Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Jeshi la Sudan latwaa tena ikulu ya rais huku wanamgambo wa RSF wakiendelea kupigana

Hatua ya jeshi kuyateka tena maeneo muhimu ya mji mkuu inaashiria hatua kuu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka miwili.

Muhtasari

Moja kwa moja

Abdalla Dzungu & Rashid Abdallah

  1. Namibia yamuapisha Rais wake wa kwanza mwanamke

    Rais mpya wa Namibia ameapishwa leo siku ya Ijumaa kuongoza nchi inayokabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira, ukosefu wa usawa na umaskini.

    Na atakuwa akikabiliana na changamoto za kiuchumi sambamba na kuwa Rais mwanamke wa pili kuwahi kuchaguliwa moja kwa moja barani Afrika na Rais wa kwanza mwanamke wa Namibia.

    "Ikiwa mambo yataenda vizuri basi itaonekana kama mfano mzuri," Netumbo Nandi-Ndaitwah aliambia podikasti ya BBC Africa Daily.

    "Lakini kama jambo lolote likitokea, kama linaweza kutokea katika utawala wowote chini ya wanaume, kuna wale ambao wangependa kusema: 'Waangalie wanawake!'

    Akiwa na umri wa miaka 72 alishinda uchaguzi kwa 57% ya kura huku mpinzani wake wa karibu Panduleni Itula akipata 26% ya kura, kulingana na tume ya uchaguzi nchini humo.

    Ni kisa katika mfululizo wa matukio katika maisha yake- Nandi-Ndaitwah akipigana na utawala uliokuwa, na kutoroka kisha kujiwezesha na kujijenga kama mwanamke mashuhuri nchini Namibia.

    Nandi-Ndaitwah amekuwa mwanachama mwaminifu chama tawala cha SWAPO tangu akiwa msichana na kuapa kuleta mabadiliko ya kiuchumi Namibia.

    Nandi-Ndaitwa alizaliwa 1952 ,kaskazini mwa kijiji cha Onamutai.

    Ni mtoto wa tisa miongoni mwa watoto 13 na babake mzazi alikuwa kiongozi wa kidini wa kanisa la Anglikana.

    Namibia ni nchi kubwa kijiografia yenye idadi ndogo ya watu milioni tatu.

    Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa wakulima wa asili ya kizungu wanamiliki takriban asilimia 70 ya mashamba ya nchi hiyo

    Jumla ya Wanamibia 53,773 waliotambuliwa kuwa wazungu katika sensa ya 2023, wakiwakilisha asilimia 1.8% ya wakazi wa nchi hiyo.

    Kiwango cha ukosefu wa ajira kiliongezeka hadi asilimia 36.9% mnamo 2023 kutoka asilimia 33.4% mnamo 2018, kulingana na wakala wa takwimu nchini.

    Nandi-Ndaitwah alisema uchumi ambao kwa kiasi fulani unategemea mauzo ya madini nje ya nchi unapaswa kufanya kazi zaidi katika kuongeza thamani ya kile ambacho nchi inachimba kutoka ardhini badala ya kusafirisha malighafi nje ya nchi.

    Pia anataka Namibia kuangazia zaidi sekta za ubunifu na kufanya sekta ya elimu kuzoea hali halisi mpya ya kiuchumi.

    Nandi-Ndaitwah ni mwanamke wa pili Mwafrika kuchaguliwa moja kwa moja kama rais, baada ya Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia.

    Rais mwingine mwanamke pekee wa bara hilo kwa sasa ni Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, ambaye alichukua nafasi hiyo baada ya mtangulizi wake kufariki dunia akiwa madarakani mwaka 2021.

    Nandi-Ndaitwah anataka kupimwa kwa ubora wake, lakini alisema kuwa ni "jambo zuri kwamba sisi kama nchi tunatambua kwamba kama vile wanaume [wanaweza kufanya], wanawake wanaweza pia kushikilia nafasi ya mamlaka".

    Pia unaweza kusoma;

  2. Genge linatumia mitandao ya kijamii kuwalaghai na kuwashambulia wapenzi wa jinsi moja - Austria

    Takriban watu 15 wamekamatwa nchini Austria na Slovakia wakituhumiwa kwa uhalifu wa chuki unaolenga jamii ya wapenzi wa jinsi moja, kulingana na polisi wa jimbo kusini mwa Austria.

    Baadhi ya maafisa 400 walishiriki katika uvamizi siku ya Ijumaa asubuhi kwa niaba ya ofisi ya waendesha mashtaka wa umma ya Graz.

    Walikamata wanaume 12 na wanawake watatu, wenye umri wa miaka 14 hadi 26, ambao wanatuhumiwa kuwalaghai watu - wengi wao wakiwa ni wapenzi wa jinsi moja - kwenye maeneo ya mbali kwa kutumia akaunti bandia za mitandao ya kijamii, kabla ya kuwapiga na kujirekodi.

    "Kundi hilo lilidai kuwa vitendo vyake vililenga watu wanaowalawiti watoto," polisi wa jimbo la Styria waliandika kwenye ukurasa wao wa X. "Kwa kweli, vitendo vya kikatili vinavyoongezeka vilielekezwa dhidi ya jamii ya wapenzi wa jinsi moja."

    Wahalifu hao walianza kuwarubuni watu kwa kutumia akaunti za mitandao ya kijamii Mei 2024. Polisi walisema washukiwa hao "walitenda kwa kisingizio cha kuwa macho".

    Wanaume waliojifunika barakoa walikutana na watu waliodanganywa katika maeneo ya mbali na kisha wakajirekodi wakiwapiga, kuwaibia na kuwadhulumu waathiriwa, polisi walisema. Kisha walipakia picha kwenye vikundi vya mtandaoni.

  3. Waziri wa ulinzi wa Israel atishia 'kuteka maeneo ya ziada' huko Gaza

    Waziri wa ulinzi wa Israel ameamuru jeshi "kuteka maeneo ya ziada huko Gaza" ikiwa Hamas haitawaachilia mateka wote waliosalia.

    Israel Katz alisema siku ya Ijumaa kwamba jeshi litaendelea na operesheni yake ya ardhini huko Gaza "kwa nguvu inayoongezeka" hadi mateka wote "hai na waliokufa" warudishwe.

    Ni ongezeko lingine la mzozo huo, ambao ulitawala wiki hii wakati Israeli ikivunja makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyowekwa tangu Januari, ili kuanza tena kampeni mashumbulizi ya mabomu. Mamia ya watu wameuawa katika ghasia zilizofuata.

    "Kadiri Hamas wanavyoendelea kukataa, ndivyo eneo ambalo litapoteza kwa Israeli," litaongezeka, Katz alisema.

    Katika taarifa yake siku ya Ijumaa, Katz alisema kuwa Israel bado inakubali pendekezo, ambalo lililetwa na mjumbe wa Marekani Steve Witkoff, "kuwaachilia watu wote waliotekwa nyara, walio hai na waliokufa, mapema na katika hatua mbili pamoja na kusitishwa kwa mapigano kati yao".

    "Tutazidisha mapigano kwa mashambulizi kutoka angani, baharini na nchi kavu na kwa kupanua ujasusi wa ardhini hadi mateka waachiliwe na Hamas kushindwa," Katz aliandika.

    Waziri wa ulinzi pia alisema Israel "itatekeleza mpango wa uhamisho wa hiari uliopendekezwa na Rais Trump wa Marekani wa wakazi wa Gaza".

    Trump alisema anataka Marekani ichukue na kuujenga upya Ukanda wa Gaza, huku akiwaondoa kabisa Wapalestina milioni mbili.

    Mamlaka ya Palestina na Hamas wamesema Ukanda huo "hauuzwi", huku Umoja wa Mataifa ukionya kwamba uhamisho wowote wa kulazimishwa kwa raia kutoka katika eneo linalokaliwa kwa mabavu ni marufuku kabisa chini ya sheria za kimataifa na ni "sawa na mauaji ya kikabila".

    Unaweza pia kusoma:

  4. Msemaji wa jeshi na mwanajeshi wauawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani ikulu

    Msemaji wa jeshi ameuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani ya RSF kwenye ikulu ya rais, jeshi linasema.

    Luteni Kanali Hassan Ibrahim ameuawa pamoja na Kapteni Emad Eldein Hassan, mfanyakazi mwenzake mwenye cheo cha chini , jeshi limeiambia BBC. Kapteni Hassan alikuwa mmoja wa washawishi maarufu wa mitandao ya kijamii wa jeshi.

    Wafanyakazi watatu wa kituo cha televisheni cha Sudan pia waliuawa walipokuwa wakiripoti kuhusu harakati za wanajeshi hao kuelekea ikulu. Walikuwa mhariri wa vipindi, mpiga picha na dereva.

    Mashambulizi hayo ya ndege zisizo na rubani yalilenga wanajeshi waliokuwa wakisherehekea ndani ya Ikulu ya Republican, saa chache baada ya wanajeshi kuliteka tena jengo hilo la mfano kutoka kwa RSF.

    Unaweza pia kusoma:

  5. Tazama: Wanajeshi wa Sudan wakijipiga picha katika ikulu ya rais

    Wanaume hao wanasikika wakipiga kelele 'Mungu ndiye mkuu zaidi' walipokuwa wakitembea kuzunguka jengo hilo katika mji mkuu Khartoum.

    Jeshi la Sudan limechukua udhibiti kamili wa Ikulu ya Rais mjini Khartoum Ijumaa, Televisheni ya Sudan na vyanzo vya kijeshi vimesema, katika mojawapo ya mafanikio makubwa katika mzozo wa miaka miwili unaotishia kusambaratisha nchi hiyo.

    Unaweza pia kusoma:

  6. Taliban yamwachilia huru raia wa Marekani aliyekuwa akishikiliwa kwa miaka miwili

    Fundi wa shirika la ndege la Marekani ameachiliwa na kundi la Taliban baada ya kuzuiliwa nchini Afghanistan kwa zaidi ya miaka miwili.

    George Glezmann, alizuiliwa Desemba 2022 akiwa mtalii, aliwasili kwa ndege nchini Qatar Alhamisi jioni kabla ya kusafiri kurejea Marekani.

    Kuachiliwa kwake kulithibitishwa na waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Taliban baada ya kuukaribisha ujumbe wa mateka huyo, ukiongozwa na Adam Boehler na maafisa wengine wa Marekani katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

    Wizara ya mambo ya nje ya Taliban ilisema kuachiliwa kwa Bw Glezmann ni "kwa misingi ya kibinadamu" na "ishara ya nia njema," huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio akiuita mpango huo ni "hatua chanya na yenye kujenga."

    Mawasiliano kati ya serikali hizo mbili kwa kawaida hufanyika kupitia nchi nyingine tangu Taliban ilipotwaa tena mamlaka mwaka 2021. Qatar imesema imewezesha makubaliano ya kumwachilia Glezmann.

    Rubio amesema Glezmann, fundi wa kampuni ya Delta Air Lines, mwenye umri wa miaka 65, ataungana tena na mkewe, Aleksandra, na akaishukuru Qatar kwa jukumu lake la "muhimu" katika kufanikisha kuachiliwa kwake.

    Wakfu wa James Foley, ambao hufuatilia kesi za Wamarekani wanaozuiliwa ng'ambo, ulisema Glezmann alikuwa na "mawasiliano ya mara chache ya simu" na mkewe alipokuwa kizuizini.

    Afya yake pia ilisemekana "ilizorota alipokuwa kizuizini," na alikuwa na "matatizo ambayo yanahitaji huduma ya haraka."

    Kabla ya Trump kuchukua madaraka mwezi Januari, Wamarekani wawili, Ryan Corbett na William Wallace McKenty, waliachiliwa kutoka Afghanistan kwa kubadilishana na raia wa Afghanistan aliyefungwa Marekani.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Waziri aliyezaa na mvulana wa miaka 15 miaka 30 iliyopita ajiuzulu

    Waziri wa watoto nchini Iceland amejiuzulu baada ya kukiri kuwa alizaa na mvulana wa miaka 15 zaidi ya miaka 30 iliyopita, wakati yeye akiwa na miaka 22.

    Ásthildur Lóa Thórsdóttir alisema katika mahojiano na vyombo vya habari alianza uhusiano na mvulana huyo alipokuwa na umri wa miaka 15, wakati yeye akiwa na umri wa miaka 22, alipokuwa mshauri katika kikundi cha kidini.

    Kisha mwanamke huyo alizaa mtoto alipokuwa na umri 23 wakati mvulana huyo akiwa na umri wa miaka 16.

    "Ni miaka 36 imepita,” amesema Thórsdóttir ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 58.

    Waziri mkuu wa Iceland, Kristrún Frostadóttir, anasema alipokea uthibitisho wa jambo hilo siku ya Alhamisi usiku na mara moja alimwita waziri wa watoto ofisini kwake, na akajiuzulu.

    Thórsdóttir alifichua katika mahojiano kwamba alikutana na baba wa mtoto wake, aitwaye Eirík Asmundsson, alipokuwa akifanya kazi katika kikundi cha kidini cha Trú og líf, na inasemekana Ásmundsson alijiunga na kikundi hicho kwa sababu ya maisha magumu ya nyumbani.

    Thórsdóttir alijifungua mtoto wao wa kiume na shirika la habari la Icelandic la RUV, limeripoti kwamba uhusiano huo ulikuwa wa siri, lakini Ásmundsson alikuwepo wakati wa kuzaliwa kwa mtoto wake na alikaa na mtoto huyo kwa mwaka mzima.

    Ukaribu wa wawili hao ulibadilika baada ya Thórsdóttir kukutana na mume wake wa sasa.

    RUV limeripoti kuwa wameona hati ambazo Ásmundsson aliziwasilisha wizara ya sheria ya Iceland akiomba kumpata mtoto wake, lakini Thórsdóttir alikataa, na badala yake akaomba apokee malipo ya msaada wa kumlea mtoto huyo kwa miaka 18 iliyofuata.

    Siri ilianza kuvuja wiki iliyopita, baada ya jamaa wa kike wa Ásmundsson kujaribu kuwasiliana na waziri mkuu wa Iceland mara mbili, ili kuelezea suala hilo.

    Frostadóttir alisema jana usiku kwamba jamaa huyo alipofichua kuwa jambo hilo linamhusisha waziri wa serikali aliomba maelezo zaidi, jambo ambalo lilipelekea kupata uthibitisho na kumtaka Waziri wa watoto ajiuzulu.

    Katika mahojiano yake ya televisheni jana usiku, Thórsdóttir alisema amekasirishwa na hatua ya mwanamke huyo kuwasiliana na waziri mkuu.

    Ingawa umri halali kisheria wa kushiriki mapenzi nchini Iceland ni 15, lakini ni kinyume cha sheria kufanya mapenzi na mtu aliye chini ya umri wa miaka 18 ikiwa wewe ni mwalimu au mshauri wake, ikiwa anakutegemea kifedha, au anakufanyia kazi. Hukumu ya juu zaidi kwa uhalifu huu ni miaka mitatu jela.

    Licha ya kujiuzulu kutoka kazi yake ya uwaziri, Thórsdottir amesema hana mpango wa kuondoka bungeni.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Watumiaji wa TikTok watoa wito wa kuondolewa kwa uhariri wa picha unaomfanya mtu aonekane mnene

    Watumiaji wa TikTok wameiambia BBC kwamba wanafikiri programu ya filter ambayo hufanya watu waonekane wanene inafaa kupigwa marufuku kwenye jukwaa.

    Kinachojulikana kama "chubby chubby", ambayo ni programu ya akili mnemba (AI) hupiga picha ya mtu na kuhariri mwonekano wake ili kuonekana kana kwamba amenenepa.

    Watu wengi wameshiriki picha zao za kabla na baada ya jukwaa na utani kuhusu jinsi wanavyoonekana tofauti - hata hivyo, wengine wanasema ni aina ya "kufedhehesha mwili" na haipaswi kuruhusiwa.

    Wataalamu pia wameonya kuwa uhariri hup unaweza kuchochea "utamaduni wa lishe yenye sumu" na kuchangia shida za ulaji.

    TikTok haijajibu ombi la maoni.

  9. 'Sherehe ya goli haikulenga kumkejeli Ronaldo' - Hojlund

    Rasmus Hojlund alitetea shangwe yake baada ya kutoka kwenye benchi na kufunga bao la ushindi kwa Denmark dhidi ya Ureno akisema hakuwa akimdhihaki Cristiano Ronaldo.

    Fowadi huyo wa Manchester United alifunga kwa utulivu baada ya kuunganisha krosi ya Andreas Skov Olsen na kupata ushindi huo katika mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mataifa.

    Alisherehekea bao hilo kwa kuiga jinsi Ronaldo anavyosherehekea mabao yake.

    "Haikuwa kumdhihaki yeye au kitu chochote, nimekuwa nikisema amekuwa na umuhimu mkubwa kwangu na maisha yangu ya soka," Hojlund alikiambia kituo cha utangazaji cha Denmark TV2.

    "Ninacheza dhidi ya mwanasoka bora zaidi duniani na kufunga na kuwa mshindi wa [mechi], haiwezi kuwa bora zaidi.

    "Kufunga dhidi yake na Ureno ni kitu kubwa, nilienda kumuona 2009, ambapo alifunga kwa mkwaju wa fauli, na nimekuwa shabiki wake tangu wakati huo."

    Nyota wa zamani wa Manchester United na Real Madrid Ronaldo, ambaye sasa anachezea klabu ya Saudi Pro League ya Al Nassr, aliichezea Ureno dakika 90.

    Juhudi za Hojlund katika dakika ya 78 zilimaanisha alifunga katika mechi mfululizo kwa klabu na nchi baada ya kumaliza ukame wa mabao 21 dhidi ya Leicester kwenye Ligi ya Premia wikendi iliyopita.

    Ushindi ulistahili kwa Wadenmark, na mkufunzi mpya Brian Riemer, na wataelekea Lisbon kwa mechi ya mkondo wa pili Jumapili wakiwa wamejiamini.

    Awali Christian Eriksen alipata mkwaju wa penalti wa kipindi cha kwanza uliookolewa na Diogo Costa, ambaye aliruka upande wake wa kulia na kuuwahi mpira huo ukielekea kona.

    Denmark walikuwa wamepewa mkwaju wa penalti baada ya Eriksen kuushika kwa mkono mpira wa Renato Veiga kwenye eneo la hatari.

  10. Trump atia saini agizo la kuivunja idara ya elimu Marekani

    Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini agizo kuu la kuvunja Idara ya Elimu, kutimiza ahadi ya kampeni na lengo la muda mrefu la baadhi ya wahafidhina.

    Akiishtumu idara hiyo kwa "kushindwa kupumua", rais wa chama cha Republican aliapa kurudisha pesa inazodhibiti kwa majimbo mahususi.

    "Tutaifunga haraka iwezekanavyo," Trump alisema, ingawa Ikulu ya White House ilikiri kwamba kuifunga idara hiyo moja kutahitaji kuungwa mkono na mabunge ya Congress.

    Hatua hiyo tayari inakabiliwa na changamoto za kisheria kutoka kwa wale wanaotaka kuzuia kufungwa kwa idara hiyo pamoja na kupunguzwa kwa wafanyikazi wake.

    Akiwa amezungukwa na watoto walioketi kwenye madawati ya shule katika Ikulu ya White House siku ya Alhamisi, Trump alisema "Marekani inatumia pesa nyingi zaidi katika elimu kuliko nchi nyingine yoyote", lakini aliongeza kuwa wanafunzi wanashika nafasi ya chini kabisa ya orodha hiyo.

    Ikulu ya White House ilisema kuwa utawala wake utachukua hatua ya kukata sehemu za idara ambazo zimesalia ndani ya mipaka ya kisheria.

    Amri ya utendaji huenda ikakabiliwa na changamoto za kisheria, kama vile juhudi nyingi za utawala wa Trump kupunguza ukubwa wa serikali ya shirikisho.

    Katika hafla ya utiaji saini, Trump alimsifu Linda McMahon, ambaye alimteua kuongoza idara hiyo, na kuelezea matumaini yake kuwa atakuwa waziri wa mwisho wa elimu.

    Alisema atapata "kitu kingine" cha kufanya ndani ya utawala. Baada ya Trump kutia saini agizo hilo, Seneta wa chama cha Republican cha Louisiana Bill Cassidy alitangaza mipango ya kuleta sheria inayolenga kuifunga idara hiyo.

    Lakini Warepublican wanashikilia kura ndogo ya 53-47 katika Seneti, na kufunga idara ya shirikisho kutahitaji kura 60, ili kufanya hatua hiyo kuwa ya kudumu .

  11. Zelensky aiambia Urusi kukoma kutoa masharti 'yasiyo muhimu' kabla ya mazungumzo ya amani

    Volodymyr Zelensky amesema maafisa wa Ukraine na Marekani watakutana kwa mazungumzo ya amani nchini Saudi Arabia Jumatatu ijayo, baada ya Kremlin kuthibitisha mazungumzo ya Marekani na Urusi siku hiyo hiyo.

    Kiongozi wa Ukraine alisema Rais wa Urusi Vladimir Putin "lazima akome kutoa matakwa yasiyo ya lazima ambayo yanaongeza muda wa vita".

    Madai ya Moscow ni pamoja na kukomesha kabisa msaada wa kijeshi kwa Ukraine.

    Zelensky pia alionya kwamba kuondoa suala la uanachama wa Nato kwa Ukraine kwenye meza - ni kitu ambacho Putin amesema hakiwezi kujadiliwa kwa amani - itakuwa "zawadi kubwa kwa Urusi".

    Pia alikanusha madai ya Ikulu ya White House kwamba alijadili kukabidhi umiliki wa vinu vya nyuklia vya Ukraine kwa Marekani wakati wa mazungumzo na Rais Donald Trump.

    Mazungumzo ya hivi punde yanajiri wakati ambapo Marekani inajaribu kusuluhisha usitishaji mapigano kati ya mataifa hayo mawili baada ya mapigano ya zaidi ya miaka mitatu.

    Zelensky na Putin wamekubaliana kusitisha mapigano kimsingi wakati wa mazungumzo na Marekani - lakini hakuna makubaliano yalioafikiwa kufikia sasa kutokana na hali zinazokinzana.

    Kiongozi wa Urusi hivi majuzi alikubali kusitisha mashambulizi ya angani dhidi ya miundombinu ya nishati - lakini mashambulizi kama hayo kutoka pande zote mbili yanaendelea.

    Zelensky alisema ujumbe wa Ukraine utaikabidhi Marekani orodha ya miundombinu inayotaka kulindwa dhidi ya mashambulizi ya Urusi katika mazungumzo ya Jumatatu.

  12. Habari za hivi punde, Jeshi la Sudan ladhibiti ikulu ya Rais mjini Khartoum

    Jeshi la Sudan limechukua udhibiti kamili wa Ikulu ya Rais mjini Khartoum siku ya Ijumaa, Televisheni ya Sudan na vyanzo vya kijeshi vimesema, katika mojawapo ya mafanikio makubwa katika mzozo wa miaka miwili unaotishia kusambaratisha nchi hiyo.

    Jeshi lilikuwa likifanya msako katika maeneo yanayozunguka ikulu kuwasaka wanachama wa Kikosi cha RSF, duru zimesema.

    Video na picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kuthibitishwa na BBC zinaonyesha wanajeshi wakishangilia kwa bunduki zao na kupiga magoti kuomba.

    Nabil Abdallah, msemaji wa jeshi, alisema kwenye TV ya serikali kwamba wanajeshi walidhibiti ikulu na majengo ya wizara katikati mwa Khartoum.

    "Vikosi vyetu viliharibu kabisa wapiganaji na vifaa vya adui, na kukamata vifaa na silaha nyingi," Abdallah aliongeza.

    Kundi la wapiganaji wa RSF kwa haraka lilichukua udhibiti wa ikulu na sehemu kubwa ya mji mkuu wakati wa kuzuka kwa vita mwezi Aprili 2023, lakini Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan katika miezi ya hivi karibuni vimerudi na kuelekea ikulu kando ya Mto Nile.

    RSF, ambayo mapema mwaka huu ilianza kuanzisha serikali sambamba, inashikilia udhibiti wa baadhi ya maeneo ya Khartoum na nchi jirani ya Omdurman, pamoja na magharibi mwa Sudan, ambako inapigania kutwaa ngome ya mwisho ya jeshi huko Darfur, al-Fashir.

    Kuteka mji mkuu kunaweza kuharakisha jeshi kuchukua kikamilifu Sudan ya kati, na kuimarisha mgawanyiko wa eneo la mashariki-magharibi kati ya nchi hizo mbili.

    Pande zote mbili zimeapa kuendelea kupigania sehemu iliyobaki ya nchi, na hakuna juhudi zozote za mazungumzo ya amani zilizotekelezwa.

    Vita hivyo vilizuka huku kukiwa na mzozo wa madaraka kati ya jeshi la Sudan na RSF kabla ya mpango wa mpito kuelekea utawala wa kiraia.

    Unaweza pia kusoma:

  13. Uwanja wa ndege wa Heathrow nchini Uingereza kufungwa siku nzima leo kutokana na kukatika kwa umeme

    Uwanja wa Ndege wa Heathrow nchini Uingereza utafungwa siku yote Ijumaa kutokana na hitilafu "kubwa" ya umeme iliyohusishwa na moto katika kituo kidogo cha kusambaza umeme.

    Uwanja huo wa ndege, ambao ndio wenye shughuli nyingi zaidi nchini Uingereza, umeonya kuhusu "usumbufu mkubwa" katika siku zijazo na kuwaambia abiria wasisafiri "kwa hali yoyote" hadi utakapofunguliwa tena.

    "Ili kudumisha usalama wa abiria wetu na wenzetu, hatuna chaguo ila kufunga Heathrow hadi 23:59 mnamo Machi 21, 2025," msemaji alisema.

    "Tunajua hili litakatisha tamaa abiria lakini tunataka kuwahakikishia kuwa tunafanya bidii iwezekanavyo kutatua hali hiyo," waliongeza.

    "Huku wafanyakazi wa zimamoto wakishughulikia tukio hilo, hatuna uwazi kuhusu ni lini nguvu za umeme zinaweza kurejeshwa kwa uhakika," msemaji wa Heathrow alisema.

    Uwanja huo wa ndege umeomba radhi kwa usumbufu huo na umewashauri abiria kuwasiliana na mashirika yao ya ndege kwa taarifa zaidi.

    Heathrow ndio uwanja mkubwa zaidi wa usafiri wa anga nchini Uingereza, ukishughulikia karibu ndege 1,300 zinazotua na kupaa kila siku.

    Rekodi ya abiria milioni 83.9 walipitia vituo vyake mwaka jana, kulingana na data yake ya hivi karibuni.

    Angalau safari 1,351 za ndege kwenda na kutoka Heathrow zitaathiriwa na hatua hii, tovuti ya ufuatiliaji wa safari za ndege ya Flightradar24 ilisema kwenye X, na baadhi ya ndege 120 zilizoathiriwa tayari ziko angani mapema asubuhi.

    Moto katika kituo kidogo cha Hayes, magharibi mwa London, umeacha maelfu ya nyumba bila umeme na kusababisha karibu watu 150 kuhamishwa kutoka katika maeneo yaliyopo na uwanja huo.

    Huduma za dharura ziliitwa kwa mara ya kwanza kwenye eneo la tukio saa 23:23 siku ya Alhamisi, na video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ilionyesha miale ya moto na moshi ukifuka kutoka kwa kituo hicho usiku kucha. Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.

  14. Maandamano ya usiku wa pili yazuka Uturuki licha ya marufuku

    Polisi mjini Istanbul wametumia gesi ya kutoa machozi na risasi za mpira dhidi ya waandamanaji katika usiku ya pili ya machafuko baada ya kukamatwa kwa Meya wa Istanbul Ekrem Imamoglu - licha ya marufuku ya siku nne ya kufanyika kwa maandamano hayo.

    Imamoglu - mwanachama wa chama kisicho na dini cha Republican People's Party (CHP) na mpinzani mkuu wa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan - alitarajiwa kutajwa kuwa mgombea urais katika uchaguzi wa urais wa 2028 baadaye wiki hii.

    Siku ya Jumatano, alikuwa mmoja wa watu 106 walioshikiliwa kwa mashtaka yakiwemo ufisadi na kusaidia makundi ya kigaidi.

    Tangu wakati huo, viongozi nchini Uturuki wamewakamata watu kadhaa kwa "machapisho ya uchochezi" kwenye mitandao ya kijamii.

    Akijibu maandamano hayo, Rais Erdogan wa Uturuki aliwashutumu wapinzani wake wa kisiasa kwa kushiriki katika maandamano hayoi.

    "Wamekiuka sheria kiasi kwamba wako katika hali ya kushambulia polisi wetu, kutoa vitisho kwa majaji, waendesha mashtaka," alisema.

    Akihutubia umati wa waandamanaji nje ya ukumbi wa jiji la Istanbul, Ozgur Ozel, kiongozi wa chama cha Imamoglu CHP, aliishutumu serikali kwa kujaribu "mapinduzi" na kusema watu walikuwa na haki ya kuandamana.

    Waziri wa Mambo ya Ndani Ali Yerlikaya alitangaza Alhamisi asubuhi kwamba polisi wamewatambua "wasimamizi wa akaunti za washukiwa" 261 mtandaoni ambao wanadaiwa kuchapisha maudhui "yaliyochochea umma kwenye chuki na uhasama" na "uchochezi wa kufanya uhalifu".

    "Washukiwa thelathini na saba walikamatwa na juhudi zinaendelea kuwakamata washukiwa wengine," alisema, akiongeza kuwa zaidi ya machapisho milioni 18.6 yalionekana mtandaoni kuhusu kukamatwa kwa watu hao wa Jumatano saa 0600 saa za ndani (0300 GMT) siku ya Alhamisi.

    Ujumbe uliotumwa kwenye akaunti ya X ya Imamoglu siku ya Alhamisi uliitaka Uturuki "kusimama dhidi ya uovu huu kama taifa", na kuwataka wajumbe wa mahakama na wa chama cha Erdogan kupambana na dhuluma.

    "Matukio haya yamepita zaidi ya vyama vyetu, maadili ya kisiasa. Mchakato sasa unahusu watu wetu, yaani familia zenu," Imamoglu alisema.

    "Ni wakati wa kupaza sauti zetu."

    Meya wa Istanbul huenda alitumia usiku wake wa kwanza kizuizini lakini manispaa hiyo bado inadhibitiwa na chama chake cha upinzani.

  15. Netanyahu amfuta kazi mkuu wa Ujasusi wa Israel kwa 'kutokuwa muaminifu'

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amemfuta kazi mkuu wa idara ya ujasusi wa taifa hilo kutokana na kushindwa kuligundua shambulio la 7 Oktoba 2023 la Hamas.

    Baraza la mawaziri la Israel lilikutana Alhamisi jioni ili kuidhinisha rasmi kufutwa kazi mapema kwa Ronen Bar, ambaye aliteuliwa Oktoba 2021 kwa muhula wa miaka mitano kama mkuu wa Shin Bet.

    Netanyahu alitangaza nia yake ya kumfukuza Bw Bar katika taarifa yake ya video siku ya Jumapili, akitaja "kutokuaminiana" kati ya wanaume hao wawili ambao alisema "kumekua baada ya muda".

