeza mvutano, na kutatiza juhudi za kufufua makubaliano ya nyuklia.
Khondab, Kinu cha maji mazito cha Arak
Kinu cha Iran cha Khondab, hapo awali kilijulikana kama kinu cha maji mazito cha Arak, ni kituo kidogo cha nyuklia. Vinu vya maji mazito kama vile vya huko Khondab vinaweza kutoa plutonium, ambayo inaweza kutumika kwa silaha za nyuklia.
Chini ya mapatano ya JCPOA ya mwaka 2015, Iran ilisitisha ujenzi wa kinu hicho. Kinu hicho kilipaswa kuundwa upya ili kupunguza uzalishaji wa plutonium na kuzuia uundaji wa plutonium ya kiwango cha silaha.
Iran iliifahamisha IAEA kuhusu mipango yake ya kuleta taarifa juu ya kinu hicho ifikapo mwaka 2026, ambacho kinaendelea kuvuta hisia za kimataifa kutokana na wasiwasi wa uwezekano wa urutubishaji. Mustakabali wa kituo hicho bado ni suala muhimu katika majadiliano kuhusu shughuli za nyuklia za Iran.
Kituo cha teknolojia ya nyuklia cha Isfahan
Kituo cha Isfahan ni ufunguo wa mpango wa nyuklia wa Iran, kinashughulika na kubadilisha uranium inayohitajika kwa ajili ya mafuta ya kinu cha nyuklia na urutubishaji.
Kituo cha Kubadilisha Uranium (UCF) huko Isfahan huzalisha gesi ya uranium hexafluoride (UF6), ambayo ni muhimu kwa urutubishaji wa Natanz na Fordow. Eneo hilo pia hutengeneza mafuta kwa vinu vya nyuklia, kikiwa ni pamoja na kile cha Bushehr.
Wakati ukaguzi wa IAEA unafanyika Isfahan, kulikuwa na wasiwasi juu ya shughuli zinazohusiana na uzalishaji wa vyuma ya uranium, ambavyo vinaweza kutumika kwa shughuli za kijeshi. Shughuli mbalimbali za nyuklia za Isfahan zinaonyesha lengo la Iran la kusimamia mzunguko kamili wa uzalishaji wa mafuta ya nyuklia.
Kiwanda cha nguvu za nyuklia cha Bushhr
Bushehr ndio kinu pekee cha nishati ya nyuklia cha Iran, kilicho katika Ghuba. Ujenzi wake ulianza miaka ya 1970 kwa usaidizi wa Wajerumani na ulikamilishwa na Urusi baada ya kuchelewa kwa muda mrefu. Kiwanda hicho kilianza kufanya kazi mwaka 2011 na kinatumia uranium inayotolewa na Urusi, huku mafuta yaliyotumika yakirejeshwa Urusi ili kuzuia kuchakatwa tena kuwa nyenzo ya silaha.
Ingawa Bushehr ni mradi wa nishati ya kiraia chini ya ulinzi kamili wa IAEA, wasiwasi upo kuhusu viwango vya usalama na ukaribu wa mtambo huo na maeneo ya tetemeko la ardhi. Bushehr ni kinu cha nguvu ya nyuklia kilicho chini ya uangalizi wa karibu wa kimataifa.
Kinu cha utafiti cha Tehran
Kinu cha Utafiti cha Tehran (TRR) ni kituo kidogo kinachotumiwa kwa utafiti na hutoa isotopu kwa matumizi ya dawa. Kilijengwa mwaka 1967 kwa usaidizi wa Marekani. Mwaka 1987 kilibadilishwa kutumia uranium iliyorutubishwa kidogo (LEU) ili kupunguza hatari ya urutubishaji.
Kinu hicho kilikosa mafuta 2009, na hivyo kupelekea Iran kuanza kurutubisha madini ya uranium hadi asilimia 20 ili kusambaza mafuta TRR, baada ya makubaliano ya kubadilishana mafuta ya LEU na Urusi na Ufaransa kushindwa. Mwaka 2012, Iran ilizalisha na kupeleka mafuta ndani katika kituo hicho cha TRR kwa mara ya kwanza.
Kituo chenye utata cha kijechi cha Parchin
Parchin, kusini-mashariki mwa Tehran, ni eneo la kijeshi ambalo linashukiwa kuwa na uhusiano na utengenezaji wa silaha za nyuklia.
Ripoti za kijasusi na picha za setilaiti zinasema majaribio ya vilipuzi ya vichwa vya makombora yametokea huko. Ingawa Iran inakanusha shughuli zozote za nyuklia, ikisema kuwa Parchin ni kwa matumizi ya kawaida ya kijeshi, na hakiwezi kukaguliwa.
Ziara ya mara moja ya IAEA mwaka 2015 haikushughulikia kikamilifu wasiwasi huo, na kuacha maswali kuhusu mwelekeo wa kijeshi wa mpango wa nyuklia wa Iran. Parchin mara nyingi hutajwa katika mijadala kuhusu nia ya nyuklia ya Iran.
Mwezi Mei 2022, mlipuko kwenye eneo hilo uliua mhandisi na kumjeruhi mwingine.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah