Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
William Ruto: Je rais mpya wa Kenya anakabiliwa na changamoto zipi?
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
Rais mpya wa Kenya William Ruto aliapishwa jana kuanza hatamu kama rais wa tano wa nchi hiyo .
kipindi chake uongozini kimeanza wakati mgumu kwa raia wa taifa hilo kama ilivyo kote duniani ambapo gharama ya juu ya maisha ,uhaba wa chakula ,kiangazi na ongezeko la bei ya bidhaa nyingine muhimu vimesababisha ukali wa hali zao .
Ni baadhi ya mambo ambayo Wakenya watakuwa wakimtaraji rais wao mpya anayerithi uongozi kutoka kwa mtangulizi Uhuru Kenyatta watakuwa wakimtarajia kuyashughulikia-kwa haraka. Hata hivyo,kuna hofu ya iwapo ahueni itakuja haraka kama wengi wanavyotarajia licha ya kuwepo matumaini makubwa ya hali kubadilika .
Katika siku yake ya kwanza kama rais siku ya Jumanne,rais Ruto alitangaza mikakati kadhaa na kutoa maelekezo ambayo anayategemea kuanza kuleta mabadiliko .
Kikubwa ambacho amesema analenga kukitekeleza ni kuwapunguzia gharama ya maisha Wakenya kama alivyowaahidi wakati wa kampeni za uchaguzi uliokamilika mwezi uliopita
Pindi tu baada ya kuapishwa kuwa rais , alitangaza kushukishwa kwa bei ya mbolea kutoka shilingi elfu sita mia tano kwa bagi moja la kilo hamsini hadi shilingi elfu tatu mia tano.
Alisema bei hiyo mpya itaanza kutekelezwa kuanzia wiki ijayo huku serikali yake ikijaribu kuibadilisha sekta ya kilimo nchini.
Hatua hiyo anaamini itasaidia kuimarisha uzalishaji wa chakula na kuchochea kushuka kwa bei ya vyakula.
Lakini ni masuala gani haswa yanayotarajiwa kumnyima usingizi rais mpya?
Deni la Kenya
Deni la umma liliongezeka na kufikia kiwango cha juu zaidi cha shilingi trilioni 8.56 ambazo ni sawa na $72 billion mwezi Mei kutoka shilingi Trilioni 1.9 mwaka 2013 wakati utawala wa rais Kenyata ulipochukua madaraka. Kulingana na wanauchumi hali hiyo inalifanya taifa hili kuorodheshwa miongoni mwa mataifa yalio kwenye hatari ya kunyimwa mikopo na shirika la fedha duniani IMF.
Kulingana na Wizara ya fedha, Kenya ilitumia takriban 57% ya tozo la raia katika kipindi cha fedha cha mwaka uliopita kulipa madeni. Mwezi uliopita wabunge waliongeza deni la Kenya kwa 11% na hivyobasi kuisaidia serikali kufadhili bajeti yake ya kipindi cha miezi 12 ijayo .
Mfumuko wa bei
Bei za bidhaa zinapanda kwa kasi kubwa katika zaidi ya miaka mitano, hali ilioilazimu serikali kuanzisha ruzuku ya chakula na mafuta. Kupanda kwa bei za bidhaa kumefanya iwe vigumu kwa Wakenya kuendelea na maisha yao kama kawaida. Kwa mfano pakiti ya kilo mbili ya unga wa mahindi ilikuwa imefikia dola mbili kutoka dola 1.2 katika kipindi cha miezi mitatu iliopita .
Hilo ni ongezeko la 67%. Hatua ya serikali kuweka ruzuku na hivyobasi kuruhusu wafanyabiashara wa unga wa mahindi kuagiza mahindi kutoka nchini Jirani, hazijafaulu licha ya bei ya bidhaa hizo kupunguzwa hadi dola moja kwa mfuko wa kilo mbili. Vita vya Urusi pia vimechangia pakubwa kupanda kwa bei za bidhaa hadi kufikia viwango vya juu.
Na takriban 30% hadi 50% ya unga wa ngano wa Kenya unatoka Urusi na Ukraine. Ukraine imekuwa ikiuza chini ya 60% ya ngano mwaka huu ikilinganishwa na 2021, suala linalosababisha kupanda kwa bei ya ngano na bidhaa zake kama vile mkate.
Vijana wasio na ajira
Kiwango cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana nchini Kenya kiliongezeka katika robo ya kwanza ya 2021, ikilinganishwa na robo ya awali. Katika kundi la umri kati ya miaka 20 na 24, kiwango hicho kilikuwa kwa 16.3% kutoka 15% katika robo ya mwaka 2020.
Miongoni mwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 19, kiwango cha ukosefu wa ajira kilikua karibu asilimia saba, baada ya kufikia kiwango cha chini kabisa cha asilimia 2.8. mwaka 2020. Takriban watu milioni 5.2 wameshindwa kupata ajira huku nguvukazi ikiongezeka kwa watu milioni 1 kila mwaka kulingana na ripoti ya benki ya dunia.
Mdororo wa uchumi
Ukuaji wa uchumi wa Kenya umefikia 5.5% mwaka 2022 ukitarajiwa kufikia 5.2% kwa wastani kati ya mwaka 2023 -24. Kasi ya ukuaji, ingawa bado ni imara, itakuwa ya wastani kufuatia ahueni ya ajabu mwaka 2021 kutokana na athari mbaya zaidi za kiuchumi za janga la corona, wakati uchumi wa nchi ulikua kwa asilimia 7.5, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuliko wastani wa ukuaji wa uchumi katika eneo la Afrika na jangwa la Sahara wa 4%.
Ufisadi
Ufisadi mara kwa mara ni mojawapo ya matatizo makubwa nchini Kenya. Mkuu wa utumishi wa umma nchini Kenya, Joseph Kinyua, anakadiria kuwa thuluthi moja ya bajeti ya taifa ya kila mwaka inapotea kwa ufisadi, huku kampuni ya uhasibu ya KPMG LLP ikisema matumizi mabaya na uhalifu pamoja na hongo na ulaghai wa zabuni hutumia takriban 10% ya pato la taifa la $95 bilioni kila mwaka.
Rais Uhuru Kenyatta alisema mwaka jana kuwa kiasi cha shilingi bilioni 2 huibwa kila siku kutoka kwa serikali. Kenya ilipata alama 30 pekee kati ya 100 zinazowezekana kwa juhudi zake za kupambana na ufisadi katika Kielezo cha Mitazamo ya Ufisadi Duniani cha 2021 cha shirika la Transparency International.
Wakati huo ulikuwa uboreshaji mdogo kutoka kwa pointi 26 ilizopata mwaka wa 2016, Kenya bado ilikuwa chini ya kiwango cha wastani wa Afrika wa 32.
IEBC ina siku saba kutangaza matokeo.
- MATAYARISHO:Uchaguzi Kenya 2022: Je Kenya iko tayari kwa uchaguzi mkuu?
- YA MSINGI:Uchaguzi Kenya 2022: Kwa nini uchaguzi wa Kenya mwaka huu ni muhimu?
- MIUNGANO:Uchaguzi Kenya 2022: Musalia Mudavadi kujiunga na naibu rais William Ruto itabadilisha siasa za Kenya?
- UNAYOFAA KUJUA:Uchaguzi Kenya 2022: Je Naibu wa rais wa Kenya William Ruto anakabiliwa na changamoto gani katika kumteua naibu wake wa rais?
- UCHAMBUZI:Uchaguzi wa Kenya 2022: Je hatua ya Rais Kenyatta kumuunga mkono Raila Odinga itamsaidia au kumharibia?
- WASIFU:William Ruto: Muuza kuku aliyepanda ngazi hadi kuwa naibu wa rais wa Kenya
- RAILA ODINGA:Uchaguzi Kenya 2022: Siwezi kuwa kibaraka wa mtu yeyote-Raila Odinga
- WAGOMBEAJI:Wafahamu wagombea 4 wanaowania urais nchini Kenya