Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini bei ya dhahabu inaongezeka kwa kasi?
Bei ya dhahabu kwa aunsi moja imepita dola 5,000 za Kimarekani. Thamani ya dhahabu imeongezeka kwa 60% mwaka wa 2025, na inazidi kuongezeka mwaka wa 2026.
Mvutano kati ya Marekani na Jumuiya ya kujihami ya NATO kuhusu eneo la Greenland, imeongeza wasiwasi kuhusu hali ya Uchumi na kutokuwa na uhakika wa siasa za kijiografia.
Sera za Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu biashara pia zinazua wasiwasi katika masoko mengi.
Trump ametishia kuiwekea vikwazo vya asilimia mia moja taifa la Canada, iwapo watatia saini mkataba wa kibiashara na China.
Dhahabu na madini mengine yenye thamani, yamegeuka kuwa rasilimali kwa wawekezaji wengi kutokana na kuyumbayumba kwa soko la biashara.
Mwezi Januari 24, bei ya fedha kwa kila ounsi ilipita dola mia moja kwa mara ya kwanza. Thamani ya fedha kuanzia mwaka uliopita na mwaka huu imeongezeka kwa asilimia mia moja hamsini.
Sababu ya hitaji la dhahabu kuongezeka
Sababu kama vile mfumuko wa hali ya juu, kushuka kwa thamani ya sarafu ya dola, kununuliwa kwa dhamana zinazotolewa na benki kuu kote duniani, na matumaini kuwa benki kuu ya Marekani itapunguza viwango vya riba mwaka huu, kumechangia kupanda kwa bei ya madini.
Kando na vita vya Ukraine na Gaza, kuondolewa kwa aliyekuwa rais wa Venezuela Nicolas Maduro madarakani, pia kumechangia kupanda kwa bei ya dhahabu.
Mojawapo wa kipengele muhimu kuhusu dhahabu ni jinsi imeadimika.
Kulingana na baraza la kimataifa la dhahabu, takriban tani 216,265 za dhahabu zimechimbwa kufikia sasa.
Kiwango hicho kinaweza kujaza takriban bwawa nne za olimpiki za kuogelea.
Nyingi ya dhahabu hizi zilichimbwa baada ya mwaka wa 1950, baada ya teknolojia ya kugundua ni wapi dhahabu zipo ardhini ilivumbuliwa.
Kulingana na uchunguzi wa jiolojia nchini Marekani, tani zingine 64,000 za dhahabu bado zinaweza kuchimbwa kutoka ardhini, ila hakutakuwa na upungufu wa dhahabu katika miaka kadhaa ijayo.
Nicolas Frappell, mkuu wa kitengo cha mauzo katika kampuni ya kusafisha dhahabu ya ABC anasema;
"Ukimiliki dhahabu, hauna deni la mtu mwingine, kama vile kununua dhamana ya benki au hisa.Ikija kwa hisa matokeo ya mauzo ya kampuni moja haiwezi kuathiri thamani ya dhahabu"
Anaongezea kuwa: "Dhahabu ni nzuri katika uwekezaji haswa wakati huu ambapo vitu havina uhakika duniani"
'Watu wamegeukia dhahabu katika uwekezaji'
Wawekezaji walipokimbia kununua madini hayo yenye thamani, bei ya dhahabu iliongezeka maradufu tangu mwaka wa 1979, na kuuzwa kwa bei ya juu zaidi mwaka wa 2025.
Kuongezeka kwa bei ya dhahabu kumetokana na wasiwasi ulioletwa na ushuru wa Trump, na pia matumizi ya akili mnemba ambayo
yalipandisha bei ya hisa na kusababisha kuongezeka kwa bei ya madini tofauti.
"Yote haya ni kutokana na sintofahamu ilioletwa na sera za Marekani" Anaelezea Nikos Kavlis, mchambuzi katika shirika la utafiti la advisory firm Metals Focus.
Jinsi tu wasiwasi kuhusu uchumi umesababisha bei ya dhahabu kuongezeka, thamani ya dhahabu pia huongezeka wakati wawekezaji wanatumai kuwa viwango vya riba vitapungua.
Viwango vya chini vya riba humaanisha kuwa kutakuwa na mapato ya chini haswa kwa dhamana za benki, na wawekezaji sasa wanageukia rasilimali kama vile dhahabu na fedha.
Benki kuu ya Marekani inatarajiwa kupunguza viwango vya riba mara mbili mwaka huu.
Ahmed Assiri ni mtafiti wa mikakati katika kampuni ya Pepperstone anasema:
"Kuna uhusiano wa kinyume hapa, kwa sababu faida ya kununua dhamana za serikali haipo tena, ndio maana watu wamegeukia dhahabu."
Sio wawekezaji pekee ndio wanaonunua dhahabu.
Kulingana na baraza la kimataifa la dhahabu, benki kuu nyingi ziliongeza tani ya dhahabu wanazohifadhi mwaka uliopita.
"Kuna mtazamo tofauti wa dolla ya Marekani, ambayo imeinufaisha dhahabu" Anasema Nikos Kavlis.
Ingawa bei ya dhahabu imekuwa ikipanda kuanzia mwanzo wa mwaka huu, Frappell anaonya kuwa soko linaoendeshwa na vyombo vya habari linaweza kuchangia bei ya dhahabu kushuka.
"Lazima kuwe na nafasi ya habari ambazo hazijatarajiwa ambayo si njema kwa dhahabu ila ni nzuri kwa dunia"
Ila si kila mmoja hununua dhahabu kwa ajili ya uwekezaji
Dhahabu hununuliwa msimu wa likizo na kupeanwa kama zawadi wakati wa sherehe tofauti kama vile harusi.
Katika sherehe za kila mwaka za Diwali nchini India, ambayo ni msimu wa kuleta utajiri na mafanikio, unasemekana kuwa wakati mzuri wa kununua madini ya thamani.
Kulingana na benki ya uwekezaji ya Morgan Stanley nchini Marekani, familia nchini India zinamiliki dhahabu zenye thamani ya dolla trillioni 3.8, ambayo ni sawa na asilimia 88.8 ya kipato cha taifa hilo.
China pia ni mnunuzi mkubwa wa dhahabu, huku raia wengi wa taifa hilo wakiwa na Imani kuwa kununua dhahabu huleta bahati nzuri.
Kavlis anasema "huwa kunakuwa na ongezeko la soko la dhahabu msimu wa mwaka mpya mwezi Februari nchini China, na tayari tunaliona hilo."
Wataalam wanasema kuna sababu za bei ya dhahabu kubadilikabadilika baada ya kuuzwa kwa bei ya juu zaidi mwezi Oktoba, na moja wa sababu hizo ni wawekeaji kutaka kuuza dhahabu kupata faida.
Makadirio ya benki ya mwaka 2026 ni yepi?
Siasa za kijiografia, sintofahamu ya kiuchumi, benki kuu kununua dhahabu, chaguo la wawekezaji na kupunguzwa kwa viwango vya riba na benki ya Marekani, ulichangia pakubwa katika ukuaji ulioshuhudiwa mwaka wa 2025.
" Hii inaweza kuzingatiwa kama wimbi sahihi ya dhahabu" Anasema Louise street, mchambuzi wa soko katika baraza la kimataifa la dhahabu.
Akijibu maswali kutoka shirika la BBC la Uturuki, Professa Özge Öner, kutoka idara ya Uchumi katika chuo kikuu cha Cambridge anasema, "dhahabu imekuwa njia ya kuwekeza yenye thamani kwa miaka mingi, na imejulikana kama njia salama ya kuwekeza wakati wa misukosuko"
Suki Cooper, mmoja wa wakurugenzi katika benki ya Standard Chartered anasema kuwa "tunadhamiria kuwa bei ya dhahabu mwaka wa 2026 itafikia dola 4,488, na kuna uwezekano wa bei hio kuongezeka zaidi."
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula