Uchaguzi wa Kenya 2022: Wakikuyu wagawanyika kati ya Ruto na Odinga

    • Author, Na Evelyne Musambi
    • Nafasi, BBC News, Nyeri

Katika jamii ya Wakikuyu wenye utajiri wa kura nchini Kenya, kuna maoni tofauti kuhusu hatua ya Rais anayemaliza muda wake Uhuru Kenyatta kumuunga mkono aliyekuwa mpinzani wake Raila Odinga, badala ya naibu wake William Ruto, kuwa mrithi wake katika uchaguzi wenye ushindani mkali unaotarajiwa kufanyika tarehe 9. Agosti.

Bw. Kenyatta - ambaye amefikia kikomo cha kikatiba cha mihula miwili madarakani - alichukuliwa kwa muda mrefu kama kinara wa kisiasa wa jami hiyo, huku wazee wake wakimtaja kwa fahari kuwa "mwana wetu".

Lakini wakati BBC ilipozuru jimbo la Nyeri - ambalo lipo katika eneo la Mlima -ilibainika kuwa uaminifu wake umepata pigo kutokana na uamuzi wake wa kumuidhinisha Bw Odinga katika kile alichokitaja kuwa jaribio la kubuni umoja wa kitaifa baada ya miongo kadhaa ya chuki za kisiasa.

Wakili Wahome Gikonyo alihisi kuwa Bw. Kenyatta amemsaliti Bw Ruto, ambaye alimsaidia kushinda uchaguzi dhidi ya Bw Odinga.

"Ruto alifanya kazi ya punda mwaka 2013 na 2017. Laiti sio yeye Uhuru hangelikuwa rais. Je hiyo ndiyo njia ya kumlipa rafiki?" Bw Gikonyo alisema alipokuwa akizungumza na BBC katika afisi yake katika mji makao makuu ya kaunti hiyo, inayojulikana kama Nyeri.

Baadhi ya wakazi, kama Mchungaji Hannah Kanyithere, alihisi Bw Kenyatta hangejiuhusisha na kinyang'anyiro cha kumtafuta mrithi wake.

"Kwanini rais anaegemea upande wowote katika uchaguzi huu? Hata kama naibu wake alikuwa mbaya, alipaswa kuw ana msimamo wa wastani," aliongeza.

Lakini dereva wa teksi Hassan Kahoro alikuwa na shauku sawa katika kumtetea Bw Kenyatta, akipendekeza kwamba, wakati ulikuwa umewadia kwa jamii ya Wajaluo kupata rais wao kwanza - Bw Odinga.

"Tunapaswa kupatia jamii ya Wajaluo nafasi ya kuongoza nchi hii. Nani alisema urais unastahili kuwa wa Wakikuyu na Wakalenjin?" Bw Kahoro alisema, huku akihutubia kundi la watu waliokuwa wamekusanyika katika soko kuu la eneo hilo.

Alikuwa anaashiria ukweli kwamba Kenya watatu kati ya marais wanne wa Kenya tangu tupate uhuru wamekuwa Wakikyu. Hayati Daniel arap Moi - ambaye alihudumu kwa muda mrefu kam rais wa Kenya (miaka24) alikuwa Mkalenjin, kama Bw Ruto.

Welder Jackson Maina pia aliridhika na hatua ya Bw Kenyatta kumuunga mkono "Baba", jina linalotumiwa ma wafuasi wake kumuita Bw Odinga mwenye umri wa miaka 77.

"Tuko imara nyuma ya rais na tuko nyuma ya Baba," alisema akiwa nje ya karakana yake.

Mji wa Nyeri umesheheni mabango ya kampeni uchaguzi mkuu unapokaribia.

Nyimbo za kuunga mkono kambi zote zinasikika.

Nyimbo moja - iliyoimbwa mwanamziki wa Kenya Ben Githae - inasema kwamba Kenya itakuwa salama mikononi mwa Bw Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua -waziri wa zamani wa haki na Mkikuyu anayechukuliwa kama "binti yao" kutoka Mlima Kenya.

Nyimbo nyingine - iliyoimbwa na Betty Maina - anawaasa watu kumpigia kura Bw Ruto, ambaye amemchagua Rigathi Gachagua- mwanabiashra Mkikuyu kutoka Kaunti ya Nyeri kama mgombea mwenza wake.

Ingawa Bw Gachagua anakabiliwa na tuhuma za ufisadi, yeye ni mhamasishaji hodari na anapendwa sana na Wakikuyu wanaohangaika.

Bi Karua ni kinara wa kisiasa ambaye ana uungwaji mkono kitaifa kando na Wakikuyu - na anajulikana kwa shauku yake ya mageuzi ya mahakama na msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi serikalini.

Lakini iwapo kura ya maoni ya hivi punde zaidi ya shirika la utafiti la Tifa itaaminika, si yeye wala Bw Kenyatta ambaye amewashawishi Wakikuyu walio wengi kumpigia kura Bw Odinga. Kura hiyo ya maoni inampa Bw Ruto uongozi kwa wingi katika Mlima Kenya - 66% dhidi ya 27% za Bw Odinga.

Katika ngazi ya kitaifa, picha ni tofauti, huku kura ya maoni ikimweka Bw Odinga mbele kwa tofauti ndogo ya 46.7% dhidi ya 44.4% - haitoshi kwake kupata urais, kwani mshindi anahitaji kura nyingi zaidi ya 50% ili kuepuka duru ya pili ya uchaguzi.

Kwa hivyo pande hizo mbili zitakuwa na kibarua cha ziada kuvutia wapiga kura katika siku za mwisho za kampeni.

Uamuzi wa Bw Kenyatta kumuunga mkono Bw Odinga haikugawanja jamii yake tu bali pia familia yake.

Binamu yake Kungu Muigai aliviambia vyombo vya habari kuwa rais alienda kinyume na wazee wa Kikuyu kwa kukiuka mapatano ya 2013, yaliyoitaka jamii kuunga mkono Wakalenjin mara tu mihula miwili ya Bw Kenyatta itakapokamilika.

Mgawanyiko huo unalalamikiwa na wazee wa jamii ya Wakikuyu, kama alivyoelezea Nduhiu Njama mwenye umri wa miaka 100, na mkazi wa Tetu huko Nyeri.

"Tulipata uhuru kwa kuwa wamoja. Tunachokiona kwa sasa ni ubinafsi ambao utatugharimu," alisema huku akionyesha picha zake za zamani.

Wakikuyu hasa ni wakulima. Mashamba ya chai na kahawa, pamoja na mashamba ya maziwa, yanaenea katika Mlima Kenya.

Barabara za vijijini zimewekwa lami na kuwarahisishia wakulima kusafirisha mazao yao.

BBC ilitembelea wakulima karibu na mji wa Othaya, ambao ulikuwa nyumbani kwa marehemu Rais Mwai Kibaki.

Alipokuwa akiwapa lishe ng'ombe wake wa maziwa, George Wambugu alisema anamuunga mkono Bw Ruto.

"Ruto ni mkulima kama mimi na alipokuwa waziri wa kilimo alileta mageuzi ambayo yaliwafanya wakulima wa chai kupata bonasi ya juu zaidi kuwahi kutokea. Najua ataboresha sekta ya kilimo," baba wa watoto watatu mwenye umri wa miaka 40 alisema, akieleza. maoni ambayo yaliungwa mkono na baadhi ya wakulima wenzake.

Unaweza pia kusoma