Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matokeo ya uchaguzi Kenya 2022: Majirani wa Kenya wanajifunza nini?
- Author, Lizzy Masinga
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Shughuli ya kuhesabu kura kwa sasa zinaendelea mara baada ya vituo vya kupiga kura kufungwa huku hesabu ya kura za urais ikipewa kipaumbele.
Kura hii ni baada ya kampeni kali iliyotawaliwa na mijadala kuhusu gharama za maisha, ukosefu wa ajira na ufisadi.
Wanaogombea wakuu wa urais ni aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga na Naibu Rais wa sasa William Ruto.
Wafula Chebukati ,mwanasheria ndiye mwenyekiti wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) inayohusika na mchakato mzima wa uchaguzi nchini Kenya.
Wakati Kenya ikijiandaa kumpokea mshindi wa uchaguzi wa urais nchini humo, jina la Wafula Chebukati ni muhimu sana katika uchaguzi wa mwaka huu, na alitarajiwa na vyama, miungano ya kisiasa , wagombea binafsi na Wakenya kwa ujumla kuendesha uchaguzi wa haki na huru ili kuhakikisha Kenya inakuwa na amani na utulivu.
Bwana Chebukati mwenye umri wa miaka 60, sio mgeni katika wadhfa wa Mwenyekiti wa IEBC. Alikula kiapo cha kuongoza tume hiyo kwa mara ya kwanza tarehe 20 Januari mwaka 2017, alipomrithi mtangulizi wake Issack Hassan.
'Mwanaume asiyetetereka'
Huku akijiandaa kumtangaza mshindi wa urais, ni dhahiri kwamba wakili huyu mwenye ''haiba ya upole'' anafahamika na wengi kuwa mtu asiyetetereka wala kuyumbishwa anapofanya kazi yake.
Ni mtu anayeongea kwa sauti ya upole na utaratibu, lakini kwa wanaomfahamu si mtu mwenye kutafuna maneno na mara nyingi anachokiongea ndicho anachokimaanisha.
Msimamo wake umekuwa na mvuto sana kwa wanaomfuatilia na kuifuatilia taasisi anayoisimamia
Majirani wa Kenya wanasema nini kuhusu uchaguzi huu?
Wakenya na raia mbali mbali wa nchi za Afrika Mashariki wametoa maoni yao kuhusu mwenendo wa uchaguzi nchini Kenya hususani mwenendo wa kura zilivyopigwa, zinavyohesabiwa na namna matokeo yanavyotoka.
Masuala mengine yaliyozua mjadala ambayo yameonekana kuwa funzo kwa upande wa nchi nyingine za Afrika Mashariki ni uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa mawakala wa vyama na wagombea wa nafasi mbalimbali.
Kutobinywa kwa mitandao ya kijamii
Hali imekuwa tofauti nchini Kenya na kufuta mtazamo kuwa kudhibitiwa kwa mitandao ni jambo la kawaida katika baadhi ya mataifa ya Afrika, ambako serikali zimekuwa zikizima mitandao ya intaneti mara kwa mara au kuzuia mitandao ya kijamii.
Wanaharakati wa kutetea haki katika dijitali wanasema ni kubana taarifa, lakini serikali zinadai inasaidia kuimarisha usalama,kwa Kenya hali imekuwa tofauti sana na ilivyokuwa ikidhaniwa.
Wakati wote wa Kampeni, kupiga kura na hata sasa ambapo kura zimeendelea kuhesabiwa nchini Kenya, mitandao ya kijamii imekuwa ikiendelea kutumiwa na raia wa Kenya, jambo ambalo limewavutia wengi wanaoufuatilia uchaguzi wa Kenya kwa karibu.
Mara nyingi wakati wa uchaguzi huwa kuna kizuizi kinachowekwa kuwazuia watu kuingia katika mitandao ya kijamii inayotumika sana.
Kwa hatua kali zaidi, serikali inaweza kuagiza kufungwa kabisa kwa huduma nzima ya intaneti.
Visa vya kufungiwa au kubanwa kwa mtandao Afrika vimekuwa vikiongezeka.
Uganda ikielekea uchaguzi mkuu wa rais na wabunge uliofanyika Januari 14, mitandao ya kijamii ilikuwa imeshafungwa tayari.
Uganda iliagiza watoaji huduma za mtandao kufunga mitandao yote ya kijamii na programu za kutuma ujumbe hadi wakati usiojulikana, kwa mujibu wa barua kutoka kwa mdhibiti wa mawasiliano nchini humo iliyonukuliwa na shirika la habari la Reuters.
"Tume ya mawasiliano Uganda inaagiza kusitisha ufikiwaji na utumiaji, wa moja kwa moja au kinyume chake, kwa mitandao yote ya kijamii pamoja na programu za kutuma ujumbe mitandaoni hadi siku isiyojulikana," Barua kutoka kwa mkurugenzi mkuu wa tume ilisema hivyo kwa watoaji huduma za mtandao.
Watumiaji walikuwa wamelalamika kwamba hawakuweza kupata mtandao wa Facebook na WhatsApp, majukwaa ya mitandao ya kijamii inayotumiwa sana katika kipindi cha kampeni kabla ya uchaguzi wa urais kwenye nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Baadhi ya Waganda wameona kuwa Kenya imetoa funzo kwa mataifa mengine.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia nchini Kenya Joe Mucheru alisema hakukuwa na dalili zozote kwamba uchaguzi huo ungefanyika katika mazingira ambayo yangehitaji hatua hiyo ya kupindukia, lakini alisema kwamba Wakenya wanapaswa kutumia mitandao ya kijamii kwa uwajibikaji.
Mucheru alisema serikali ina haki ya kuchukua hatua zozote zinazohitajika ili kuhakikisha udumishaji wa utulivu wa umma, na kuongeza kuwa Wizara yake inafanya kazi kwa karibu na ile ya Mambo ya Ndani katika kutathmini vitisho vyovyote vinavyoweza kutokea na kujiandaa kwa hali yoyote.
Pia unaweza pia kusoma