Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mila au sayansi? Simulizi za wanawake kuhusu tiba asili za kujifungua kwa urahisi
Nje ya wodi ya uzazi katika Hospitali ya Mamadou Diop, eneo la Liberté 6 Extension mjini Dakar, wanawake watatu wajawazito waliokaribia kujifungua walikuwa wakitembea huku na kule. Mmoja wao alionekana mchovu sana; hatua zake zilikuwa nzito na za pole pole. Wenzake wawili walitembea kwa kasi kidogo zaidi.
Kwa maelezo yao, mkunga wa hospitali, ambaye hatukuweza kuzungumza naye, ndiye aliyewaomba wafanye matembezi hayo kama aina ya mazoezi mepesi, wakisubiri muda mwafaka wa kujifungua. Mwanamke aliyeonekana mchovu zaidi tayari alikuwa ameanza uchungu wa kujifungua.
Kwa tabasamu dogo la huzuni, Khady Ndiaye anasimulia kuwa alipitia hali kama hiyo miaka miwili iliyopita alipomzaa mtoto wake wa kwanza wa kike. Sasa anakaribia kujifungua mtoto wake wa pili.
"Maumivu hayazoeleki kamwe," anasema.
Ingawa hatukuweza kupata maoni ya mkunga wa hospitali, Dkt. Jean-Claude Togbé, daktari wa kawaida katika kliniki moja mjini Lomé, Togo, anaeleza kuwa kuusogeza mwili husaidia kufungua nyonga ya mwanamke na kumweka mtoto katika nafasi nzuri, jambo linalorahisisha na kuharakisha kujifungua.
"Ndiyo maana tunawashauri wajawazito kufanya mazoezi, hasa katika wiki za mwisho kabla ya kujifungua," anasema. Hata hivyo, anaonya kuwa si michezo yote inafaa kwa wajawazito. "Mazoezi kama yoga yanafaa sana kwa wanawake wajawazito," anaongeza.
Mbali na mazoezi yanayopendekezwa na wataalamu, baadhi ya wanawake hutumia njia nyingine za asili ili kupunguza maumivu na kuepuka uchungu wa muda mrefu wa kujifungua.
Katika nchi nyingi za Afrika, matumizi ya vinywaji vya mitishamba (majimaji ya mizizi au majani yaliyochemshwa) ili kusaidia kufunguka kwa mlango wa uzazi na kuimarisha uchungu yameenea sana.
Je, chai ya mitishamba husaidia kujifungua?
Baadhi ya wajawazito hupata dalili kama kuongezeka uzito, maumivu ya mishipa ya mwili, au miguu kuwa mizito na kuvimba.
Kwa mujibu wa Afefa Bolou, mkunga mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka kumi huko Lomé, dalili hizi mara nyingi huashiria kuwa ujauzito unakaribia mwisho.
Hata kabla ya kufikia hatua hiyo, wanawake wengine huanza kutumia tiba za jadi au mimea asilia ili kuharakisha au kuchochea uchungu wa kujifungua. Tassi Mama, aliyekuwa mkunga wa jadi na mtaalamu wa mitishamba mjini Comé, Benin, anasema mimea inayotumiwa si hatari ikiwa itatumika kwa usahihi.
"Hizi si mimea migumu au yenye sumu," anasisitiza.
Kwa mujibu wake, chai ya majani ya papai yaliyokomaa na kukaushwa husaidia kumweka mtoto katika mkao mzuri na kurahisisha kujifungua.
"Mwanamke anapaswa kuanza kuinywa kuanzia mwezi wa saba wa ujauzito, asubuhi na jioni," anasema.
Pia anashauri kunywa maji yenye ute yanayotokana na bamia iliyochemshwa, hasa katika mwezi wa mwisho wa ujauzito.
"Husaidia mtoto kushuka vizuri na kufanya kujifungua kuwa rahisi," anaeleza.
Marceline Attiogbé, mmoja wa wanawake waliotumia njia hiyo, anathibitisha kuwa ilimsaidia.
