Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Marekani yaombwa kuangalia upya uhusiano na Uganda
- Author, Na Laillah Mohammed
- Nafasi, BBC Swahili, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Mweyekiti wa kamati ya masuala ya kigeni katika bunge la Seneti Nchini Marekani Jim Risch amesema kwamba angapenda wizara ya mambo ya kigeni ya nchi hiyo kuangazia upya uhuasiano kati ya nchi hiyo na taifa la Uganda.
Matamshi yake yametolewa siku chache baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Uganda ambapo Rais Yoweri Kaguta Museveni amerejea madarakani kwa awamu ya saba baada ya kushinda kiti cha Urais kwa asilimia 71 ya jumla ya kura zilizopigwa.
Mpinzani wake wa karibu, kinara wa chama cha upinzani NUP, Robert Kyagulanyi Ssentammu almaarufu Bobbi Wine, amekataa kukubali matokeo hayo baada ya kuibuka wa pili kwa kupata asilimia 20 ya jumla ya kura zilizopogwa.
Kwa mujibu wa mbunge huyo wa Marekani, 'Uchaguzi uliofanyika nchini Uganda kama ilivyofanyika nchini Tanzania hivi maajuzi, ulikuwa shughuli ambayo haikuwa na ukamilifu hata kidogo wala uwazi. Ilikuwa njia tu ya kulazimisha kurejea kwa Museveni kwa awamu yake ya saba na kuongeza hatamu yake uongozi kwa zaidi ya miongo minne.'
Rais Museveni amepokea jumbe za kumpongeza kutoka kwa viongozi wa kimataifa akiwemo Rais wa Urusi Vladimyr Putin ambaye alimtakia kila la kheir anaposubiri kulishwa kiapo cha kuhudumu katika muhulu huu mpya.
Marekani imesema kwamba japo Uganda na Tanzania ni washirika wake wakuu hasa katika masuala ya usalama, uongozi wa Uganda hasa unasimamia nchi kwa kutumia nguvu dhidi ya wakosoaji wake wa kisiasa ndani ya nchi.
'Serikali ya Uganda inadhulumu raia kwa kuwafunga wanasiasa bila ya makosa, kuwateka watu, kuwatisha raia na wakosaji wake na matumizi mabaya ya mamlaka,' alisema Seneta Risch ambaye ni mjumbe wa jimbo la Idaho nchini Marekani.
Taarifa yake imetolewa siku moja tu kabla ya kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi almaarufu Bobbi Wine kudai kwamba mke wake Barbie Kyagulanyi alitengwa na maafisa wa polisi ndani ya chumba kimoja nyumbani mwake na kuchapwa na kuumiza.
''Kundi la wanajeshi waliovalia barakoa usoni, kimevamia makazi yangu na kuwachapa mke na watoto wangu. Kwa sasa wametenga mke wangu Babrbie Kyagulanyi peke yake na wala sifahamu wanachokidhamiria kufanya,' Wine aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijami wa X.
Kufuatia tangazo hilo viongozi kadhaa wa kisiasa kutoka Afrika Mashariki wamechangia na kulaani kile ambacho wamekitaja ni serikali ya Uganda kuzidi kuwanyanyasa wananchi wake.
''Kuendea kudhulumiwa kwa Bobbi Wine na familia yake ni jambo ambalo halikubaliki kabisa. Ni makosa,' alisema Martha Karua, wakili wake Kizza Besigye na kinara wa chama cha PLP nchini Kenya.
Wine amekuwa akitafutwa na Mkuu wa Jeshi la Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye mapema wiki hii aliandika msururu wa jumbe kwenye ukurasa wake wa X akisema kwamba Wine ni mtu anayetafutwa na mamlaka na kwamba asipojisalimisha kwa polisi basi huenda wakamsaka na kumuuwa.
Jenerali Kainerugaba alifuta baadhi ya jumbe hizo ila aliendelea kumtusi Wine na kumtaja kama msaliti ambaye anataka kuzusha vurugu nchii Uganda na kudai pia kwamba mwanasiasa huyo anapokea ufadhili kutoka nje kwa ajili ya kuvuruga usalama wa nchi.
Polisi nchini Uganda hawajatoa tamko lolote kuhusu madai hayo ya Bobbi Wine kuhusu kudhulumiwa kwa familia yake, ila katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa juma lililopita walikanusha madai kwamba alikuwa ametekwa na kuzuiliwa katika kituo cha kijeshi.
Wine mwenyewe alitoa taarifa baadaye kusema kwamba yupo mafichoni na kwamba alikwepa mtego wa polisi na jeshi na kwamba alikuwa anahofia maisha yake na yale ya familia yake ambayo kwa wiki nzima sasa imekuwa ndani ya nyumba yake bila kuw ana ruhusa ya kuondoka.