Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Sudan: Hofu na matumaini katika mji mkuu ulioharibiwa wa Khartoum
- Author, Barbara Plett Usher
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Katikati ya uharibifu huko Khartoum, utulivu unatawala baada ya wiki za mapigano makali katika vitongoji vya mji mkuu wa Sudan.
BBC imeweza kuingia katika mjini huo siku chache tu baada ya jeshi la Sudan kuuteka tena kutoka kwa wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), kufuatia mapigano ya miezi sita katika eneo la kati la nchi hiyo.
Khartoum, ambayo zamani ilikuwa kitovu cha biashara nchini Sudan na makao makuu ya serikali ya Sudan, umekuwa ni mji ulioteketea.
Kutekwa tena kwa mji mkuu huo kunaashiria mabadiliko katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili, vilivyochochewa na mzozo wa madaraka kati ya jeshi na RSF.
Huku Wasudan wakisherehekea Eid katika mitaa ya mji mkuu, wakiamini kuwa vita vimekwisha – lakini muelekeo hasa wa mzozo huo kwa sasa haujulikani.
Ikulu iliyoharibiwa
Kwanza tulielekea kwenye Ikulu ya rais, ambayo RSF, iliidhibiti tangu mwanzo wa vita. Ikulu ilikuwa kambi muhimu kwa wapiganaji wao.
Sakafu za Ikulu zimefunikwa na uchafu na glasi zilizovunjika, na vumbi limefunika viti vilivyotumika kwa shughuli rasmi. Baadhi ya michoro bado inaning'inia kwenye kuta, na shada la taa za mapambo lililoharibiwa linaning'inia.
Takriban vitu vyote vilivyokuwemo ndani ya jumba hilo viliporwa, hata nyaya za umeme ziling'olewa ukutani. Sehemu ya mbele ya jumba hilo ndiyo iliyoharibiwa zaidi, baada ya kulipuliwa na ndege za RSF muda mfupi baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa Ikulu hiyo.
Lango kuu la kuingilia ikulu lilivunjwa, damu iliyokauka bado imetapakaa juu ya ngazi, na madirisha sasa yamekuwa matundu yanayotazama Mto Nile.
"Nilifurahi sana kuwa katika Ikulu ya rais," askari mmoja alisema tulipokuwa tukitembea kwenye zulia chafu jekundu.
Aliongeza, "hii ni mara yangu ya kwanza katika eneo hili."
Ikulu ni ishara muhimu ya nguvu za kijeshi. Wanajeshi waliimba, kucheza, na kushangilia wakati wa likizo ya Eid al-Fitr ilipoanza. Migahawa ya ndani iliwahudumia kwa karamu, na wakazi wengi wa mji mkuu wanawasifu kama mashujaa.
Majengo yaliyoharibiwa
Gharama ya ushindi huu ni kubwa sana. Kiwango cha uharibifu katikati mwa Khartoum ni cha kustaajabisha. Wizara za serikali, benki, na majengo ya ofisi yameharibiwa na kuchomwa moto.
Njia ya kurukia ndege za kimataifa iligeuzwa kuwa kaburi la ndege zilizoharibika, majivu yakifunika ofisi za pasipoti na vituo vya polisi.
Tuliendesha gari polepole, tukipitia mabaki ya mabomu ambayo hayakulipuka. Sehemu za miili ya watu, na mafuvu mawili yalionekana wazi kwenye makutano ya barabara, na kulikuwa na mwili ulioharibika umbali wa mita 100 kutoka katika gari yetu.
Tulisimama kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Mathayo, lililojengwa na Waingereza mwaka 1908. Hapa ndipo wanapoishi Wakristo walio wachache nchini humo.
Dari iliyopakwa rangi nzuri bado iko imara, lakini msalaba umeanguka, na kuna shimo katika moja ya kuta kutokana na kombora.
Hata hivyo, jengo la kanisa kuu lilionekana kuwa imara kuliko majengo mengine mengi tuliyoona.
Askari mmoja aliyekuwa akiondoa kifusi, alituambia uharibifu ulisababishwa na mabomu yaliyotokea katika eneo la karibu na kanisa hilo.
Mwanzoni mwa vita, RSF walichukua udhibiti wa maeneo ya majengo ya kidiplomasia, na kusababisha nchi na makampuni kuwahamisha wafanyakazi wao haraka. Kuna nembo ya Rapid Support Forces ilichorwa ukutani kwenye lango la Ubalozi wa Uingereza.
Kioo cha jengo hilo kisicho pitisha risasi bado kipo, lakini kina alama za risasi. Magari yaliyoharibiwa bado yako kwenye maegesho nyuma ya ubalozi, na barabarani. Bendera ya Uingereza bado inaning'inia katika ngazi ya jengo lililochakaa.
Vita hivi ni vita vya tatu vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan katika kipindi cha miaka 70, na ni vita vibaya zaidi nchini humo. Migogoro ya awali ilitokea katika maeneo mengine ya nchi, lakini hivi vimeharibu mji mkuu wa Sudan, na kuzidisha migawanyiko, na kutishia kuigawanya nchi.
Matumaini yenye mashaka
Mbali na eneo la mapigano, sherehe za Eid zimeenea mitaani, na watu huko Khartoum wanaamini kwamba vita vimekwisha, ingawa vinaendelea mahali pengine.
Jeshi la Sudan linakabiliwa na shutuma za uhalifu wa kivita, huku kukiwa na ripoti kwamba maelfu wamekimbia mapigano katika siku za hivi karibuni.
Hata hivyo, watu jijini Khartoum wanasherehekea kumalizika kwa udhibiti wa Rapid Support Forces katika jiji lao.
Katika kitongoji cha Al-Jereif Magharibi, anga ilijawa na furaha wakati wa hafla ya kuandaa chakula kwa ajili ya jamii.
"Nahisi kama nimezaliwa upya," anasema Othman Al-Bashir, baada ya kuzungumza kuhusu aliyoyashuhudia wakati wa vita. Anasema alijifunza Kiingereza kutoka BBC World Service.
Duaa Tariq, mwanaharakati wa demokrasia, akiwa sehemu ya vuguvugu lililopindua utawala wa takribani miongo mitatu wa Omar al-Bashir mwaka 2019, anasema, "tunasherehekea Eid kwa mara ya kwanza baada ya miaka miwili."
Aliongeza, "Kila mtu amevaa kwa ajili ya Eid, ikiwa ni pamoja na mimi! Tunajisikia huru, tunajihisi wepesi, hata hewa inanukia tofauti."
Ugavi wa chakula bado ni haba mjini, lakini kuna hali ya matumaini miongoni mwa wakazi.
"Najisikia vizuri, najisikia salama, ingawa nina njaa," anasema mzee mmoja anayeitwa Qasim Ajra. "Unajua, haijalishi. Uhuru ndio muhimu."
"Kama unavyoniona nimebeba simu," alisema huku akinionyesha simu mfukoni. "Hatukuweza kubeba simu ya rununu takribani wiki mbili zilizopita."
Simu za mkononi zilikuwa ni muhimu kuwasiliana na ulimwengu wa nje, pia zilikuwa ni shabaha kuu ya wizi kutoka kwa wapiganaji wa Rapid Support Forces.
Sheikh huyo mzee ana matumaini kwamba Khartoum na Sudan yote zitapona, "nadhani serikali italeta wawekezaji wa Marekani, Saudi, Canada na China. Nadhani wataijenga upya nchi hii."
Sauti za wanawake
Wanawake wengi pia wana matumaini; kwamba wanaweza kulala tena baada ya kulazimika kukesha usiku kucha wakihofia kuvamiwa na wanachama wa RSF.
Kiwango cha hofu na hasara kilikuwa kikubwa sana, kuna hadithi nyingi za unyanyasaji, vitisho na wasiwasi.
"Watoto wetu wana kiwewe," anasema Najwa Ibrahim.
Aliongeza, "wanahitaji wanasaikolojia kuwasaidia. Dada yangu ni mwalimu, na nimejaribu kuwasaidia watoto, lakini hilo halitoshi."
Akirejelea miaka iliyofuata baada ya kuondolewa madarakani kwa Bashir, wakati Sudan ikiwa chini ya serikali ya pamoja ya kiraia na kijeshi iliyokuwa ikijitahidi kurejesha utawala wa kiraia na hali ya sasa.
Mwanaharakati Duaa Tariq ana maswali mengi kuhusu athari za vita, "nini kitatokea kwa mashirika ya kiraia, watendaji, wanaharakati, na wapigania uhuru? Sina uhakika juu ya mustakabali wetu kwa sasa".
"Tunawaombea watu wa Darfur, Mungu awalinde," anasema Hawa Abdel Shafie mwenye umri wa miaka 16, akimaanisha eneo linalodhibitiwa na RSF magharibi mwa Sudan, ambalo linakabiliwa na mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu na linatarajiwa kuwa kitovu cha vita.