"Nilikunywa chai ya majani ya papai asubuhi na jioni. Mwezi wa tisa nikaacha na kuanza kufanya mazoezi. Nilifanya hivyo baada ya hospitali kuniambia mtoto wangu alikuwa mkubwa," anasimulia.
Pia, chai ya majani ya rasiberi hutajwa kuwa husaidia wakati wa uchungu wa kujifungua. Hata hivyo, Tassi Mama anakumbusha kuwa tiba hizi si miujiza na anasisitiza umuhimu wa ushauri kabla ya kuzitumia.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa lishe Angèle Kouto, majani ya rasiberi yana kemikali iitwayo frangine, ambayo husaidia kuchochea mfuko wa uzazi na kufanya uchungu uwe wa mpangilio mzuri.
"Kuna hatari ..."
Licha ya umaarufu wake, tiba hizi za asili zinaibua mjadala mkali.
Wataalamu wengi wa afya, hasa madaktari, wanazipinga au kuzitazama kwa tahadhari kubwa.
Afefa Bolou anasema wazi kuwa hakuna daktari anayependekeza wajawazito kunywa chai za mitishamba ili kujifungua kwa urahisi. Anasema kuna hatari ya matumizi yasiyo sahihi na bado hakuna tafiti za kutosha kuhusu kemikali zilizomo kwenye mimea hiyo.
Anatahadharisha kuwa kunywa mitishamba bila ushauri wa kitaalamu kunaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwemo mtoto kufariki tumboni.
"Wakati mwingine tunakuta maji ya uzazi yana rangi isiyo ya kawaida. Baada ya kuuliza, tunagundua mama alikuwa akinywa chai za mitishamba," anaeleza.
Anakiri kuwa katika hali chache, wakunga huwashauri wajawazito kutumia chai ya majani ya mpapai kwa muda mfupi ili kumsaidia mtoto kushuka. Hata hivyo, matumizi ya muda mrefu yanaweza kusababisha maji ya uzazi kupasuka mapema kabla ya uchungu kuanza, jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya mtoto.
Kukosa subira kwa baadhi ya wagonjwa
Kwa mujibu wa mkunga huyo, wakati mwingine shinikizo hutoka kwa wazazi au wakwe wa mwanamke mjamzito, ambao kwa siri humpa mitishamba au dawa za jadi.
"Baadaye mwanamke huanza kupiga kelele kwa maumivu makali, bila sisi kujua kilichotokea," anasema kwa masikitiko.
Anasisitiza kuwa hakuna dawa inayoweza kuondoa kabisa maumivu ya uchungu wa kujifungua. Kazi ya wakunga ni kufuatilia hali ya mama, kumsaidia kutembea, kumfundisha mbinu za kupumua, na kumpa moyo ili mtoto azaliwe salama.
Mlinde mtoto na uamini mtaalamu
Dkt. Jean-Claude Togbé anasisitiza kuwa ujauzito ni kipindi nyeti sana.
"Kama daktari, siwezi kumshauri mjamzito anywe mitishamba ili kujifungua. Ufuatiliaji mzuri wa kitabibu unatosha," anasema.
Anakiri kuwa kuna hali maalumu zinazohitaji hatua za kitabibu, lakini hizo hufanywa chini ya uangalizi wa wataalamu.
Kulingana naye, utafiti wa kimatibabu, hasa barani Afrika, bado haujathibitisha ufanisi wa dawa hizi za asili au tiba za nyumbani ambazo wanawake wengi hutumia leo. Kwa hiyo anapendekeza tahadhari kubwa katika matumizi yao.
Tassi Mama, kwa upande wake, anakiri kuwa wajawazito wanaotumia chai hizi za mitishamba wanahitaji mwongozo ili kuhakikisha hawazidi kiwango kilichopendekezwa. Hata hivyo, anasalia kuamini kwamba mimea, hasa ile aliyotaja awali, ina ufanisi katika kusaidia wanawake wakati wa ujauzito.
"Tulikuwa tukitumia hii kusaidia wanawake kujifungua. Ni kweli tiba ya sasa imeendelea, lakini mimea pia ina thamani yake," anahitimisha.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid