Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Wahudumu wa afya katika hospitali ya kuhudumia wagonjwa wa ebola wagoma Uganda

Madaktari wanaofanya kazi katika hospitali ya Mubende nchini Uganda wamegoma wakiishutumu serikali kwa kutowapatia vifaa vya usalama, posho za hatari na bima ya afya.

Moja kwa moja

  1. Tumefika tamati ya taarifa zetu za moja kwa moja, mpaka kesho panapo majaaliwa

  2. Wahudumu wa afya katika hospitali ya kuhudumia wagonjwa wa ebola wagoma Uganda

    Madaktari wanaofanya kazi katika hospitali ya Mubende nchini Uganda wamegoma wakiishutumu serikali kwa kutowapatia vifaa vya usalama, posho za hatari na bima ya afya.

    Hospitali hiyo, iliyoko umbali wa kilomita 150 kutoka mji mkuu, Kampala, inahifadhi kituo kikuu cha kutengwa kwa wagonjwa wa Ebola huku mlipuko huo ukiendelea kuenea katika eneo la kati.

    Wafanyakazi wote 34, wakiwemo madaktari, wafamasia na wauguzi walisema katika taarifa kwamba hawatarejea kazini na wanataka kuhamishwa hadi kwenye kituo kilicho na mazingira salama ya kufanya kazi.

    Wahudumu sita wa matibabu wanasemekana kuambukizwa virusi hivyo na kwa sasa wametengwa wakingoja matokeo ya maabara.

    Mamlaka zinasema kumekuwa na takriban visa 36 vinavyoshukiwa kuwa vya Ebola, ingawa si vyote vimethibitishwa.

    Takriban vifo 23 vinashukiwa kusababishwa na virusi hivyo.

    Mlipuko wa aina ya Ebola (Sudan) ulitangazwa nchini humo wiki iliyopita.

    Kifo cha kwanza kilichothibitishwa kilikuwa kijana wa miaka 24, ambaye alipoteza watu sita wa familia yake katika wiki mbili za kwanza za Septemba.

    Chanjo zinazopatikana dhidi ya virusi vinavyosababisha kuvuja damu haziwezi kutumika nchini Uganda kwa sababu zinafaa tu katika kukabiliana na aina ya Zaire ambayo ilikuwa nyuma ya mlipuko wa 2013 - 2016 huko Afrika Magharibi.

  3. Ndege zisizo na rubani za Uturuki zaungana kupambana na al-Shabab Somalia

    Somalia imethibitisha kuwa ndege zisizo na rubani za Uturuki zimejiunga na mashambulizi yanayoendelea ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wa al-Shabab wanaoshirikiana na al-Qaeda.

    Waziri wa Mambo ya Ndani wa Somalia Ahmed Mo'alim Fiqi aliiambia televisheni ya kibinafsi ya Universal Somali kwamba ndege za uchunguzi na kivita zinazomilikiwa na Uturuki zilitoa msaada wa anga kwa jeshi la Somalia.

    Katika wiki za hivi karibuni vikosi vya serikali ya Somalia na koo zenye silaha katikati mwa mikoa ya Hiiraan na Galgudud zimewaondoa al-Shabab kutoka baadhi ya maeneo.

    Televisheni ya taifa iliripoti kwamba jeshi lilipanua mashambulizi dhidi ya al-Shabab katikati mwa Somalia hadi sehemu za eneo la kusini-magharibi la Gedo, ambako wanamgambo hao wanashikilia baadhi ya maeneo.

    Uturuki ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikiunga mkono serikali ya Somalia.

    Mogadishu ni mwenyeji wa kambi kubwa zaidi ya kijeshi ya Uturuki iliyo ng'ambo, iliyofunguliwa mwaka 2017, ambapo maelfu ya wanajeshi wa Somalia wamekuwa wakifanya mazoezi.

  4. Gari la chakula cha msaada lashambuliwa Tigray

    Vifusi vya shambulio la ndege zisizo na rubani katika eneo la Tigray nchini Ethiopia viligonga lori lililokuwa limebeba misaada ya kibinadamu na kumjeruhi dereva siku ya Jumapili, msemaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP ameliambia shirika la habari la Reuters.

    "Shambulio hilo lilimejeruhi dereva aliyepewa kazi na WFP na kusababisha uharibifu mdogo kwa lori la WFP," msemaji huyo alinukuliwa akisema.

    Lori hilo lilikuwa likipeleka chakula kwa wakimbizi wa ndani huko Tigray, Reuters inaripoti.

    Msemaji wa kundi la waasi la TPLF Getachew Reda alitaja tukio hilo kuwa "uhalifu wa kutisha."Mashambulio kadhaa ya awali ya anga yameripotiwa na waasi wa Tigray tangu makabiliano mapya yalipozuka tarehe 24 Agosti - ambayo hayajakubaliwa na mamlaka ya shirikisho.

  5. Jengo la ghorofa saba laanguka Kenya na kuua watu watatu

    Takriban watu watatu wamefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya jengo lililokuwa likijengwa kuporomoka katika kaunti ya Kiambu karibu na mji mkuu wa Kenya Nairobi. Kuna hofu kwamba huenda watu wengi zaidi wamenaswa kwenye vifusi.

    Walioshuhudia wanasema jengo hilo liliangukia kwenye jengo lililo karibu. Shughuli za uokoaji kwa sasa zinaendelea huku wengi wakihofiwa kukwama kwenye vifusi. Wachimbaji wamehamishwa hadi kwenye eneo hilo ili kuondoa uchafu.

    Polisi wanasema kuwa jengo hilo liliporomoka kwenye nyumba moja katika Kaunti ya Kiambu na kuwatega wakazi kwenye vifusi.

    Watu waliookolewa akiwemo mtoto mchanga wamepelekwa katika hospitali iliyo karibu. Timu za dharura zinafanya juhudi kubwa kufikia manusura zaidi wakiwemo wafanyakazi wa ujenzi. Polisi wanachunguza kilichosababisha kuporomoka kwa jengo hilo.

    Hili ndilo tukio la hivi karibuni zaidi kutokea katika eneo linalolaumiwa kwa usanifu mbaya wa miundo au ujenzi wa holela.

  6. Mshindi wa bahati nasibu achoshwa na maombi ya misaada kila siku

    Mshindi wa bahati nasibu ya India amesema analemewa sana na maombi ya usaidizi wa kifedha hivi kwamba anajuta kupata jackpot hiyo.

    Anoop, dereva wa magari kutoka jimbo la kusini la Kerala, alikuwa ameshinda rupia 250m ($3.06m, £2.9m) katika bahati nasibu ya serikali ya jimbo mapema Septemba.

    Lakini wiki moja baadaye, alichapisha video akiomba watu asiowajua waache kumsumbua yeye na familia yake.

    Anoop anasema kwamba anafikiria kuhamisha nyumba ili kuepuka tahadhari nyingi za umma.

    Baada ya habari kuibuka za ushindi wake, familia yake ilitafutwa na vyombo vya habari vingi."Nilifurahi sana niliposhinda," anasema kwenye video yake ya hivi majuzi.

    "Kulikuwa na watu na kamera nyumbani na tulifurahi."Lakini hivi karibuni hali ilitoka nje ya udhibiti, anasema."Siwezi kutoka nyumbani, siwezi kwenda popote. Mtoto wangu ni mgonjwa na siwezi kumpeleka kwa daktari."

    Anoop - ambaye atapokea rupia 150mn baada ya ushuru wa serikali - anasema watu wanaanza kuwasili nyumbani kwake kila asubuhi.

    "Ninachoweza kumwambia kila mtu ni kwamba bado sijapata pesa. Hakuna anayeonekana kuelewa shida yangu, haijalishi ninasema mara ngapi," anasema.

    Anoop anasema yeye na familia yake wamekuwa wakikaa na jamaa kukwepa tahadhari.Serikali ya jimbo hilo imesema itapanga mpango wa siku wa mafunzo kwa Anoop kuhusu usimamizi wa fedha ili kumsaidia kutumia pesa hizo vyema.

  7. Habari za hivi punde, Shambulio la bunduki latokea katika shule Urusi

    Mtu mwenye silaha amefyatua risasi katika shule moja katikati mwa Urusi, na kuua takriban watu sita na kujeruhi ishirini, maafisa wa Urusi wanasema.

    Waathiriwa ni pamoja na wanafunzi na mlinzi wa shule katika jiji la Izhevsk, kulingana na vyombo vya habari vya Urusi.

    Shambulizi hilo lilifanyika katika shule nambari 88, ikiwa na karibu wanafunzi 1000 na walimu 80.

    Mshambuliaji huyo ameripotiwa kujiua na chanzo cha kufyatua risasi hakijafahamika.

    Vyombo vya habari vya Urusi vimechapisha video mtandaoni ambazo zinaonekana kurekodiwa ndani ya shule ambayo shambulizi lilitokea.

    Video moja inaonekana kuonyesha damu sakafuni na tundu ambalo risasi ilipita kwenye dirisha, huku watoto wakiinama chini ya madawati.

    Mshambuliaji huyo aliripotiwa kuwa na bastola mbili, kulingana na mbunge wa jimbo aliyenukuliwa na shirika la habari la Tass.

    Shule hiyo iko katikati mwa Izhevsk, jiji lenye wakazi wapatao 650,000, karibu na majengo ya serikali kuu.

    Walimu na wanafunzi wamehamishwa.

    Soma zaidi:

  8. Urusi: Waandamanaji wakamatwa kwa kupinga usajili wa wanajeshi wa akiba

    Watu katika eneo la Dagestan nchini Urusi wamekabiliana na polisi katika maandamano ya hivi punde kupinga hatua ya Urusi ya kusajili wanajeshi 300,000 wa akiba.

    Zaidi ya watu 100 walikamatwa wakati wa maandamano katika mji mkuu wa mkoa wa Makhachkala, OVD-Info, mfuatiliaji huru wa haki za binadamu wa Urusi alisema.

    Kundi hilo liliongeza kuwa lina wasiwasi na ripoti za ‘’kuzuiliwa kwa nguvu’’ kunakotokea katika eneo hilo.

    Dagestan ni eneo lenye Waislamu wengi nchini Urusi ambalo wakati mmoja lilijulikana kwa vurugu kali.

    Uchambuzi wa hivi majuzi wa idhaa ya BBC ya Kirusi ulionyesha kuwa wanajeshi wasiopungua 301 kutoka Dagestan wamefariki, mara 10 zaidi ya huko Moscow.

    Takwimu ya kweli inaweza kuwa ya juu zaidi.

    Zaidi ya watu 2,000 wamekamatwa kwenye maandamano makubwa tangu Rais wa Urusi Vladimir Putin atangaze kuwakusanya wanajeshi wa akiba siku ya Jumatano.

    Wakati maandamano makubwa yamefanyika katika miji mikubwa kote nchini Urusi katika siku za hivi karibuni - huku zaidi ya watu 700 wakikamatwa Jumamosi pekee - picha za waandamanaji wa Dagestani wakipigana na polisi ni ishara ya kuzuka kwa ghasia dhidi ya viongozi.

    Mamia ya video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha waandamanaji wakikabiliana na polisi na maafisa wengine wa usalama huko Makhachkala, huku OVD-Info ikiripoti kuwa maafisa waliamua kutumia bunduki na virungu dhidi ya umati.

    Katika video moja, mwanamume aliyezuiliwa na maafisa anampiga kichwa afisa wa polisi, kabla ya kupigwa na wengine.

    Video nyingine ilionyesha afisa wa usalama akitoroka kutoka kwa kundi kubwa la waandamanaji, ambao baadhi yao walijaribu kumkamata na kumtega alipokuwa akikimbia.

    Kwengine, kundi kubwa la wanawake lilikabiliana na afisa anayelinda kituo cha kuandikisha waajiri na kulaani kwa hasira vita vya Ukraine, huku mmoja akimwambia afisa huyo kwamba ‘’Urusi iko kwenye eneo la nchi nyingine’’.

    ‘’Kwa nini unawachukua watoto wetu,’’ wanawake walipiga kelele.

    Nani alishambuliwa? Urusi ilishambuliwa? Hawakuja kwetu. Ni sisi tunaishambulia Ukraine. Urusi imeishambulia Ukraine! Acha vita!’’

    Soma zaidi:

  9. Giorgia Meloni: Mrengo wa kulia Italia ndio unaoonekana kushinda uchaguzi

    Kiongozi wa mrengo wa kulia Giorgia Meloni amepata ushindi katika uchaguzi wa Italia, na yuko mbioni kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke nchini humo.

    Bi Meloni anatarajiwa kuunda serikali ya mrengo wa kulia zaidi tangu Vita vya Pili vya Dunia.

    Hiyo itasababisha wasiwasi katika sehemu kubwa ya Ulaya kwani Italia ni nchi ya tatu kwa uchumi wa EU.

    Anatazamiwa kushinda 26% ya kura, kulingana na matokeo ya muda, mbele ya mpinzani wake wa karibu Enrico Letta . Bw Letta aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu kwamba ushindi huo wa mrengo mkali wa kulia ulikuwa "siku ya huzuni kwa Italia na Ulaya" lakini chama chake kitatoa "upinzani mkali na usiobadilika".

    Hata hivyo, akizungumza baada ya kupiga kura, Bi Meloni alisema chama chake cha Brothers of Italy ‘’kitatawala kwa ajili ya kila mtu’’ na hakitasaliti imani ya watu.

    ‘’Waitaliano wametuma ujumbe wa wazi kuunga mkono serikali ya mrengo wa kulia inayoongozwa na Brothers of Italy,‘’ aliwaambia waandishi wa habari huko Roma, akishikilia bango linalosema ‘’Asante Italia’’.

    Anatabiriwa kushinda hadi 26% ya kura, kulingana na matokeo ya muda, mbele ya mpinzani wake wa karibu Enrico Letta kutoka mrengo wa kati kushoto.

    Muungano wa mrengo wa kulia wa Bi Meloni - ambao pia unajumuisha mrengo wa Matteo Salvini na aliyekuwa Waziri Mkuu Silvio Berlusconi wa Forza Italia - sasa unaonekana kuwa na udhibiti wa Seneti na Baraza la Manaibu, kwa karibu 44% ya kura.

    Mafanikio makubwa ya chama chake katika kura yalifichua ukweli kwamba washirika wake walifanya vibaya, huku chama cha Bw Salvini kikishuka chini ya 9%, na Forza Italia hata chini zaidi.

    Miaka minne iliyopita, chama cha Brothers of Italy cha Italia kilipata ushindi kidogo tu zaidi ya 4% ya kura lakini wakati huu walinufaika kutokana na kukaa nje ya serikali ya umoja wa kitaifa iliyoporomoka mwezi Julai.

    Uamuzi wa nani atakuwa kiongozi wa pili wa Italia ni wa rais, Sergio Mattarella, na hiyo itachukua muda.

  10. Israel yakubali wanajeshi 20 wa Ukraine kutibiwa

    Wanajeshi 20 wa Ukraine waliojeruhiwa vibaya watafanyiwa matibabu nchini Israel, Balozi wa Israel mjini Kyiv Mikhail Brodsky alisema.

    Kulingana na yeye, matibabu ni pamoja na kuwekewa viungo bandia.

    Usafirishaji wa waliojeruhiwa uliandaliwa na Ubalozi wa Israeli, Kituo cha Mashav cha Israeli na Wizara ya Afya ya Israeli na Ukraine.

    Soma zaidi:

  11. Maambukizi ya Ebola yaongezeka Uganda huku mlipuko ukizidi ukienea

    Takriban watu wawili zaidi sasa wamethibitishwa kufariki kwa Ebola. Hii inafanya jumla ya vifo kufikia ishirini na tatu. Hizi ni pamoja na zile ambazo zimethibitishwa kupitia matokeo ya maabara (sita) na wale wanaoshukiwa.

    Idadi ya watu wanaoshukiwa kuwa na Ebola inaendelea kuongezeka nchini Uganda.

    Wizara ya afya inasema kumekuwa na wagonjwa 34 wanaoshukiwa kuambikizwa.

    Timu za afya zinaendelea kufuatilia watu ambao wanaweza kuwa wamekutana nao.

    Mlipuko huo ulianza katika wilaya ya kati ya Mubende lakini sasa umeenea katika wilaya mbili jirani.

    Bado hakuna kesi zilizothibitishwa katika mji mkuu Kampala.

    Huu ni mlipuko wa nne wa Ebola nchi ya Uganda kukabiliwa nao.

    Nchi jirani zimesema ziko katika hali ya tahadhari.

    Soma zaidi:

  12. Rihanna kutumbuiza kipindi cha mapumziko katika Super Bowl

    Mwanamuziki nyota wa Pop Rihanna ataongoza onesho la muda wa mapumziko kwenye fainali za mpira wa miguu wa Kimarekani Super Bowl itakayofanyika Februari huko Arizona, NFL imetangaza.

    Mshindi huyo mara tisa wa Grammy alitangaza habari hiyo kwa kutuma picha ya mpira wenye chapa ya NFL kwenye Twitter.

    Waandaaji walimwita nyota huyo mwenye umri wa miaka 34kama mtu mwenye kipaji kinachoweza kubadilisha 'vizazi’ katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Jumapili usiku.

    Onesho hilo ni moja ya nafasi zinazoangaziwa zaidi katika muziki, huku tamasha la mwaka huu la dakika 14 likishuhudia watazamaji zaidi ya milioni 120, NFL ilisema.

    Wanamuziki nyota walipanda kutumbuiza wakiwemo Dr Dre, Snoop Dogg, Eminem, Mary J Blige na Kendrick Lamar. Onesho hilo lilipata Tuzo la Emmy.

    "Rihanna ni msanii wa kizazi kipya ambaye amekuwa na nguvu katika kipindi chote cha kazi yake," mkuu wa Muziki wa NFL Seth Dudowsky alisema.

    Naye Jay-Z, ambaye kampuni yake ya burudani ya Roc Nation itasaidia kuandaa onyesho hilo, alimtaja nyota huyo kuwa "mwanamke mwenye unyenyekevu ambaye anapita kiwango cha matarajio kila kukicha".

    "Mtu aliyezaliwa kwenye kisiwa kidogo cha Barbados na kuwa mmoja wa wasanii mashuhuri kabisa. Alijijenga kbiashara na burudani," aliongeza.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Zelensky awataka Warusi kujisalimisha

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika video ya jioni ambayo ni jambo la kawaida, amewahimiza Warusi kutoroka zoezi la usajili wa wanajeshi wa akiba au kujisalimisha kwa Ukraine kama chaguo lao la kwanza.

    ‘’Ninatangaza tena: kuna njia ya kukabiliana na hili. Usijisalimishe kwa usajili wa kihalifu. Toroka. Au jisalimishe kwa Ukraine mara ya kwanza,’’ Zelensky alisema.

    ‘’Kirusi wengi zaidi wakijaribu kulinda maisha yao wenyewe, ndiyo vile vita hivi vya uhalifu vya Urusi vitaisha’’.

    Akijibu maandamano ya leo huko Dagestan, Zelensky alisema kuwa hawa ni watu ambao wanapigania maisha yao na maisha ya watoto wao, na kuwataka Warusi wote kufanya hivyo.

    ‘’Kwa sababu ukija kumaliza maisha ya watoto wetu, hatutakuacha urejee ukiwa hai,’’ Rais wa Ukraine aliongeza.

    Katika ujumbe uliopita wa video siku ya Jumamosi, Zelensky aliahidi matibabu ya kibinadamu kwa wanajeshi wote wa Urusi waliojisalimisha.

    Soma zaidi:

  14. Kenya iko tayari kununua mafuta kutoka Urusi - Ruto

    Rais wa Kenya, William Ruto, ameiambia BBC kuwa yuko tayari kununua mafuta kutoka Urusi.

    Nchi kadhaa zimekataa kushirikiana na Moscow tangu uvamizi wa Ukraine lakini Bw Ruto amesema anazingatia chaguzi zote zilizopo.

    Kenya inakabiliwa na mzozo mkubwa wa kiuchumi, na kusababisha bei ya chakula na mafuta kupanda.

    Licha ya kupanda kwa bei ya mafuta Bw Ruto alitetea uamuzi wake wiki jana wa kufuta baadhi ya ruzuku za mafuta.

    Alisema isiyo endelevuna zinakabiliwa na unyanyasaji.

    soma zaidi:

  15. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja