Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Bila Marekani ni vigumu kuikabili Urusi- Zelensky
Zelensky anasema hayo kufuatia majibizano yake na Trump yaliyosababisha kuvunjika kwa kikao chao ambacho sasa kimeweka rehani mustakabali wa kutafuta muafaka wa vita vya Ukraine
Moja kwa moja
Na Martha Saranga na Munira Hussein
Waislamu waanza mwezi mtukufu wa Ramadhani
Waislamu zaidi ya bilioni 1.8 duniani wameanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Saudi Arabia na mataifa mengine mengi ya Mashariki ya Kati yalitangaza kuanza kwa Ramadhan Ijumaa usiku baada ya kuonekana kwa mwezi mwandamo katika ufalme huo, ambao ni makao ya maeneo mawili matakatifu zaidi ya Uislamu.
Algeria, Misri, Jordan, Libya, Sudan na Tunisia pia zilitangaza kuwa zitaanza kufunga kuanzia Jumamosi, pamoja na maeneo ya Palestina yaliyoathiriwa na vita vya Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Waislamu wa madhehebu ya Sunni nchini Lebanon pia walianza kufunga Jumamosi.
Ofisi ya Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei, na kiongozi mkuu wa Shia wa Iraq, Ali al-Sistani, walitangaza Jumapili kuwa siku ya kwanza ya Ramadhan.
Morocco, Tanzania na Kenya pia itaanza kufunga kuanzia Jumapili. Nchini Pakistan na India, uangalizi wa mwezi utafanyika Jumamosi jioni, na kufunga kunatarajiwa kuanza Jumapili.
Katika Kusini Mashariki mwa Asia, nchi yenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu duniani, Indonesia, imeanza Ramadhan siku ya leo Jumamosi, huku mataifa jirani kama Malaysia, Brunei na Ufilipino yakitarajiwa kuanza mwezi huu wa ibada siku ya Jumapili.
Kufunga Ramadhan ni moja ya nguzo tano za Uislamu, ikiwataka waumini kujizuia kula, kunywa, kuvuta sigara na kushiriki tendo la ndoa wakati wa mchana.
Waislamu pia wanahimizwa kutoa sadaka kwa maskini.
Soma pia;
Kifo kingine cha Ebola charipotiwa Kampala
Wizara ya afya nchini Uganda imeripoti kwa mara nyingine kuhusu ugonjwa wa Ebola jijini Kampala,siku chache baada ya kuwaaachilia watu 8 ambao maafisa walisema wamepona virusi hivyo kufuatia kupatiwa matibabu katika hospitali za rufaa Mulago na Mbale,kwa mujibu wa Daily monitor.
''Kufuatia mlipuko wa virusi vya Ebola nchini Sudan Januari 30 mwaka huu, wizara ya afya inaufahamisha umma kuhusiana na mgonjwa mmoja aliyepatikana Mulago'' gazeti la Daily Monitor lilinukuu taarifa ya wizara ya afya.
Mgonjwa aliyefariki alibainika kuwa mtoto aliyekuwa na umri wa miaka minne na nusu.
Mgonjwa huyo alifikishwa hospitali na kufikwa umauti akiwa na dalili za Ebola kutoka Hospitali ya Mulago siku ya Jumanne, Februari 25.
Hadi leo, jumla ya wagonjwa 10 wameshathibitishwa.
Wizara ya afya ya Uganda imesisitiza kuendelea kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti virusi hivyo ikiwemo kuwasaka waliokutana na kuambukizwa, kuwafuatilia kuwadhibiti wasikutane na kuambukiza wengine na kutoa chanjo.
''Wataalamu wametaja dalili zinazojulikana kuwa za Ebola ni pamoja na homa kali, uchovu, maumivu ya kifua, kuharisha, kutapika damu, na macho kupata manjano'', ilieleza wizara ya afya ya Uganda.
Soma pia;
Vatican yasema Papa Francis amelala vizuri baada ya changamoto ya kiafya usiku
Papa Francis, ambaye amekuwa hospitalini kwa zaidi ya wiki mbili akipambana na homa ya mapafu, alilala kwa utulivu na alikuwa akipumzika siku ya Jumamosi baada ya hali yake ya afya kuzorota siku iliyotangulia, Vatican ilisema.
Papa mwenye umri wa miaka 88 alipata tatizo la kupumua siku ya Ijumaa, jambo lililoibua upya wasiwasi kuhusu hali yake ya afya.
Katika taarifa fupi ya mstari mmoja, Vatican ilisema usiku uliopita ulipita kwa utulivu.
Siku ya Ijumaa, Vatican ilisema Papa Francis alipata tatizo la ghafla la kupumua, likijumuisha "kutapika kwa kuingiza pumzi na kuzorota kwa ghafla kwa hali ya kupumua".
Alihitaji msaada wa kunyonya (aspiration) ili kuondoa matapishi kwenye njia zake za hewa, Vatican ilisema, na pia alihitaji mashine ya kupumua isiyo ya uvamizi (non-invasive mechanical ventilation) – jambo ambalo linamaanisha hakuwekewa mirija ya kupumulia (intubation), hali ambayo ingehitaji kumlewesha kwa dawa.
Francis amepata vipindi kadhaa vya matatizo ya kiafya katika miaka miwili iliyopita na huwa katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya mapafu kwa sababu alipata pleurisy akiwa kijana na sehemu ya pafu lake iliondolewa.
Papa hajaonekana hadharani tangu alipoingia hospitalini, ikiwa ni kipindi kirefu zaidi cha kutokuwa mbele ya watu tangu aliposhika madaraka ya upapa mnamo Machi 2013.
Soma pia;
Rais wa kwanza wa Namibia Sam Nujoma azikwa Windhoek
Mazishi ya raisi wa kwanza wa Namibia aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95 yamefanyika jumamosi, ambapo viongozi wa zamani na wa sasa wa Afrika walihudhuria katika jiji kuu Windhoek.
Muasisi mkuu katika mapambano ya uhuru wa nchi hiyo alifariki wiki mbili zilizopita akiwa na umri wa miaka tisini na tano.
Viongozi kadhaa wa Afrika walihudhuria mazishi, wakiwemo Cyril Ramaphosa kutoka Afrika Kusini, Joao Lourenco kutoka Angola na Emmerson Mnangagwa kutoka Zimbabwe.
Gari la jeshi lilibeba jeneza la Sam Nujoma - lililozungushiwa bendera ya Namibia yenye rangi ya buluu, nyekundu na kijani - hadi eneo la Heroes' Acre nje ya mji mkuu Windhoek.
Eneo hili maalum kwa ajili ya makaburi ya waasisi waliopigana dhidi ya utawala wa kikoloni wa Ujerumani na baadaye utawala wa Afrika Kusini.
Rais wa sasa, Nangolo Mbumba, aliongoza shughuli za kutoa heshima za mwisho akimuelezea Sam Nujoma kama mtu mkuu miongoni mwa viongozi waliopata kutokea nchini humo.
Aliongoza Namibia katika vita vikali vya msituni dhidi ya serikali ya ubaguzi wa rangi ya Afrika Kusini hadi taifa hilo kupata uhuru.
Baada ya uhuru, wakosoaji wa Nujoma walieleza utawala wake kama wa kiimla.
Soma pia;
Ukraine iko tayari kusaini mkataba wa madini - Zelensky
Zelensky, ambaye anasema Ukraine "iko tayari kusaini mkataba wa madini" lakini anendelea kutoa wito wake wa kuhakikishiwa usalama na Marekani.
Ni vigumu kuikabili Urusi bila msaada wa Marekani.
"Kusitisha mapigano bila dhamana ya usalama ni hatari kwa Ukraine," anasema.
Zelensky anasema kwamba Rais wa Marekani Donald Trump anataka kumaliza vita, "lakini hakuna anayetaka amani kuliko sisi tunavyohitaji."
"Usitishaji mapigano hautatekelezwa na Putin.
Amekiuka makubaliano ya kusitisha mapigano mara 25 katika miaka kumi iliyopita. Amani ya kudumu ndiyo suluhisho pekee," anasema.
Zelensky anasema "haiwezekani kubadilisha msimamo wa Ukraine kuhusu Urusi."
"Warusi wanatuua. Urusi ni adui, na hiyo ndiyo hali tunayokabiliana nayo.
Ukraine inataka amani, lakini lazima iwe amani ya haki na ya kudumu.
Kwa hiyo, tunahitaji kuwa na nguvu katika meza ya mazungumzo."
Soma pia;
Ukraine inahitaji kusikilizwa na si kusahaulika - Zelensky
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, anasema ni muhimu "Ukraine isikilizwe na kwamba hakuna atakayesahau hilo, iwe wakati wa vita au baadaye."
Aliandika katika mtandao wa Telegram, akisema ni muhimu kwa watu wa Ukraine "kujua kwamba hawako peke yao" na kwamba "maslahi yao yanawakilishwa katika kila nchi, kila pembe ya dunia."
"Shukrani kwa msaada wenu katika kipindi hiki kigumu, kwa jitihada zote kwa ajili ya Ukraine na rai awa Ukraine na kwa msaada wenu - sio tu wa kidiplomasia na kifedha, bali pia wa kisiasa na wa maombi," anaandika.
Kiongozi huyo wa Ukraine alikutana na Donald Trump katika Ikulu ya Marekani ijumaa kwa ajili ya kutia saini mkataba wa madini adimu ya Ukraine, mkataba ambao hata hivyo haukutiwa saini baada ya kikao kuvunjika.
Kundi la Wakurdi la PKK latangaza kusitisha mapigano na Uturuki
Kundi lililopigwa marufuku la Kikurdi la PKK limetangaza kusitisha mapigano na Uturuki baada ya kiongozi wake aliyeko gerezani Abdullah Ocalan kulitaka vuguvugu hilo kusalimisha silaha.
Katika taarifa yake siku ya Jumamosi, PKK lilisema linatumai Uturuki itamwachilia Ocalan, ambaye amekuwa katika kifungo tangu 1999, ili aweze kuongoza mchakato wa kusalimisha silaha.
