Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mlipuko wa Ebola Uganda: Kwa nini hali ni mbaya?
Mlipuko wa Ebola nchini Uganda unaonekana kuwa mgumu zaidi kukabiliana nao kuliko milipuko ya hivi karibuni, lakini Rais Yoweri Museveni amekataa wito wa kuweka karantini maeneo yaliyoathirika zaidi.
Hadi kufikia sasa watu 31 wamethibitishwa kuambukizwa kuwa na virusi vya ugonjwa huo, ingawa inahofiwa idadi hiyo inaweza kuwa zaidi.
Ebola ni nini?
Ni virusi hatari vyenye dalili za awali ambazo zinaweza kujumuisha homa ya ghafla, udhaifu mkubwa, maumivu ya misuli na koo.
Dalili zinazofuata zinaweza kujumuisha kutapika, kuhara na katika hali nyingine kutokwa na damu ndani na nje, inayojulikana kama haemorrhaging
Kipindi cha kati ya kuambukizwa na vijidudu na kuonekana kwa dalili za ugonjwa kinaweza kudumu kutoka siku mbili hadi wiki tatu. Ebola inaweza kuhusishwa na magonjwa mengine kama vile malaria na typhoid.
Kwa nini mlipuko huu wa sasa ni mbaya sana?
Ukweli kwamba ilikuwa wiki tatu kabla ya kesi ya kwanza kugunduliwa mnamo 20 Septemba imesababisha wasiwasi.
Ebola huenea kati ya binadamu mmoja hadi mwingine kwa kugusana moja kwa moja na maji maji ya mwili na mazingira machafu. Mazishi yanaweza kuwa hatari hasa ikiwa waombolezaji wanawasiliana moja kwa moja na mwili.
Kesi nyingi kati ya 31 zilizotambuliwa ziko katika wilaya ya kati nchini Uganda ya Mubende, ambapo watu sita wamefariki.
Hata hivyo, huenda idadi ya waliofariki ikawa juu kwani wizara ya afya inasema kulikuwa na vifo 18, vinavyohusishwa na visa vilivyothibitishwa, ambapo sampuli hazikuchukuliwa kwani walizikwa kabla ya kupimwa.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linakadiria kiwango cha vifo vya kesi ni kati ya 41% na 100%.
Je, kuna chanjo?
Wasiwasi mwingine ni kwamba hii ni Ebola aina ya Sudan, ambayo hakuna chanjo iliyoidhinishwa, tofauti na aina ya kawaida ya Zaire.
Hii inamaanisha kuwa hakujakuwa na chanjo ya wafanyikazi wa afya, ambao walishughulikia kesi sita kati ya zilizothibitishwa.
Ugonjwa aina ya Zaire ulisababisha mlipuko mkubwa zaidi kuwahi kutokea wa Ebola Afrika Magharibi kuanzia Desemba 2013 hadi 2016. Zaidi ya watu 11,000 walifariki.
Huku kukiwa na visa zaidi ya 28,000 nchini Guinea, Liberia na Sierra Leone, wanasayansi walifanya utafiti wa kina kuhusu chanjo ya Ebola.
Miaka miwili baada ya janga hilo kuisha, chanjo ya Ervebo ambayo wakati huo haikuwa na leseni, iliyotengenezwa na Merck, ilitumiwa wakati wa kuzuka kwa aina ya Zaire, magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ilipewa kibali na WHO, ambayo ilisema ilikupungiuza maambukizi na kuokoa maisha.
Chanjo ya pili ya Johnson & Johnson imeidhinishwa kutumiwa na Wakala wa Dawa wa Ulaya (European Medicines Agency).
Lakini hakuna chanjo yoyote kati ya hizi ambayo imejaribiwa dhidi ya aina ya Sudan.
Hata hivyo Rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema serikali yake inachunguza kama inafaa kuwajaribu.
Je, Uganda inakabiliana vipi na mlipuko huo?
Lengo ni kufuatilia mawasiliano - kutafuta wale ambao wamekuwa karibu na wagonjwa, haswa wale waliohudhuria mazishi katika jamii.
Kituo cha afya chenye vitanda 51 kinafanya kazi katika wilaya ya Mubende, kitovu cha mlipuko huo, na kituo cha pili kinatarajiwa kuanzishwa hivi karibuni.
Rais Museveni alisema maabara mbili zinazohamishika zitatumwa Mubende kufikia Ijumaa, ili watu wasisafiri kwa uchunguzi na hivyo kuhatarisha kueneza virusi.
Madaktari wameelezea wasiwasi wao juu ya ukosefu wa vifaa vya kutosha vya kinga binafsi (PPE) kama vile glavu na barakoa. Pia wametaka eneo lililoathiriwa liwekwe chini ya karantini.
Hata hivyo, Rais Museveni alipuuzilia mbali vikwazo vya aina hiyo, akisema: "Ebola haienei kama corona[virusi]" kwani sio ugonjwa wa hewa.
Alisema masoko, shule na maeneo ya ibada yataendelea kuwa wazi, lakini aliwataka watu kuzingatia usafi binafsi na kuepuka kukaa karibu karibu.
Ebola inasambaa vipi?
Ebola imefika kwa binadamu kutoka kwa wanyama walioambukizwa, kama vile sokwe, popo na swala wa msituni.
Nyama ya msituni - wanyama wa porini wanaowindwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu inadhaniwa kuwa hifadhi ya asili ya virusi.
Kisha huenea kati ya binadamu kwa kugusana moja kwa moja na maji ya mwili wa mtu mwenye virusi kama vile damu, mate, matapishi, shahawa, uchafu ukeni, mkojo, kinyesi na jasho.
Wanaume ambao wamepona Ebola pia wamekutwa na virusi kwenye shahawa zao kwa muda baada ya kupona.
Ni tahadhari gani zinaweza kuchukuliwa?
Ili kuzuia maambukizo, wataalamu wa afya wanashauri kuepuka kugusana na walioambukizwa, ikiwa ni pamoja na kuacha kupeana mikono, kunawa mikono kwa sabuni na maji na kusafisha nyuso kwa maji ya klorini.
Pia ni muhimu kutenganisha wagonjwa na watu wanaokutana nao walio kwenye mawasiliano. Kwa kawaida nchi huweka vituo kwa ajili ya kesi zinazoshukiwa na vituo vya matibabu kwa kesi zilizothibitishwa kimaabara.
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo inapakana na Uganda, walionusurika na Ebola walikuwa na jukumu kubwa katika kutoa huduma kwa wagonjwa walioambukizwa kwani imethibitishwa kuwa hawawezi kuambukizwa tena.
Ingawa, timu za matibabu lazima zivae PPE kamili wakati wa kuhudumia wagonjwa ili kuzuia maambukizi.
Miili, kwenye mifuko ya kubebea miili lazima izikwe na wale waliovaa PPE vizuri. Ubunifu wa hivi karibuni zaidi umejumuisha kuwa na mifuko ya miili yenye vifuniko vilivyo wazi usoni ili kuwezesha familia kuutazama mwili kwa usalama kabla ya kuzikwa.