Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Waliniburuza chini nilipowaambia siwezi tena kutembea'
- Author, Madina Maishanu
- Nafasi, BBC Africa
- Akiripoti kutoka, Kurmin Wali
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Sarah Peter anauguza jeraha la kichwa alilopata baada ya kupigwa kichwani na mtutu wa bunduki.
Sarah, sio jina lake halisi, alikuwa kanisani katika kijiji cha kaskazini mwa Nigeria Jumapili asubuhi wakati washambuliaji walipovamia kanisa lao, kuwateka waumini na kuondoka nao.
Mama huyo aliye na umri wa miaka 60- alipigwa kichwani na mtutu wa bunduki na mmoja wa washambuliaji hao.
"Damu ilikuwa imetapakaa kila mahali," anasema akionyesha sehemu alipoumizwa kishwani mwake.
"Niliumia sana," aliongeza kusema, huku athari ya kiwewe alichopata kutokana na na tukio hilo ikiwa bado inaonekana usoni mwake.
"Waliendelea kuniburuza chini nilipowaambia siwezi tena kutembea. Waliponiacha nikajificha mpaka nikawa siwaoni tena. Nilikuwa mnyonge lakini nilijitahidi kutambaa chini mpaka nikarejea kijijini."
Makumi ya wengine walichukuliwa kutoka katika tawi la Kanisa la Cherubim na Seraphim Movement na makanisa mengine mawili huko Kurmin Wali, kijiji kilicho kilomita 135 (maili 84) kaskazini mwa mji mkuu, Abuja.
Ingawa watu 11 walifanikiwa kutoroka, akiwemo Sarah, zaidi ya watu 160 bado hawajulikani waliko, kulingana na tawi la ndani la Jumuiya ya Kikristo ya Nigeria.
Wanakijiji waliosalia wana hofia huenda wakavamiwa tena na washambuliaji hao.
Mamlaka haijatoa takwimu zozote za watu waliopotea.
Kurmin Wali iko karibu na msitu wa Rijana katika jimbo la Kaduna, maficho ya magenge yenye silaha, yanayojulikana hapa kama "majambazi", ambao wamekuwa wakiwavamia na kuteka wakaazi katika eneo hilo.
Hakuna kundi lililodai kuhusika na uvamizi huo wa Jumapili, lakini shambulio hilo ni sehemu ya mzozo mkubwa wa usalama nchini Nigeria, huku utekaji nyara kwa ajili ya fidia ukizidi kuongezeka.
Kuwalipa watekaji nyara ni kinyume cha sheria nchini Nigeria lakini mara nyingi inashukiwa kuwa pesa zimekabidhiwa ili kuwakomboa wale waliotekwa. Katika kisa cha hivi punde, hakuna malipo ya fidia yaliyoripotiwa.
Kumekuwa na mtazamo wa kimataifa kuhusu suala hilo baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kudai mwaka jana kwamba idadi kubwa ya Wakristo wamekuwa wakilengwa na kuuawa. Mwezi uliopita, jeshi la Marekani lilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo ya watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wenye itikadi kali za kidini kaskazini-magharibi mwa Nigeria.
Maafisa wa Nigeria wamekanusha kwamba Wakristo wamekuwa wakitengwa kwa sababu ya imani yao, na kuongeza kuwa ukosefu wa usalama umewaathiri Waislamu, Wakristo na wale wasio na dini.
Hali ya taharuki imetanda katika kijiji cha Kurmin Wali.
Mkuu wa kijiji alisema watu wamekuwa wakiishi kwa hofu kwa mud muda sasa. Wakaazi wa eneo hilo wamekuwa wakiomba mamlaka kuimarisha usalama na kuwashutumu kwa kujaribu kuficha kilichotokea katika uvamizi wa Jumapili.
Hali ya taharuki ilitanda kwa saa 48 watu wlikuwa wamechanganyikiwa baada ya shambulio hilo baada ya maafisa hapo awali kukanusha kilichotokea, licha ya ripoti za mashahuda, na hatimaye kuthibitisha tukkio hilo Jumanne jioni.
"Walituambia tusitoe taarifa yoyote, wanataka kututisha lakini lazima tueleze kilichotukuta. Pia wamekuwa wakiwazuia baadhi ya waandishi wa habari kufika mjini," alisema kijana mmoja mwenye umri wa miaka 20 ambaye hakutaka kutajwa jina.
Haijabainika ni kwa nini mamlaka inasitasita, lakini gavana wa jimbo la Kaduna Uba Sani aliambia BBC kwamba maafisa walitaka kuthibitisha maelezo kwanza kabla ya kutoa taarifa.
Lakini, hiyo haielezi ni kwa nini mkuu wa polisi wa eneo hilo na afisa wa serikali hapo awali walikanusha kwamba kulikuwa na shambulio lolote, akielezea ripoti hizo kama "uongo unaotolewa na watu ambao wanataka kusababisha machafuko".
BBC pia ilikabiliwa na wakati mgumu kufikia kijiji Kurmin Wali, baada ya mwanasiasa na maafisa wa usalama kujaribu kuwazuia waandishi wa habari kufika eneo la tukio.
Lakini hatimaye waandishi wetu walifanikiwa kufika. ''Mazingira katika jengo la Kanisa la Cherubim and Seraphim Movement yaliashiria mambo hayakuwa ya kawaida siku hiyo. Viti vya plastiki vilikuwa vimetapakaa kila mahali vingine vimeangushwa chini, vitabu vya maombi vimetawanyika sakafuni na vyombo vya muziki vilikuwa vimevunjwa.
Karibu na hapo, Christopher Yohanna alikuwa akimtazama kwa huzuni binti yake wa miaka miwili. Alisema alifanikiwa kuwatoroka wavamizi hao akiwa na mtoto wake.
"Tulikuwa kanisani tuliposikia kelele. Tulipotoka na kujaribu kukimbia, tuliwaona watu wenye silaha walikuwa tayari wamezingira kijiji."
Alibahatika kutokamatwa, lakini amevunjika moyo kwa sababu wake zake wawili na watoto wengine walichukuliwa.
"Sijui familia yangu iko wapi, maisha yangu sasa hayana thamani ," alisema.
Gavana Sani alitembelea Kurmin Wali siku tatu baada ya shambulio hilo, na kuahidi kuanzisha kituo cha kijeshi, hospitali na barabara katika eneo hilo. Pia alitangaza hatua za misaada kwa wakaazi walioathirika, ikiwa ni pamoja na msaada wa matibabu.
"Hatuwezi kuwahamisha kwa sababu wanapaswa kulima... lakini ili kuhakikisha kwamba tunawalinda mbele, tunahitaji kuwa na kambi ya kijeshi karibu na eneo hilo kati ya kijiji hicho na msitu wa Rijana," aliiambia BBC.
Pia alisema juhudi zinaendelea kufanya kazi na vyombo vya usalama kuwaokoa wale ambao bado wako mateka.
"Tulipokutana na [wanakijiji] nilithibitisha kwamba tuko pamoja nao na... hatutamwacha hata mmoja wao."
Huku wakaazi wa Kurmin Wali wakisubiri kwa hamu kurudi kwa wanafamilia wao, wanatumai kuwa gavana atatimiza ahadi yake.