'Nusu ya marafiki zangu waliuawa' - wasichana wanaorejea katika shule iliyojikuta katikati ya vita

Muda wa kusoma: Dakika 6

IIlikuwa siku ya kawaida kwa pacha waliona umri wa miaka 18 Makarem na Ikram wakati shule yao iliposhambuliwa.

Makarem alikuwa na somo la fasihi naye Ikram alikuwa akifunza somo la sayansi wakati waliposikia "sauti ya ajabu " ikutoka nje ya darasa, ilikuwa shule nchini Sudan.

Kisha makombora yakaanza.

Makarem anasema bega lake "liliinama"kwani alishambuliwa huku wanafnzi wenzake wakilala chini sakafuni kuepuka kushambuliwa napia kutafuta mahali salama pa kujificha

"Tulikuwa tumejificha nyuma ya ukuta mara msichana mmoja aliye kuwa amesimama kando yangu aliuwekelea mkono wake juu ya bega langu na kusema, 'Bega lako linatoka damu.'"

Katika mtafaruku huo, dada hao wawili waliokuwa katika madarasa tofauti walijaribu kufikiana lakini hawakuweza. Baadaye, Ikram alimtafuta dada yake, bila kujua tayari alikuwa amepelekwa hospitali.

Sawa na wengine waliokuwa wamejeruhiwa, Makarem alipelekwa hospitali na wakazi ambao waliwakimbiza wakaazi waliojeruhiwa hospitali kwa kutumia gari au mkokoteni unaovutwa na wanyama kwasababu hakukuwa na huduma za ambulensi katika jiji la, el-Obeid ambapo shule yao ilikuwa.

Hatimaye, walimu wake na wanafunzi wenzake walifanikiwa kumshawishi Ikram aachane na shughuli ya kuwatafuta manusura na kurudi nyumbani.

Makarem aliporudi nyumbani kutoka hospitalini baadaye siku hiyo ndipo familia yake ilibaini kuwa bado yu hai.

"Nilimsubiri nje ya mlango na nilipomuwona anakuja sote tulilia," anasema Ikram, ambaye alikuwa katika sehemu ya shule ambayo haikushambuliwa, hivyo hakujeruhiwa.

Mwalimu wa kiingereza wa Makarem na Ikram pamoja wa wanafunzi wenzao 13 waliuawa ma makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulizi dhidi ya shule ya wasichana ya Abu Sitta, huko el-Obeid, katika jimbo la Kordofan Kaskazini, mwezi Agosti, 2024. Kwa kawaida shule hiyo huwa na wanafunzi 300.

Mamlaka za kikanda ziliwashtumu wanamgambo wa kundi la Rapid Support Forces (RSF) - ambao wapigana na jeshi ya serikali ya Sudam- kwa kurusha makombora.

RSF haijawahi kutoa tamko lolote kuhusiana na tukio hilo na haikujibu ombi la BBC kupata la kauli yao .Haijabainika ikiwa shambulizi dhidi ya shule hilo lilifanywa kimakusudi.

Makarem anasema nusu ya marafiki zake shuleni hapo waliuawa na nusu ya wengine kulijeruhiwa.

Pamoja na kujeruhiwa bega, pia alipata jeraha kichwani, lakini aliruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kupata matibabu ya kimsingi.

Lakini siku kadhaa baadaye, baada ya kupata maumivu makali ya kichwa, alifanyiwa uchunguzi wa CT scan ambayo ilionyesha kuwa ana kipande kidogo cha mabaki ya makombora kichwani mwake.

"Iliniuma sana na ilinibidi nitumie dawa nyingi za kutuliza maumivu," anasema.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vilianza Aprili 2023 na vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 150,000 na mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao.

Umoja wa Mataifa unasema nchi hiyo sasa inastahimili mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.

Inakadiriwa kuwa watoto milioni 13 kati ya milioni 17 wenye umri wa kwenda shule ambao wamesalia nchini Sudan hawako shuleni, kulingana na UN.

Shule ya Abu Sitta ilifungwa kwa muda wa miezi mitatu baada ya shambulio hilo ili kufanyiwa ukarabati.

Makarem na Ikram mwanzoni walisema hawawezi kurejea mahali ambapo marafiki na mwalimu wao waliuawa.

"Lakini nilipoona marafiki zangu wanarudi na kunieleza kuwa mambo yalikuwa sawa, niliamua kurudi," anasema Ikram.

Hata hivyo, kurudi shuleni kulirudisha kumbukumbu za uchungu.

"Nilikuwa nikifumba macho kila wakati ninapolekea darasani ili kukwepa kuangalia eneo ambalo shambulizi hilo lilitokea," Ikram anasema.

Wanafunzi kadhaa walipewa msaada wa kisaikolojia shuleni waliporejea, anasema mwalimu mkuu Iman Ahmed.

Vitanda na wauguzi pia viliwekwa shuleni ili kuwaruhusu wanafunzi waliojeruhiwa kufanya mitihani yao bila kipingamizi.

Licha ya el-Obeid kukabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani, wanafunzi katika shule hiyo walikuwa wakicheza na kucheka uani wakati BBC ilipoizuru Desemba.

Mwalimu mkuu anaelezea dhamira ya wasichana hao kuendelea na masomo, licha ya yaliyowapata, "kama aina ya ukaidi na uaminifu kwa wale waliopotea".

Lakini hali ya watoto wanaojaribu kupata elimu el-Obeid bado haijatengamaa

Jiji hilo lilizingirwa na RSF kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu, hadi jeshi la Sudan lilipochukua udhibiti wake tena Februari 2025.

Japo sasa kuna utulivu, shule kadhaa zimegeuzwa kuwa makazi ya watu wanaokimbia vita.

El-Obeid ni makao ya takribani watu milioni moja waliokimbia makaazi yao katika maeneo mbalimbali, kulingana na kamishna wa misaada ya kibinadamu wa jimbo hilo.

Ibtisam Ali, mwanafunzi wa shule ya sekondari ambayo imebadilishwa, anasema hawezi kuondoka darasani hadi mwisho wa siku ya shule kwa sababu uwanja umejaa watu waliotoroka mwakao.

"Hata kwenda chooni imekuwa changamoto kwetu," anasema.

Walid Mohamed Al-Hassan, waziri wa elimu katika jimbo la Kordofan Kaskazini, alisema kuwepo kwa wakimbizi mashuleni kumesababisha matatizo - ikiwa ni pamoja na usafi wa mazingira - lakini hizo ni "hali za vita na athari zake".

'Nina matumaini'

Licha ya vita na kila kitu kilichotokea, Makarem na Ikram, ambao sasa wana umri wa miaka 19, wana matumaini kuhusu mustakabali wao.

Ikram alimaliza masomo yake shuleni na sasa anasomea Kiingereza katika chuo kikuu cha el-Obeid.

Alitiwa moyo na mwalimu wake wa Kiingereza, Fathiya Khalil Ibrahiem, ambaye aliuawa katika shambulio hilo.

Kifo cha marafiki zake kilimfanya aazimie zaidi kumaliza masomo yake, anasema.

"Niliendelea kujikumbusha kwamba tunapaswa kuwa na utashi ili kufikia kile ambacho hawakuweza kufikia."

Makarem naye anataka kuwa daktari kama wale waliomtibu baada ya kujeruhiwa.

Alifaulu mitihani yake ya shule ya upili lakini hakupata alama zinazohitajika ili kusomea udaktari katika chuo kikuu.

Makarem anasema vipande vya mabaki ya makombora vilivyosalia kichwani mwake, ambavyo haviwezi kuondolewa kwa upasuaji, vilimfanya apate matatizo kmwanzoni.

"Ningeweza tu kusoma kwa saa moja na kisha kupumzika kwa saa nyingine. Ilikuwa ngumu sana."

Dk Tarek Zobier, daktari wa magonjwa ya mfumo wa neva nchini Sudan, alisema athari za kimatibabu za kuwa na babaki ya vipande vya makombora kichwani hutofautiana.

Watu wengine hawatapata dalili zozote na wanaweza kuishi bila uingiliaji wa matibabu.

Lakini ikiwa mwathiriwa akipatwa matatizo kama vile spasms, hana budi kufanyiwa upasuaji.

Kwa Makarem, naumivu yametulia kidogo, ingawa huwa mbaya zaidi wakati wa baridi wakati wa baridi. Anategemea dawa za kutuliza maumivu inapohitajika.

Ameamua kurudia mwaka wake wa mwisho shuleni ili aweze kufanya tena mitihani wa kitaifa.

"Ninaamini kwamba nitaweza kufikia alama ninayolenga.

"Nina matumaini ya siku zijazo," anasema.

Taarifa ya ziada ya Salma Khattab

Ili kuwasaidia watoto nchini Sudan na nchi nyingine zinazozungumza Kiarabu ambao wamenyimwa au kuzuiwa kupata elimu, BBC inazindua msimu mpya wa toleo la Kiarabu la kipindi cha elimu kilichoshinda tuzo ya Dars - au Somo.

Kipindi cha kwanza kitarushwa Jumamosi tarehe 24 Januari, kwenye BBC News Arabic TV. Vipindi vipya hurusha kila wiki Jumamosi saa 09:30 GMT (11:30 EET), na marudio Jumapili saa 05:30 GMT (07:30 EET) na wiki nzima.

Kipindi hicho kipatikana kwenye majukwaa ya kidijitali, ikijumuisha BBC News Kiarabu YouTube.