Taliban 'hawaoni wanawake kama binadamu', asema Malala

Muda wa kusoma: Dakika 3

Malala Yousafzai amewataka viongozi wa Kiislamu kuipinga serikali ya Taliban nchini Afghanistan na sera zake za ukandamizaji kwa wasichana na wanawake.

"Kwa ufupi, Taliban nchini Afghanistan hawaoni wanawake kama binadamu," aliuambia mkutano wa kilele wa kimataifa ulioandaliwa na Pakistan kuhusu elimu ya wasichana katika nchi za Kiislamu.

Bi Yousafzai aliwaambia viongozi wa Kiislamu "hakuna chochote cha Kiislamu" kuhusu sera za Taliban ambazo ni pamoja na kuzuia wasichana na wanawake kupata elimu na kazi.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 27 alihamishwa kutoka Pakistan akiwa na umri wa miaka 15 baada ya kupigwa risasi kichwani na mshambuliaji wa kundi la Taliban wa Pakistani ambaye alimshambulia kwasababu ya kuzungumzia kuhusu elimu ya msichana.

Unaweza kusoma

Akihutubia mkutano mjini Islamabad siku ya Jumapili, mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel alisema "amejawa na furaha" kurejea nchini mwake. Amerejea Pakistan mara chache tu tangu shambulio la 2012, baada ya kurejea kwa mara ya kwanza mnamo 2018.

Siku ya Jumapili, alisema serikali ya Taliban imeunda tena "mfumo wa ubaguzi wa kijinsia".

Taliban walikuwa "wakiwaadhibu wanawake na wasichana wanaothubutu kuvunja sheria zao zisizoeleweka kwa kuwapiga, kuwaweka kizuizini na kuwadhuru", alisema.

Aliongeza kuwa serikali "hufunika uhalifu wao katika uhalali wa kitamaduni na kidini" lakini kwa kweli "huenda kinyume na kila kitu ambacho imani yetu inasimamia".

Serikali ya Taliban ilikataa kujibu ombi la BBC la kutoa maoni yake kuhusu mwanaharakati huyo. Hapo awali wamesema wanaheshimu haki za wanawake kwa mujibu wa tafsiri yao ya utamaduni wa Afghanistan na sheria za Kiislamu.

Viongozi wa serikali ya Taliban walialikwa kwenye mkutano huo unaoendeshwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), serikali ya Pakistani na Jumuiya ya Waislamu Ulimwenguni, lakini hawakuhudhuria.

Waliohudhuria mkutano huo walijumuisha makumi ya mawaziri na wasomi kutoka nchi zenye Waislamu wengi ambao walitetea elimu ya wasichana.

Tangu kundi la Taliban lilipodhibiti tena Afghanistan mwaka 2021, serikali yake haijatambuliwa rasmi na serikali moja ya kigeni. Mataifa yenye nguvu ya Magharibi yamesema sera zao zinazowawekea vikwazo wanawake zinahitaji kubadilika.

Afghanistan sasa ndiyo nchi pekee duniani ambapo wanawake na wasichana wanazuiwa kupata elimu ya sekondari na ya juu ,takribani milioni moja na nusu wamenyimwa kusoma shule makusudi.

"Afghanistan ndiyo nchi pekee duniani ambako wasichana wamepigwa marufuku kabisa kupata elimu zaidi ya darasa la sita," alisema Bi Yousafzai siku ya Jumapili.

Taliban wameahidi mara kwa mara kwamba watakubaliwa tena kwenda shuleni mara masuala kadhaa yatakapotatuliwa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mtaala ni wa "Kiislamu". Hili bado halijatokea.

Mnamo Desemba, wanawake pia walipigwa marufuku kupata mafunzo ya wakunga na wauguzi, na kufunga safari yao ya mwisho ya kupata elimu zaidi nchini.

Bi Yousafzai alisema elimu ya wasichana iko hatarini katika nchi nyingi. Alisema huko Gaza, Israel "imepunguza mfumo mzima wa elimu".

Aliwasihi waliokuwepo "watangaze ukiukwaji mbaya zaidi" wa haki ya watoto wa kike kupata elimu na kusema kuwa migogoro katika nchi zikiwemo Afghanistan, Yemen na Sudan ina maana "mustakhbali mzima wa wasichana unaibiwa".

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga