Barua ya maridhiano ya Zelensky kwa Trump inaonyesha hana chaguo jingine

    • Author, James Waterhouse
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Ikiwa uamuzi wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wa kurekebisha uhusiano na mwenzake wa Marekani Donald Trump ni wa busara au la, inategemea ni nani unayemuuliza swali hilo.

"Uamuzi huu ni mbaya sana," anasema mwanablogu na mtumishi wa jeshi Yuriy Kasyanov, ambaye anadhani Marekani "haitaisaidia Ukraine kwa chochote" baada ya mkataba wa madini kutiwa saini.

Jana usiku, kiongozi wa Ukraine alitoa hotuba yake ya jioni kwenye ua nje ya Ofisi ya Rais ya Kyiv. Ni sehemu ile ile ambapo alitoa hotuba maarufu ya "sisi sote tuko hapa" akiwa na baraza lake la mawaziri katika siku ya pili ya uvamizi wa Urusi.

Wakati huo, alikataa ofa za kuondoka Ukraine. Watu wengi katika nchi za Magharibi walitarajia Urusi itafika mji mkuu ndani ya siku chache, na rais atakamatwa au kuuawa.

Miaka mitatu imepita, na sasa inaonekana chaguo lake la kuendelea kupigana linabadilika hatua kwa hatua.

Amesema yuko tayari kufanya kazi chini ya "uongozi imara" wa Trump na ni "wakati wa kurekebisha mambo."

Mazungumzo ya malumbano huko Washington katika Ikulu ya rais, na Trump "kusitisha" misaada ya kijeshi ya Marekani, kumemlazimu Zelensky kupigia goti dira ya amani ya Trump.

Hadi wiki iliyopita, Zelensky alikuwa bado ameshikilia kuwa Ukraine itakubali tu amani ikiwa itahakikishiwa usalama wake, vinginevyo itaendelea kupigana.

Pia alimshutumu Trump kwa kuishi katika "upotoshaji" baada ya rais wa Marekani kurudia baadhi ya madai ya Moscow.

Haya yote yalifungua mabishano makali siku ya Ijumaa kati ya Zelensky na Trump na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, ambao walimtuhumu Zelensky kwa "kuivunjia heshima" Marekani na hatimaye kumwambia aondoke.

Kiongozi wa Ukraine alipata mapokezi mazuri kutoka kwa viongozi wa Ulaya mwishoni mwa juma - lakini wakati wanaahidi kusaidia kuilinda Ukraine katika siku zijazo, walisema wazi kwamba kufikia amani kutahitaji ushiriki wa Marekani.

Kisha, siku ya Jumanne, Trump alisitisha usaidizi wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine, na kuzusha wasiwasi kwamba Ukraine itaweza kupigana kwa muda wa miezi kadhaa tu – na hilo likamfanya Zelensky kusaka amani na hali hiyo.

Pia unaweza kusoma

Barua ya Zelensky

Katika barua yake kwa rais wa Marekani, ametoa maelezo juu ya hatua ya kwanza ya mchakato wa amani namna itakavyoweza kuwa, ikiwa ni pamoja na usitishaji vita vya majini na angani - pendekezo ambalo awali lilipendekezwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron mwishoni mwa juma.

Trump amesema anashukuru kwa barua hiyo, ikiwa ni ishara ya kutuliza mvutano kati ya viongozi hao wawili, na Zelensky amekubali kufanya makubaliano ya amani.

Na jambo kubwa zaidi ni nia ya Zelensky sasa ya kutia saini mkataba wa madini bila hakikisho la usalama wa Ukraine – ni jambo ambalo alilionyesha kuwa ni la muhimu hadi siku za hivi karibuni.

Marekani inasema kuwepo kwa makampuni ya Marekani yanayochimba madini kutatosha kuifanya Urusi kutotaka kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano. Lakini biashara za Marekani hazikuizuia kabisa Moscow kutofanya uvamizi wake.

Jambo kubwa zaidi ni Urusi kukataa kujishusha ili kufanya makubaliano yoyote ya amani.

Pengine Zelensky ameishiwa na mbinu za kisiasa, huku washirika wake wa Ulaya wakikubali kwamba bado wanaihitaji Marekani, Washington panaonekana bado ndio mahali pekee kwake kukimbilia.