Mkuu wa jeshi la Sudan Kusini amewapa wanajeshi siku saba kuumaliza uasi
Mkuu wa majeshi ya Sudan Kusini amewapa wanajeshi siku saba “kuukandamiza uasi” mashariki mwa nchi, ambao unatishia usalama wa mji mkuu, Juba.
Hivi karibuni, Jeshi la Ukombozi wa Watu wa Sudan kwa Upinzani (SPLA-IO) limevamia na kuteka maeneo kadhaa katika jimbo la Jonglei, kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa eneo hilo aliyeliambia BBC, ingawa taarifa hizo hazikuweza kuthibitishwa kwa njia huru.
Mapigano ya hivi karibuni yameutishia mji mkuu wa Jonglei, Bor, ulioko umbali wa takribani saa mbili kwa gari kutoka Juba.
Kiongozi wa SPLA-IO, Makamu wa Kwanza wa Rais aliyesimamishwa kazi, Riek Machar, kwa sasa yuko mahakamani akikabiliwa na mashtaka ya mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya ubinadamu, ambayo ameyakanusha.
Kuna hofu kwamba mapigano haya yanaweza kuchochea tena vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Vikosi vya ziada vya jeshi la Sudan Kusini sasa vimetumwa mjini Bor, ambao ulikuwa mji wa kwanza kutekwa na majeshi ya upinzani katika mgogoro wa miaka 2013–2018. Mji huo unaonekana kuwa kituo muhimu cha kimkakati kuelekea mji mkuu.
“Tuliwaleta hapa kwa ajili ya ujumbe maalum,” alisema mkuu wa majeshi ya ulinzi, Jenerali Paul Nang Majok, akiwaambia wanajeshi wake.
“Ninawapa siku saba tu kukamilisha hilo, kuwamaliza waasi katika maeneo hayo na kuyarejesha chini ya udhibiti wetu.”
Jeshi la Sudan Kusini linaungwa mkono na wanajeshi kutoka Uganda. Idadi yao halisi haijulikani. Ripoti moja imetaja idadi ya wanajeshi 4,000, lakini taarifa hiyo haijathibitishwa.
Unaweza kusoma;