Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa Tigray, Ethiopia: Kwa nini ulimwengu mzima una wasiwasi na mzozo huu?
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken anasafiri kuelekea Kenya, ambako atakuwa akizungumzia mzozo wamajirani wa Kenya, Ethiopia.
Raia wa Marekani na Uingereza wametakiwa kuondoka nchini Ethiopia "ndege za abiria ziko tayari", kwa mujibu wa waziri wa Uingereza.
Kama ilivyotokea Kabul Mwezi Agosti, ushauri huu wa kuondoka, ulitolewa kutokana na ishara za kikosi cha waasi kutoka eneo la kaskazini la Tigray kuonekana kama kinaweza kuingia katika mji mkuu, Addis Ababa.
Mwaka mmoja wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, vimesababisha hali mbaya ya kibinadamu, huku kelele kutoka mataifa ya nje zikizidi kusikika.
Shinikizo la kidiplomasia kutoka Afrika na Marekani linazidi kuongezeka, kwani kinachotokea Ethiopia kina athari kubwa kwa eneo lote la ukanda huu na ulimwengu mzima.
Kwa nini ni muhimu kufuatilia mzozo wa Ethiopia?
Takwimu zinazoihusu zinashangaza.
Takriban watu 400,000 wanadaiwa kukabiliwa na njaa kaskazini mwa nchi hiyo, 80% ya dawa muhimu za binadamu hazipatikani na zaidi ya watu milioni mbili wamelazimika kuyakimbia makazi yao kukwepa mzozo.
Serikali ya shirikisho imeshutumiwa kwa kuzuia kwa makusudi misaada ya kibinadau kufika Tigray, jambo ambalo yeyewe inakanusha.
Aidha, upo ushahidi wa mauaji yanayofanyika kinyume cha sheria, mateso na ukatili wa kijinsia unaofanywa na pande zote mbili.
Lakini pia kuna maslahi ya kimkakati. Ethiopia, yenye wakazi milioni 110 - ya pili kwa ukubwa katika bara la Afrika, imekuwa mshirika mkuu na dhabiti wa mataifa ya Magharibi katika eneo hilo lenye hali tete.
Kuna wasiwasi kwamba mapigano ya sasa yanaweza kusababisha ghasia zaidi katika taifa hili lenye makabila mengi ambayo inaweza hata kusababisha kusambaratika. Ikiwa mamilioni ya watu wakikimbia mzozo uliokithiri, nchi jirani hazitaweza kuvumilia hali hiyo.
Ethiopia inapakana na nchi sita, mbili kati ya nchi hizo tayari na zenyewe zinakabiliwa na mzozo - Sudan Kusini na Somalia - na nyingine moja, Sudan, ndiyo kwanza imeshuhudia mapiduzi ya kijeshi hivi karibuni.
Ethiopia ina wanajeshi katika majeshi ya pamoja ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa wanaopambana na wanamgambo wa Kiislamu nchini Somalia na kuna hofu kwamba wanaweza kuondolewa iwapo watahitajika kurudi nyumbani.
Kabla ya kuelekea kwenye ziara yake barani Afrika, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Bw. Blinken alionya kwamba vita vikichachamaa ni "janga kwa watu wa Ethiopia na pia kwa wengine katika eneo hilo".
Wanajeshi kutoka Eritrea tayari wanapigana nchini Ethiopia na mzozo wa muda mrefu unaweza kusumbua majirani wengine.
Lakini nchi zilizo mbali zaidi pia zimeripotiwa kuguswa na mzozo huo.
Mwezi uliopita, shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa Uturuki imekubali kuliuzia jeshi la Ethiopia, ndege za kijeshi zisizo na rubani. Mkataba huu wa mauziano ulitishia uhusiano kati ya Uturuki na Misri, ambayo ina mzozo na Ethiopia kuhusu ujenzi wa bwawa kubwa katika Mto Nile, ripoti hiyo iliongeza.
Ethiopia pia imenunua silaha kutoka China na Iran, na ndege zinazofanya safari zake kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu zinatumiwa kuzisafirisha silaha hizo, tovuti ya ulinzi ya Oryx inaripoti.
Kwa mtazamo wa Marekani, Ethiopia imeonekana kwa muda mrefu kuwa mshirika wa kutegemewa, hasa wakati wa kile kinachoitwa Vita dhidi ya Ugaidi.
Iko mstari wa mbele kwneye vita dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu nchini Somalia kuisaidia Marekani kutumia anga yake wakati wa vita vya Iraq. Ilikuwa ni moja ya nchi chache za Kiafrika kujiunga na "muungano wa walio tayari" wa Marekani kwenye vita vya Iraq.
Serikali thabiti nchini Ethiopia imekuwa muhimu kwa uhusiano huo. Marekani imekuwa ikiisaidia Ethiopia kifedha, ikiikabidhi dola $4.2bn kama msaada kati ya mwaka 2016 na 2020.
Je, mji mkuu uko hatarini?
Baada ya wapiganaji wa Kikosi cha Ukombozi cha Watu wa Tigray (TPLF) kuzidi kusonga mbele kupitia barabara kuu inayotoka kaskazini kuelekea Addis Ababa, hali ya wasiwasi iliongezeka.
Marekani ilitoa wito wa kuondoka kwa raia wake na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alitangaza hali ya hatari na kuomba kutuma wanajeshi zaidi.
Mamlaka ya Addis Ababa ilitoa wito kwa watu kusajili silaha.
Kundi jingine la waasi linaloshirikiana na TPLF lilisema pia linakaribia kuingia katika mji mkuu huo.
Hakujatulia katika jiji hilo na mivutano yenye hisia za kikabilia ikizidi kuongezeka, huku wengine wakishutumu mamlaka kwa kuwalenga watu wa Tigrayan na kuwakamata.
Lakini vikosi vya Tigrayan bado viko zaidi ya kilomita 300 kutoka mji - karibu na mji wa Kombolcha.
Je, kuna mazungumzo yoyote ya amani?
Wasiwasi uliopo sasa ni kwamba mzozo unaingia katika hatua mpya na itazidi kuwa vigumu kwa pande zote mbili kurudi nyuma na kufikia makubaliano.
Pia kuna hofu kwamba mapigano yanaweza kuenea kote nchini.
TPLF imeungana sasa na msururu wa makundi mengine pia yanayoipinga serikali katika muungano mpya unaotaka kuuuondoa utawala wa Waziri mkuu wa Bw Abiy.
Mjumbe wa Umoja wa Afrika katika eneo hilo, Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, amegusia kuhusu "nafasi finyu iliyopo".
"Muda ni mfupi wa kuingilia kati," aliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa baada ya kuzungumza na pande zote mbili wakati wa ziara ya hivi majuzi nchini Ethiopia.
Anatoa wito wa mazungumzo na suluhu ya kisiasa, ingawa bado hajaeleza jinsi jambo hilo linaweza kufikiwa.
Majibu ya balozi wa Ethiopia wa Umoja wa Mataifa, Taye Atske Selassie, yalijumuisha matatizo ambayo wapatanishi watakabiliana nayo. Alisema aliheshimu wito wa mazungumzo lakini akaendelea kuelezea TPLF kama "kundi la uhalifu".
Msingi wa mzozo huu wa Ethiopia ni kutoelewana kati ya Waziri Mkuu Abiy na kundi la TPLF, ambayo kwa karibu miaka 27 lilitawala nchi nzima, sio Tigray pekee.