Hatua hiyo inafuatia wito wake wiki hii unaolenga kutamatisha miongo minne ya makabiliano kusini-mashariki mwa Uturuki ambapo makumi kwa maelfu ya watu wameuawa.
Tangazo lake limekuja miezi kadhaa baada ya Devlet Bahceli, kiongozi wa chama cha MHP chenye msimamo mkali na mshirika wa serikali ya Uturuki, kuanzisha mpango wa kumaliza mzozo huo.
PKK - kundi linalosimamia Chama cha Wafanyakazi wa Kikudrdi lilitaka mamlaka kumpunguzia adhabu Ocalan na kuongeza "lazima aweze kuishi na kufanya kazi kwa uhuru na kuwa na uwezo wa kufanya uhusiano na mtu yeyote anayetaka, ikiwa ni pamoja na marafiki zake".
Kundi hilo lilianza uasi tangu mwaka 1984, kwa lengo la kuwatengenezea Wakurdi makazi yao, ambao ni takriban asilimia 20 ya watu milioni 85 wa Uturuki.
Lilipigwa marufuku na kutangazwa kuwa kundi la kigaidi nchini Uturuki, Ulaya, Uingereza na Marekani.
Soma Pia;
Zelensky anataka mapambano tu - Trump
Trump aliwaambia waandishi wa habari ijumaa "kikao hakikwenda vizuri kabisa."
Alisema Zelensky "alijiamini kupita kiasi" katika mazungumzo, na kurudia madai kwamba Zelensky anatumia vibaya fursa ya majadiliano ya mustakabali wa amani.
Trump alisema Zelensky angekuwa "jasiri" kama angesaini mkataba wa madini uliopendekezwa na Marekani.
"Anataka kuendelea kupigana, sisi tunataka kumaliza vifo," Trump aliongeza.
Alipoulizwa kuhusu kiongozi wa Ukraine anapaswa kufanya nini ili kurejesha tena mazungumzo, Trump alisema "lazima aseme 'anataka amani'.
Hata hivyo rais huyo wa Marekani alirejelea msisitizo wa tishio lake la kuondoa msaada wa Marekani akisema; "tumalize hili au tumruhusu apigane."
Viongozi hao walikutana Ikulu ya Marekani kwa ajili ya kutia saini mkataba wa madini adimu ya Ukraine, mkataba ambao hata hivyo haukutiwa saini baada ya kikao kuvunjika.
Soma pia;
Zelensky asema uhusiano wao na Trump unaweza kurekebishwa
Katika kikao hicho,viongozi hao walikuwa wanakutana kwa ajili ya kutia saini mkataba wa madini adimu.
Hata hivyo kikao chao kilivurugwa baada ya kuanza kushutumiana kwa maneno makali na kunyoosheana vidole kuhusu vita vya Ukraine na Urusi.
Katika majibizazo yao Ikulu , Trump alimwambia kiongozi huyo wa Ukraine kwamba anacheza na vita ya tatu ya dunia. Trump alisema ' 'Unacheza na Vita ya tatu ya dunia'.
Alisema hivyo baada ya Zelensky kuonekana kutounga mkono mazungumzo ya Trump na makamu wake, JD Vance kuhusu namna Ukraine inavyoshughulika na mzozo wake na Urusi.
Kwa upande wake Zelensky alimwambia Trump ' usimchekee muuaji', akimrejelea rais wa Urusi, Vladmir Putin.
Marekani inataka Ukraine ikubaliane na Urusi kumaliza mzozo huo kwa namna ambayo Zelensky hakubaliani nayo.
Pia Trump pamoja na makamu wake wa rais, JD Vance walimtuhumu Zelensky kwa kutokua na heshima na kushindwa kuishukuru Marekani kwa msaada mkubwa inayoutoa kwa taifa hilo kwenye vita yake na Urusi.
'Unajifanya mwamba' alisema Trump huku Zelensky akisema ' yanayoendelea Ukraine huwezi kuyahisi sasa, ila baadaye utayahisi", akirejelea maumivu ya vita. Kwenye hili Trump alidakia kusema " usitusemee tutakavyohisi sie".
Trump alimwambia pia Zelensky "amemkosea heshima" na kusema "tufanye makubaliano au tuondoke".
Baada ya maneno makali kikao chao kilichokuwa kinarushwa moja kwa moja kilivunjika na hata kile ambacho wangefanya baadae mbele ya wanahabari pia kilivunjika.
Zelensky aliondolewa kwa maelekezo ya Ulinzi wa Ikulu na kuondoka kwa hasira, hakusindikizwa na mwenyeji wake kama ilivyo ada kwa viongozi wakuu wa nchi wanapotembeleana.
Baadae, akiongea na Fox News, Zelensky alisema ugomvi wao hapo jana haukuwa wa manufaa kwa pande zote mbili, lakini anadhani kwamba unaweza kurekebishwa.
Trump yeye aliandika kwenye mtandao wa X kwamba Zelensky anaweza kurejea mezani tena akiwa tayari kwa mazungumzo.
Soma pia;
Hujambo, karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja