Mama na watoto walivyonaswa kati ya migogoro miwili

    • Author, Akisa Wandera
    • Nafasi, BBC News, Renk
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Wakati mapigano makali ya Sudan yalilipo fika katika mtaa anaoishi Sarah Williams nkatika mki mkuu wa Khartoum, yeye na wanawe walinaswa katikati ya mashambulizi.

Risasi zilipenyeza kwenye nyumba yao, huku majumba yakiteketea baada ya nyaya za stima kulipuka na kusababisha moto.

"Tulikuwa tukitambaa chini," anakumbuka tukio hilo, akiwa amemshikililia mwanawe wa kiumme kwa karibu. "Ilikuwa vurugu."

Bi Williams, 33, ni mama wa watoto watano kutoka nchini Sudan Kusini.

Alilazimika kutoroka vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipozuka 2013, miaka miwili baada ya taifa lake kupata uhuru kutoka kwa Sudan.

Lakini furaha ya kupata uhuru ilitoweka mara baada ya mzozo wa kuwania madaraka kati ya Rais Salva Kiir na naibu wake Riek Machar kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyogharimu maisha ya takriban watu 400,000 na kuwalazimu watu milioi 2.5 kukimbia makazi yao.

Soma Pia:

Bi Williams alikuwa miongoni mwao. Baada ya kuwasili mjini Khartoum ambapo palikuwa mahali salama wakati huo, alianza upya maisha yake, na kujikimu kwa kufanya kazi za ndani kwa familia moja mjini humo..

Lakini hakuwa na budi kukimbia tena baada ya mapigano kuzuka mjini humo mwaka wa 2023 kati ya vikosi vinavyomtii mtawala wa kijeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa wakati huo Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti.

"Mzozo ulikuwa kati yao," Bi Williams anasema. "Lakini baadaye walianza pia kuwaua raia wa Sudan Kusini, ingawa hawakuwa sehemu ya mgogoro wao."

Katika miaka miwili iliyopita, mzozo nchini Sudan umesababisha vifo vya zaidi ya watu 150,000, na kuwalazimisha wengine zaidi ya milioni 12 kutoroka makwao, na kugeuza sehemu kubwa za Khartoum kuwa vifusi.

Nyumba yake iliposhambuliwa, alipakia vitu vyake vichache na kurejea Sudan Kusini.

Hata hivyo, mzozo sasa umeanza tena huko pia, huku Umoja wa Mataifa (UN) ukionya kwamba mkataba wa amani wa 2018 kati ya Kiir na Machar unakabiliwa na tishio la kuvunjika.

Kwa sasa safari ya Bi Ms Williams imeishia katika mji wa Renk. Mji wa mpakani ambao wakati mmoja ulikuwa mtulivu sasa umegeuk kitovu cha usafiri na shughuli chungu nzima zinazohusisha wakimbizi kutoka Sudan na majirani zao wa Sudan Kusini.

Bi Williams ambaye amekwama Renk kwa ktakribani miezi mitano anataka kurejea nyumbani kwao huko Nasir i katika jimbo la Upper Nile.

Hata hivyo,ni hatari kusafiri kuelekea Nasir - mji wa bandari ambao ni ni muhimu kimkakati kwasababu uko kando ya mto Sobat - kwani umegeuka kuwa eneo la vita.

"Mbele yetu kuna machafuko," aliiambia BBC huku akimshikilia binti yake aliye na umri wa miaka minne, na kumtingisha kwa upole mwanawe wa kiume wa mwaka mmoja.

Sauti yake imetulia lakini macho yake yanaashiria mazito anayopitia kutokana na hali ngumu inayomkabili.

Vikosi vya serikali na waasi wa White Army - waliomuunga mkono Machar wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe - wameripotiwa kukabililiana mjini Nasir, huku kukiwa na taarifa za mashambulizi ya makombora, na mapigano ya kuvizia na wakaazi kufurushwa makwao.

Bi Williams hajafanikiwa kuwasiliana na jamaa zake waliokuwa nyumbani huko Nasir.

"Sijui walikimbilia wapi mapigano yalipoanza … hata sijui kama wako hai," anasema kwa upole.

Mapigano nchini Sudan Kusini yamewafanya watu kama Bi Williams kukwama katika kituo cha mpakani cha Renk. Kambi ndogo ya wakimbizi iliyofunguliwa hapo sasa unawahifadhi zaidi ya watu 9,000 - mara tatu zaidi ya kiwango kinachostahili.

Mamia ya watu husubiri chini ya jua kali ili kuabiri boti zinazoelekea Malakal. Safari inachukua siku mbili na nusu chini ya Mto Nile. Abiria huketi juu mizigo yao au chini.

Miongoni mwao ni Mary Deng, ambaye alitoroka Wad Madani, kitovu cha mapigano makali katika mzozo wa Sudan.

"Mtoto huyu alikuwa na umri wa siku moja tu tulipovuka mpaka," anasema. "Kwa jumla tuko 16. Hatukuwa na hela - lakini tulimtumainia Mwenyezi Mungu."

Anashikilia rundo la hati - tikiti ya familia yake kutoka mjini Renk.

Huduma za matibabu zimewekwa kwa mipaka yao. Zahanati ya mpakani ya Joda - iliyojengwa kwa mabati - ndiyo kituo pekee cha afya kinachofanya kazi katika eneo hilo.

"Zaidi ya watoto 600 wamezaliwa hapa tangu vita vilipoanza," anasema mfanyakazi wa afya. "Lakini tunaweza tu kufanya kazi wakati wa mchana sasa, hakuna ufadhili wa zamu za usiku."

Mlipuko wa kipindupindu ulitangazwa mjini Renk mwezi Oktoba mwaka jana. Ilienea katika sehemu kubwa ya Sudan Kusini, ukiwemo mji mkuu Juba, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 450.

Tatek Wondimu Mamecha, afisa wa kushughulikia hali ya dharura wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Sudan Kusini, anaonya kuhusu hatari inayoendela kuwakodolea macho wakimbizi hao.

"Japo mlipuko wa kipindupindu umedhibitiwa, hali bado ni tete. Hivi sasa, idadi ya watu wanaougua ugonjwa wa malaria inaongezeka na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka msimu wa mvua utakapowadia," aliambia BBC.

Bw Tatek anaongeza kuwa athari za hatua ya utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump kupunguza kwa misaada ni mbaya sana.

"Washirika wetu watano wamesitisha huduma au kupunguza shughuli zao kwa 50%.

Hospitali ya rufaa kama Renk imepoteza nusu ya wafanyikazi wake, wakiwemo madaktari wa upasuaji, madaktari wa uzazi, madaktari wa watoto, hali ambayo imewaachia mzigo mkubwa madaktari waliosalia.

"Kituo hiki kinawahudumia takribani wagonjwa 350 hadi 400 kwa siku," Bw Tatek anasema.

Mgogoro wa wakimbizi unaoshuhudiwa katika mji wa mpakani wa Renk ni ishara ya wazi kwamba maelfu ya watu wamenaswa kati ya migogoro miwili, maeneo ya Sudan Kusini sio tena mahali salama kwa watu wanaokimbia mzozo wa miaka miwili nchini Sudan.

Mvutano umeongezeka nchini Sudan Kusini tangu mwezi Machi wakati Machar alipowekwa chini ya kifungo cha nyumbani baada ya kutuhumiwa na washirika wa Kiir kwa kuunga mkono makundi yenye silaha - madai ambayo chama chake kinakanusha.

George Owino, mwenyekiti wa shirika la ufuatiliaji lililoundwa chini ya mkataba wa amani wa 2018 kusaidia katika utekelezaji wake, ameonya kwamba mapigano ya hivi punde "yanatishia msingi wa makubaliano."

Anaiambia BBC kwamba tatizo kuu ni kwamba viongozi wa kisiasa wanaendelea kuwaamuru wanajeshi wapinzani, na kushindwa kuwajumuisha katika jeshi la umoja

wa kitaifa.

"Uhusiano kati ya siasa na nguvu za kijeshi bado uko sawa," Bw Owino asema.

"Viongozi wanapotofautiana, inageuka haraka kuwa makabiliano ya silaha - kile ambacho makubaliano yalipaswa kuzuia."

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 2013 vilizuka baada ya Kiir kumfukuza Machar kama makamu wa rais, akimtuhumu kwa kupanga mapinduzi, huku Machar akipinga shutuma kwamba Kiir alikuwa "dikteta".

Vita mbaya vya wenyewe kwa wenyewe vilimalizika kufuatia makubaliano ya amani ya 2018 ambayo Machar aliteuliwa tena kama makamu wa rais.

"Kulikuwa na mazungumzo zaidi ndani ya urais. Hilo limepungua," Bw Owino asema.

Umoja wa Afrika (AU) hadi sasa umeshindwa katika juhudi zake za kurejesha mchakato wa amani, wakati Uganda imetuma wanajeshi wake Sudan Kusini ili kuimarisha nafasi ya Kiir.

Chama cha Machar kinasema hatua hiyo inadhoofisha uhuru wa Sudan Kusini, na makubaliano ya amani ya 2018.

Uganda na serikali ya Kiir inatetea uamuzi huo ikisema inaimarisha makubaliano ya muda mrefu ya usalama kati ya mataifa hayo mawili.

Hata hivyo, wadadisi wa wanasema hatuoa hiyo inaonyesha jinsi nguvu ya Kiir mamlakani ilivyo dhaifu, huku hofu ikiongezeka kwamba vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe vinaweza kuanza tena.

Huku hayo yakijiri katika nchi jirani ya Sudan, vita vya wenyewe kwa wenyewe vinaendelea kupamba moto, huku Jenerali Dagalo akitangaza kuundwa kwa serikali sambamba.

Hatua yake imekuja licha ya kwamba vikosi vyake vimepoteza udhibiti wa Khartoum baada ya mapigano makali. Mji huo sasa umesalia na magofu baada ya majengo yake kulipuliwa kwa mabomu.

Bi Williams anasema hana nia ya kurejea Khartoum, na ameamua kuwa ni bora kujaribu kujenga upya maisha yake nyumbani, "hata kama hali ni mbaya".

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi