Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi wa Kenya 2022: Kwa nini sababu ya kikabila inaweza kupoteza nguvu zake
Wakati Kenya inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 9, mwandishi wa BBC Dickens Olewe anaandika kwamba migawanyiko wa kikabila kwa muda mrefu imekuwa jinamizi katika siasa za taifa - ingawa kuna ishara hali hii sasa inaweza kubadilika.
Asubuhi yenye baridi kali tarehe 20 Januari 1994 nilikaribishwa darasani kwa dhihaka.
Sikumbuki mengi yaliyosemwa lakini maneno haya yamesalia katika kumbukumbu yangu.
"Mungu wako amekufa," mwanafunzi mwenzangu aliniambia.
Jaramogi Oginga Odinga, makamu wa rais wa kwanza wa Kenya ambaye baadaye alikuwa kigogo wa siasa za upinzani, alikuwa amefariki.
Licha ya kwamba tulikuwa katika shule ya msingi, sote tulikuwa na uelewa kuhusu siasa zinazoegemea misingi ya kikabila, kwa hivyo mwanafunzi mwenzangu alijua kifo hicho kilikuwa na athari kubwa ya kisiasa kwa jamii ya Wajaluo.
Kejeli za kikabila zilikuwa jambo la kawaida katika viwanja vya michezo vya shule na hata madarasani, ambapo baadhi ya walimu walitumia dhana potofu kusifia au kukemea tabia za wanafunzi.
Hii ilionekana, na bado inaonekana kama ucheshi usio na madhara, lakini wakati mwingine hubadilika kuwa mbaya.
Wakati mwingine wa kushangaza ulikuja miaka minane baadaye wakati msichana mwenye umri wa miaka minne mwenye kujiamini aliponijia katika siku yangu ya kwanza ya kujitolea katika shirika la kusaidia familia maskini jijini Nairobi, na kuuliza swali moja kwa moja kwa Kiswahili: "Wewe ni kabila gani?"
Hakufurahishwa na jibu langu, hasa kwa sababu baadaye niligundua kwamba kabila langu lilikuwa sehemu ya mjadala mkali na wenzake - maslahi yao ambayo yanawezekana yalichochewa na mazungumzo ya kisiasa ya wakati huo.
Udadisi wa utotoni ulikuwa mzuri, lakini nilihisi usumbufu. Maadili ya kijamii yalinifundisha kuchukia maswali kama hayo, haswa yanapowekwa wazi. Pia nilikuwa na wasiwasi jibu langu lingemaanisha nini kwake.
Siasa za Kenya zimetawaliwa na ushindani kati ya makabila yake zaidi ya 40, lakini ni makali zaidi kati ya makabila makubwa zaidi.
Wanasiasa mara nyingi hutumia chuki za kihistoria na tofauti za kitamaduni kuchochea vurugu ili waweze kushinda uchaguzi.
Mkakati huu wa kipuzi ni wa zamani na matokeo yake ya kusikitisha yanaendelea kushuhudiwa kote duniani.
Nchini Kenya, ukabila umetumika kwa njia ya upendeleo - wakati mwingine ndiyo sifa pekee inayozingatiwa kwa kazi, kura katika uchaguzi, au hata kupata upendeleo wa kawaida kutoka kwa mtu aliye na mamlaka.
Imetumiwa kama silaha ya kuwadhalilisha na kuwahangaisha wengine - hali inayozaa fikra ya kuzingirwa kwa wale wanaobeba mzigo huo, na hisia ya kustahiki miongoni mwa wanaonufaika nayo.
Siasa kwa hivyo inakua kigezo muhimu, badala ya kushughulikia masuala muhimu ambyo yana athari ya moja kwa moja kwa wananchi.
Kenya ilishuhudia ghasia mbaya za kikabila kufuatia mzozo wa uchaguzi wa mwaka 2007, wakati zaidi ya watu 1,500 waliuawa, mamia ya wengine kujeruhiwa na takriban watu 600,000 kulazimika kutoroka majumbani mwao.
Vurugu hizo huenda ziliathiri Kenya vibaya tangu uhuru.
Nchi ambayo kwa kiwango kikubwa ilikuwa na amani, na hata kutoa hifadhi kwa maelfu ya wakimbizi kutoka nchi tofauti barani, ilijigeukia yenyewe. Maumivu ya wakati huo bado yanaendelea.
akati wa uchaguzi huu, baadhi ya familia zinapanga kuhamia katika maeneo yalio na watu wengi wa kabila lao ili kuepuka kudhulumiwa, ilhali wanandoa wa makabila mchanganyiko mara nyingi hukabiliana na changamoto kubwa kuamua ni wapi pangekuwa salama zaidi.
"Kenya ina historia ya kusikitisha ya uhasama ambao haujawahi kusuluhishwa, yapata miaka 50, na bado huchochea ghasia na wanasiasa wamekuwa wazua hofu kati ya jamii," Sam Kona, kamishna katika Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC), aliambia BBC.
"Watu hawaoni ukweli kwamba haya ni mashindano ya kugombea madaraka kati ya wasomi, na mara yanapoisha, wasomi wanatangamano bila kujali ikiwa walishinda au la," aliongeza.
Bw Kona alisema mivutano miongoni mwa jamii katika kaunti sita ambazo NCIC imezitaja kuwa maeneo hatari katika uchaguzi ujao ni kwa sababu ya "kukosa fursa za kupatanisha".
Alidokeza kuwa Kenya ilipitisha katiba mpya mwaka wa 2010, na kuunda majimbo 47 - na magavana wao - ili kukomesha kadhia ya mshindi-kuchukua-yote.
Iliahidi kuwa majimbo yote yataangaziwa kwa usawa, na yatapokea kiasi cha haja cha mgao wa bajeti ya kitaifa kupanga maendeleo yao wenyeweili kuepusha hitaji la vikundi tofauti kushindania kwa rasilimali.
"Cha kusikitisha ni kwamba baadhi ya Wakenya bado wanaona urais kuwa chanzo kikuu cha mamlaka - hali inayosababisha mvutano," Bw Kona alisema, akiongeza kuwa NCIC imeimarisha juhudi za kuendeleza amani katika maeneo yanayoweza kukumbwa na ghasia.
Mtaalamu wa masuala ya utawala John Githongo alilazimika kutoroka nchini mwaka wa 2005 kwa sababu alichukuliwa kuwa msaliti na baadhi ya watu wa jamii yake ya Wakikuyu baada ya kufichua kashfa kubwa ya ufisadi katika utawala wa Rais wa wakati huo hayati Mwai Kibaki, Mkikuyu mwenzake.
Aliiambia BBC kwamba uhamasishaji wa kikabila haukuonekana wazi katika kampeni hii ya uchaguzi, haswa kwa sababu Naibu Rais William Ruto ameufanya kama mchuano kati ya "familia za kikabila" na "wanaharakati".
Anamshirikisha mpinzani wake mkuu, Raila Odinga, mwanasiasa mkongwe wa upinzani na mtoto wa makamu wa kwanza wa rais wa Kenya, katika kundi la zamani, pamoja na Rais Uhuru Kenyatta, mtoto wa rais wa kwanza. Huku akijionyesha kama bingwa wa "hustlers" - jina linalohusishwa na Wakenya maskini.
Bw Odinga amekosoa utumiaji wa neno hilo na anachukulia kama jaribio la kugawanya Wakenya kulingana na matabaka, na ameelekeza kampeni yake katika ujumbe wa umoja.
Lakini katika mabadiliko makubwa kutoka kwa kampeni za awali, wagombeaji wakuu hao wawili wamejibizana kuhusu sera zao za kiuchumi na kijamii.
Hili halishangazi kwani uchaguzi huu unakuja katikati ya mzozo wa gharama ya maisha, uliozidishwa na ukosefu mkubwa wa ajira na deni kubwa la taifa.
Katika hatua ya kuingilia kati hali hiyo wiki chache kabla ya uchaguzi, serikali ya Rais Kenyatta ilitangaza kuwa unga wa mahindi - unaotumiwa kutengeneza chakula kikuu nchini, ugali - utapewa ruzuku ili kupunguza bei yake.
Bw Ruto anachukulia hatua hiyo kama jaribio la kuimarisha nafasi ya Bw Odinga katika uchaguzi huo.
Bw Kenyatta anamuunga mkono Bw Odinga katika uchaguzi huu , ingawa Bw Ruto ni naibu wake.