    Hatua hiyo ilizua hasira na kuchochea zaidi maandamano dhidi ya serikali mjini Jerusalem, ambayo yalishuhudia maelfu ya Waisraeli wakiungana na waandamanaji wanaopinga mashambulizi mapya ya Israel dhidi ya Gaza.

    Tangu Jumanne, Israel imeanzisha wimbi kubwa la mashambulizi dhidi ya kile ilichosema kuwa ni wapiganaji wa Hamas katika ardhi ya Palestina, na hivyo kumaliza mapatano tete ambayo yalikuwa yamedumu kwa muda wa miezi miwili.

    Shin Bet ni wakala wa kijasusi wa ndani wa Israeli na una jukumu muhimu katika vita. Shughuli na uanachama wake ni siri za serikali zinazoshikiliwa kwa karibu.

    Bw Bar ametaja uamuzi wa kumtimua kuwa umechochewa kisiasa. Mwanasheria Mkuu wa Israel Gali Baharav-Miara - mkosoaji mkubwa wa Netanyahu ambaye mwenyewe anakabiliwa na kesi ya kufutwa kazi - alidai kuwa Bw Bar hangeweza kufukuzwa kazi hadi uhalali wa hatua hiyo kutathminiwa.

    Barua iliyotumwa na Netanyahu kwa wajumbe wa serikali yake kabla ya mkutano huo ilirejelea "kupotea kwa uaminifu wa kitaalam na kibinafsi" kati ya waziri mkuu na Bw Bar, na kupendekeza kumalizika kwa muhula wake tarehe 20 Aprili.

    "Kupotea kwa uaminifu wa kitaaluma kumeimarishwa wakati wa vita, zaidi ya kushindwa kwa uendeshaji wa 7 Oktoba [2023], na hasa katika miezi ya hivi karibuni," ilisema, ikirejelea mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israeli ambayo yalisababisha vita vya Israel-Gaza.

    Takriban watu 1,200 waliuawa na 251 kuchukuliwa mateka wakati wa mashambulizi hayo. Israel ilijibu kwa mashambulizi makubwa ya kijeshi, ambayo yameua zaidi ya Wapalestina 48,500, wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas inasema.

  16. Putin atavunja makubaliano ya amani na Ukraine yasipolindwa - Uingereza

    Rais wa Urusi, Vladimir Putin, atavunja makubaliano ya amani na Ukraine ikiwa hayatakuwa na ulinzi, amesema Sir Keir Starmer, baada ya kuhudhuria mkutano wa viongozi wakuu wa jeshi mjini London.

    Waziri Mkuu wa Uingereza alisema makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano kati ya Urusi na Ukraine yatakuwa ya kudumu tu ikiwa kutakuwa na mipango ya kiusalama.

    Alikuwa akizungumza huko Northwood, London, ambapo zaidi ya nchi 20 zilihudhuria mkutano wa faragha kujadili mapendekezo ya kupeleka wanajeshi nchini Ukraine ili kusaidia kuhakikisha usalama wa nchi hiyo kama sehemu ya makubaliano yoyote ya amani.

    Sir Keir alisema mipango ya usalama lazima iwe kwa Urusi kuwa kutakuwa na "matokeo makali" ikiwa itavunja makubaliano yoyote.

    Waziri Mkuu huyo alisema Uingereza na washirika wake wanapiga hatua kutoka kwenye "msukumo wa kisiasa" hadi "mpango wa kijeshi", ambao alisema lazima ufanyike sasa kabla ya makubaliano kufikiwa.

    Alisema: "Ni muhimu sana tufanye kazi hiyo kwa sababu tunajua jambo moja kwa uhakika, nalo ni kuwa makubaliano yasiyo na kitu chochote nyuma yake ni jambo ambalo Putin atavunja.

    "Tunajua hilo kwa sababu lilitokea hapo awali. Niko wazi kabisa akilini mwangu kuwa litatokea tena."

    Sir Keir alikanusha mpango wa kuondoa wanajeshi wa Uingereza kutoka nchi kama Estonia ili kuwapeleka Kyiv, akisema: "Hakuna kurudi nyuma kuhusu ahadi zetu kwa nchi nyingine."

    Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, John Healey, alihudhuria mkutano huo wa faragha wa viongozi wa kijeshi kutoka nchi zinazounda kile ambacho Sir Keir ameita "muungano wa wenye nia".

    Downing Street ilisema viongozi hao wa kijeshi wangekuwa wakihusika katika "mpango wa kina" wa maelezo ya uwezekano wowote wa kupelekwa kwa wanajeshi Ukraine.

    Uingereza iliitisha mkutano wa wakuu wa jeshi baada ya mkutano wa kilele uliofanyika mapema mwezi huu ulioshirikisha nchi 26.

  17. Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja