Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Miaka 10, Marais 8 - Kuna nini Peru karibu kila mwaka rais mpya?
Ndani ya kipindi cha chini ya muongo mmoja, taifa la Peru limepitia mabadiliko ya uongozi ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika historia yake ya karibuni. Tangu mwaka 2016, marais wanane wameapishwa kuiongoza nchi hiyo, wengine wakidumu madarakani kwa miezi au hata siku chache tu. Hali hii imeibua maswali makubwa kuhusu uimara wa taasisi za kisiasa za taifa hilo.
Kuondolewa kwa Rais José Jerí kwa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye na Bunge kumemfungulia njia José María Balcázar kushika wadhifa wa urais kwa muda hadi Julai 28, wakati rais mpya atakayechaguliwa ataapishwa. Tukio hilo limeongeza orodha ya viongozi walioondoka madarakani kabla ya kukamilisha mihula yao.
Katika kipindi hiki, Peru haijashuhudia mapinduzi ya kijeshi, bali imekuwa ikishuhudia kile ambacho wachambuzi wanakiita "mapinduzi ya kikatiba", mchakato ambapo Bunge linatumia mamlaka yake kumng'oa rais kwa misingi ya kisheria lakini katika mazingira yenye mgawanyiko mkubwa wa kisiasa.
Kwa wananchi wa kawaida, mabadiliko haya ya mara kwa mara yameathiri imani kwa viongozi na taasisi za dola. Kauli inayosikika mara kwa mara mitaani ni kwamba nchi ipo kwenye mzunguko usioisha wa migogoro ya kisiasa.
Marais waliotawala Peru miaka 10 iliyopita
Kuanzia 2016 hadi 2018, Pedro Pablo Kuczynski aliongoza nchi hiyo kabla ya kujiuzulu kufuatia kashfa za rushwa zilizohusishwa na sakata la Odebrecht. Nafasi yake ilichukuliwa na Martín Vizcarra, ambaye baadaye aliondolewa madarakani mwaka 2020 kwa tuhuma za "kimaadili," hatua iliyozua maandamano makubwa nchini humo.
Baada ya kuondolewa kwa Vizcarra, Manuel Merino aliapishwa lakini alidumu kwa siku tano pekee kutokana na shinikizo la maandamano ya umma. Uongozi wa mpito ukakabidhiwa kwa Francisco Sagasti, ambaye aliongoza taifa hilo hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.
Mwaka 2021, Pedro Castillo aliingia madarakani baada ya ushindi mwembamba katika uchaguzi mkuu. Hata hivyo, aliondolewa miaka mwaka mmoja baadaye mwaka 2022 kufuatia jaribio lake la kulivunja Bunge kabla ya kupigwa kwa kura ya kumng'oa. Makamu wake, Dina Boluarte, akawa rais lakini naye alikabiliwa na maandamano makubwa na shinikizo la kisiasa kabla ya kuondolewa madarakani.
Rais wa muda José Jerí alidumu kwa miezi minne tu kabla ya kuondolewa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka. Sasa jukumu la kuiongoza Peru kwa mpito lipo mikononi mwa José María Balcázar, anayetarajiwa kukabidhi madaraka kwa rais mpya atakayechaguliwa. Je atafika mwezi Julai? hakuna anayejua
Karibu kila mwaka rais mpya, kwanini?
Chanzo kikuu cha mabadiliko haya ya mara kwa mara ni kipengele cha Katiba ya Peru kinachoruhusu Bunge kumwondoa rais kwa misingi ya "kukiuka maadili." Ingawa lengo lake lilikuwa kuhakikisha uwajibikaji, kifungu hicho kimekuwa silaha ya kisiasa katika mazingira ya mgawanyiko mkubwa wa vyama.
Aidha, Peru imekumbwa na kashfa za rushwa kwa miaka mingi, hasa zile zilizohusishwa na kampuni ya Odebrecht, ambazo ziliwahi kuwahusisha viongozi kadhaa wa juu serikalini. Kashfa hizi zimeendelea kudhoofisha uhalali wa marais walioko madarakani.
Mgawanyiko mkali kati ya mhimili wa Bunge na ule wa Rais umechangia hali ya mvutano wa kudumu. Marais wengi wameingia madarakani bila kuwa na wingi wa wabunge wanaowaunga mkono, jambo linalowafanya wawe katika hatari ya kuondolewa wakati wowote.
Zaidi ya hayo, ukosefu wa imani ya wananchi kwa wanasiasa umeongeza shinikizo la umma kila mara kunapotokea tuhuma au migogoro. Maandamano ya mara kwa mara yamekuwa kichocheo cha mabadiliko ya ghafla ya uongozi.
Je, ndiyo nchi inayoongoza kwa mabadiliko ya uongozi?
Katika historia ya bara la Amerika ya Kusini, mataifa kadhaa yamewahi kushuhudia mapinduzi au misukosuko ya kisiasa. Hata hivyo, ni nadra kwa taifa lenye mfumo wa kidemokrasia thabiti kubadilisha marais mara nane ndani ya kipindi cha chini ya miaka kumi bila mapinduzi ya kijeshi.
Kwa kulinganisha, nchi nyingi katika eneo hilo zimekuwa na mabadiliko ya uongozi kupitia uchaguzi wa kawaida, huku marais wakimaliza mihula yao. Hali ya Peru inaonekana kuwa ya kipekee kwa kasi ya mabadiliko ndani ya mfumo wa kikatiba.
Wachambuzi wa siasa wanasema hali hii inaashiria mgogoro wa kimuundo si tu mgogoro wa watu binafsi bali wa mfumo mzima wa kisiasa. Bila marekebisho ya kikatiba au mageuzi ya kisiasa, mzunguko huu kuondolewa madarakani marais unaweza kuendelea.
Uchaguzi ujao unatazamwa kama fursa ya kurejesha utulivu wa kisiasa. Lakini iwapo mizizi ya migogoro haitashughulikiwa, Peru inaweza kuendelea kubeba sifa ya kuwa moja ya mataifa yenye mabadiliko ya haraka zaidi na ya muda mfupi ya uongozi wa kitaifa.
Taarifa hii inatokana na mchango wa Vanessa Buschschlüter na Yang Tian na vyanzo vingine