Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matokeo ya uchaguzi Kenya:William Ruto alivyokabili panda shuka na kuibuka mshindi
- Author, Na Evelyne Musambi
- Nafasi, BBC News, Nairobi
Naibu Rais wa Kenya William Ruto amekaidi kila changamoto na kushinda uchaguzi wa urais uliokuwa na ushindani mkali katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
Ushindi wake ulikuwa finyu, wa kustaajabisha, na wenye utata mkubwa kwani wajumbe wanne kati ya saba wa tume ya uchaguzi walikataa matokeo hayo huku kukiwa na madai ya wizi wa kura.
Kulikuwa na matukio ya fujo ndani ya kituo kikuu cha kuhesabia kura. Mizozo ilizuka jukwaani huku mkuu wa tume hiyo Wafula Chebukati akionekana kukaribia kutangaza matokeo.
Bw Chebukati baadaye alirejea kumtangaza Bw Ruto kuwa mshindi, na kusisitiza kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.
Matokeo rasmi yanaonyesha kuwa Bw Ruto alijiimarisha katika ngome za Raila Odinga, mpinzani wake mkuu. Pia alishinda kwa kishindo katika eneo la Mlima Kenya - kitovu cha kisiasa cha mgombea mwenza wa Bw Odinga Martha Karua na Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta.
Hii ilisaidia kurahisisha uchaguzi kwa upande wa Bw Ruto.
Alikuwa ni mtu 'duni' au, kama alivyopendelea kujiita, "hustler", akipambana na kile alichokiona kama jaribio la nasaba mbili kubwa za kisiasa za Kenya - Odingas na Kenyattas - kusalia madarakani. Simulizi hii iliwagusa vijana wengi wa Kenya.
Ruto mwenye umri wa miaka 55 alikuwa nyuma ya Odinga katika kura za maoni, na akakabiliana na mpinzani mkubwa - Bw Odinga - ambaye, katika hali isiyo ya kawaida, aliungwa mkono na mpinzani wake wa muda mrefu, Rais Kenyatta.
Rais sasa atalazimika kukubali kilichotokea na kukabidhi hatamu za uongozi kwa naibu wake - mtu ambaye alimtaja wakati wa kampeni kuwa "haaminiki".
Haya yote yanatokana na matokeo kuwa ya kweli - na sio ya udanganyifu kama wafuasi wa Bw Odinga wanavyodai.
Msimamo wao umeimarishwa na wengi wa makamishna wa tume ya uchaguzi wakisema hawawezi kuchukua "umiliki" wa matokeo hayo, lakini Bw Chebukati alisisitiza kwamba yanaakisi matakwa ya Wakenya.
"Ninasimama mbele yenu licha ya vitisho na kunyanyaswa. Nimetekeleza wajibu wangu kwa mujibu wa sheria za nchi," Bw Chebukati alisema.
Hakuna shaka kuwa ushindi mdogo wa Bw Ruto - na mgawanyiko ndani ya tume - unaonyesha kuwa taifa limegawanyika.
Jinsi Bw Ruto atakavyounda serikali yake itaamua iwapo nchi itaunganishwa tena.
Huku ukabila ukiwa sababu kuu katika siasa za Kenya, Bw Ruto atalazimika kuhakikisha serikali yake inawakilisha makabila makuu ya Kenya - hasa jamii ya Waluo ya Bw Odinga.
Mjaluo hajawahi kukalia kiti cha urais katika historia ya Kenya, na jamii inalazimika kuhisi kutengwa na kuudhika kufuatia tamko kwamba Bw Ruto - ambaye anatoka kabila la Wakalenjin - alikuwa ameshinda.
Bw Ruto alitoa hotuba yake ya ushindi akisema atafanya kazi na "viongozi wote" na atajitahidi kuhakikisha taifa "lina umoja na ustawi".
Alisema aliwasiliana na Bw Odinga kabla ya tangazo hilo na wakakubaliana kwamba vyovyote itakavyokuwa, wanapaswa kufanya mazungumzo.
Bw Odinga bado hajazungumza, lakini alikaa mbali na hafla ya kutangazwa rasmi kwa matokeo hayo.
Bado haijabainika iwapo atapinga matokeo hayo mahakamani kama alivyokuwa akifanya huko nyuma.
Amepoteza chaguzi nne zilizopita. Hii ilionekana kuwa nafasi yake nzuri ya kushinda huku Bw Kenyatta akimfanyia kampeni nyingi, akiwataka wapiga kura kutompigia kura Bw Ruto.
Bw Kenyatta alikiri wakati wa kampeni kwamba alivunja mkataba wa kumuunga mkono Bw Ruto katika uchaguzi huu. Alihalalisha hilo kwa kumlinganisha naibu wake na dereva mwenza ambaye alitupa vitu nje ya gari huku dereva akishughulika kuliongoza.
Kulingana na Bw Ruto, Bw Kenyatta alimfanyia kampeni Bw Odinga kwa sababu alitaka "rais kibaraka".
Akiwa na umri wa miaka 77, haijabainika iwapo Bw Odinga atawania kiti cha urais kwa mara ya sita katika uchaguzi ujao wa 2027.
Bw Ruto, mmoja wa wakulima wakubwa wa mahindi nchini, ameshinda katika jaribio lake la kwanza katika kiti cha urais - na atakuwa rais wa pili mwenye umri mdogo wa Kenya baada ya Rais Kenyatta kushinda mwaka wa 2013 akiwa na umri wa miaka 50.
Yeye ni mtu talanta ya uzungumzaji,mwenye nguvu - akijihusisha na siasa miongo miwili iliyopita katika tawi la vijana la chama tawala wakati huo - na alivuta umati mkubwa wa watu wakati wa kampeni.
Amefanikiwa kupata kura katika ngome za Bw Odinga katika maeneo ya pwani, magharibi na kaskazini mashariki mwa nchi
Ushindi wake ni wa ajabu zaidi kwani alishinda kwa kishindo katika ngome ya Bw Kenyatta ya Mlima Kenya, kitovu cha Wakikuyu ambao ndio kambi kubwa zaidi ya wapiga kura nchini Kenya.
Chama cha Bw Ruto pia kilichukua viti vingi katika eneo hilo katika uchaguzi wa ubunge, useneta na wadhifa wa ugavana, na kukiondoa chama cha Bw Kenyatta cha Jubilee.
Katika kura ya urais, hata alimshinda Bw Odinga katika maeneo bunge ya Bi Karua na Bw Kenyatta.
Wafuasi wa Bw Ruto katika Mlima Kenya ambao walizungumza na BBC kabla ya uchaguzi walisema waliona haja ya kuheshimu mapatano ya 2013 ili kurudisha uungaji mkono wake kwa mtoto wao Bw Kenyatta.
Ni jambo la kufedhehesha kwa Bw Kenyatta, ambaye sasa anaondoka ofisini huku sifa yake ikichafuliwa miongoni mwa watu wake -Wakikuyu .
Binamu yake, ambaye ni mwenyekiti wa chama cha wazee, alisema watamuunga mkono Bw Ruto.
Ushindi huo utapongezwa na vijana wengi, ambao waliunda ngome kubwa ya kumuunga mkono.
Bw Ruto alibuni msemo wa "Hustler Nation" kurejelea vijana wanaohangaika kutafuta riziki, na kuahidi "mbinu ya chini kabisa" ya uchumi, akisema itawanufaisha maskini.
Sasa atalazimika kutekeleza ahadi yake.
Itakuwa kazi ngumu kwani kiwango rasmi cha ukosefu wa ajira miongoni mwa wale wenye umri wa kati ya miaka 18 na 34 ni karibu 40%, na uchumi hautengenezi nafasi za kutosha kuwapa nafasi za kazi vijana 800,000 wanaojiunga na nguvu kazi kila mwaka.
Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma