Tetesi za soka Ulaya: Juventus yamtaka Kolo Muani & Zirkzee

Muda wa kusoma: Dakika 3

Juventus wanaongeza jitihada za kumsajili mshambuliaji wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 27, Randal Kolo Muani, ambaye yupo kwa mkopo Tottenham akitokea Paris St-Germain, na Spurs wanaweza kumchukua mshambuliaji wa Crystal Palace Jean-Philippe Mateta (28) kama mbadala endapo Kolo Muani ataondoka. (Mail)

Mshambuliaji wa Uholanzi Joshua Zirkzee pia ni chaguo lingine la Juventus, huku Manchester United sasa wakiwa tayari kumruhusu mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 kuondoka kwa mkopo. (Gazzetta dello Sport)

Manchester United pia wanatafakari mustakabali wa beki wa England Harry Maguire. Klabu hiyo haijafanya mazungumzo ya maana na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32, ambaye mkataba wake unaisha mwishoni mwa msimu huu. Tayari timu kadhaa kutoka Italia na Uturuki zimewasiliana na wakala wake. (Athletic)

Klabu za Ligi kuu ya Saudi Arabia zinapanga kumsajili mshambuliaji wa Paris St-Germain na Ufaransa Ousmane Dembélé (28) baada ya Kombe la Dunia la majira ya kiangazi. (Sky Sports)

PSG wameanza mazungumzo ya kuongeza mkataba wa kocha Luis Enrique, ambaye mkataba wake wa sasa na mabingwa wa Ligi ya Mabingwa unaisha mwaka 2027. (Le Parisien)

Kiungo mshambuliaji wa Uturuki Kenan Yildiz (20) amehusishwa na klabu kadhaa za ligi kuu England, lakini yuko karibu kuongeza mkataba wake ili kusalia Juventus. (Sky Sports Germany)

Atletico Madrid wanataka kumsajili kiungo wa Ujerumani Leon Goretzka, ambaye mkataba wake na Bayern Munich unaisha majira ya kiangazi, na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 anafikiria ofa hiyo. (Sky Sports Germany)

Klabu ya Serie A inayopambana kuepuka kushuka daraja Fiorentina imewasiliana na West Ham kuhusu kumsajili beki wa England Kyle Walker-Peters (28) na kiungo wa Ufaransa Soungoutou Magassa (22) kutoka kwa wapiga nyundo hao. (Gazzetta dello Sport, via Football Italia)

Bournemouth wako kwenye mazungumzo na Inter Milan kuhusu kumsajili winga Luis Henrique mwenye umri wa miaka 24. The Cherries wanapendekeza kumsajili kwa mkopo Mbrazil huyo kukiwa na kipengele cha kumnunua baadaye kwa takriban pauni milioni 18. (Talksport)

Jesse Lingard (33) yuko kwenye mazungumzo na klabu za England na Italia. Kiungo huyo wa zamani wa Manchester United, aliyechezea timu ya taifa ya England mara 32, ni mchezaji huru baada ya kuondoka FC Seoul mwezi Desemba. (Mail+)

River Plate wamekubaliana dili la kumsajili kiungo mshambuliaji wa Chelsea na Ecuador mwenye umri wa miaka 18, Kendry Paez, ambaye alitumia nusu ya kwanza ya msimu huu kucheza Strasbourg kwa mkopo. (Fabrizio Romano)

AC Milan wanatafuta beki na wanaweza kumnasa Radu Dragusin wa Tottenham. Beki huyo wa Romania mwenye umri wa miaka 23 pia anawindwa na Roma na Napoli. (Calciomercato)