DNA ya Man Utd: Ni nini na ina mizani gani?

    • Author, Phil McNulty
    • Nafasi, Chief football writer
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Manchester United wanatafuta meneja mpya wa klabu, baada ya kuondolewa kwa Ruben Amorim, na mara nyingine tena wito ni: Meneja anayefaa "DNA" ya klabu.

"DNA" hii? Ni mtindo wa haraka, mashambulizi, soka la kuvutia na kuchanua vipaji vipya- kumbuka Busby Babes na Class of 92.

Baada ya kuondolewa kwa Amorim, beki wa zamani wa United, Gary Neville, anaamini Red Devils wanahitaji meneja "anayefaa DNA ya klabu ya soka".

Si Man Utd pekee, mchezaji wa zamani wa Liverpool, John Aldridge, alishikilia hoja hii baada ya sare ya 0-0 dhidi ya Leeds:

"Inaonekana tumepoteza DNA yetu. Hakuna hamasa, hamu au mawazo mapya."

Wakati changamoto zinajitokeza, ''DNA'' hushurutisha klabu irejee kwa kile inachong'aa nacho, inachosimamia na kile kimeipatia sifa na kufika mahali walipo sasa.

Hiyo inaweza kufafanua kwa nini mmiliki aliye na hisa chache Man Utd Sir Jim Ratcliffe na wenzake wanaangalia watu wenye historia tajiri Old Trafford wanapotafuta meneja wa muda.

Darren Fletcher amechukua udhibiti wa Burnley Jumatano, huku Ole Gunnar Solskjaer – aliyeondolewa mwaka 2021 – na Michael Carrick pia wakichukuliwa kama wagombea.

Fletcher na Carrick wamefanikiwa kushinda mataji 10 ya Ligi Kuu ya England kwa pamoja, huku Solskjaer akishinda sita na kufunga moja ya mabao maarufu zaidi katika historia ya United, bao la kumshinda Bayern Munich kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa 1999 huko Barcelona.

Hata Fletcher alihisi haja ya kutafuta "baraka" za Sir Alex Ferguson kabla ya kuchukua udhibiti wa muda, ishara ya ushawishi wa mzee huyo wa miaka 84.

Kwa kumbukumbu, Ferguson alishinda mataji 13 ya Ligi Kuu, Mabingwa 2 ya Ulaya, na mara mbili ya ligi na FA Cup mara 2.

Lakini sasa, je, bado ni lazima kutafuta baraka zake miaka 13 baada ya kustaafu? Je, kitendo hicho kitalirejesha United kwenye kutafuta DNA iliyopotea?

Peter Schmeichel, goli wa zamani wa United, alisema kwenye BBC Radio 5 Live:

"Manchester United si klabu yoyote. Wamepitia Mourinho, Van Gaal… wakubwa wote, na haikufanya kazi.

Wanaingia, wanajua muda wao ni mfupi, wanaleta mfumo wao na hauendi bila kucheza kwa mtindo wa Manchester United.

"Klabu lazima ifikirie kwa kina nani anayeweza kufanya kazi hii. Tumemsikia Thomas Tuchel, Julian Nagelsmann, Xavi, Zinedine Zidane, majina makubwa, lakini je, wanaelewa Manchester United kweli?"

Kwa hivyo, je, DNA ya klabu kweli ipo? Au ni dhana tu? Je, meneja lazima awe na uhusiano wa zamani na klabu ili kuelewa DNA yake?

Pia unaweza kusoma:

DNA ya klabu ni nini?

Mashabiki wa soka wanaamini ni msimbojeni wa klabu.

DNA ya klabu ni mtindo wake wa mchezo, hisia zinazojitokeza punde tu unapotaja jina lake, na falsafa ya ushindi.

Gary Neville akielezea DNA ya United kwa Sky Sports:

"Barcelona hawatabadilika kwa mtu yeyote. Sidhani United inapaswa kubadilika kwa mtu yeyote. Klabu lazima ipate meneja mwenye uzoefu, anayependa soka la haraka, la mashambulizi, lenye furaha na shauku."

Hii ilikuwa alama ya United chini ya Sir Alex Ferguson, na hata zamani chini ya Sir Matt Busby, ikijumuisha kuendeleza vipaji vipya kama "Busby Babes" na "Class of 92" – Neville, Beckham, Giggs, Scholes na wengine.

Wengi wa waliokuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya baadaye ya klabu sasa ni watu wenye ushawishi mkubwa kwenye vyombo vya habari, hali inayoongeza presha na uchunguzi wa kila jambo linalotokea klabuni.

Hakika, Amorim, katika siku zake za mwisho akiwa Manchester United, alisema:

"Kama watu hawawezi kuvumilia akina Gary Neville na ukosoaji wa kila kitu, basi tunahitaji kuibadilisha klabu."

Wakati John Aldridge aliposema Liverpool wamepoteza "DNA" yao, alikuwa akimaanisha shauku, hamasa na hisia zilizokuwa msingi wa mafanikio ya klabu hiyo, hali iliyojionyesha hivi karibuni kupitia soka la mashambulizi la kuvutia walilocheza chini ya Jurgen Klopp.

Hata hivyo, nyakati hubadilika.

Katika soka la kisasa, sarafu yenye thamani zaidi ni ushindi, haijalishi unaufikia kwa mtindo gani.

Ni klabu zipi zina 'DNA'?

Kwa kawaida, dhana ya DNA ya klabu huamuliwa na mashabiki wanaoonja mafanikio na kuamini kuwa hakuna njia nyingine ya kushinda zaidi ya ile waliyoizoea.

Manchester United wanaamini wanaifahamu DNA yao, kama ilivyo kwa Liverpool, klabu inayojivunia uhusiano wa kina kati ya mashabiki na meneja, pamoja na uelewa wa hisia kali zinazochochea moto wa Anfield.

Kwa Barcelona, DNA yao ya umiliki wa mpira ni zao la enzi za Johan Cruyff akiwa mchezaji na kocha. Baadaye, falsafa hiyo ilirudishwa na kuenziwa na waliomtarajali na kucheza chini yake, akiwemo kocha wa Manchester City, Pep Guardiola.

Ajax nao ni nadra kuachana na misingi iliyowapa Kombe la Ulaya mara tatu mfululizo kati ya 1971–73, falsafa ya Total Football iliyobuniwa na kocha nguli Rinus Michels, kisha kutekelezwa kwa vitendo na Cruyff. Mfumo huo pia ulitegemea sana ukuaji wa vipaji chipukizi wa Kiholanzi.

Kwa Real Madrid, DNA ni kitu kimoja tu: kushinda. Hali ni hiyo hiyo kwa Bayern Munich.

Klabu mbili zilizofanikiwa zaidi katika miaka ya karibuni, Manchester City na Paris Saint-Germain, zimechukua mataji ya ndani na kushinda Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza, bila kuwa na DNA inayoonekana wazi. Na ukweli ni huu: haijalishi.

Pia unaweza kusoma:

Ndani ya Ligi Kuu ya England, kuna mifano miwili ya klabu zinazoamini zina DNA, lakini madai yao mara nyingi hukosa uzito.

Kuna kile kinachoitwa "The West Ham Way", falsafa inayotajwa tangu enzi za Ron Greenwood miaka ya 1960, huku mashabiki wakijivunia mchango wa West Ham kwenye ushindi wa England wa Kombe la Dunia 1966 kupitia Bobby Moore, Geoff Hurst na Martin Peters.

Sam Allardyce alikosolewa kwa mtindo wake alipokuwa meneja wa klabu hiyo, lakini baadaye aliandika kwenye wasifu wake:

"Mashabiki walikuwa wanaaminishwa kimakosa kwamba kihistoria klabu ilikuwa na mtindo wa kucheza unaofanana na Barcelona, jambo ambalo ni upuuzi.

Niliwahi kuwaita mashabiki waliopotoshwa, na ninasimamia kauli hiyo. Sijui nani aliyeanzisha kauli ya 'The West Ham Way', lakini imekuwa mzigo mzito shingoni mwa klabu."

David Moyes alivunja ukame wa miaka 43 wa West Ham bila taji kwa kushinda Europa Conference League mwaka 2023, lakini wengi hawakuridhishwa na mtindo wake wa uchezaji.

"Nimekuwa meneja," alisema baadaye, "lakini siwezi kukuambia 'The West Ham Way' ni nini."

Kwa upande wa Tottenham, kauli mbiu ya klabu "To Dare Is To Do" huchukuliwa kama tamko la mtindo wa uchezaji.

Wakati Ange Postecoglou alipoteuliwa kuwa meneja Juni 2023, mwenyekiti wa wakati huo Daniel Levy alisema:

"Ange analeta mtazamo chanya na soka la kasi, la mashambulizi. Ana rekodi nzuri ya kukuza wachezaji na anaelewa umuhimu wa uhusiano na akademi kila kitu ambacho ni muhimu kwa klabu yetu."

Ni kweli Postecoglou alileta soka la mashambulizi, lakini pia alileta vipigo 22 na kumaliza msimu uliopita akiwa nafasi ya 17 kwenye Ligi Kuu.

Hata ushindi wa ligi ya Europa katika fainali ya kushangaza dhidi ya Manchester United ambayo ilionekana kudharau dhana yoyote ya "DNA", haukuweza kumuokoa dhidi ya kufutwa kazi.

DNA ni ukweli au hadithi ya kimapenzi?

Unapotamka neno "DNA" ni ishara tosha mapenzi ulonayo kwa klabu au unaelezea mtindo wa mchezo wao ambao umekuwa ukiaminishwa kutoka vizazi hadi vizazi.

Mourinho alishinda Ligi ya Europa na League Cup, lakini hakuwa akicheza kwa mtindo wa DNA ya United, alishinda tu.

Wale wanaounda nguvu hii ya ajabu ni wachache sana, viongozi kama vile Bill Shankly na Klopp huko Liverpool, na Ferguson huko Old Trafford.

"DNA" ni msimbo wa kuvutia wa kile kinachofanya vilabu kushinda, ikihitaji wachezaji bora, meneja hodari na historia ya ushindi.

Wito wa Man Utd ''kurudi kwenye DNA yake'' ni sahihi, lakini swali ni nani anaweza kuirejesha? Je, wanataka? Je, Meneja lazima awe na uhusiano wa zamani na klabu ili kuelewa ''DNA yake''?

Mtu kama Sir Alex Ferguson hapatikani mara kwa mara, kiuhalisia dunia inahitaji mtu awe na haiba kubwa, uongozi hodari, na historia ya ushindi.

Soma pia:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid