Uchaguzi wa Kenya 2022: Je hatua ya Rais Kenyatta kumuunga mkono Raila Odinga itamsaidia au kumharibia?

    • Author, Joseph Kioko
    • Nafasi, Mchambuzi Kenya

Msemo 'kikombe chenye sumu' hutumika mara kwa mara katika Siasa kuelezea kazi au usaidizi anaopewa mtu, ambapo mwanzoni, mtu huyo hufikiri kuwa ameheshimiwa lakini baadaye akagundua msaada huo aliopewa ni, mzigo, ambao huenda ukaharibu sifa yake au matarajio yake.

Msemo huo unajiri siku chache tu baada ya rais Uhuru Kenyatta kumuunga mkono rasmi kiongozi wa ODM Raila Odinga , hatua inayotarajiwa kuzua hisia tofauti miongoni mwa Wakenya wapipga kura katika mkutano uliofanyika katika Ikulu ya Sagana mjini Nyeri.

Katika hatua ya rais Uhuru Kenyatta kumuunga mkono aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, ni rahisi mtu kushawishika kwamba ni hatua itakayomuwezesha kiongozi huyo kuafikia azma yake ya kuwania urais na upande mwengine kuna wale ambao huenda wakafikiria kwamba hatua hiyo huenda ikamharibia.

Ujio wa 'Handshake'

Uamuzi wa mahakama ya juu zaidi ya Kenya kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa Rais wa 2017 na kuamuru uchaguzi mpya ufanyike, ambao ulisusiwa na muungano wa upinzani wa NASA, ulizua mazingira ya mgawanyiko ndani ya nchi.

Kulikuwa na hisia kwamba kura halisi zilizopigwa hazikuhesabiwa na badala yake kulikuwa na watu binafsi au "mifumo" ilioamua mshindi hali ambayo ingewatenga watu wa jamii fulani na viongozi mgao wa rasilimali za nchi.

Ni nia ya kushughulikia mapungufu haya miongoni mwa mengine, kwamba Rais Uhuru na Waziri Mkuu Raila Odinga walifanya Handshake Machi 2018, ambayo iliashiria mwanzo wa ushirikiano wa kisiasa kati ya wahusika wawili wakuu wa kisiasa.

Katika jitihada za kutatua changamoto za kihistoria zilizokuwa zikiikabili nchi, wakuu hao wawili waliunda kamati ya watu mashuhuri iliyozunguka nchi nzima kukusanya na kukusanya maoni kutoka kwa wananchi, maoni hayo yalifupishwa na kuwa waraka wa kisiasa unaoitwa Ripoti ya Ujenzi wa Madaraja BBI ambayo ilibadilika na kuwa Mswada wa marekebisho ya katiba "mpango maarufu" ambao ulipaswa kuwasilishwa kwa umma kupitia kura ya maoni.

Mpango huu maarufu wa BBI hatahivyo ulitangazwa kuwa "batili na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa na kwa sasa unasubiri uamuzi wa Mahakama ya Juu zaidi ya Kenya.

Kando na mpango wa BBI, mshikamano wa kisiasa kati ya viongozi hao wawili umesababisha ishara nyingi kwamba Waziri Mkuu Raila Odinga ndiye mgombea urais anayependekezwa zaidi ra Rais Uhuru.

Kenyatta kumuunga mkono Odinga

Rais amejitokeza waziwazi kuonyesha mshikamano na kuunga mkono muungano wa Azimio ambao ni gari la muungano ambalo Raila Odinga atatumia kuwania urais katika uchaguzi Mkuu ujao wa Agosti, rais pia amekuwa mwenyeji wa ujumbe katika ikulu ya Nairobi kuwa mgombeaji wa muungano wa Azimio (Raila Odinga) ndiye anayempendelea zaidi.

Kando na kuwa mwenyeji wa wajumbe na pia kutumia rasilimali za serikali kushinikiza uongozi wa Raila Odinga, Rais pia amewasiliana na wanasiasa wengine wakuu na Magavana katika juhudi za kuwavutia kujiunga na muungano wa Azimio na kumuunga mkono Raila Odinga.

Muungano wao na hatua ya kumuunga mkono Raila Odinga inahitaji pia kuonekana katika mtazamo wa kihistoria, ambapo baba za mabwana hawa wawili walikuwa Rais na Makamu wa rais mtawalia. Wakakti taifa hili lilipojipatia uhuru.

Baadaye walitofautiana kimawazo na mzozo mkubwa wa kisiasa ukatokea ambao sio tu ulikumba familia hizo mbili bali pia ulipanda mbegu za kutoaminiana miongoni mwa makabila yao.

Huku watu wa kabila la mkoa wa kati nchini Kenya wakifurahia uongozi wa nchi kupitia Rais Jomo Kenyatta, Rais Mwai Kibaki na kwa sasa Rais Uhuru Kenyatta, Jamii ya watu wa eneo la uliokuwa mkoa wa Nyanza hawajabahatika katika masuala ya uongozi wa nchi. ni mitazamo hii ya kutaka kurekebisha "ukosefu" huu wa usawa wa kihistoria ambao unaonekana kumsukuma Rais Uhuru Kenyatta kutaka kuunga mkono uonozi wa Raila Odinga.

Na ili kuleta usawa huo wa uongozi , Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akitofautiana na naibu wake William Ruto kuhusu uongozi wa taifa la Kenya kuzunguka kati ya watu wamakabila mawili , lile la watu wa uliokuwa mkoa wa kati na ule wa mkoa wa Bonde La Ufa, hali ambayo anadai huenda imesababisha usawa wa kushirikishwa kwa jamii nyingine katika uongozi wa taifa hilo - na ndio sababu ameamua kumuunga mkono Raila Odinga.

'Miradi ya kisiasa'

Ni muhimu kuelewa kwamba uchaguzi Mkuu ujao wa Agosti 9 nchini Kenya utakuwa uchaguzi wa 3 tangu kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi na kupitishwa kwa ukomo wa mihula miwili kwa wahudumu wa kiti cha urais. Uchaguzi Mkuu wa 2002 uliwakilisha mwisho wa ukomo wa mihula miwili ya Rais Moi na katika jaribio la kusimamia mrithi wake KANU ilishindwa.

Wakati wa uchaguzi huo, Rais Moi alimpendekeza mwanasiasa kijana Uhuru Kenyatta kuwa mrithi wake mbele ya wanasiasa wengine wakuu wa KANU, ambao wakiongozwa na Raila Odinga waliasi na kujiunga na Mwai Kibaki katika muungano wa upinzani wa National Rainbow Coalition (NARC).

Uhuru Kenyatta wa KANU alishindwa na Rais Mwai Kibaki wa NARC, licha ya kuhusika sana katika kampeni na serikali ya wakati huo ya KANU kumuunga mkono. Uchaguzi Mkuu wa 2013 uliwakilisha mpito wa 2 ambapo rais aliye madarakani alizuiwa na sheria kugombea wadhifa huo.

Kwa upande wake Rais Mwai Kibaki hakuonyesha kwa njia yoyote upendeleo kwa wagombeaji wowote waliokuwa na nia ya kuwania Urais.

Kwa vyovyote vile wagombea wakuu wote katika uchaguzi walikuwa wajumbe wa baraza lake la mawaziri wakihudumu nyadhifa tofauti wakati huo. Katika uchaguzi wa 2013, muungano wa Uhuru Kenyatta na William Ruto (TNA/URP) ulishinda muungano wa Waziri Mkuu wa wakati huo Raila Odinga na Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka (CORD), hali ambayo ilirudiwa tena 2017.

Kwa hivyo uchaguzi huu ujao utashuhudia uhamishaji wa 3 wa mamlaka kwa mujibu wa katiba ya Kenya. Jinsi marais hao wa zamani walivyofanya na kusimamia mabadiliko yao itakuwa muhimu katika kutathmini iwapo kweli uungwaji mkono wa Rais Uhuru kwa Waziri Mkuu Raila Odinga ni kikombe chenye sumu au ubabe wa kisiasa.

Ni historia pekee ndiyo itakayotuhukumu.